Kupaa kwa bei ya sukari DSM shida ni upungufu au panic purchase?

kindikwili

JF-Expert Member
Oct 5, 2016
1,862
2,871
Wakuu amani ya bwana iwe nanyi!

Toka juzi zimeanza tetesi kwamba bei ya sukari inapanda nasema ni tetesi kwasababu sikuwa na uhakika. Jana nikiwa ofisini nilimsikia bosi wangu akimpigia simu mwanaye akanunue sukari kilo 20, nikamuuliza mbona unanunua kilo nyingi hivyo (maana najua kwake hana familia kubwa), akanijibu sukari imeanza kuwa adimu na bei inapanda kwa kasi. Basi huyo mwanaye alipotoka huko akadai amenunua sukari kilo moja kwa tsh 3500. Leo mfanyakazi mwingine anasema kwao sukari kilo ni tsh 4000 na kwamba upatikanaji wake umeanza kuwa mgumu huko kwao.

Asubuhi hii nimemtuma mke wangu aulizie bei ya sukari huko mtaani kujua wapi bei ni ndogo ili akachukue walau kilo tano, bei ya chini kakuta ni shilingi 3500 na bei ya juu ni shilingi 4000. Kumbuka hatuishi eneo moja na bosi wangu au huyu mfanyakazi mwenzangu aliyesema kwao pia bei imekuwa kubwa. Kwahiyo JAPO SIWEZI KUJUMUISHA KWAMBA BEI YA SUKARI KWA NCHI NZIMA IMEPANDA AU KUNA UPUNGUFU WA SUKARI (Maana mimi si mamlaka) itoshe tu kusema kwamba bei kwa baadhi ya maeneo kwa hapa dsm imepanda sana ukilinganisha na bei ya sukari tarehe za mwanzo wa mwezi April ambayo sukari ya pakiti ilikuwa Tsh 2500 na ya kupima ilikuwa Tsh 2400 mtaani kwetu.

Inawezekana upandaji huu wa bei umesababishwa na moja ya mambo yafuatayo:

1. Ugonjwa wa corona uliosababisha ugumu wa biashara hasa kutoa mizigo nje- Lakini toka corona ianze sijasikia kama meli za mizigo zimezuiliwa duniani kote. Kama nchi zinazolima sukari kwa wingi kama Brazil na Pakistan wamezuia meli za mizigo kusafiri basi ndiyo chanza cha upandaji huu wa bei ila kama hawajakataza basi siyo sababu.

2. Sababu ya pili inaweza kuwa ukadiriaji mbaya wa mahitaji ya sukari (poor projection/forecasting of demand)-Kwamba huenda wenye mamlaka walikadiria vibaya uhitaji halisi ya sukari ukilinganisha na sukari unaozalishwa nchini ili upungufu uagizwe kutoka nje, matokeao yake sukari ikawa pungufu ya uhitaji.

3. Matumizi haramu ya fursa ya corona- Kwamba wafanyabishara wanafanya hujuma kwa wananchi na kutumia corona kama kisingizio cha ugumu wa kuagiza sukari ili wauze sukari waliokuwa nayo kabla ya corona kwa bei kubwa- Kama ni kweli mamlaka iwashughulikie hawa watu mara moja.

4. Ongezeko la matumizi ya sukari kutokana na wanafunzi na baadhi ya watu kuwa majumbani, kwamba badala ya matumizi madogo ya sukari ya awali mahitaji yameongezeka kutokana na uwepo wa wanywa chai wengi yaani wanafunzi na wafanyakazi wengine wanaofanyia kazi nyumbani

5. Manunuzi yanayotokana na hofu ya bei kuzidi kupanda (panic purchase)- Hii ni ile hali ya watu kudhani kwamba huenda bei ya vitu vikapanda hivyo wananunua mahitaji kwa wingi zaidi ya matumizi ya awali. Hali hii hutengeneza demand kubwa na ya ghafla ukilinganisha na supply ya wakati huo hali inayopelekea wauzaji kupandisha bei (theory of demand and supply) - Kama hali ni hiyo basi mamlaka husika lazima iwatoe wananchi wasiwasi kwamba sukari , unga ,mchele na matumizi mengine muhimu yapo nchini kwa kiwango cha kutosha ili wasije wakaanza kununua kila kitu kwa panic kuweka akiba ambayo ni hatari maana itapandisha bei ya kila kitu.

Nimejaribu kuweka nadharia kadhaa ya sababu ya kupanda kwa bei ya sukari ghafla kulikojitokeza ndani ya wiki hii huenda nisiwe sahihi ila ukweli ni kwamba bei ya sukari imeanza kupanda.

