TAFAKURI JADIDI
Kama vile tumelogwa au kulaaniwa
Johnson Mbwambo
MSHINDI wa Tuzo ya Nobel katika tiba, James Watson, mwishoni mwa mwaka jana alirushiwa makombora ya shutuma kutoka sehemu mbalimbali duniani alipotamka kwamba mtu mweusi ana akili kidogo kuliko mtu mweupe. Wako waliomwita mbaguzi mkubwa wa rangi na wengine hata kufikia hatua ya kumtukana kwa kumwita nguruwe mweupe.
Baada ya gazeti hili kuianika hadharani, hapa nchini, kauli yake hiyo tata aliyoitoa Marekani, baadhi ya waandishi wachambuzi wa hapa nchini nao walijitosa kuchangia mjadala huo wa Watson; lakini zaidi kwa kuyaweka katika darubini matendo yetu wenyewe sisi watu weusi. Nilisisimshwa na mchango wa Ayub Rioba na wa Padri Privatus Karugendo kuhusu mjadala huo.
Bado nakumbuka moja ya aya za Padri Karugendo katika makala yake inayotuhimiza tukae chini (sisi watu weusi) na kujiuliza kunani katika akili zetu? Padri Karugendo aliandika hivi: Tunavuna madini ya Tanzanite lakini hatuwezi kuyauza mpaka aje Mzungu. Tunasema tuna mafuta lakini tukitaka kuyachimba tunamwita Mzungu, japokuwa tumekuwa tukizalisha wahandisi na wanajiolojia kila mwaka.
Nilikwepa, wakati huo, kuingia katika mjadala wa kauli hiyo ya Watson; ingawa moyoni nilikuwa naungana na wale waliomwona Watson kuwa ni nguruwe mweupe tu anayewachukia Waafrika (weusi).
Lakini miezi mitatu tangu Watson aitoe kauli hiyo, nimekuwa nikitafakari suala hilo kichwani mwangu kwa kuangalia mienendo ya viongozi wetu (weusi) hapa Tanzania na kwingineko Afrika ; na ninavyozidi kulitafakari suala hilo ndivyo ninavyozidi kukubaliana na kauli ya Padri Karugendo kwamba ni lazima weusi tukae chini tujiulize kunani katika akili zetu?
Miezi kadhaa iliyopita, CHADEMA ilitangaza hadharani orodha ya viongozi mafisadi na pia kuibua skandali ya ufisadi ndani ya BoT; hususan ujenzi wa maghorofa yake pacha. Cha kushangaza viongozi wa juu, akiwemo Rais wa nchi, walipuuza madai hayo na kuwakejeli watoa hoja hizo huku wengine wakitishia kwenda mahakamani. Sote bado tunakumbuka kauli ya Rais kuhusu waliokuwa wanalalamikia ufisadi kwamba kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala.!
Lakini sote pia tunajua kilichotokea majuzi kwenye skandali moja tu (kati ya nyingi zilizopo) ya Richmond; kwani kelele za mlango zilipozidi, mwenye nyumba hakupata usingizi na mwisho wake ni kuachia ngazi kwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wawili Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha. Hatimaye kelele za mlango zikasababisha mwenye nyumba kuwatosa viongozi hao watatu na kuunda upya baraza la mawaziri.
Ukweli ni kwamba Lowassa, Karamagi na Msabaha wote walikuwepo katika orodha ile ya ufisadi ya CHADEMA. Na hao wameibuliwa na ripoti moja tu ya Kamati ya Bunge ya Richmond. Nina hakina tungekuwa na kamati nyingine za Bunge kuchunguza mikataba ya Kiwira, IPTL, Buzwagi, Net Group Solutions na mikataba mingine mingi tu ya serikali, na kamati hizo zikaundwa na wapenda nchi wa sampuli ya Dk. Mwakyembe, ni robo tu ya mawaziri wa sasa wangepona!
Kwa sababu, kama alivyosema mchambuzi Lula Mwananzela katika safu yake kwenye gazeti hili, wiki iliyopita, mawaziri wa baraza la sasa na lililopita wanatoka CCM. Na ukishakuwa na chama kichafu na kilichooza kimaadili, bila shaka mawaziri kutoka chama hicho watakuwa hivyo hivyo. Mwimbaji Tina Turner anaimba What you see is what you get.
Ukiwa na chama kichafu utapata serikali chafu. Huo ndiyo ukweli. CCM na serikali yake ni wachafu kweli kweli. Na ndiyo maana baada ya Lowassa na baadhi ya wanamtandao wenzake kusambaratishwa, kilichobakia sasa ni majungu na kupakana matope ndani ya chama hicho na ndani ya serikali yenyewe; huku waandishi wa habari wachache ambao ni mamuluki wakifaidi vilivyo kuchukua pesa huku na kule kuwachafua hata wale wanaoonekana mbele ya umma kuwa ni waadilifu; japo kidogo.
