Kupinga ''nguvu ya Umma'' ni kupinga demokrasia na kutukuza udikteta. | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kupinga ''nguvu ya Umma'' ni kupinga demokrasia na kutukuza udikteta.

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by FortJeasus, Sep 21, 2012.

 1. FortJeasus

  FortJeasus JF-Expert Member

  #1
  Sep 21, 2012
  Joined: Jan 19, 2012
  Messages: 568
  Likes Received: 61
  Trophy Points: 45

  Deusdedit Jovin, Raia Mwema Toleo namba 260,Tar 19 Sept.-25 Sept.

  TUHUMA tata zilizotolewa na kina Samuel Sitta dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na ambazo nimezijadili kwa kifupi katika toleo lililopita la gazeti hili, zimenihamasisha kutafakari kwa kina kuhusu changamoto za kiitikadi zinazotukabili katika safari ya kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa rais na wabunge ifikapo mwaka 2015.
  Baada ya kutafakari kwa kina nimejiridhisha kwamba kuna haja ya kufanya muhtasari, ufafanuzi na utetezi wa itikadi ya CHADEMA kwa kubainisha kila "hoja au wazo linalotolewa kimantiki"1 ili kusisitiza mafundisho yake ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na vinginevyo.
  Kila wazo au hoja ya aina hiyo nitakuwa nairejea kama "tasinifu ya kiitikadi" (ideological thesis) ya CHADEMA. Vyanzo vya "tasnifu za kiitikadi" (ideological theses) za CHADEMA ni Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2006, Ilani za Uchaguzi, nyaraka za kiutendaji za chama, na pia nyaraka za kielektroniki, kwa maana hotuba mbalimbali za viongozi wa chama.
  Na leo, ili kuonyesha ukweli kwamba kina Sitta wanaopinga "nguvu ya umma" wanapinga demokrasia na kukumbatia udikiteta, nimeamua kufanya muhtasari, ufafanuzi na utetezi wa "tasinifu ya kiitikadi" (ideological thesis) ya CHADEMA ifuatayo:
  "CHADEMA tunaamini na kutambua kuwa "kuchaguliwa" kuunda utawala wa kuongoza nchi hakumaanishi wachaguliwa kujitwalia mamalaka ya UMMA na kisha kuyatumia mamlaka hayo kuwakandamiza "waliowachagua" kwa sababu tu ya kutetea maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma.
  Hivyo basi, falsafa ya "Nguvu na Mamlaka ya Umma" ndiyo njia ya msingi ya kubadilisha fikra na uongozi unaokandamiza umma, ili kuibua fikra mpya na kuweka uongozi unaoweza kumilikiwa, kuhojiwa, na kuwajibishwa na umma kwa kutumia vyombo vilivyopatikana kwa utashi wa wengi kupitia chaguzi huru na za haki" (Katiba 2006, ibara ya 3.6 na 3.7).
  Katika nyaraka za CHADEMA "tasinifu ya kiitikadi" hii inarejewa kama "tasinifu ya nguvu ya umma" (people's power thesis) au "tasnifu ya kidemokrasia" (democratic thesis). Ni "tasinifu ya nguvu ya umma" inayoitofautisha CHADEMA na vyama vingine vya siasa vyenye harufu ya udikiteta. Aya zifuatazo zinakusudia kuweka bayana ukweli huu katika upeo usio na shaka.
  Demokrasia ni mfumo wa utawala unaozingatia "nguvu ya umma"
  Awali ya yote, napenda kuweka bayana kuwa, mafundisho ya CHADEMA kuhusiana na "tasinifu ya nguvu ya umma" hayana tofauti yoyote na mafundisho yanayotolewa na walimu wa sekondari na wakufunzi wa vyuo vyetu wanapokuwa wanafundisha madarasani. Kwa mfano, "tasinifu ya nguvu ya umma" imo katika kitabu kiitwacho "Mwongozo wa Somo la Uraia Kwa Ajili ya Walimu wa Sekondari na Wakufunzi wa Vyuo" kama kilivyochapishwa na Taasisi ya Elimu Tanzania mwaka 2002 kwa idhini ya Dk. Naomi B. Katunzi. Katika kitabu hiki, "tasinifu ya nguvu ya umma" imejadiliwa katika somo la 11 na 12 kuanzia ukurasa wa 45 hadi 51.
  Kwa namna fulani basi, Taasisi ya Elimu Tanzania, Walimu wa Sekondari na Wakufunzi wa Vyuo wanaofundisha somo la uraia, wanafanya kazi ya kueneza itikadi ya CHADEMA. Kwa maoni yangu, hii ndiyo sababu iliyoifanya CHADEMA kupata mteremko katika siasa zake za hivi karibuni.
  Mtazamo huu unaungwa mkono na sababu zifuatazo: CHADEMA, walimu wa sekondari, wakufunzi wa vyuo na wanafunzi wao wanakubaliana katika yafuatayo: kwamba, neno "demokrasia" linatokana na maneno mawili yaliyo katika lugha ya Kigriki; kwamba, na neno la kwanza ni, "demos" linalomaanisha "umma"; kwamba, neno la pili ni "kratos" linalomaanisha "nguvu" au "mamlaka"; na kwamba neno "demokrasia" linamaanisha mfumo wa utawala unaozingatia "nguvu ya umma." Katiba ya CHADEMA (2006) imeyataja wazi wazi maneno "nguvu na mamlaka ya umma (the people's power)" katika ibara ya 3.1.
