Kuna tofauti gani kati ya motivational speakers wa nje na wa Tanzania ambao ni 'waganga njaa'"?

kirerenya

JF-Expert Member
Aug 27, 2013
1,696
2,252
Kuna mtu ameniuliza swali lenye utata nikaona ni vyema kuandika makala hii ili kutoa ufafanuzi yakinifu. Ameniuliza "kuna tofauti gani kati ya motivational speakers wa Ulaya na Marekani kama Donald Trump na Ben Carson au Benjamin Carson ambao ni matajiri na motivational speakers wa Tanzania ambao ni 'waganga njaa'"?.

Maoni yangu binafsi ni kama ifuatavyo: Swali limeulizwa katika whatsapp group ijulikanayo kama 'Mentoring and Networking' na ni swali zuri sana lililokuja kwa wakati muafaka. Lakini kwa faida ya wengi nimeona ni vyema kuliandikia makala. Kwanza kabisa ni vizuri kufahamu kuwa 'motivational speaking' ni tawi la 'public speaking'.

Public Speaking au 'kuzungumza katika hadhara au katika halaiki' ilianza zamani sana baada ya binadamu kuanza kuishi pamoja katika miji. Historia inaonesha kwamba Public Speaking ilianza takribani miaka 2,500 iliyopita katika miji ya kwanza kukua ikiwa ni pamoja na Greece au Ugiriki na Rome au Roma kule nchini Italia.

Wanafalsafa wa kwanza kuelezea kuhusu Public Speaking walikuwa ni pamoja na Aristotle (384-322 BCE), Cicero (106-43 BCE) na Quintilian (c. 35-95 CE) kutoka nchini Ugiriki. Enzi hizo Public Speaking ilitumika sana katika siasa ili kutoa ushawishi wa watu hasa miji mikubwa ilipoanza kujitokeza ikiwa ni pamoja na Mesapotamia. Mesapotamia ni neno la kigiriki linalomaanisha 'kati ya mito miwili' na leo hii inaitwa nchi ya IRAQ na baadhi ya maeneo machache ya Syria na Uturuki.

Kama nilivyoeleza katika maneno yangu ya utangulizi, Motivational Speaking ni tawi mojawapo la Public Speaking. Siku zijazo nitaeleza matawi mengine ya Public Speaking, lakini kwa lengo la kujibu swali la mwanachama wa Mentorship and Networking, Motivational Speaking ni aina ya uzungumzaji unaohamsha hisia inayopelekea vitendo au kitendo fulani kufanyika.

Motivational Speaking haijaanza leo. Imeanza kipindi cha kukua kwa miji na kipindi cha kukua kwa Public Speaking ingawa haikutofautishwa sana na Public Speaking. Hivyo yoyote aliyefanya Motivational Speaking alihesabika anafanya Public Speaking. Na hata wao wazungumzaji hawakujijua kama ni Motivational Speakers.

Kwa mfano watu kama Julius Ceacer (Mfalme wa dola ya Rome), George Washington (Rais wa kwanza wa Marekani), John F. Kennedy, Julius K. Nyerere, Winston Churchil, Adolf Hitler, Dr. Martin Luther King Jr, Malcom X nk wanaelezwa kuwa ni moja kati ya binadamu waliopata kuwa na uwezo mkubwa wa kuzungumza na kushawishi kupitia hotuba.

Na moja kati ya hotuba maarufu zinazozungumzwa kuwa na ushawishi mkubwa katika historia ya dunia ni hotuba iliyotolewa na mwanaharakati wa kutetea haki za watu weusi nchini Marekani aliyejulikana kama Dr. Martin Luther King Jr. aliyoitoa Augost 28 mwaka 1963, katika maandamano ya kudai haki za watu weusi, maandamano yaliyofanyika katika jiji la Washington DC.

Lakini Motivational Speaking kama kazi "career' ilianza kupata umaarufu mkubwa baada ya vita ya kuu ya pili ya dunia hasa nchini Marekani baada ya kuibuka kwa 'motivational theories' hasa makazini zinazoeleza kuwa binadamu hahamasiki kwa mshahara peke yake bali anahamasika kwa vitu vingine ikiwa ni pamoja na kutiwa moyo, kuhamasishwa kwa maneno na kuonyeshwa njia.

