Kupotea tulikopotea ni kupotea ‘kukubwa’ by Jenerali Ulimwengu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kupotea tulikopotea ni kupotea ‘kukubwa’ by Jenerali Ulimwengu

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by 654, Mar 4, 2012.

 1. 654

  654 Senior Member

  #1
  Mar 4, 2012
  Joined: Feb 1, 2012
  Messages: 173
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  KATIKA maandiko mengi ya magazeti, katika makala za redio na televisheni, katika matamko lukuki yanayotolewa katika mikutano ya hadhara na soga za vijiweni, kila mahali nimekuwa nikisikia ujumbe mmoja mkuu.

  Ujumbe huo ni kwamba tumepotea, nchi inayumba, imekosa mwelekeo, haina uongozi na inakabiliwa na hatari ya kukumbwa na zahama kubwa iwapo haitapata mtu au watu wa kuinusuru.

  Matamko haya yamekuwa yakiibuka mara kwa mara, na mara nyingine yanatolewa na watu ambao hawawezi kushutumiwa kwamba ni watu wasiopenda Serikali iliyomo madarakani, ama watu wanaotaka kuleta fujo, ama wenye ajenda ya siri na kadhalika, kadiri tunavyoendelea kuishi ndivyo watu wengi zaidi wanavyojitokeza kusema "twafa."

  Vielelezo vingi vinaweza kutuonyesha ni kwa nini watu wengi zaidi wanapiga kelele za aina hii, kwa nini asasi nyingi zaidi zinatanabahisha kuhusu mustakabali wa ovyo, kauli nyingi zaidi zinaashiria kudhoofu kwa hali ya nchi yetu kiasi kwamba baadhi ya matamko yanasema wazi wazi kwamba sasa labda ingefaa tuwe na utawala wa mkono wa chuma.

  Nimelisikia hili mara kwa mara katika maongezi ya makundi madogo madogo. Lakini pia, hivi karibuni, nimeyasikia haya yakisemwa hadharani, katika mahafali ya halaiki. Kasisi mmoja amekaririwa akisiema kwamba nchi hii inahitaji kuwa na mtawala "mkali' kama Paul Kagame wa Rwanda. Hii ina maana yake, na haiwezi kupuuzwa, kwa sababu najua kwamba wengi wetu wamesikia maneno kama haya mahali pengi.

  Dhana inayozungumzwa hapa ni ile inayoitwa kwa Kiingereza "benevolent dictator," yaani dikteta wa nia njema. Maana yake ni mtu ambaye hatajali sana utawala wa kidemokrasia, na wala hatasita kuwanyima watu uhuru wa kuwaza, kusema na kutenda, lakini atafanya hivyo kwa nia njema ya kuliendeleza taifa lake na kuwaletea manufaa watu wake.

  Inaelekea yule kasisi aliyetutaka tumtafute Kagame wetu alikuwa anafikiria dhana hii ya dikteta mwenye nia njema, na hivyo ndivyo ninavyowasikia wengi wakisema. Hii bila shaka inasababishwa na jinsi ambavyo Kagame alivyoiendesha nchi yake tangu mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

  Aliichukua nchi iliyokuwa imevunjika kabisa, imezama katika lindi la majonzi na ukiwa na uharibifu ambao haujashuhudiwa na dunia kwa miongo mingi, kisha akaiinua, kaisimamisha, akaiimarisha taratibu na kwa ustadi mkubwa na akaionyesha njia ya kupitia kuelekea kwenye maendeleo.

  Rwanda hivi sasa ni nchi ya kutolewa kama mfano katika nyanja mbalimbali. Ni nchi inayopiga hatua kubwa na za haraka kiasi kwamba nchi zilizoizunguka zinaonekana kama zilizodumaa au zinazorudi nyuma.

  Vigezo vingi vya kimataifa, pamoja na taarifa za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba nchi hii ndogo inakwenda mbele kwa kasi kubwa, pamoja na kwamba haina utajiri mkubwa na watu wake bado wanayo makovu ya kisaikolojia yanayotokana na maafa ya mwaka 1994.

  Ni kweli kwamba ingekuwa vigumu kwa Rwanda kupiga hatua ilizopiga kama ingejiruhusu kuingia katika ukinzani wa kisiasa na kuruhusu kila mtu ajifanyie anavyotaka. Kagame amekuwa mkali mno kuhusu uzembe, rushwa na ufisadi kiasi kwamba mara kadhaa ameshutumiwa kwamba anafinya haki za binadamu na kuviza utawala wa kidemokrasia. Anatekeleza kile kinachoitwa "guided democracy", kwa tafsiri nyepesi, "demokrasia elekezi."

  Hayuko peke yake. Meles Zenawi wa Ethiopia hupenda kueleza kwamba nchi yake inaendeshwa na kile kinachoitwa "developmental state," yaani "dola ya kimaendeleo" ambayo hata hivyo, sifa yake moja kubwa ni kwamba inabana uhuru wa raia kuamua masuala mengi. Wala Kagame na Zenawi si wa kwanza katika hili, kwani dola nyingi za Afrika mara tu baada ya Uhuru zilifuata mkondo huo, ikiwa ni pamoja na Tanzania chini ya Mwalimu Julius Nyerere na utawala wa chama kimoja.