  Katika ulimwengu wa leo, demokrasia inamaanisha maamuzi ya wengi kupitia wawakilishi wao waliowachagua moja kwa moja na kuwaingiza katika vikao vya maamuzi kama vile Bunge na Baraza la Madiwani. Lakini si hivyo tu. Pia, demokrasia inamaanisha maamuzi ya wengi kupitia wawakilishi wao waliowachagua kwa njia ya mzunguko na kuwaingiza katika vikao hivyo vya maamuzi. Mwakilishi aliyechaguliwa na wananchi kwa njia ya mzunguko ni yule ambaye ameteuliwa na mwakilishi aliyechaguliwa moja kwa moja na wananchi.
  Kwa mfano, Rais anachaguliwa moja kwa moja na wananchi; halafu anawateua mawaziri, majaji, na watumishi wengine wa umma. Kwa kuwa, Rais amechaguliwa moja kwa moja na wananchi, uteuzi wake unahesabiwa ni uchaguzi uliofanywa na wananchi kwa njia ya mzunguko kupitia mkono wa Rais.
  Mtu aliyechaguliwa moja kwa moja anaweza kuwajibika moja kwa moja kwa mtu aliyemchagua au akawajibika kwa njia ya mzunguko kwa mtu aliyemchagua kupitia kwa mwakilishi wa mtu aliyemchagua au vyote kwa pamoja.
  Kadhalika, mtu aliyeteuliwa anaweza kuwajibika moja kwa moja kwa mtu aliyemteua au akawajibika kwa njia ya mzunguko kwa mtu aliyemteua kupitia kwa mwakilishi wa mtu aliyemteua au vyote kwa pamoja. Picha yenye kichwa cha maneno "Uongozi wa Kidemokrasia kwa mujibu wa itikadi ya Nguvu ya Umma" inaonyesha mahusiano yanayopaswa kuwepo kati ya mchaguaji, mteuaji na mteuliwa.
  Katika mchoro huu, ambao unawakilisha mtazamo huu wa CHADEMA, Rais anawajibika kwa Bunge na Wapiga kura, kwa maana kwamba Bunge na Wapiga kura wanayo nguvu ya veto dhidi yake muda wowote kupitia kura ya maoni ili kumwondoa madarakani (power of recall through a referendum). Pia, utaona kwamba kwa kuzingatia mtazamo huu wa CHADEMA, madaraka ya Rais katika kuteua watumishi wa mahakama yamefyekwa.
  Sasa bunge ndilo lenye mamlaka hayo. Yaani, majaji wanawajibika kwenye bunge. Hii ndiyo njia pekee ya kuachana na urais wa kifalme.
  Hiki ndicho kinachomaanishwa na Katiba ya CHADEMA (2006) pale inapotamka maneno yafuatayo: "Hivyo basi, falsafa ya "Nguvu na Mamlaka ya Umma" ndiyo njia ya msingi ya kubadilisha fikra na uongozi unaokandamiza umma, ili kuibua fikra mpya na kuweka uongozi unaoweza kumilikiwa, kuhojiwa, na kuwajibishwa na umma kwa kutumia vyombo vilivyopatikana kwa utashi wa wengi kupitia chaguzi huru na za haki" (Katiba 2006, ibara ya 3.7).
  Mtazamo huu wa CHADEMA ni kinyume kabisa na mtazamo wa itikadi ya kidikiteta. Katika mfumo wa uongozi wa kidikiteta, kuchaguliwa kuunda utawala wa kuongoza nchi kunamaanisha wachaguliwa kujitwalia mamalaka ya UMMA na kisha kuyatumia mamlaka hayo kuwakandamiza waliowachagua kwa sababu tu ya kutetea maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma.
  Lakini, katiba ya CHADEMA inapinga vikali jambo hili kupitia misamiati ifuatayo: "CHADEMA tunaamini na kutambua kuwa "kuchaguliwa" kuunda utawala wa kuongoza nchi hakumaanishi wachaguliwa kujitwalia mamlaka ya UMMA na kisha kuyatumia mamlaka hayo kuwakandamiza "waliowachagua" kwa sababu tu ya kutetea maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma (Katiba 2006, ibara ya 3.6).
  Majumuisho na hitimisho
  Kwa ujumla, huwa kitaalamu tunasema kwamba "democracy is inversely proportional to dictatorship." Yaani, kadiri maamuzi na matendo ya kidemokrasia yanavyoshamiri maamuzi na matendo ya kidikiteta yanafifia.
  Na kinyume chake ni kweli. Yaani, kadiri maamuzi na matendo ya kidemokrasia yanavyofifa maamuzi na matendo ya kidikiteta yanashamiri. Matendo ya kidikiteta ni matendo ya kuwaburuza watu kana kwamba ni roboti bila kujali kwamba wanayo akili na utashi.
  Kwa mfano, wananchi wakiamua kupitia sanduku la kura kwamba huduma za elimu na afya zitolewe kama "faida ya wote" lakini vyombo vya dola vikachakachua matokeo ya kura na hatimaye kuhakikisha kwamba huduma za elimu na afya zinatolewa kama "faida ya wengi" inayobagua wachache, kama kina Sitta wanavyopendekeza, huo unakuwa ni udikiteta. Kwa hiyo, kupinga "nguvu na mamlaka ya umma" ni kupinga demokrasia na kutukuza udikiteta.


