Kusambaza picha za ukatili wa kingono kwa watoto mtandaoni humuathiri mtoto; sio kuifunza jamii

Sema Tanzania

JF-Expert Member
May 18, 2016
251
465
Mwezi Novemba mwaka huu, Huduma za Simu kwa Mtoto kutoka nchi za Afrika pamoja na nchi za Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika zimekutana na kufanya mkutano uliongazia hali ya ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili wa kingono mtandaoni. Kati ya changamoto kubwa za kumlinda mtoto mtandaoni imekuwa ni tabia ya wanajamii, wakiwemo wazazi na waalimu, kuwaadabisha watoto huku wakiwarekodi. Imefikia hatua ya watu kurekodi hata pale mtoto anapoelezea tukio la ukatili wa kingono na kisha kusambaza mitandaoni kwa lengo la ‘kusaidia na kuwakanya wazazi wengine wawalinde watoto wao.’

Katika makala haya ya malezi leo tumeona tuzungumze juu ya elimu kuhusu ulinzi wa watoto mitandaoni, na athari za kusambaza maudhui ya ukatili wa kingono kwa watoto mtandaoni. Pia tutakujuza kuwa zipo namna bora za kumsaidia mtoto awe salama mtandaoni.

Mara nyingi tumeona picha na video za watoto wakifanyiwa ama kuhojiwa kuhusu ukatili wa kingono zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Facebook na Instagram. Wengine hudhani kusambaza ndio kumsaidia mtoto aliyeathirika na vitendo hivi, wengine husambaza maudhui hayo iwe angalizo na fundisho kwa wanajamii wakiwataka wawalinde watoto. Wapo pia wale ambao hurekodi na kusambaza maudhui haya ikiwa ni burudani na hata biashara.

Ukweli ni kwamba usambazaji wa picha na video hizi humuumiza mtoto anayeoneka humo zaidi na sio kumsaidia kama tulivyodhamiria. Kila picha ama video yenye maudhui ya unyanyasaji wa kingono kwa mtoto inapopakiwa, inaposambazwa, inapopakuliwa au inapotazamwa, mtoto huyo huathirika na unyanyasaji huo upya. Huyu ni mtoto aliye hai na amepitia ukatili wa kutosha tayari. Tumhurumie!

Mfano mwaka 2017 ilisambazwa video ya mtoto mdogo akikatika dansi sakafuni huku akirekodiwa na kuimbiwa wimbo maarufu wa ‘Chura’. Mchukua video anasikika akimhoji mtoto, “Dorica, nani kakufundisha?”…Mahojiano yanaendelea na wote wanasikika wakicheka. Usambazaji wa video kama hii unaendelea kumdhalilisha mtoto huyu ambaye sura yake imeonekana na jina lake kutajwa. Ingawa makala haya hayawezi kudhibitisha kwa asilimia mia moja kuwa jina linalotajwa katika video hiyo ni kweli ndilo jina la mtoto, kitendo kile ni mfano mzuri wa namna mtoto anavyokalitiwa kingono.

Inayumkinika ya kwamba yapo mapungufu katika malezi ya mtoto huyu anayeonekana katika video lakini suluhisho sio kusambaza video hii. Badala yake, watu wanaowafahamu wazazi wa binti huyu, wawape elimu ya malezi bora kwa mtoto wao na sio kumdhalilisha mtoto. Watumiaji wa mitandao wanaweza kusaidia kulinda watoto walioathirika na unyanyasaji wa kingono wa aina hii kwa kutoa taarifa za picha au video zenye maudhui haya katika tovuti hii: Tanzania - IWF - Karibu katika tovoti ya IWF ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Hili ni jambo la heri jamani tutumie muda wetu mtandaoni kuhakikisha watoto wetu, watoto wa majirani zetu na watoto wa taifa letu wanapata malezi na ulinzi makini kwa kuwa mabolozi matumizi mazuri ya mitandao.

Kwa ustawi wa watoto wetu tunatoa wito kwa jamii nzima ya watumiaji wa mitandao kuelewa kuwa hayupo mtu mmoja au taasisi moja au hata serikali inayopaswa kusukumiwa lawama zote za matukio ya unyanyasaji wa watoto mitandaoni. Jukumu ni langu. Jukumu ni lako. Kunyoosha kidole kwa wazazi wa mtoto unayesambaza picha yake hakukufanyi wewe kutohusika kama sehemu ya unyanyasaji.

Nini kifanyike basi? Hatua ya kwanza ni kutosambaza maudhui yeyote unayojua yana ukakasi wa kumnyanyasa mtoto husika. Hatua ya pili ni kutoa taarifa katika tovuti ya taifa ya kuzuia unyanyasaji watoto mtandaoni: Tanzania - IWF - Karibu katika tovoti ya IWF ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Namna hii picha ama video hiyo itaondolewa mtandaoni mara moja. Watoto hawa ni wetu sote. Tuwalinde.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook, Instagram na Jamiiforums: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
 
Back
Top Bottom