Hivi sasa tayari tumeshaanza kusikia minongono ya kinachoitwa Agenda 21; mtandao ambao inadaiwa umeundwa kwa ajili ya kumsafisha Lowassa ili eti aonekane ni mtu msafi na kwamba kujiuzulu kwake kwa sababu ya kashfa ya Richmond ni kuwajibika tu kisiasa. Kwamba eti hahusiki hata kidogo na skandali hiyo, eti pamoja na ukweli kwamba yeye alikuwa PM, lakini hawajui na hakuwajua wamiliki halisi wa Richmond, wala wa Dowans na wala maswahiba wao! Na sisi kama Watanzania tunatakiwa tuamini hivyo pasi shaka yoyote!
Kwa mambo yanavyokwenda, haitashangaza tukianza kusoma habari za kumchafua Dk. Mwakyembe na hata Rais Kikwete au mawaziri kuchafuana wenyewe kwa wenyewe. Vyovyote vile; hayo yatakuwa yanathibitisha tu uozo uliopo ndani ya CCM na serikali yake.
Sitaki kuijadili CCM kwa undani (ilikotoka na inakokwenda) kwa sababu naamini Jenerali Ulimwengu amefanya hivyo kwa mapana na marefu katika safu yake kwenye gazeti hili, na bado anaendelea na mjadala huo. Lakini kila ninapokifikiria chama hiki CCM huwa nashindwa kuelewa ni vipi chama kilichosheheni maprofesa na madaktari serikali yake itumbukie katika ufisadi wa kiwango hicho tulichokiona katika Richmond na katika akaunti ya EPA ndani ya BoT; huku wananchi wakiogelea katika lindi la umasikini.
Maprofesa na madaktari hao wanafanya nini ndani ya chama na ndani ya serikali ya sampuli hiyo? Kwa nini hawaitumii elimu yao kuleta mageuzi chanya yanayosubiriwa kwa hamu ndani ya chama hicho na ndani ya serikali? Hivi kweli walikwenda shule ili kuitumia elimu yao kuwakamua damu Watanzania masikini hadi tone la mwisho?
Najua ukiwauliza baadhi yao watakwambia kuwa CCM haiambiliki na kwamba hawana ushawishi mkubwa ndani ya serikali kuchochea mageuzi hayo, lakini kama ndivyo; mbona hatujasikia hata mmoja tu akijingatua kutoka chamani au serikalini kwa sababu ya kutokukubaliana na namna mambo yanavyoendeshwa?
Kwa nini wasomi hao wa kiwango cha hali ya juu wakubali kuwa party wa utawala unaowatumbukiza wananchi katika umasikini zaidi (bei ya juu ya kutisha ya umeme ni mfano mmoja tu)? Kama wasomi wetu waliopelekwa shule kwa pesa za masikini wanakubali kuwa party ya serikali ya namna hiyo, basi, nakubaliana na Padri Karugendo kwamba sisi weusi tunapaswa kukaa chini na kujiuliza; kunani katika bongo zetu?
Najua kuna tamaa na ushawishi kwa wasomi hawa ya kupata mapesa mengi hadi kuwa mabilionea na kuishi maisha ya raha. Lakini ni nani hapa duniani ataishi milele kwa kuwa na mapesa mengi; achilia mbali kuwa huwa wanayapata kwa kuparamia migongo ya Watanzania wenzetu ambao ni masikini wa kutupwa? Wako wapi kina Sani Abacha, kina Mobutu na kina Haile Selassie? Kama mapesa mengi yangekuwa yanahakikisha maisha ya milele, leo hii si bado tungekuwa nao duniani kina John D. Rockfeller na Aristotelis Onasis?
Kwa hakika, nikiiangalia CCM na idadi ya maprofesa na madaktari iliyonayo na skandali zinazoiandama serikali yake; nakikumbuka chama tawala cha Zimbabwe cha ZANU-PF. Nilipotembelea Zimbabwe kwa mara ya mwisho mwaka 2002, NEC ya ZANU-PF ilikuwa na maprofesa na madaktari 16. Leo hii, Zimbabwe ndiyo inayoongoza duniani kwa mfumuko mkubwa wa bei.
Inflation rate ya Zimbabwe sasa imefikia asilimia 100,000 . Gharama ya mkate mmoja katika jiji la Harare ni sawa na dola 78 (Sh.92,000)! Na bado maprofesa na madaktari hao wamo ndani ya ZANU-PF! Na bado baadhi ya Wazimbabwe, pamoja na mateso yao yote, wanaona hakuna chama kama ZANU-PF. Wanamwona Robert Mugabe kama vile ni kiongozi aliyeshushwa na Mungu! Na katika uchaguzi mkuu wa mwezi ujao, watamchagua kwa kishindo kiongozi huyo anayewalaza njaa! Kwa hili na mengine mengi; kwa nini nisimwamini Watson kwamba bongo za sisi weusi zina walakini?
