Kurudisha mamlaka kwa Umma ndio kanuni kuu ya utawala bora na wa kidemokrasia Zanzibar

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,880
2,000

Wasomi wa sheria na wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanakubaliana ya kwamba ‘nguvu ya umma’ ni mamlaka ya juu zaidi katika nchi. Kauli hii inaweza kuwashangaza wengi wanaoamini kwamba Katiba ndio mamlaka ya mwisho katika nchi. Bila shaka hilo ni sahihi pia, na yote haya husimama katika mukatadha tofauti. Kwa upande mmoja, dhana ya Katiba kuwa na mamlaka ya juu zaidi katika nchi ni mnasaba katika mazingira ya kidemokrasia ambapo kwa kiasi kikubwa utawala wa sheria unaheshimika. Hivyo, matakwa ya wananchi hupaswa kuzingatia na kufuata mtiririko mzima wa mfumo wa kisheria bila ya kujali matokeo ya mwisho ya madai yao.

Kwa upande mwengine, ni pale ambapo ‘nguvu ya Umma’ inapostahiki kutumika kukiuka mfumo wa kiutawala na sheria kandamizi ili kufikia maslahi mapana zaidi ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na kuleta mabadiliko ya haraka ya Serikali. Muktadha huu huweza kutokea ama kwa sbabu Katiba na sheria zilizopo zinakandamiza wananchi, au hutumika kulinda maslahi ya wachache wenye nguvu na madaraka dhidi ya raia. Au sheria hukanyagwa na watawala bila kujali katika kuhakikisha wanabaki madarakani kwa namna yoyote ile. Katika namna hii, ambapo watawala wameigeuza Katiba na sheria zake kuwa kitabu cha hadithi za ‘Alfu Lela Ulela’ kwa kuziheshimu wanapotaka, kuzivuruga wanapotaka, huku wakikandamiza haki za raia bila kujali, kutesa, kuua, na kuligawa taifa, basi ‘nguvu ya Umma’ inakuwa ni mamlaka ya juu zaidi katika nchi. Na ni nguvu ya Umma pekee huwa ndio suluhisho dhidi ya wapiganaji mamluki (jeshi, polisi, usalama wa taifa, na vikosi vya Serikali) ambao hutumika kutia hofu na kukandamiza raia.

Kimsingi, kurudisha mamlaka kwa Umma ndio kanuni kuu ya utawala bora na wa kidemokrasia na ndio chimbuko la Katiba yenyewe na sheria zake zote. Matumizi ya nguvu ya umma hata hivyo huweza kufanikiwa pale ambapo umoja wa kitaifa umeimarika dhidi ya ukabila, ukanda, ubaguzi wa kidini, na matabaka ya kijamii. Wazanzibari wanayo sifa hii ya umoja, hivyo wanao uwezo wa kutumia nguvu ya Umma kujinasua na utawala wa kidikteta. Nitafafanua kwa kina nukta nilizozitaja na nieleze kwa nini Wazanzibari wanaweza kujinasua na utawala wa mabavu wa SMZ.

Watawala wa Zanzibar Wanaitawala Sheria

Dhana ya utawala wa sheria inataka sheria itawale juu ya mamlaka zote na sio watawala kuitawala sheria. Mfano, Serikali kama muanzilishi wa mchakato wa utungwaji wa sheria husika, baada ya sheria hiyo kuanza kutumika, hata serikali yenyewe na viongozi wake wanapaswa kuwa chini ya muongozo wa sheria hiyo. Kwa maana hii sheria si nyenzo ya mtawala kuwatawala watawaliwa, bali sheria hupaswa kuwa juu ya wote wawili yaani mtawala na mtawaliwa. Ndipo waswahili wakasema ‘sheria ni msumeno’.