   
 2. masopakyindi

  masopakyindi JF-Expert Member

  #2
  Sep 21, 2012
  Joined: Jul 5, 2011
  Messages: 13,909
  Likes Received: 2,336
  Trophy Points: 280
  Mkuu acha ndoto za mchana, demokrasia viile vile maana yake ukomo wa uongozi.
  Uwe ndani ya chama au vinginevyo, fuatilia vuongozi wako na vipindi walivyokaa madarakani.
   
 3. t

  thatha JF-Expert Member

  #3
  Sep 21, 2012
  Joined: Apr 29, 2011
  Messages: 15,234
  Likes Received: 179
  Trophy Points: 160
  Demokrasia isipotumika vizuri(inapovuka mipaka) dawa yake ni UDIKTETA.
   
 4. t

  thatha JF-Expert Member

  #4
  Sep 21, 2012
  Joined: Apr 29, 2011
  Messages: 15,234
  Likes Received: 179
  Trophy Points: 160
  Safi sana, Hilo nilikuwa nimelisahau, na ndiyo maana wanasiasa wengi wanaowalaghai wananchi kuwa wanakuza demokrasia nchini utakuta wanachama wao wanaowaunga mkono ni wale wafuata mkumbo 2, nitolee mfano ndani ya CDM wanaunga mkono M4C ni watu ambao wako nchini ya miguu ya viongozi wakuu wa chama hicho, wale wanaamini kuna udikteta ndani ya CDM wako mbali sana na M4C, jambo ambalo hata ZITTO mwenyewe ameliongelea kwenye ukurasa wake wa TWITTER ambapo alisema watu wanafikiri CDM imekuwa maarufu 2011 nadhani waelewa watakuwa wamejua ZITTO alikuwa na maana gani
   
 5. FortJeasus

  FortJeasus JF-Expert Member

  #5
  Sep 21, 2012
  Joined: Jan 19, 2012
  Messages: 568
  Likes Received: 61
  Trophy Points: 45
  Hoja ya Ndugu Deusdedit ni kuwa kupinga nguvu na mamlaka ya umma ama demokrasia ni kukumbatia udikteta.
  Kwamba demokrasia ni mfumo bora zaidi wa utawala kuliko aina zingine.
  Na kwamba kwa asili mwanadamu angependa kushiriki na kushirikishwa katika kuamua na kupanga masuala yanayomuhusu.
  Ningependa tujikite katika mada iliyo mbele yetu badala ya kupotosha bandiko na kuingia kujadili watu.
   
Loading...