Kuondoka kwa mattaka ni afadhali ya atcl?? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kuondoka kwa mattaka ni afadhali ya atcl??

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Pdidy, May 25, 2011.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  May 25, 2011
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,441
  Likes Received: 5,693
  Trophy Points: 280
  0diggsdigg

  [​IMG]VYOMBO vingi vya habari leo vimechapisha habari ya kustaafu kwa David Mattaka, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania(ATCL). Kiongozi huyo wa shirika hilo, aliitisha mkutano wa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam na kusema kuwa ameachia uongozi wa shirika hilo kutokana na kufika umri wa kustaafu, tofauti na kauli za baadhi ya watu wanaodai kuwa hakustaafu, bali amejiuzulu.

  Tunampa pole mkurugenzi huyo kutokana na adha aliyoipata mara baada ya kustaafu, kwa kulazimika kuitisha mkutano wa wanahabari kwa lengo la kukanusha uvumi ulioenezwa na watu ambao huenda hawamtakii mema wanaosema kwamba hakuacha kazi hiyo kwa hiari, bali ameshinikizwa kujiuzulu. Tunadhani kuwa adha aliyopata kiongozi huyo ni kubwa pengine kutokana na ukweli kuwa ameliacha shirika la ATCL likiwa limekufa likisubiri kuzikwa rasmi na Serikali wakati wowote.

  Tunasema tunampa pole kwa sababu kitendo cha kuitisha mkutano wa waandishi wa habari kutangaza kustaafu siyo kitendo cha kawaida, kwani wajibu wa kutangaza kustaafu kwa mfanyakazi ni wa mwajiri, siyo mwajiriwa. Hatari inayoweza kutokana na hatua hiyo, ni kutokea kwa tafsiri nyingi, ikiwa ni pamoja na kwamba mamlaka iliyomteua imemfukuza kazi au kumuamrisha ajiuzulu.

  Ni bahati mbaya kuwa mkurugenzi huyo ameliacha shirika hilo katika hali hiyo ya kusikitisha. Pia ni bahati mbaya kuwa anaacha kuliongoza shirika hilo katika mazingira ya aina hiyo, ambayo yanaweza kutafsiriwa na wengi kuwa ni ya aibu. Tunasema hivyo kwa sababu maelezo aliyoyatoa katika mkutano wake na waandishi wa habari hayaonyeshi kutoka katika kinywa cha mtumishi aliyestaafu akiwa na mafanikio ya kujivunia, bali mstaafu mwenye hasira, lawama, majuto na visingizio lukuki visivyo na msingi wala mashiko.

  Tukiangalia hali lililomo shirika hilo la ATCL hivi sasa, tunashindwa kumwelewa mkurugenzi huyo mstaafu alipowaambia wanahabari kuwa, katika utendaji wake katika shirika hilo, anajivunia kubadilisha nembo ya shirika hilo na kuliondoa shirika hilo chini ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini lililokuwa limeingia ubia. Anasema anamshukuru Mwenyezi Mungu kustaafu salama pasipo matatizo yoyote katika shirika hilo, ingawa anasikitika kuliacha shirika hilo likiwa halina ndege hata moja.

  Nini lengo la kauli hiyo kama siyo kuamsha na kuchochea hasira za Watanzania? Hivi kweli kubadilisha nembo na kuliondoa shirika katika ubia pekee kunaweza kutafsiriwa kama jambo la kujivunia? Hata kama nembo ingebaki ileile na ATCL ingebaki katika ubia na shirika hilo la ndege la Afrika Kusini, lakini shirika hilo likatoa huduma kwa ufanisi, Watanzania wangeridhika na hali hiyo. Hata hivyo, tukumbuke kuwa alipokabidhiwa uongozi wa shirika hilo zaidi ya miaka minne iliyopita, shirika hilo lilikuwa na matatizo kadhaa, lakini hayakuwa sugu kiasi cha kushindikana iwapo uongozi ungekuwa na dira, weledi na mipango endelevu.

  Kichekesho ni pale mkurugenzi huyo anapodai kuwa uongozi wake ulikuwa na nia ya kulifufua shirika hilo tangu alipoteuliwa na Rais Kikwete mwaka 2007, lakini ulishindwa kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake. Kwa mfano, anadai kuwa, kati ya mwaka 2007/2008, mafuta ya ndege yalipanda kwa asilimia 50, hivyo kuyafanya mashirika yote ya ndege yaliyokuwa hayapati ruzuku kutoka serikalini, kuanguka. Lakini hasemi kwanini mashirika ya ndege, likiwamo la Precisionair la Tanzania, hayakuanguka na sana sana yaliendelea kukua na kushamiri.

  Sisi tunadhani kuwa kuondoka kwa mkurugenzi huyo katika shirika hilo, siyo tu ni faraja kwa Watanzania wote, bali pia ni habari njema katika muktadha wa ufanisi katika shirika hilo wakati Serikali ikitafakali namna ya kulijenga upya kutokana na majivu ya shirika hilo marehemu. Ni imani yetu kuwa Serikali imepata fundisho tosha na mara hii itaunda shirika jipya na kuweka uongozi wenye dira, weledi na uadilifu.
   
Loading...