Kurejea usafiri Reli ya Kati hivi karibuni ni habari njema | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kurejea usafiri Reli ya Kati hivi karibuni ni habari njema

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, May 25, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  May 25, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,616
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Maoni ya Katuni  Ni habari njema kufuatia taarifa kwamba huduma za usafiri kwa njia ya Reli ya kati kutoka Jijini Dar es Salaam kwenda mikoa ya Tabora, Kigoma na Mwanza zinatarajiwa kuanza tena wakati wowote kuanzia sasa.
  Usafiri huu utarejea baada ya wataalamu wa jeshi la Wananchi(JWTZ) na Wizara ya Miundombinu kukamilisha ukarabati wa sehemu ya reli iliyokuwa imeharibiwa na mafuriko yaliyoikumba wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro Desemba mwaka jana.
  Mafanikio haya yanatokana na agizo la rais Jakaya Kikwete kwa wizara hiyo kushirikiana na JWTZ kuhakikisha kuwa eneo hilo la reli linakarabatiwa kwa muda wa miezi mitatu.
  Ni mafuriko yaliyoleta athari kubwa ikiwa ni pamoja na kufanya mamia ya watu kukosa mahali pa kuishi na mali zao kuharibiwa.
  Katibu Mkuu wa wizara ya Miundombinu, Omar Chambo akizungumza juzi alisema kuwa jumla ya sh. bilioni 15.6 zimegharimu ukarabati huo. Na kwamba kama hatua za majaribio, tayari treni ya mizigo imeanza safari kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma ili kuimarisha eneo hilo lililokarabatiwa.
  Akaongeza hata hivyo kuwa bado zinahitajika sh.bilioni 20 kwa kazi kubwa iliyobaki ya kuimarisha reli hiyo kwa kujaza kokoto. Kujenga madaraja mapya katika baadhi ya maeneo na kuelekeza Mto Mkondoa ili upite katika njia yake ya zamani.
  Kwanza tuchukue fursa hii kuwapongeza wataalamu wa JWTZ pamoja na Wizara ya Miundombunu kwa kazi kubwa iliyofanyika hata kufikia hatua hiyo nzuri ya ukarabati wa eneo hilo la reli ili huduma irejee kama ilivyokuwa awali.
  Hakuna asiyefahamu umuhimu wa reli hiyo ya kati ambayo ni kiunganishi muhimu kwa wananchi wa ukanda wa kati na Ziwa kuanzia mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Kigoma, Shinyanga na Mwanza.
  Ni usafiri unaotumiwa hasa na wananchi wa kawaida kutokana na unafuu wake wa nauli ili kuwawezesha kwenda ama kwenye shughuli zao mikoani au vijijini kwao.
  Usafiri huu umekuwa wa nafuu na maarufu kutokana na ukweli kwamba kwa kutumia barabara nauli ni zaidi ya maradufu na siyo kila mtu anaweza kumudu gharama hizo.
  Pia, barabara zinazounganisha mikoa hiyo bado nyingi ziko katika hatua mbalimbali za matengenezo au ujenzi na hivyo kuwafanya wasafiri kupendelea zaidi usafiri wa reli ambao huuona salama zaidi hasa majira ya kiangazi ambapo hakuna mvua.
  Adha ya usafiri kupitia reli hujitokeza zaidi wakati wa mvua nyingi ambapo miundombinu huharibika. Na hasa hicho ndicho kilichotokea Kilosa na maeneo mengine korofi ambayo huleta maafa kutokana na kutokuwepo madaraja imara kwenye Mto Mkondoa.
  Bila shaka serikali sasa imeliona tatizo lilipo ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kufanya ukaguzi katika miundombinu iwe ya reli au barabara hasa kipindi kabla ya mvua kubwa kama zile za masika.
  Haipendezi tusubiri hadi maafa yatokee kama yale ya Kilosa ndipo tuzinduke na kuanza kukimbizana huku na kule kufanyia ukarabati maeneo yeye utata kama hayo ya Kilosa. Ni muhimu sana tukawa tunaziba nyufa badala ya kusubiri kujenga kuta ili kuepuka gharama kubwa ambazo zingeweza kuepukwa.
  Hata hivyo, inaleta faraja kutokana na kauli ya Bw. Chambo kwamba wizara inatarajia kuanza kufanya uchambuzi yakinifu na usanifu wa reli ya kati ili iweze kujenga reli ya kisasa zaidi kwa lengo la kuwaondolea kero wananchi wa kanda ya ziwa wanaotumia reli hiyo.
  Mpango huo ni mzuri na ni matarajio yetu kwamba maandalizi yatafanyika mapema ili mradi huo muhimu utekelezwe katika kipindi muafaka, hivyo kuwapa ahueni wananchi wanaotumia reli hiyo ya kati.
  CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
   
Loading...