Mfano wa hizi theories ni (Hertzberg’s Two-Factor Theory, Maslow’s Hierarchy of Needs, Hawthorne Effect, Expectancy Theory naThree-Dimensional Theory of Attribution). Hata wataalam waliobobea katika taaluma ya uongozi na menejimenti ikiwa ni pamoja na hayati Peter Drucker wanaeleza umuhimu wa hamasa 'motivation' kwa watu wote katika kazi.

Kwasababu hii motivational speakers wa kwanza kabisa walikuwa ni wanazuoni na wakufunzi ambao walihamasisha watu kwa kutumia tafiti na elimu walionao (hawakuwa matajiri kama Donald Trumpna Ben Carson). Hata hapa kwetu Tanzania, taasisi za Serikali na sekta binafsi zilipohitaji watoa mada katika makongamano, hazikwenda sehemu nyingine yoyote zaidi ya kuwatafuta wahadhiri wa vyuo vikuu hasa madaktari wenye Phd na Maprofesa walioandika tafiti.

Lakini mwanzani mwa miaka ya 60 walianza kuibuka watu ambao hawakuwa wanazuoni lakini walikuwa na uwezo mkubwa wa kuhamasisha watu. Mmoja ya watu hao anajulikana kama Jim Rohn (the father of motivational speaking) ambaye alikuwa mfanyabiashara. Jim Rohn kwa mara ya kwanza alialikwa kuzungumza katika taasisi ijulikanayo kama Rotary Club yenye matawi yake katika nchi mbalimbali duniani.

Baada ya kumsikiliza wanachama wa Rotary walifurahia sana ujumbe wake na Jim Rohn akaanza kupata mialiko mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzungumza na wafanyakazi wa makampuni mbalimbali ikiwa ni pamoja na kampuni kubwa nchini Marekani iliyojulikana kama Standard Oil.

Jim Rohn akapata umaarufu mkubwa sana na kuanzia hapo taasisi na makampuni yakagundua kuwa kuna watu ambao sio wakufunzi wala wanazuoni wenye uwezo wa kuongeza ufanisi wa watu binafsi na watu waliopo makazini. Ili kujifunza zaidi kutoka kwa Jim Rohn unaweza ukamfuatilia kupitia You Tube au kununua vitabu na DVDs zake.

Jim Rohn alifuatiwa na wengine wengi ikiwa ni pamoja na Zig Ziglar, Deepak Chopra, Dr. Wayne W.Dyer nk. Kutokana na motivational speaking watu hawa waliingia katika kundi la watu maarufu 'celebrities' ma kutengeneza pesa nzuri kutokana na kugusa maisha ya watu na kupata wafuasi.

Jambo lingine ambalo utagundua kuhusu Motivational Speakers ikiwa ni pamoja na Zig Ziglar ni kwamba hao hawakuwa wazungumzaji wa maneno matupu tu, walikuwa ni watu wenye historia ya kufanya vitu vitokee katika maisha yao binafsi. Mfano mzuri ni Zig Ziglar ambaye inasemekana alikuwa ni mmoja kati ya wauzaji wazuri sana (salesman) kabla hajaamua kuingia katika fani ya Motivational Speaking na uandishi wa vitabu.

Toka kipindi hicho watu wengi zaidi wakapata hamasa ya kuwa Motivational Speakers ikiwa ni pamoja na wanasiasa, watangazaji, watu maarufu, wanazuoni, wanamuziki, watumishi wa Mungu, wanamichezo nk. Mpaka leo hii baadhi ya watu wanaopata pesa nyingi kutokana na Motivational Speaking ni pamoja na Tony Blair, Bill Clinton, Ben Carson, Donald Trump, Michael Jordan, John Maxwell, Brian Tracy, Robert Kiyosaki, Oprah Winfrey, Jane Goodal nk.

Kuna makundi makubwa 6 ya Motivational Speakers. Kundi la kwanza linaitwa Iconic speakers (hawa ni wazungumzaji ambao wana wafuasi wengi kutokana na mambo makubwa waliyoifanyia jamii au nchi au dunia. Kimsingi matendo yao yanazungumza. Katika historia watu ambao wamewahi kuingia katika hadhi hii ni pamoja na Nelson Mandela, Desmond Tutu, Malcom X nk.