Kuna kila aina ya ushahidi kwamba Serikali ya Zanzibar na viongozi wake wamekuwa wakiikanyagakanyaga Katiba ya Zanzibar na sheria zake kadri wapendavyo kukidhi utashi wao wa kisiasa. Kwa hapa nitoe mifano michache ya matukio ya hivi karibuni tokea kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba mwaka 2015. Bila shaka tukio la kwanza lilikuwa ni ufutwaji wa matokeo ya uchaguzi kinyume na Katiba ya Zanzibar na sheria ya uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984. Mamluki mtiifu wa Serikali ya CCM, Jecha Salim Jecha, ambaye watawala wamempendekeza apewe tunzo kwa uharamia wake wa kupindua maamuzi halali ya umma wa Wazanzibari, alijipa mamlaka asiyokuwa nayo yeye binafsi wala tume kwa ujumla wake kufuta matokeo halali na yaliyokuwa yamekamilika ya uchaguzi wa Oktoba 2015. Vyombo vyote vya uangalizi wa uchaguzi, vya ndani na vya nje vikiwemo hata vile kutoka taasisi za Afrika, vilithibitisha kuwa zoezi zima la uchaguzi lilikuwa huru na haki. Cha kushangaza zaidi, tena bila hata aibu, serikali ya CCM ikaamua kunyofoa matokeo ya wabunge na rais wa Muungano kuwa ati yalikuwa yako sawa kutoka katika matokeo hayo hayo yaliyofutwa.

Kiufupi, kila kilichotokea baada ya hapo, kilikuwa ni kinyume na Katiba na sheria za Zanzibar, ikiwemo uchaguzi wa ‘kisanii’ wa marudio wa Machi mwaka 2016, pamoja na Serikali iliyotokana nayo. Pia, msingi mkuu wa utawala wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ulioanzishwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kupitia marekebisho ya Kumi ya mwaka 2010, ambayo yalipata ridhaa ya wananchi kupitia kura ya maoni, nao ulitupiliwa mbali. Watawala wakaamua kutawala bila kisisi wakidai kutumia Katiba hiyo hiyo, ni kama vile kusoma kitabu kilichogeuzwa maandishi yake juu chini huku unajidai umeelewa. Ni kejeli ilioje kwa utawala wa sheria? Ni dharau ilioje kwa Wazanzibari walio wengi? Hivyo, ni sawa kusema kwamba watawala wa Zanzibar wameitawala sheria, wameikanyaga kwa kisigino. Je haujafika wakati kusimamisha mamlaka ya umma kwa nguvu ya Umma?

Utawala wa mabavu, na vitisho

Wananchi walio wengi katika nchi zilizopitia tawala za kiimla kihistoria ni wenye hamu na ari ya mabadiliko ya mfumo wa utawala. Wazanzibari, hususan vijana na umri wa kati wanakataa kufungamana na siasa za kimirengo ya kihistoria na za kikabila zinazohubiriwa na chama tawala. Hata hivyo, bado raia wengi wa Zanzibar wapo katika hofu kubwa kutokana na ama uzoefu wao wa kihistoria tokea mfumo wa kimabavu wa chama kimoja na utawala wa vitisho wa kimapinduzi, au kutokana na matukio ya hivi karibuni ya uvunjwaji wa haki za binadamu ndani ya mfumo wa vyama vingi.

Tayari Wazanzibari wamechoshwa na vurugu, ubaguzi, ukandamizaji, na uonevu unaofanywa na Serikali ya SMZ kwa misingi ya itikadi za kisiasa na rangi zao. Pia wamechoshwa na juhudi kadhaa za utatuzi wa migogoro ya kisiasa zilizojulikana kama ‘Muafaka 1’, ‘Muafaka 2’, na ‘Maridhiano’. Juhudi zote hizi zimekuwa zikichukuliwa na serikali ya CCM kwa kebehi na kuvurugwa na kupuuzwa utekelezaji wake. Matokeo yake suluhu hizi zimegeuzwa kama zana za kutuliza hali ya kisiasa nchini ili watawala waendelee kubaki madarakani, na si vyenginevyo. Bila ya woga wala aibu tena katika mazingira rasmi ya kiserikali, viongozi wa SMZ wameendelea kusisitiza kwamba hawatotoa serikali kwa vipande vya karatasi, yaani njia ya chaguzi za kidemokrasia.

Isitoshe, kwa kuelewa kwamba wanayoyafanya ni kinyume na utawala wa sheria na demokrasia, watawala wa Zanzibar wamekuwa wanatumia vyombo vya ulinzi kuwapiga raia wasio na hatia, kuwanyang’anya mali zao, kuwatia hofu, na kuwanyanyasa ili kukandamiza upinzani dhidi ya Serikali. Ripoti za Haki za Binadamu kama vile ripoti ya shirika la haki za binadamu ‘Human Right Watch’ ya mwaka 2002 kuhusiana na Mauaji ya mwaka 2001 imeoredhesha vitendo vya KIGAIDI kabisa na visivyoelezeka kupatwa kutendwa na vikosi vya ulinzi nchini dhidi ya wakaazi wa Zanzibar hususan Pemba. Vitendo ambavyo haviwezi kusahaulika miongoni mwa waathirika. Mengine yakifanywa na vikundi visivyo rasmi maarufu kama Janjawidi kwa baraka ya chama tawala na serikali.