Lakini ukishangaa ya Tanzania (CCM) na ya Zimbabwe (ZANUPF); hebu angalia ya Afrika Kusini (ANC); taifa ambalo ndilo kubwa kiuchumi katika Afrika. Si siri kwamba toka makaburu waikabidhi serikali kwa weusi (ANC) mwaka 1994, uchumi wa nchi hiyo umekuwa ukisuasua tofauti na ulivyokuwa zama za makaburu; achilia mbali ukweli kwamba zama hizo weupe ndiyo walionufaika zaidi na kukua kwa uchumi kuliko weusi.
Katika kudhihirisha kwamba mambo si shwari katika serikali ya chama tawala cha ANC, nchi hiyo, kwa mara ya kwanza sasa inakabiliwa na mgao mkubwa wa umeme. Na hapa tunazungumzia taifa tunaloamini kwamba ni super power katika Afrika.
Lakini miongoni mwa kinachoufanya uchumi wa nchi hiyo usuesue, ni viongozi weusi kuegemea zaidi katika shughuli za kutafuta mali kuliko katika kuwatumikia wananchi na kuiendeleza nchi yao kiuchumi. Viongozi hao weusi wamekuwa na tamaa za kupita kiasi za kuwa mabilionea; bila kujali hali ya umasikini wa wanaowaongoza. Matokeo ya uchu huo wa pesa wa kupita kiasi wa viongozi weusi, ni skandali moja baada ya nyingine inayowahusisha viongozi wake zikiwemo zile za kusaka ten percent katika mikataba.
Lakini makaburu waliona dalili ya hilo hata kabla ya kukabidhi utawala kwa walio wengi (weusi); na ndiyo maana mwaka 1999 wakaamua kuunda kikosi maalumu kuwachunguza na kuwafikisha mahakamani viongozi wanaojihusisha na ufisadi.
Kikosi hicho kinachoitwa The Scorpions na ambacho kauli-mbiu yake ni Justice in Action (Haki Inapofanya Kazi) katika muda mfupi tu wa uhai wake kiliwezesha kutiwa mbaroni kwa watuhumiwa 2,000 wa rushwa wakiwemo vigogo kadhaa. Miongoni mwa vigogo waliofikishwa mahakamani na kuhukumiwa vifungo ni mfanyabiashara maarufu, Schabir Shaik na aliyekuwa Mkuu wa Nidhamu wa ANC ndani ya Bunge, Tony Yengeni.
Mpaka hapo, kazi ya The Scorpions haikutiliwa shaka au kunyooshewa kidole. Mambo yalianza kubadilika pale tu The Scorpions kilipoanza kumchunguza Rais mpya wa ANC, Jacob Zuma na kuamua afikishwe mahakamani baada ya kubainika kwamba ana kesi ya kujibu ya rushwa. Hapo, The Scorpions kikaonekana kibaya mbele ya ANC. Yakaibuka madai mapya kwamba kinaendeshwa kikaburu (ingawa maofisa wake wengi ni weusi) na Rais Thabo Mbeki akashinikizwa akivunje. Hatimaye Rais Mbeki akasalimu amri, na majuzi ikatangazwa bungeni kuwa The Scorpions kinavunjwa na shughuli zake zitahamia Jeshi la Polisi.
Hatua hiyo ya kukivunja The Scopions baada ya kuwa kimepata mafanikio makubwa ya kuigwa kwingineko Afrika (ikiwemo Tanzania) kuliwashangaza wengi ndani na nje ya Afrika Kusini.
Wengi bado wanajiuliza: Katika nchi ambayo ni miongoni mwa zinazoongoza duniani kwa uhalifu wa kutumia silaha na rushwa kubwa kubwa, unaivunjaje asasi muhimu katika vita dhidi ya rushwa yenye mafanikio kiasi hicho, kwa sababu tu ya kumwokoa kiongozi mmoja (Zuma)? Inawezekana ni kweli wanachama wa ANC wanampenda Zuma, lakini si wanapaswa kuipenda Afrika Kusini zaidi ya wanavyompenda Zuma?
Ukilitafakari kwa undani suala la kuvunjwa kwa kikosi hicho, hapo ndipo unapoweza kutilia shaka ukamilifu wa bongo za sisi watu weusi. Ni kama vile tumerogwa au kulaaniwa. Unapata hisia hizo ukiitazama Tanzania (CCM), ukiitazama Zimbabwe (ZANU-PF), na ukiangalia kinachotokea Afrika Kusini (ANC) hivi sasa.
Tafakari!