Kushikiwa kiti kwenye daladala jijini Dar es Salaam Shilingi 500

YEHODAYA

JF-Expert Member
Aug 9, 2015
36,908
51,904
Dar es Salaam. Usafiri kafiri, ndivyo unavyoweza kuutumia msemo huo wa Kiswahili kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam ambao baadhi yao hawajui utamu wa kukalia kiti ndani ya daladalazinazofanya safari zake katika maeneo tofauti.

Kupata kiti imegeuka anasa kwa baadhi yao, lakini ni neema kwa wengine walioamua kujiongezea kipato hasa nyakati zenye abiria wengi vituoni.

Haijalishi kama umewahi kufika kituoni au umechelewa, kupata kiti ni ndoto ambayo unaweza kuota kwa mwaka mzima na isitimie.

Ukitaka kupata kiti ndani ya daladala katika baadhi ya maeneo utapaswa kuilipia Sh500 tofauti na nauli inayotozwa na kondakta kwa eneo unalokwenda.

Kiwango hiki cha fedha unapaswa kukilipa kabla ya safari kuanza na kwa mtu ambaye si lazima awe kwenye safari hiyo.

Mwananchi imefuatilia katika baadhi ya vituo vyenye msongamano wa abiria, baadhi ya vijana wamejiajiri kushikilia viti kwa abiria wanaoshindwa kugombea gari au wasiotaka kusimama wakati wa safari husika.

Maeneo yaliyokithiri

Ruti zilizokithiri kwa vitendo hivyo ni magari ya Mbezi yanayokwenda Gongo la Mboto, Gongo la Mboto yanayokwenda Segerea - Kawe na Segerea- Chanika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, vijana wanaofanya kazi hizo, akiwemo Johnson Gerald, amesema utaratibu huo wa kushikia abiria viti ulianza kipindi ambapo Uviko-19 umepamba moto na Serikali kuagiza watu wasirundikane na wakishaenea kwenye viti basi liondoke.

“Kipindi ambacho Serikali ilitoa agizo la abiria kutojazana, kupata gari ilikuwa ni tabu, hivyo wasiokuwa na nguvu za kugombea ndio tukawa tunawasaidia kwa kutulipa Sh500 nasi tunawashikia viti,” anasema Gerald.

Hata hivyo, alipoulizwa kwa nini sasa bado wanaendelea na utaratibu huo hadi leo licha ya mabasi kujaza abiria tofauti na ilivyokuwa wakati wa Uviko-19, Gerald anasema ni katika kutafuta njia ya kujiingizia kipato na kuwepo kwa abiria wanaotaka kushikiwa viti kutokana na kushindwa kuhimili kugombania gari linapoingia kituoni hapo.

Akizungumzia kuhusu hela anayoipata kwa siku, Gerald amesema kwa sasa kwa kufanya kazi hiyo huondoka na Sh7000 hadi Sh8000 kwa siku, ikiwa ni tofauti na kipindi cha Uviko-19 alipokuwa akipata Sh15,000 hadi Sh20,000.

Alipoulizwa ni muda gani hasa magari yanakuwa ya shida, anasema ni asubuhi kwa magari ya Segerea-Kawe, huku yale ya Gongo la Mboto-Segerea usafiri wake unakuwa tabu jioni kuanzia saa 12.

Gengemkeni Mitomingi, anayefanya shughuli hiyo kituo cha daladala Mbezi, anasema hawamlazimishi mtu kulipa kiwango hicho cha fedha, bali ni mahitaji yake mhusika kwa kuwa huulizwa kwanza na akikubali ndipo kazi hufanyika.

Kudhibiti wizi

Mitomingi anasema matukio ya wizi wakati wa kugombania gari yamekuwa ni mambo ya kawaida katika maeneo mengi, lakini kwao ni tofauti kwa kuwa wanafahamiana na wameshakubaliana kuyadhibiti.

“Tukigundua kuna tusiyemfahamu kaingia huwa tunatoa taarifa kwa ulinzi shirikishi na tunakoelekea tunataka tuwe na vitambulisho kabisa,” anasema.

Jamal Abdul ambaye anafanya shughuli hiyo kituo cha Gongo la Mboto kwenye mabasi yanayokwenda Chanika, anasema kuwashikia watu viti kwenye daladala kunawasaidia wajiepushe na mambo yasiyofaa mtaani, ikiwemo uhalifu na kujiunga kwenye makundi ya uhalifu.