Hivi karibuni, pamoja na uvunjwaji mkubwa wa Katiba na sheria, serikali imeendeleza kutumia vitisho, na kupiga raia kwa kutumia kikundi cha maharamia kijulikanacho kama ‘Mazombi’. Kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa wa Haki za Binadamu pamoja na kuzorota sana hali ya uchumi kufikia hadi raia wamechoshwa na hali hii. Kimsingi, kiu ya mabadiliko ni kubwa miongoni mwa raia kutokana na kuchoshwa na uonevu. Hata hivyo, Wazanzibari wamekata tamaa na ufanisi wa njia za kidiplomasia za usuluhishi wa migogoro. La kushangaza zaidi, bado wanaendelea kuweka matumaini yao kwa viongozi wa kisiasa hususan wa chama cha upinzani kutumia busara kuweza kurudisha haki yao ya kidemokrasia. Njia ambayo imeonekana kushindwa kufanikiwa kwa muda mrefu sasa na nchi inaendelea kudidimia.

Ni maoni yangu kwamba Wazanzibari wanapaswa waache kuwatwisha jukumu viongozi wa kisiasa na kuwalazimisha watoe matamko ya lipi la kufanya. Wazanzibari wao wenyewe wanao uwezo, umoja, na mshikamano wa kutosha kuweza kuliondoa genge hili la wahuni na wahalifu linaloitawala Zanzibar na kuwanyanyasa raia. Kinachotakiwa ni kujitambua tu. Hata msaada wa kijeshi kutoka Bara ambao umekuwa ukitumika kutishia raia na kuliweka madarakani genge hili, hautaweza kuzima nguvu ya umma ya Wazanzibari wakiamua. Ni wajibu wetu katika jamii miongoni mwa wanaharakati na watetezi wa haki kuanzisha harakati hizi.

Mshikamano wa Kijamii ni msingi wa nguvu ya Umma.

Nilieleza hapo awali kwamba jamii iliyogawanyika kwa misingi ya ukabila, ukanda, na udini ina nafasi ndogo sana kujumuisha nguvu zake kujinasua na utawala wasiouridhia. Kwa mda mrefu sana Serikali ya CCM imekuwa ikijaribu kuwaaminisha watu kwamba Zanzibar kuna tatizo kubwa la ukabila, ukanda, na uvyama. Wakayahubiri haya sio tu katika majukwaa yao ya kisiasa, bali pia katika matendo ya serikali yao na sera zake za kibaguzi. Dhambi ile ile ya wakoloni kutumia rangi ya ngozi kuwabagua watu katika ajira imekuwa ndio falsafa yao kuu ya utawala. Wamekuwa wakitamani kuwagawa Wazanzibari kwa rangi zao, asili zao na maeneo wanayotoka kwa kutumia hivyo kama vigezo vya ajira serikalini. Hata hivyo, kwa mwenye kuifahamu jamii ya Zanzibar vizuri, anaelewa ya kwamba propaganda na sera hizi za kibaguzi hazijafanikiwa kujipenyeza katika maisha ya kijamii Zanzibar.

Kwa mfano, pamoja na kubaguliwa na serikali katika nyanja tofauti, jamii ya Wapemba na watu wenye asili ya Uarabu, hakuna chochote kinachoashiria kwamba jamii imegawika katika misingi hiyo. Wazanzibari ni wamoja na wenye upendo baina yao na muingiliano mkubwa wa kirangi, na kiasili. Ukiwaita machotara, basi Wazanzibari wote katika familia zao ni machotara. Hata hayo makabila maarufu yanayotajwa kuwa ndio ya kizanzibari kama vile ‘wahadimu’, ‘washirazi’, ‘waswahili’ yanapoteza maana kwao, kwa sababu wao hawapendi kujitambulisha na ukabila. Ukimuuliza mzanzibari kabila yake, usishangae akakujibu kuwa kabila yake ni ‘muislam’ au ni ‘mzanzibari’. Kwa sababu dhana ya ukabila haipo katika fikra zao, na makabila wanayonasibishwa nayo kwao wao ni kama misemo tu maarufu hayana maana kwao. Mtu huyo huyo mmoja anaweza kujiita Mhadimu, au Mshirazi, au Mtumbatu, au mswahili, au hata muarabu kwa mujibu wa muktadha aliopo na kutokana na muingiliano mkubwa wa kijamii. Mahusiano yao yameimarika zaidi kutokana na kutokuwepo na migogoro yanayotokana na tofauti ya dini baina yao, kwa vile asilimia zaidi ya 95 ni waislam. Kwa mwenye kubisha akumbuke Wazanzibari walivyoitikia wito wa jumuiya ya Uamsho kuhusu hatma ya nchi yao bila ya vikwazo vya ukabila, rangi zao, wanapotoka, wala mirengo yao ya kisiasa. Zanzibar ilivuma kwa sauti moja.

