Kupiga marufuku masomo ya ziada (tuition) ni sahihi ili kuwapunguzia mzigo wanafunzi na wazazi

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,034
sfsafas.jpg
Masomo ya ziada ama tuition yamekuwa yakionekana kama kimbilio la wazazi na wanafunzi wengi, wakiamini kwamba njia hii inatoa fursa kubwa kwa mwanafunzi kufanya vizuri katika masomo yake na katika mitihani yake. Lakini kwa nchi nyingi za Afrika mara nyingi walimu wanaofundisha masomo ya ziada wanakuwa ni walewale wa shule, ambapo mkazo na juhudi kubwa huwa wanazielekeza kwenye masomo haya ya ziada kuliko ya darasani, wakifahamu kuwa huwa yanawaingizia pesa nyingi zaidi.

Nchini China hivi sasa serikali chini ya Baraza lake la Taifa tarehe 24 Julai iliamua kulikazia macho suala la masomo ya ziada, na kupitisha rungu lake kwenye sekta hii ambayo imestawi sana, kwa kutoa sera inayokataza masomo baada ya muda wa kawaida na siku za wikiendi.

Hatua hiyo inalenga kuwapunguzia shinikizo wanafunzi pamoja na kuwapunguzia mzigo wa fedha wa wazazi ili kuongeza kiwango cha uzazi ambacho kinaonekana kupungua siku hadi siku. Hivi karibuni tu China ilitoa sera inayoruhusu Wachina kuzaa watoto hadi watatu. Lakini inaonekana mwitikio wa wazazi umekuwa mdogo sana, wengi wakilalamikia gharama za maisha wakati wa kumlea au kumtunza mtoto, ikiwemo ada za shule na nyinginezo. Hivyo wengi wamejikuta wakisema kwamba “hapana hatuwezi kuongeza watoto hadi watatu”

Ikumbukwe kwamba hata China iliporuhusu watoto wawili, ni familia chache tu zilizoamua kuongeza mtoto, seuze kuongeza mtoto wa tatu. Kwa kuliangalia hilo serikali ya China sasa imeamua kuwapunguzia mzigo mkubwa walionao wazazi ikiwemo kuondoa masomo ya ziada ambayo yanaonekana kuwagharimu zaidi kuliko hata kitu kingine.

Mbali na hapo kanuni hii mpya inalenga kuondoa pengo la elimu yaani kutokuwepo kwa usawa kwenye elimu nchini, ambalo linazidishwa na mfumo wa "hukou" ambao unaweka ukomo wa wanafunzi kusoma katika shule nje ya sehemu ambayo kaya yake haijasajiliwa.

Kwa minajili hiyo, biashara zote za kujipatia faida za kutoa masomo nje ya shule, kwa masomo ya msingi kama vile hesabu, sayansi, na historia, ambapo masomo ya wikendi, mafunzo yanayotolewa wakati wa likizo, pamoja na masomo kwenye mtandao kwa watoto walio chini ya miaka sita pia yamepigwa marufuku. Na badala yake Baraza la Taifa la China limesema litaboresha elimu kwa njia ya mtandao, bila ya kuhitajika malipo. Nchini China kuna vituo maalumu vinavyotoa masomo ya aina hii, ambavyo vinaendeshwa chini ya kampuni za kujipatia faida.

Hata hivyo hili linaonekana ni pigo kubwa kwa wazazi na wanafunzi wanaopenda masomo ya ziada, ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Jumuiya ya Elimu ya China hadi kufikia mwaka 2016 takriban asilimia 75 ya watoto wa shule wanahudhuria madarasa baada ya masomo ya muda wa kawaida, na ushahidi wa kuaminika unaonyesha kuwa asilimia hiyo imeongezeka. Lakini pigo kubwa zaidi litakuwa kwa kampuni zinazoendesha biashara hii.

Kwa ufupi baada ya kutangazwa mabadiliko haya, imeripotiwa kuwa hisa nyingi zinazohusiana na biashara ya elimu nchini China zimeanguka kwa zaidi ya asilimia 50, ambapo matajiri na wamiliki wengi wa biashara hii sasa wapo hatarini kupoteza hadhi zao za kuitwa mabilionea.

Kwa upande wa nchi za Afrika pia suala la masomo ya ziada linachukuliwa kwa uzito mkubwa na wazazi na wanafunzi. Mathalan nchini Tanzania wazazi wengi wanaona ni njia nzuri ya kuwapatia mafunzo watoto wao lakini serikali haijaupatia baraka utaratibu huu kwani inaona kuruhusu masomo ya aina hii ni sawa na kwenda kinyume na sera ya serikali ya utoaji elimu bila malipo, hasa kwa shule zinazowalazimisha wazazi kuchangia fedha kwa ajili ya masomo haya.

Baadhi ya viongozi pia wamekuwa wakionesha hisia zao za kutokubali kupigwa marufuku kwa madarasa haya. Juni 21 mwaka huu, mbunge wa Bukoba Vijijini mkoani Kagera, Jason Rweikiza alivutana bungeni na waziri wa elimu, sayansi na teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, kuhusu zuio la michango ya wazazi, katika kugharamia masomo ya ziada (tuition)

Mivutano hii haipo bungeni tu, hata wazazi kwa wazazi pia hawakubaliani, kuna wale wanaoona ni utaratibu mzuri hasa kwa wenye uwezo, lakini kwa wazazi wasio na uwezo wanahisi kama watoto wao wananyimwa fursa ya kupata elimu sawa na wenzao. Kwani kama nilivyosema awali watu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba walimu wanafundisha vizuri zaidi wanapokuwa kwenye madarasa ya ziada kuliko wanapokuwa kwenye madarasa ya shule, ambako wameajiriwa na serikali.

Kwa serikali ambazo zinaweza kudhibiti mienendo kama hii ya kuwafanya baadhi ya wanafunzi wajihisi wanyonge kutokana na kutokuwa na uwezo wa kulipia ada za masomo ya ziada, ni vyema zikachukua hatua za kupiga marufuku, lakini iwe kama sera ya China inavyosema, kwamba katika kupiga marufuku ni lazima kuhakikisha mkazo unawekwa katika kuboresha elimu bila malipo. Hapo ndipo usawa wa kielimu utakapoonekana kwa wote.
 
Nchi nyingi zilishaanza kuchukua hatua baada ya huu mtindo mpya wa maisha unao ondoa haki za watoto katika ukuaji wao na haki zao za kujifunza na kucheza.

Mtu unakuta anapeleka mtoto wa miaka 3 shule, unajiuliza huyu ana akili kweli? Watoto lazima wapewe haki yao ya kufurahia utoto, kucheza, ku explore hii Dunia, sio mtoto anazaliwa tu akimaliza kunyonya anapelekwa shule.

Mbaya zaidi huyo mtoto akifikisha miaka 5 akitoka shule anapelekwa tuition, yaani mtoto wa chini ya miaka 10 anapelekwa tuition ili iweje?

Watoto hawana muda wakupumzika, hawana muda wa kucheza, hawana muda wa kulala, muda wao wa kulala ni kama wa watu wazima, mtoto wa miaka 5 anatoka nyumbani sa 12 asubuhi anarudi sa 12 jioni.

Nchi nyingi za Ulaya na Asia wanachukua hatua kali sana kufumua mifumo ya elimu ya sasa, kuwapa watoto muda mwingi wa kujifunza nje ya mfumo wa shule, kuwapunguzia masomo, kuwapunguzia ama kuondoa home works za masomo, nchi kama Finland, mtoto chini ya miaka 7 haendi shule, mtoto chini ya miaka 16 hafanyi mtihani. Hii ndio sasa imekua mfumo bora zaidi wa Elimu Duniani.
 
Back
Top Bottom