Kuondoka kwa Kampuni ya Richmond/Dowans sasa kwabakia kitendawili | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kuondoka kwa Kampuni ya Richmond/Dowans sasa kwabakia kitendawili

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Aug 31, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Aug 31, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,886
  Likes Received: 83,368
  Trophy Points: 280
  Date::8/30/2008
  Kuondoka kwa Kampuni ya Richmond/Dowans sasa kwabakia kitendawili
  Na Kizitto Noya
  Mwananchi

  SIKU tatu baada ya serikali kuelezea utekelezaji wa mapendekezo ya bunge kuhusu mkataba wa Richmond Development Company, utata umegubika hatma ya mitambo ya kampuni iliyorithi mkataba huo, Dowans baada ya serikali na Tanesco kushindwa kusema lini itaondolewa nchini.

  Mitambo ya Dowans bado iko kwenye viwanja vya Tanesco, Ubungo jijini Dar es Salaam lakini hata baada ya mkataba baina ya mashirika hayo kusitishwa, Tanesco haijui Dowans wataondoka lini.

  Mmoja wa maafisa wa Dowans aliiambia Mwananchi Jumapili kuwa kampuni hiyo haina mpango wa kuondoa mitambo yake nchini kwa kuwa haijaambiwa na Tanesco kufanya hivyo isipokuwa iliambiwa tu kuacha kuiuzia umeme.

  "Suala hapa ni kuacha kuiuzia umeme Tanesco na siyo kuondoa mitambo wala kuzalisha umeme. Kukoma kwa mkataba wa Dowans na Tanesco hakufukuzi mitambo wala kuzuia kuzalisha umeme nchini," alisema.

  Alisema Dowans imetii sheria ya kutoiuzia umeme Tanesco lakini mitambo yake bado iko nchini na itaendelea kuwapo mpaka Tanesco yenyewe ieleze ina mpango gani na mitambo hiyo.

  Afisa Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud alisema hajui suala lolote linaloendelea kuhusu mitambo hiyo na maelezo ya kutosha yanaweza kupatikana ama kwa Dowans wenyewe au kwa Waziri wa Nishati na Madini.

  Aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa, "Mimi ninachojua Tanesco tumesitisha malipo kwa Dowans, haya masuala mengine yanayohusu mitambo ya Dowans wanajua wenyewe au Waziri, sio Tanesco," alisema Badra.

  Msemaji wa Dowans hakupatikana kuzungumzia suala hilo kutokana na kushindwa kutoa ushirikiano kwa waandishi tofauti wa Mwananchi Jumapili waliofika ofisini kwao kupata maelezo kuhusiana na suala hilo.

  Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja jana alishindwa kuzungumzia suala hilo akisema hajui na wanaoweza kutoa maelezo yanayoridhisha kuhusu mitambo ya Dowans ni Tanesco wenyewe.

  "Mimi sijui chochote kuhusu mitambo ya Dowans, kwa nini usiwaulize Tanesco wenyewe?" alihoji Ngeleja.

  Hata hivyo, baada ya gazeti hili kumweleza Ngeleja kuwa Tanesco walimtaka yeye kama msemaji wa serikali kuhusu suala la Dowans kuzungumzia suala hilo, alitaka apewe muda wa kuwasiliana nao ili apate majibu.

  "Sasa kama ni hivi naomba nipe muda niwasiliane na Tanesco halafu nitakupa jibu," alisema Ngeleja ambaye alipopigiwa baadaye alitaka aendelee kupata muda zaidi.

  Kampuni ya Richmond iliingia mkataba wa kuzalisha umeme wa megawat 100 na kuiuzia Tanesco, lakini ilibainika baadaye kuwa mkataba huo haukuwa halali na hivyo kusitishwa Agosti Mosi mwaka huu.

  Malipo kwa Dowans yalisitishwa kama sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya bunge baada ya uchunguzi wa kamati yake chini ya Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe kubaini kuwa mkataba wa Richmond na Tanesco, uliingiwa kifisadi.


  Kulingana na mkataba huo ambao hata hivyo umekwishavunjwa, Tanesco ilikuwa na jukumu la kulipia gharama za usafirishaji wa mitambo ya Dowans kutoka Ubungo kwenda mahali popote ambapo mwekezaji angetaka kuipeleka.


  Mbali na kusitisha mkataba huo, bunge pia liliitaka serikali kuwawajibisha maafisa wake waandamizi wanaodaiwa kuhusika katika mkataba huo na Msajili wa Makampuni (BRELA) aifute Richmond kwenye orodha yake.

  Pia Bunge liliitaka serikali kuwafungulia kesi ya jinai wamiliki wa Richmond, kuchunguza ripoti ya Takukuru kuhusu kampuni hiyo, kuitafuta taarifa halisi ya Takukuru kuhusu Richmond, kuepuka matumizi ya mawakala katika manunuzi ya umma na Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA) kupewa meno na kufanya kazi kwa kujitegemea.

  Mapendekezo mengine ya bunge kuhusu Richmond ni kupitia upya mikataba yote na kuanzisha maktaba ya kumbukumbu za mikataba katika Ofisi ya Bunge, serikali kuiwajibisha timu yake inayoshauri Mikataba (GNT) na kuwawajibisha waaliokuwa Mawaziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi.

  Utekelezaji wa Mapendekezo hayo yalisomwa bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Agosti 28 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine alisema serikali imeanza kuwachunguza mawaziri wa zamani wa wizara ya Nishati na Madini, Dk Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, kutokana na tuhuma za rushwa katika mkataba huo

  Mbali ya uchunguzi huo, Waziri Pinda alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hosea na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Athur Mwakapugi, wametakiwa kujieleza kutokana na kushindwa kuwajibika katika mchakato huo hadi kulitia taifa hasara.

  Kwa mujibu wa Pinda uchunguzi dhidi ya mawaziri hao wa zamani ambao kwa nyakati tofauti waliongoza Wizara ya Nishati na Madini, unalenga kuona kama walihusika na rushwa wakati wa utoaji zabuni.

  Waziri Mkuu alifafanua kwamba, katika azimio namba 8 na 14, licha ya mawaziri hao kujiuzulu, serikali imeamua kujiridhisha ndiyo maana imeagiza vyombo vya dola vifanye uchunguzi wa kina kuona kama walihusika na jinai ya rushwa kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa dhidi yao.

  Pinda alifafanua kwamba, tayari serikali imeanza utekelezaji wa azimio namba 14 ambalo pia linamtaja Katibu Mkuu Mwakapugi, Mrindoko na namba tano linalomtaja Mwanasheria Mkuu kwamba wameandikiwa barua za kutakiwa kujieleza kwa Rais Jakaya Kikwete, kwa ajili ya kumchukulia hatua kwa kuwa ndiye mamlaka ya kikatiba kufanya hivyo.

  Alifafanua kwamba, Hosea na Mwakapugi wametakiwa kujieleza kwa Katibu Mkuu Kiongozi (Philemon Luhanjo) ambaye atatoa maelekezo kwa serikali namna ya kutekeleza zaidi maazimio hayo.

  Aliongeza kwamba, Takukuru inatakiwa kueleza kwanini ilishindwa kubainisha kasoro kama ilivyofanya Kamati ya Bunge katika mkataba wa Richmond na pia vipi haikubaini kupuuzwa ushauri wa Mamlaka ya Zabuni (PPRA).

  Kuhusu azimio namba 10 ambalo linahusu malipo ya dola za Marekani 4.8 milioni kwa Dowans, alisema uchunguzi wa kina BoT ulibaini kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni halali kwani kililipwa kwa ajili ya kuingiza mitambo kwa ndege.

  Waziri Mkuu aliongeza kwamba, baada ya serikali kufanyia kazi mapendekezo hayo ya Bunge imebaini kulikuwa na mapungufu ya usimamizi na uwajibikaji wakati wa mchakato wa mkataba huo hadi ulipotiwa saini Juni 23 mwaka 2006.

  Pinda alifafanua kwamba, RDC haikusajiliwa Brela na kuongeza kwamba, hadi sasa haijathibitika uhusiano kama Richmond hiyo ya nje ilikabidhi majukumu yake kwa Richmond ya nchini.

  Hata hivyo, alisema maelekezo ya serikali ni kwamba Brela ifute Richmond Tanzania (LTD), na kufafanua kwamba tayari kampuni hiyo ilipewa barua ili ijitete lakini hadi sasa haijafanya hivyo.

  Kuhusu kama RDC ilighushi nyaraka na kupata zabuni hiyo, alisema jinai huchunguzwa na polisi na kwamba tayari jeshi hilo linachunguza kuona kama wamiliki walifanya kosa hilo la jinai kupata zabuni.

  Sakata la Richmond lilitikisa nchi kuanzia Juni mwaka 2006, miezi michache baada ya serikali ya awamu ya nne kuingia madarakani na nchi kukabiliwa na ukame na uhaba wa nishati, hivyo kulazimu serikali kutafuta mitambo ya dharura ya kukodi kwa ajili ya kufua umeme.

  Mpango huo uliingiza serikali ya awamu hiyo ya nne katika kashfa nzito ambayo ilifanya Bunge kuunda Tume yake chini ya Mbunge wa Kyela Dk Harrison Mwakyembe, ambayo katika mkutano wa 10 wa Bunge la Februari ilitoa matokeo yake ambayo yalisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, Dk Msabaha na Karamagi, kujiuzulu.
   
Loading...