Pamoja na kufanywa ionekane kwamba Wazanzibari wameweka mbele itikadi za vyama na eti kuna mivutano mikubwa ya kisiasa baina ya wafuasi wa vyama, bado utaifa wao kama Wazanzibari wanauthamini mno. Kimsingi ukichambua itikadi zao za kisiasa utakuta hazishajiishwi katika misingi ya ukabila wala ukanda bali ni matokeo ya matendo ya serikali ya SMZ. Hata hivyo, bado serikali ya CCM inaendelea kupandikiza chuki za kisiasa na zenye madhumuni ya kuigawa jamii bila ya mafanikio. Wazanzibari hawajitambulishi kwa Upemba wao au Uunguja wao, bali wao ni Wazanzibari kwanza kabla ya chengine chochote, hata Utanzania ni kofia ya pili kwao. Na ndio maana serikali ya CCM imeendelea kupoteza imani miongoni mwa Wazanzibari kwa kasi ya kutisha licha ya kujaribu kuficha takwimu hizi kwa wizi wa kura, kuongeza wapiga kura hewa, kuwanyima wenye haki kupiga kura, na kujitangazia matokeo wanayotaka wao. CCM wanafahamu fika ya kwamba Serikali ikishikwa na upinzani na uchafu wote huu kusafishwa, ndipo itajulikana asilimia sahihi ya wafuasi wa chama chao, na bila shaka ni aibu kubwa kwao.

Hitimisho

Nimeeleza kwa ufupi namna gani katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja uliopita Wazanzibari wameshuhudia genge la watawala wa Zanzibar linavyokejeli na kukandamiza utawala wa sheria pamoja na uhuru wa watu. Mbali na uporaji wa wazi wa maamuzi ya kidemokrasia ya Wazanzibari walio wengi juu ya nani awatawale, serikali ya CCM ikaendelea kuwakandamiza raia kwa vitisho, vipigo, udhalilishaji, na kuzidi kudorora kwa hali ya uchumi bila ya kujali.

Ni wazi kwamba ipo sehemu kubwa ya jamii ya Wazanzibari ambao wamekuwa wahanga au waathirika wa vitendo vya serikali ya SMZ kwa kiasi kisichoelezeka. Tumefika kiasi kwamba, hata pakitokea mabadiliko ya utawala itatubidi tuanze na kupoza vidonda vya waathirika hawa kama vile ilivyofanyika Afrika Kusini kupitia mapendekezo ya Kamati ya Upatanishi (Truce Commission) iliongozwa na Askofu Desmond Tutu. Vyenginevyo, tutajenga taifa na jamii ambayo imejawa na visasi kutokana na vitendo vilivyofanywa na wenye madaraka Zanzibar. Jamii ambayo wengine wamepoteza wazee wao na hawakujua makaburi yao yalipo. Jamii ambayo watoto wake wameathirika kwa kupoteza muelekeo wa kimaisha kutokana na wazee wao kujeruhiwa, au kutoweza kuwahudumia kutokana na ulemavu waliopatiwa na serikali. Jamii ambayo watu wake wameshindwa kufikia malengo muhimu kama vile elimu na mahitaji yao kutokana na ubaguzi wa kisiasa, kikabila, na kikanda unaofanywa na serikali ya SMZ. Jamii ambayo sehemu kubwa ya jamii imeathirika kutokana na kutengwa katika utawala na uchumi wa nchi kiasi kuathirika kimaendeleo.