  Kimsingi, falsafa ya utawala wa chama kimoja ilitokana na fikra kwamba katika nchi ya watu masikini, wajinga na wagonjwa ingekuwa kupoteza muda na kufuja rasilimali za nchi kama tungeruhusu malumbano ya kisiasa yasiyokoma, ambayo yangewagawa wananchi na kuwachelewesha katika jitihada za kujiletea maendeleo.

  Mtazamo ulikuwa ni kujenga nchi kwanza, kuwaondoa wananchi kutoka katika unyonge wa kiuchumi na kijamii, na labda baadaye, wakiwa wamejikomboa kiuchumi ndipo waonje anasa ya malumbano ya kisiasa.

  Mtazamo huo hauko mbali mno na jinsi wanavyoenenda watawala wa China, ambao wameshikilia utawala wa Chama cha Kikomunisti ambacho hakina mpinzani huku wakiisukuma nchi yao kimaendeleo kwa kasi ambayo haijawahi kuonekana duniani. Hivi leo, ingawaje China bado ni nchi inayoendelea lakini uchumi wake ni wa pili duniani kwa ukubwa na watu wake wana maisha bora ya kiuchumi. Haitachukua muda mrefu kabla haijawa nambari moja duniani.

  Niliwahi kuandika katika makala zangu za miaka ya 1990 kwamba falsafa inayomtaka mama kuku awaache vifaranga wake watembee wanavyotaka ili kuwapa nguvu na uzoefu wa kujitegemea ni falsafa inayohubiriwa na mwewe, mama kuku akiiafiki atakuwa ni kichaa au vifaranga alionao kawaazima, si wake. Zenawi, amekataa kabisa kabisa kuachia vifaranga wake watembee peke yao kwa kujua kwamba mwewe atakuwa anawasubiri.

  Ndiyo maana ameshikilia msimamo kama wa Nyerere, kwamba dola ya Ethiopia itasimamia masuala ya uchumi, na itaendesha mipango ya uchumi na mendeleo, itakuwa na benki zake, itakuwa na viwanda vyake, na kila mgeni anayetaka kuwekeza nchini humo atalazimika kuingia ubia na dola au na raia wa Ethiopia. Kwa jinsi hii, uchumi wa Ethiopia umo mikononi mwa Wahabeshi wenyewe, na unakwenda kwa kasi inayoonekana kwa macho, si kwa takwimu peke yake.

  Bila shaka hapa kuna nafasi ya mjadala muhimu. Je, ni sawa kubana uhuru wa raia kujiamulia mambo yao kwa kuwa dola inawaletea maendeleo? Je, kufanya hivyo si kujidanganya kwa kuwa maendeleo ya kweli ya watu ni yale wanayojiletea wenyewe, na si yale wanayobambikizwa na watawala wao? Je, maendeleo ya kubambikizwa na dola yanaweza kuwa endelevu?

  Maswali haya ni muhimu, kama vile ilivyo muhimu kujiuliza vile vile kuhusu huyo anayeitwa dikteta wa nia njema. Je, huyo dikteta wa nia njema anapatika vipi, ni wa kuchaguliwa au anajitokeza tu kutoka kambi ya jeshi na kukamata madaraka na kisha kuonyesha nia njema aliyo nayo kwa kutenda mambo mema?

  Anapokuwa amevurunda anaondolewa vipi madarakani, au akisha kuwa kakamata madaraka ndiyo haiwezekani tena kumuondoa? Je, madaraka yake yana kikomo au anajiamulia yeye mwenyewe kujiwekea mipaka yake?

  Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba madaraka aliyopewa na Katiba ya nchi yalikuwa yanamwezesha kuwa dikteta kama angependa. Na katika nyanja nyingi ni kweli kwamba alikuwa dikteta pale alipopenda, na akawa mwanademokrasia pale alipopenda.
  Hatimaye alijiondoa mwenyewe madarakani pale alipoamua kwamba utawala wake ulikuwa umedumu kwa muda mrefu mno na kwamba kulikuwa na haja ya kuweka kikomo cha urefu wa utawala wa mtu mmoja yeyote. Je, dikteta wa nia njema atakuwa na busara kama hizo, na kama hana wananchi watafanya nini?

  Nayaibua masuala haya kwa sababu nadhani sasa tumefikia wakati ambapo watu wengi wanatambua kwamba tumo ndani ya matataizo makubwa kiuongozi. Nami naafikiana na wale wanaosema kwamba nchi imekosa uongozi na viongozi; ina utawala na mifumo ya kiutawala bila kujua kwa uhakika inaelekea wapi. Watawala wenyewe hawaonyeshi dalili za kujua wanataka kuipeleka wapi, wanababaisha, wanabahatisha, wanatangatanga.

  Tulivyo, hatujui tunataka kujenga dola ya aina gani. Hata tunaposikiliza madai ya Katiba mpya, hatusikii mjadala kuhusu dola ya aina gani tunataka kujenga.

  Sana sana kuna vipengele kadhaa ambavyo vinalengwa na makundi ya kisiasa, na vipengele hivi vinalengwa kwa sababu wanasiasa "uchwara" wanaamini vitawanufaisha wao au vitawaumiza. Hawajadili wala hawaangalii misingi ya aina ya dola wanayotaka kuijenga na kwa sababu gani. Kupotea tulikopotea ni kupotea kukubwa.

  May The Good LORD lead us into finding the right path!!!
   
Loading...