Kundi la pili ni Honolarly Spekers (hawa wanaweza wakawa hawazungumzi ili kulipwa pesa lakini kwa nafasi zao wanasikilizwa na wanauwezo wa kuhamasisha (wengi wanawaita hawa kama wageni rasmi katika shughuli mbalimbali). Kimsingi huwezi kualikwa kuwa mgeni rasmi mahala kama huna nafasi yoyote katika jamii.

Kundi la tatu ni Professional Speakers (hawa kuzungumza kwao ni kazi kama unavyomuona mhasibu au mkandarasi. Baadhi ya Professional Speakers wamesomea na wanajiendeleza. Wengi pia ni waandishi wa vitabu, wanatoa DVDs na wanaalikwa kuzungumza kwa makubaliano ya malipo.

Ili uwe Professional Speaker ni lazima uwe umebobea katika mada fulani fulani ili uweze kukubalika katika soko. Mfano wa Professional Speakers ni pamoja na Brian Tracy, Azim Jamal, Robin Sharma, Anhony Robbins nk. Hawa ni watu wenye makampuni ya kufundisha (training companies) wameajiri wafanyakazi, wengine wana wafanyakazi zaidi ya 500 na kuwapata kufanya nao kazi unaenda kwa makampuni yao kama unavyoenda Cocacola kununua makreti ya soda) haumpigii simu au kukutana naye Mlimani City kama unavyokutana na Paul Mashauri.

Kundi la nne ni 'Achievers'. Hawa wamejikuta wanakuwa Motivational Speakers kutokana na mafanikio yao katika kazi zao. Hapa ndipo wanapoingia watu kama Donald Trump na Ben Carson. Kwa Africa unaweza ukawazungumzia watu kama Patrice Motsepe (Afrika ya kusini), Reginald Mengi (Tanzania), Ali Mfuruki (Tanzania), Aliko Dangote (Nigeria), Rupita Nyongo (Kenya) nk.

Kundi la tano linaitwa Inspirational Story Tellers ( hawa ni aina ya wazungumzaji ambao wana uwezo au kipaji cha kuhamasisha kupitia hadithi. Hadithi hizi zinaweza kuwa za kweli (true stories) au fictional (zisizo za kweli zenye lengo la kuelimisha). Ni aina ya uzungumzaji ambao unatumia mifano halisi na isiyo halisi kufikisha ujumbe.

Chimbuko la uzungumzaji wa namna hii ni katika vitabu vitakatifu. Yesu Kristo alizungumza na wafuasi wake kwa aina hii ya uzungumzaji. Binafsi napenda kutumia staili hii ya uzungumzaji kwa sababu haichoshi watu na inamfanya mtu kuwa na uwezo wa kukumbuka kilichozungumzwa. Kumbuka binadamu anakumbuka kwa picha na mifano.

Kundi la mwisho ni la aina ya wazungumzaji ambao hawana jina maalum lakini uhamasishaji wao unatokana na matukio fulani fulani yaliyowatokea au yaliyotokea katika mazingira yao. Mfano 'Immaculée Ilibagiza' ni mzungumzaji kutoka Rwanda ambaye alifanikiwa kunusurika kutoka katika mauaji ya halaiki ya Rwanda Genocide iliyotokea April 7 mpaka Julai mwaka 1994.

Namna mzungumzaji huyu anavyoeleza jinsi alivyonusurika na namna anavyooanisha tukio lile na matukio mengine ya kimaisha inawafanya watu watafakari mara mbili kuhusu maisha. Binafsi nikiwa mwaka wa pili chuo kikuu cha Dar es Salaam, kupitia mradi wa AYA, nilipata nafasi ya kutembelea makambi ya wakimbizi yaliyopo Kibondo na Kasulu Kigoma na simulizi nilizozipata kutoka kwa wakimbizi wale inatosha kabisa kutengeneza mada 1,000 za kuzungumza.

Kuwa Motivational Speaker sio kazi rahisi. Ni kazi ngumu kama zilivyo kazi nyingine. Ni kazi yenye ushindani kama zilivyo kazi nyingine na kazi yenye kipato kikubwa kama zilivyo kazi nyingine. Wazungumzaji wakubwa kama John Maxwell wanatoza mpaka shilingi Milioni 250 kwa siku kuzungumza katika tukio lako nje ya gharama za usafiri na malazi (business class katika ndege na 5 Star Hotel accomodation) na gharama hizi si za kwake peke yake bali na wasaidizi wake wasiopungua wawili.