Hivyo, ni dhahiri kwamba Wazanzibari wanazo sababu nyingi za kulazimisha kufanya maamuzi kwa kutumia nguvu ya umma kuleta mabadiliko kutokana na kuchoshwa na utawala dhalimu. Na kutokana na uzoefu wa mda mrefu kuwa njia za utatuzi wa migogoro zimekuwa zikikejeliwa na hazileti mabadiliko yanayotarajiwa, kuna kila sababu ya kukata tamaa juu ya mabadiliko kwa njia ya mazungumzo. Ni wazi kuwa lolote litakalotokea kwa njia ya mazungumzo lazima liwe na maslahi kwa watawala, kinyume chake hawatakubali kuheshimu maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya mwezi Oktoba 2015 kama yalivyo.

Wazanzibari pia wanazo sifa za kijamii kuweza kuunganisha nguvu ya umma dhidi ya udikteta. Wanao umoja na mshikamano na mapenzi ya taifa lao. Mahusiano yao ya kijamii yamezishinda propaganda za kibaguzi zinazohubiriwa na serikali ya SMZ pamoja na sera zake za kiupendeleo. Wanajitambua kama jamii moja yenye mchanganyiko wa watu wa makabila tofauti na hilo sio tatizo kwao. Ni wajibu wao kutumia mshikamano huu kabla haujavurugwa na hila za watawala wanaozidi kupandikiza chuki na mipasuko kila kukicha.

By: Anonymous ~ Mzanzibari Fyoko
 

makilo

JF-Expert Member
Dec 15, 2015
1,541
2,000
Duh Mi nilidhani the bold kaleta story mpya kumbe kiongozi kaamua kutema mapovu.
 

jisanja

JF-Expert Member
Nov 17, 2013
1,074
2,000
huyu ana shida ila shida kubwa sana n huku bara....bara hawawezi kumkubalia ajiuzulu...nahis akijiuzulu wanaweza kummaliza.....ninachojua maamuzi mengi ya zenj yanafanywa na bara,,,,,,ukiendelea kusubiri huyu ajiuzulu bila ruksa ya magogoni utasubiri sanaaa
 

Vandetta

JF-Expert Member
Dec 5, 2013
667
500
Sefu alisema bado masaa tu apewe nchi yake!!!! Bado tunasubiri hatuchoki.
 

Sexless

JF-Expert Member
Mar 11, 2017
5,662
2,000
Mbinu mbadala inahitajika Zanzibar ili cuf iweze kutawala. Hii ya sanduku la kura naona isha gonga mwamba.
 

Pascal Mayalla

Platinum Member
Sep 22, 2008
36,310
2,000
MAKALA/TAHARIRI
Watawala wa Zanzibar Wanaitawala Sheria

Dhana ya utawala wa sheria inataka sheria itawale juu ya mamlaka zote na sio watawala kuitawala sheria. Mfano, Serikali kama muanzilishi wa mchakato wa utungwaji wa sheria husika, baada ya sheria hiyo kuanza kutumika, hata serikali yenyewe na viongozi wake wanapaswa kuwa chini ya muongozo wa sheria hiyo. Kwa maana hii sheria si nyenzo ya mtawala kuwatawala watawaliwa, bali sheria hupaswa kuwa juu ya wote wawili yaani mtawala na mtawaliwa. Ndipo waswahili wakasema ‘sheria ni msumeno’.

Kuna kila aina ya ushahidi kwamba Serikali ya Zanzibar na viongozi wake wamekuwa wakiikanyagakanyaga Katiba ya Zanzibar na sheria zake kadri wapendavyo kukidhi utashi wao wa kisiasa. Kwa hapa nitoe mifano michache ya matukio ya hivi karibuni tokea kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba mwaka 2015. Bila shaka tukio la kwanza lilikuwa ni ufutwaji wa matokeo ya uchaguzi kinyume na Katiba ya Zanzibar na sheria ya uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984. Mamluki mtiifu wa Serikali ya CCM, Jecha Salim Jecha, ambaye watawala wamempendekeza apewe tunzo kwa uharamia wake wa kupindua maamuzi halali ya umma wa Wazanzibari, alijipa mamlaka asiyokuwa nayo yeye binafsi wala tume kwa ujumla wake kufuta matokeo halali na yaliyokuwa yamekamilika ya uchaguzi wa Oktoba 2015. Vyombo vyote vya uangalizi wa uchaguzi, vya ndani na vya nje vikiwemo hata vile kutoka taasisi za Afrika, vilithibitisha kuwa zoezi zima la uchaguzi lilikuwa huru na haki. Cha kushangaza zaidi, tena bila hata aibu, serikali ya CCM ikaamua kunyofoa matokeo ya wabunge na rais wa Muungano kuwa ati yalikuwa yako sawa kutoka katika matokeo hayo hayo yaliyofutwa.

