Kuongoza watu si kazi nyepesi

Aman Ng'oma

JF-Expert Member
Nov 8, 2011
961
533
Unaweza ukatamani uongozi lakini ukifikiria ugumu wa kuongoza watu, ile tamaa yote uliyokuwa nayo inaweza ikakuishia mara moja. Taharuki zimekuwa nyingi. Ni kama gari linapoendeshwa, dereva mara kwa mara anapangua gia moja baada ya nyingine na gari inakwenda. Haipiti muda bila kuibuka kwa mjadala mzito na wa moto. Unapoisha mjadala mmoja au kupoa kidogo, mjadala mwingine unaibuka. Unapokuwa kiongozi unapaswa kuwa na kifua kipana kwelikweli kustahimili mikiki ya mijadali inayoibuliwa, vinginevyo unaweza kujikuta ukijilaumu mwenyewe kwanini ulikuwa kiongozi. Na kama utakuwa na roho nyepesi unaweza kujifungia ndani ofisini ukilia peke yako. Huo ndiyo uongozi, mazuri yako hayaonekani isipokuwa mabaya.

Inavyoonekana, ni kama tumezoea kuishi kwa mijadala, akili nyingi inatumika kufikiri namna ya kuzima mijadala badala ya kufikiri namna bora ya kuwaletea wananchi maendeleo. Wakati mwingine ukiwa mtu wa kutoa maamuzi ya haraka unaweza kukosea. Unaweza kutoa maamuzi kwa msukumo wa watu badala ya uhalisia. Siku zote watu wanaibua mambo wakati mwingine kwa lengo la kubadili upepo fulani unaokuwa umevuma na kutamalaki katika jamii kwa lengo la kuwahamisha watu kifikra na kimtazamo, lakini wakati mwingine watu wanataka kupima uwezo wa viongozi wao kwenye kuamua na kuchukua hatua sahihi na kwa wakati. Watu wanataka kuona maamuzi ya haki yakitendeka na kwamba kunakuwa na hukumu inayofanana kwa watu wawili tofauti, wenye nafasi tofauti lakini wenye kosa au tuhuma moja, rejea sakata la vyeti feki kwa watumishi wa uma.

Mijadala mipana kwenye nchi za kidemokrasia inatoa ufumbuzi wa matatizo mengi. Lakini muhimu inapunguza mihemuko ya watu kwa kuruhusu kutoa madukuduku yaliyo mioyoni mwao.

Hivi karibuni tulikuwa na mjadala mzito wa madawa ya kulevya, sasa hivi mjadala huo kama umegeuka, nguvu yake imepungua kidogo, watu wamemgeukia kiranja mkuu mwanzilishi aliyekuwa akiiongoza vita hivyo na kumuhusisha sijui na mambo gani tena. Watu wote sasa hivi wanamjadili yeye. Mjadala ulianza kidogo kidogo lakini sasa hivi umepamba moto hasa. Kimsingi mjadala ulikuwa ni mdogo sana. Kilichotakiwa mtuhumiwa mwenyewe kuwahi haraka kuuzima mjadala huo kwa kutoa vielelezo husika.

Nakumbuka kuna mawaziri wawili nao waliwahi kutuhumiwa hivyo hivyo, lakini hawakutaka uzushi ule uonekane kuwa ni kweli, mara moja waliweza kutolea ufafanuzi na mjadala ukafungwa. Walielewa kunyamaza ilihali umetuhumuwa ni sawa na kuwaaminisha watu kuwa kisemwacho ni kweli. Lakini vile vile kunatoa mwanya kwa watu kuweza kukuchimba zaidi.

Kaka vita uliyoamua kuipigana ni vita kubwa na ngumu. Na ulipaswa kutambua kuwa uliwagusa watu wengi sana, hivyo lazima maadui zako wakutafutie sehemu ya udhaifu wako, yaani ile point of weakness na kimsingi kabla ya kuanza vita hivi ulipaswa kulijua hili mapema na kuweza kuja na mbinu na mikakati ambayo ingekurahisishia katika ushindi wa vita hivi. Kwa mfano laita uwanja wa vita ungeliusomwa mapema, ungelisaidia kujua nani atangulizwe mstari wa mbele na silaha gani itumike.

Nadhani hata hivyo, bado hujachelewa, ibuka hewani brother, ibuka ili uondoe shaka za watu. Watu hawapendi kuona kitu kingine bali usafi wako tu. kunyamaza haisaidii kabisa katika hili sakata na hasa hapa tulipofikia. Mtu pekee wa kumaliza vita hivi unavyopigwa ni wewe mwenyewe kuja na ithibati. Tuhuma si lazima ziwe kweli. Ndiyo maana ni muhimu kuzitolea ufafanuzi mapema.

Aman Ng'oma
Dodoma
0767989713
 
Back
Top Bottom