Wengine kama Oprah Winfrey wanaweza kufikia shilingi za kitanzania bilioni moja kwa siku. Wazungumzaji wa Tanzania kwa sasa wapo wanaolipwa mpaka shilingi milioni 15 kwa siku na wapo wanaolipwa mpaka shilingi milioni mbili kwa saa moja. Kitu ambacho watu wengi hawajui ni kwamba wapo watanzania wengi ambao ni wazungumzaji wakubwa wenye majina nje ya Tanzania ambao watanzania hawafahamu.

Mmoja kati ya wazungumzaji hao ni Ali Mfuruki, CEO, Infotech. Miaka 10 iliyopita nilitaka kumualika Ben Carson Tanzania na nilitakiwa kulipa shilingi milioni 250 kwa siku. Hivyo utagundua kuwa Motivational Speakers hawana tofauti na wasanii wakubwa wa muziki katika kupata kipato.

Leo hii kumualika Chris Brown katika concert kwa siku si chini ya shilingi za kitanzania milioni 700 mpaka 800 kwa masaa 3. Miaka 4 iliyopita kuwaleta P. Square Tanzania ilikuwa si chini ya shilingi milioni 250.

Unaweza ukajiuliza kwanini motivational speaking katika nchi za Ulaya na Marekani zimekuwa kwa kasi kuliko Afrika. Kwanza ilianzia huko, pili kihistoria, nchi za kimagharibi zilichukua uchumi huru (liberal economies) ambao unaamini katika uwezo wa mtu mmoja mmoja tofauti na nchi nyingi za kiafrika ambazo zilipendelea uchumi wa dola (centralized economies).

Lakini mabadiliko ya miaka ya 80 hasa baada ya uchumi wa nchi nyingi kubadilika ikiwa ni pamoja na Tanzania baada ya (Structural Adjustment Programs-SAPs) na kuruhusuwa kwa uchumi wmchanganyiko yaani 'mixed economies' na kuanza kwa sekta binafsi, suala la watu kuamini kuwa mtu mmoja anaweza kuhamasisha na kumasasishwa akafanya kitu kikaonekana ikapewa nafasi.

Lakini pili, nchini Marekani na Ulaya, tasnia ya Motivational Speaking imekuwa kubwa kiasi kwamba kuna vyama na taasisi ambazo zimeundwa kuratibu (regulate) sekta hiyo kama unavyoona TCRA (inayoratibu mawasiliano) au BODI YA FILAMU (inayoratibu filamu). Nchini Marekani kwa mfano kuna taasisi inaitwa International Association of Speakers Bureaus (International Association of Speakers Bureaus) ambayo pamoja na mambo mengine imeweka viwango vya nani anaweza kuwa Motivational Speaker na nani hajafikia viwango.

Taasisi hii inafanya kazi kuhakikisha kuwa fani hii inaheshimika na kupata kile inachostahili. Ili uweze kukubalika katika soko lazima ukubalike na taasisi hii, lazima uwe na cheti na taasisi hii inaweka mpaka makundi ya Motivational Speakers kama vile High Profile Speakers, On Demand Speakers nk.

Hii inamaanisha kwamba Motivational Speakers wanajitahidi kufanya kazi nzuri ili wapate 'rating' nzuri kupitia IASB. Kwa hivi sasa juhudi zinafanyika kupata taasisi ya namna hiyo Tanzania ili kuweka viwango na kuleta heshima kwa wazungumzaji.

Mpaka leo hii soko la Motivational Speakers Afrika limekuwa sana. Nchi kama Afrika ya kusini ina speakers bureaus nyingi sana ambazo zinawawakilisha motivational speakers. Mara nyingi motivational speakers wana menejimenti kama unavyoona wanamuziki na wachezaji wa soka.

Hata makubaliano ya wao kuja kuzungumza yanafanywa na menejimenti zao na si wao wenyewe kwa sababu wengi wana majukumu mengi, wana mikutano mingi na ili kukua katika fani waliyopo wanaandika sana vitabu na kutengeneza content.

Si rahisi kupata bahati ya kuonana nao na kuzungumza nao, wengi ni watu maarufu wenye kupendwa na kuheshimika hivyo unaonana nao siku ya tukio. Ratiba yao ni ngumu sana, wanasafiri sana na hawana muda wa kupoteza. Zaidi ya Afrika ya kusini, pia Nigeria, Kenya na Tanzania wanakuja kwa kasi sana katika fani ya Motivational Speaking.