Kwa upande wake Husein Amri wa kituo kipya Gongo la Mboto, anasema baadhi ya wanaofanya shughuli hiyo ni madereva wenye leseni na makondokta.

Anasema wamekuwa wakiendesha magari ‘deiwaka’ pale dereva wa gari husika anapopata dharura au kutaka kupumzika, hivyo kwa wakati ambao wanakuwa hawajapata kazi ndio wanafanya shughuli hiyo.

“Hapa ndio tukitoka majumbani kwetu tunasema tunakuja ofisini, sasa huwezi ukaja siku nzima ukakaa tu bila kufanya chochote cha kukuingizia fedha, ukizingatia kuwa unahitajika kula, nauli na bado unatakiwa uache hela nyumbani kwa ajili ya familia, hivyo kujiongeza muhimu.”

Abiria wafurahia

Baadhi ya abiria wameliambia Mwananchi, kuwa vijana hao kuna wakati wamekuwa msaada mkubwa kwao ukizingatia kuna watu hawana nguvu ya kugombea, wengine ni wagonjwa au wazee.

“Mtu unaona ya nini uvunjwe mkono, uibiwe au kuchaniwa pochi yako wakati wa kugombea kuingia kwenye gari wakati kuna mtu unaweza kumpa Sh500, ukapata kiti ukakaa kwa amani, wanatusaidia kwa kweli,” anasema Fatina Mbarouk.

Maria Abraham anasema umuhimu wa vijana hao katika kituo cha daladala Mbezi huonekana zaidi kwa mtu anayetoka safari akiwa na mizigo yake.

“Hawa vijana wanatusaidia,hasa tunaotoka mikoani tukiwa tumebeba mizigo na magari kutukataa, lakini hawa mbali ya kukushikia siti pia wanazungumza na kondokta kuhusu kukubebea mizigo yako na hivyo kukufanya usikae sana kituoni,” anasema Maria.

Karim Mansuri anasema licha ya vijana hao kusaidia baadhi ya watu, lakini hawapaswi kuchekewa kwani kuna wakati huwa chanzo cha kufanya usafiri uwe wa tabu kwa abiria.

“Haiwezekani wewe umepambana umegombea gari, halafu unaingia ndani unakuta siti tayari imekaliwa na mtu, ghafla unaona abiria mwingine anaingia anapishwa anakaa na kwa kuwa wanajuana na madereva na makodakta huwa wakienda kupandia mbali magari haya na kuingia nayo kituoni.

Fina Mwampamba anasema utaratibu huo unawaongezea gharama za usafiri abiria, hasa watu wanaotoka majumbani mwao wakiwa na nauli taslimu.

Uongozi hauwatambui

Kaimu Kamanda Mkuu wa kituo cha Mbezi, Maunga Maulid anasema hawawatambui vijana hao na wanapambana na vitendo hivyo, lakini abiria ndio wanachangia uwepo wao.

Mwenyekiti wa madereva kituo cha Mbezi, Azimio Msoma anasema hao ni wapiga debe walioamua kubuni njia mpya ya kujipatia fedha isivyo halali na baadhi ya abiria wakati mwingine hawataki kulipa tena nauli wakidai walishalipa.

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), inasema watu hao hawatambuliki na wanachokifanya ni kinyume na sheria.

Kaimu Mkurugenzi wa Latra Mhandisi Hanya Mbarawa, anasema watafanyia kazi taarifa ya vijana hao ili kujua ukubwa wa tatizo hilo na kama itabainika kuwa kuna uhaba wa magari wataangalia namna ya kuongeza katika ruti hizo ili abiria wasafiri bila bughudha.

Source:Gazeti la Mwananchi
 
Mwandishi kadanganya kwenye hizo ruti ,magari ya chanika gongo la mboto yapo kibao ,segerea chanika hakuna watu wengi pia,Segerea -Kawe pia hamna usumbufu asubuhi labda kurudi usiku toka Kawe .

Hakuna wanaouza seats segerea ,kutoka segerea magari ya mnazi moja ndo watu kibao ila hamna hayo mambo .
Hayo mambo yapo magari yanayotoka Mbagala asubuhi na jioni
 
Hii imenikuta juzi kati ingawa kwa sura tofauti.

Nipo makumbusho nataka kwenda buza ila naona abiria wengi mno wa njia moja hivyo ni kugombania.

Nkaamua kiustaarabu nifanye kama nayafata magari kule yanapotokea bahati nzuri kufika kwenye lile tuta la pili kona ya kwenda bakita nikapata gari na nikachagua siti ya dirishani.

Sasa kimbembe ni pale gari inakaribia kukata kona ya stand konda anadai nauli kabisa nikampa buku lakini cha ajabu bado anadai nauli kwa maana aitoshi.

Namuuliza konda iweje unidai nauli wakati mimi ndio nakudai chenchi akanambia wewe umepanda ya kurudi nayo hivyo unapswa ulipe nauli mbili.Aisee nikatoa mimacho hiyo na konda akajiongeza ikabidi akate ile ile 300 yake ili mambo yasiwe mengi.
 
Mwandishi kadanganya kwenye hizo ruti ,magari ya chanika gongo la mboto yapo kibao ,segerea chanika hakuna watu wengi pia,Segerea -Kawe pia hamna usumbufu asubuhi labda kurudi usiku toka Kawe .

Hakuna wanaouza seats segerea ,kutoka segerea magari ya mnazi moja ndo watu kibao ila hamna hayo mambo .
Hayo mambo yapo magari yanayotoka Mbagala asubuhi na jioni
Mimi nimewahi kuona Kariakoo -Tegeta huo mchezo. Kuna mmoja aliuziwa seat kama 1000 Tsh, konda alivyokuja kudai chake jamaa akasema ashalipa ila hakumbuki kampa nani
 
Mimi nimewahi kuona Kariakoo -Tegeta huo mchezo. Kuna mmoja aliuziwa seat kama 1000 Tsh, konda alivyokuja kudai chake jamaa akasema ashalipa ila hakumbuki kampa nani
mi huwa siwaanini hata hao wanaouza city ,kuna kipindi nilipokuwa mbagala ,nikitaka kupanda magari ya kwenda stesheni naenda Zakiem nageuza nayo
 
Hii inawahusu jamaa zangu wa kule Mbagala na Gongo la mboto hasa mida ya asubuhi wakienda kazini.
 
Hii inawahusu jamaa zangu wa kule Mbagala na Gongo la mboto hasa mida ya asubuhi wakienda kazini.
Daah! Nakumbuka wakati fulani hapo Riverside darajani pale jamaa zikisema ' mbagalaaaaa" unaona raia wanagombania mlango, wengine wanapitia dirishani, ukitoka hapo check mfukon, simu hauna, noti imeenda, siti hujapata
 
Mwandishi kadanganya kwenye hizo ruti ,magari ya chanika gongo la mboto yapo kibao ,segerea chanika hakuna watu wengi pia,Segerea -Kawe pia hamna usumbufu asubuhi labda kurudi usiku toka Kawe .

Hakuna wanaouza seats segerea ,kutoka segerea magari ya mnazi moja ndo watu kibao ila hamna hayo mambo .
Hayo mambo yapo magari yanayotoka Mbagala asubuhi na jioni
Acha ku generalize, hakuna route yenye usumbufu kiboya kama hizo ulizotaja. Wanamambo ya kijinga Sana..
 
Mwandishi kadanganya kwenye hizo ruti ,magari ya chanika gongo la mboto yapo kibao ,segerea chanika hakuna watu wengi pia,Segerea -Kawe pia hamna usumbufu asubuhi labda kurudi usiku toka Kawe .

Hakuna wanaouza seats segerea ,kutoka segerea magari ya mnazi moja ndo watu kibao ila hamna hayo mambo .
Hayo mambo yapo magari yanayotoka Mbagala asubuhi na jioni
Unajua mziki wa Segerea Makumbusho kwa asubuhi na Makumbusho Segerea kwa jioni?
 
Acha ku generalize, hakuna route yenye usumbufu kiboya kama hizo ulizotaja. Wanamambo ya kijinga Sana..
mkuu segerea ipi? Kama ni segerea mwisho stendi sijawahi kuona watu wanashikiwa seats maana mi almost kila siku natokea segerea kwenda kwenye mishemishe.
 
Back
Top Bottom