MAPENDEKEZO KWA MAMLAKA ZA SUKARI
1. Naomba wizara ya kilimo na mamlaka zake zifanye tathmini ya haraka ya uwepo wa sukari na mahitaji mengine ya haraka ili kuweza kufanya maamuzi sahihi na ya haraka tunapoelekea kwenye mfungo wa ramadhani na vita ya corona
2. Kama sukari ipo ya kutosha nchini mamlaka zitoe taarifa ya haraka kwa wananchi kuacha kupanic na kuanza kununua akiba na hii si kwa sukari tu bali kwa mahitaji yote muhimu wasije wakaingiza taifa kwenye inflation kwa uoga tu usio wa kweli

3. Kama kweli kuna upungufu wa sukari mamlaka ZISITANGAZE KWA UMMA (Si kwamba nataka wafiche taarifa ila kutangaza kutakuwa na madhara mara dufu)BADALA YAKE ZICHUKUE HATUA YA HARAKA KUNUSURU HALI INAYOWEZA KUWA MBAYA ZAIDI

4. Wananchi wapewe elimu juu ya madhara ya kutumia sukari nyingi na ikiwezekana washauriwe kutumia asali inapowezekana

5. Kama chanzo ni uzembe wa watu basi hatua za kinidhamu zichukuliwe juu yao bila kusita

HATUA YA MUDA MREFU NA YA KUDUMU

Mheshimiwa Rais wa JMT Ndg. JPM kuna vijana wengi mno nchi hii wamepata mafunzo JKT kwa kujitolea, kwa mujibu wa sheria na wengine wamemaliza vyuo na hawana ajira wakati huo huo hii nchi yetu ina mabonde ya kutosha kuweza kulima miwa inayoweza kutengeneza sukari kama malighafi ya sukari.

Naomba uchukue hatua mahususi kuwaagiza wizara ya kilimo, wizara ya viwanda na wizara ya kazi, ajira na vijana watafute mabonde ya kutosha kisha wanunue matrector ya kutosha halafu wajenge kambi hata kama ni za mahema kama za wakimbizi halafu wawatangazie vijana wanaotaka kwa hiari yao waende wakalime miwa kwa kilimo cha kisasa huku wakiishi kwenye makambi hayo, (hii ni baada ya corona lakini).

Hapa tutakuwa tumeua ndege wawili kwa jiwe moja yaani tutakuwa tumepunguza tatizo la ajira kwa vijana , pili upungufu wa sukari utakuwa historia. Tukifanikiwa kwenye miwa then strategy hii inahamia kwenye Alizeti na michikichi kwa ajili ya mafuta ya kupikia na mazao mengine. Ni aibu hii nchi kuagiza mahitaji ya mazao nje ya nchi miaka 59 ya uhuru huku tukiwa na ardhi nzuri, maji ya kutosha na vijana wenye nguvu tena wasio na ajira.

Wakuu nimesema na narudia tena sijasema sukari hamna au kuna upungufu wa sukari nchini (hii ni kazi ya mamlaka) , mimi nimesema bei ya sukari kwa DSM imepanda kwa mujibu wa mtaa wangu na mitaa mingine niliyopata taarifa zake. Pili naomba kama una la kuchangia uchangie kistaarabu kama wewe ni MATAGA au sijui UFIPA usije na siasa hapa huna facts kajadili mengine.

Kindikwili
 
Ipo hivi viwanda vya sukar havifanyi kazi mwaka mzima huwa kunakuwa na kitu kinaitwa msimu sasa kwa mfano inaweza kutokea kiwanda kikawa kinakwenda kufunga msimu lakin huwa wanaacha stop mzigo wa kutosha.

Kwa uhaba huu huenda ikawa wakati wanafunga msimu kwenye magodaoni hawakuacha sukar ya kutosha wakati huo huo kumbuka uvunaji wa miwa kwenda kiwandani ulikumbwa na changamoto ya maji hivyo uvunaji ukawa mgumu sababu ya mafuriko na mamvua ya muda mrefu.

Kumbuka uvunaji wa muwa huanza kwa kuchoma moto asante
 
Mzururaji,
Kama hiyo ndiyo case basi mamlaka na wizara zingechukua hatua kuagiza sukari kuja kusupplement huo upungufu.

Hilo unalolisema liko miaka yote na si kila mwaka bei huwa zinapanda unajua ni kwanini ni kwasababu hata wakati viwanda vyote vinafanyakazi bado uzalishaji huwa hautoshi na sukari unatolewa nje kwa kibali sasa katika case kama hii wangeruhusu selected business people kuingiza sukari kuja kumaliza tatizo hilo.
 
kindikwili,
Wenyeviwanda watuambie ukweli hizi mvua wanaweza kuvuna miwa? Miwa inahitaji jua kukomaa na kutoa sukari hivyo huenda uzalishaji umepungua hivyo mahitaji kuwa makubwa kuliko bidhaa iliyoko sokoni.

Na wiki iliyopita nilisoma mahali kuwa serikali imeagiza tani kadhaa nje ya nchi hivyo hii hali haina uhusiano na CORONA. Kama ni CORONA Mchele na Maharage yangepaa kuliko sukari
 
Kwanza nani kakwambia sifanyi kazi, pili najua wewe hujasoma nimeandika nini badala yake umesoma title tu ukakimbilia kujibu. Nachukia watu wajinga ila nachukia wasomi wajinga wasiotaka kusoma na kutafakari kabla ya kujibu zaidi.
Acha kuumiza kichwa na hao watu wanao kaa kwa mashemeji zao ambao hawaaminiki hata dukani huwa hawatumwi!
 
Ile kukataza kuingiza sukari toka nje pia imechangia sana.

Mkuu wamekataza lini kuingiza sukari? mimi ninavyojua sukari huingizwa kwa kibali maalumu nafikiri watoaji kibali ni Sugar Board pale wanapoona kuna gap kati ya internal production and demand ili kucover hiyo gap.
 
kindikwili,
Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro akishirikiana na OCD wilaya ya hai mkoani Kilimanjaro, wameunda mtandao wa kusimamia sukari kutorosha kutoka Kenya kupitia mpaka wa holili Tanzania. Matajiri wa Kenya wanaleta sukari kwa malori upande wa holili Kenya, inavushwa kupitia njia za pori na kuingia himo tayari kusagirishwa kuelekea mji wa Moshi na Arusha kwa kusindikizwa na jeshi la polisi kilimanjaro.

Kazi ya OCD wilaya ya hai ni kuhakikisha kuwa barrier iliyowekwa eneo la kwa Kia inakuwa wazi wakati magari yakipitisha sukari kuelekea arusha.mtandao huu umeendelea kuwa mkubwa kiasi kwamba unashirikisha wakenya wengi kuingia nchini kuleta sukari Jambo ambalo linasababisha kuenea kwa ugonjwa wa corona kwa kasi.

uchunguzi tulioufanya tumegundua kuwa mama ntilie waliokuwa wakifanya biashara ya chakula holili baada ya Kenya kufunga mpaka,wamekosa wateja hivyo kuanza biashara ya kuuza sukari ya magendo na kuzisafirisha kuingia Moshi na Arusha.

Biashara hii kwa Sasa wagonjwa wanatoroka Kenya na kuingia Tanzania kupitia uuzaji wa sukari ya magendo.serikali isipochukua hatua za haraka za kuwaondoa au kuwahamisha RPC Kilimanjaro, mkuu wa kituo cha polisi himo na OCD wilaya ya Hai.

Kuna janga la corona litawamaliza Watanzania ikiwa ni pamoja na serikali kukosa Kodi kupitia biashara haramu ya sukari.sasa wagonjwa wa corona wameanza kuokotwa barabarani wakitokea Kenya eneo la himo wakiwa wanakuja na sukari kutoka Kenya ili wauze wapate nauli kukimbilia tanzania.

IGP Tanzania, tupia macho Kuna janga kubwa linakuja la kuchanganya biashara ya sukari na ugonjwa wa corona.Tumetafuta njia za kumpata mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa mkoa wa kilimanjaro ili kumjulisha kwa njia ya simu hatukufanikiwa.

Tunaomba suala hili lichukuliwe hatua za haraka kulinusuru Taifa letu na serikali yetu kwani viongozi wache wenye ulagi wa fedha wataliangamiza Taifa.
 
joshua_ok,
Dogo kuwa na heshima kwa kaka zako na jukwaa hili basi, kwa taarifa yako wafanya maamuzi wengi wa nchi hii kila siku wanapitia hapa JF na wanasoma maoni ya wadau.

Pili kuna vyombo vya serikali wanapitia JF kila mara na kuangalia habari zenye maslahi chanya na hasi kwa taifa hili, hivyo hapa hatupigi kelele bali tunaongea na watawala na wafanya maamuzi.
 
6 Reactions
Reply
Back
Top Bottom