Kiufupi, kila kilichotokea baada ya hapo, kilikuwa ni kinyume na Katiba na sheria za Zanzibar, ikiwemo uchaguzi wa ‘kisanii’ wa marudio wa Machi mwaka 2016, pamoja na Serikali iliyotokana nayo. Pia, msingi mkuu wa utawala wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ulioanzishwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kupitia marekebisho ya Kumi ya mwaka 2010, ambayo yalipata ridhaa ya wananchi kupitia kura ya maoni, nao ulitupiliwa mbali. Watawala wakaamua kutawala bila kisisi wakidai kutumia Katiba hiyo hiyo, ni kama vile kusoma kitabu kilichogeuzwa maandishi yake juu chini huku unajidai umeelewa. Ni kejeli ilioje kwa utawala wa sheria? Ni dharau ilioje kwa Wazanzibari walio wengi? Hivyo, ni sawa kusema kwamba watawala wa Zanzibar wameitawala sheria, wameikanyaga kwa kisigino. Je haujafika wakati kusimamisha mamlaka ya umma kwa nguvu ya Umma?

By: Anonymous ~ Mzanzibari Fyoko
Mkuu Kakke, kwanza naunga mkono kuwa mamlaka kuu ni umma, umma huo ndio ndio umeiweka katiba, katiba ikaweka sheria, taratibu na kanuni za kushughulikia kila jambo.

Ili kuhalalisha kurejelewa kwa nguvu ya umma, ni pale tuu ambapo juhudi za matumishi ya katiba, sheria na taratibu, zimeshindikana!.

Kwenye issue nzima ya Zanzibar, samahani sana kuwaita Wazanzibari ni mazezeta tuu, kwa kushindwa kutumia sheria, taratibu na kanuni kumdhibiti Jecha!. Uchaguzi wote unaendeshwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni, alichofanya Jecha kweli kabisa ni kinyume cha sheria, taratibu na kanuni na ni haramu. Ila pia zipo sheria taratibu na kanuni za kuishughulikia haramu hiyo, kwa nini hamkuitumia kama sio uzezeta tuu?. Haramu ili iwe ni haramu lazima iharimishwe!, haramu isipoharimishwa hugeika halali, kwa hoja kuwa Wanzanzibari wote kwa umoja wetu, mliunga mkono haramu hiyo.

Uchaguzi wa marudio, ni uchaguzi uliotokana na haramu isiyoharimishwa, hivyo matokeo ni halali!

Mtake msitake, uchaguzi umekwisha, Dr. Shein ni rais halali, uchaguzi mwingine ni hadi 2020!, hakuja jingine lolote la kufanya labda mumlilie Mwenyezi Mungu kupitia itkafu, au albadir ili afanye yake, kama Waislamu wote dunioima waliwahi kumsomea Itqwaf Sulman Rashidie, wa zile Aya za Kishetani, lakini hakuna lolote lililomfika, itakuwa mazezeta fulsani wenye sheria wameshindwa kuzitumia, imebaki kazi kupiga tuu kelele?!.

Paskali.
Ukweli Mchungu Zanzibar: Hakuna Mgogoro Wowote wa Kisiasa, Shein ...
Uhalali wa Rais Dr. Shein Wa Zanzibar ni Kutokana na Uchaguzi ...

Zanzibar Issue: Kwanini watu wanapiga kelele tu bila kuchukua ...
Zanzibar: Japo SMZ ya SUK sio de jure tena bali ni de facto ...
Kuna haja ya kuhofia kurudiwa Uchaguzi Zanzibar? | JamiiForums ...
Imethibitishwa pasi na shaka kuwa ni kweli kabisa, Zanzibar ...
Uchaguzi wa Marejeo Zanzibar ni Huru na Haki! Tuyasubiri Matokeo ...
Wanaofikiria uchaguzi mwingine Zanzibar wanapoteza muda ...
Pemba Chini ya CCM kuneemeka au Kujutia Kuichagua CUF Chaguzi ...
Kumuepushia aibu ya Kushindwa, CCM isimsimamishe Dr. Shein ...
Balozi Karume: 'CCM pekee iwe inasimamisha mgombea urais Zanzibar ...
Dr. Shein Mfute Kazi Haraka, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Kabla ...
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom