Waufukweni
JF-Expert Member
- May 16, 2024
- 4,912
- 16,522
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, ametoa maelekezo kwa Mtendaji Mkuu wa DAWASA kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jimbo la Segerea inapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu. Akijibu swali la Mbunge wa Segerea (CHAUMMA), Agnesta Kaiza, bungeni Juni 3, 2026, Mhandisi Kundo alisema wananchi wa Segerea hawahitaji ratiba zisizotabirika za maji bali wanahitaji kuona kuwa Serikali yao inawajali kwa kuwapatia huduma ya uhakika.
Amesema si jambo la kawaida kwa wananchi kuendelea kukabiliwa na changamoto za maji huku mbunge wao akilazimika kuendelea kuibua malalamiko hayo mara kwa mara. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, amesisitiza kuwa baada ya maelekezo hayo kutolewa, Serikali inatarajia kuona matokeo ya haraka yatakayoboresha hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya Segerea.
Mhandisi Kundo alimtaka Mkurugenzi wa DAWASA kulifanyia kazi suala hilo kwa ukaribu mkubwa ili kuepusha changamoto hiyo kuwa ya kudumu. Akikumbusha kuwa tayari Waziri Mkuu ameshatoa maelekezo kwamba viongozi wasizowee changamoto za wananchi, bali wachukue hatua na kuhakikisha matokeo yanaonekana. Aidha, alisema endapo kutakuwa na mgao wa maji, wananchi wanapaswa kupewa taarifa maalum mapema ili waweze kupanga matumizi yao kwa ufanisi.