Nilipata bahati ya kuwa mmoja wa watu walioanza mapema sana kushiriki katika motivational speaking. Kilichonifanya nianze kutafiti zaidi kuhusu motivational speaking ilikuwa ni ukaribu wangu na urafiki wangu na Eric Shigongo ambaye yeye alipenda na anapenda sana Public Speaking.

Eric alikuwa ana DVDs za Dr. Martin Luther King Jr. na mara nyingi tulipokuwa pamoja katika gari lake alipenda kusikiliza na aliniazima baadhi ya CDs. Hivyo nikiwa chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka wa mwanza, nilianza kuwaalika baadhi ya watu kuja kuzungumza na wanafunzi akiwemo Eric Shigongo mwenyewe baade Dr. Reginald Mengi nk.

Hii ndiyo ilinifanya nianzishe East Africa Speakers Bureau (EASB) baada ya kumaliza shule na mchango wake katika kukuza fani hii hauwezi kupuuzwa kwani ilirasimisha tasnia ya wazungumzaji na kuhamasisha umma wa watanzania kuamini kuwa unaweza ukazungumza na kupata pesa.

Kabla ya hapo ulikuwa huwezi kupata nafasi ya kuzungumza labda uwe ni mwanasiasa, tajiri au msomi wa chuo kikuu(lecturer) Nakumbuka hata nilipohojiwa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha Generali on Monday Channel Ten, Generali aliniuliza swali la kizushi akasema Paul unafikiri tunahitaji more speakers au more doers? na hivi kweli mtu anaweza akaja akazungumza tu na akapata pesa?

Hii inamaana kwamba mwanzo siku zote ni mgumu. Tulipokuwa tunaanza ukisema speakers watu wanafikiri ni speakers za redio na ukisema speakers bureau watu wanafikiri ni spika wa bungeni. lakini leo huwezi kupita wiki hujasikia kuna kongamano na kutakuwa na speakers kadhaa. Haya ni mafanikio makubwa.

Lakini jambo la kutia moyo zaidi ni kwamba kuna watu wengi sana ambao leo hii wapo hapo walipo sababu walimsikia, kumuona au kuongea na motivational speaker. Mimi ni mmoja wa watu hao. Inawezekana hata nisingemaliza chuo au ningevuta bangi au ningekufa kwa madawa ya kulevya kama nisingesoma kitabu cha Think BIG cha Ben Carson au kama nisingesikiliza hotuba za watu kama Joel Osteen, Eric Thomas, Les Brown nk.

Lakini mimi binafsi pia nimekutana na watu ambao walihudhuria makongamano tuliyoanza kuyaandaa toka mwaka 2003 na wanakiri kuwa hapo walipo ni kwa sababu ya Motivational Speakers. Wengine leo hii ni wabunge, wengine mawaziri, wengine wafanyabiashara, wengine wanamuziki na wengine ni wanataaluma. Toka mwaka 2007 tulijitahidi sana kutengeneza speakers na tulifanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Baadhi ya watu tuliopata kuwaalika ni kama Azim Jamal, dr. Reginald Mengi, Eric SHigongo, Rev. Getrude Rwakatare, Dr. Chris Mauki, Dr. Juma Mwapachu, Felix Mosha, Mama Sara Masasi, Joseph Kusaga, Sir. Andy Chande, James Mwan'amba, Modesta Lilian Mahiga, Iddi Simba, Costantine Magavilla, Nehemia Kyando Mchechu, Dr. Manu Chandaria, Obafemi Banigbe, Charles Washoma, Mama Salma Kikwete na wengine wengi, idadi ni kubwa lakini lengo langu ni kuonesha kuwa huwezi kupata Motivational Speakers kama hakuna juhudi za kuwatengeneza na kuwatambulisha katika soko.

Hauhitaji kuwa na pesa nyingi au kuwa na nafasi katika jamii kuwa Motivational Speaker. Unahitaji kupenda kufanya hivyo (passion) maarifa (knowledge), taaluma (skills), muda (time) mbinu (strategy) na mazoezi (practice). Wapo watu ambao hawakuwa matajiri wala hawakuwa maarufu lakini leo ni matajiri na ni maarufu kwa sababu ya Motivational Speaking.

Mimi sio tajiri lakini wapo watu walionipa nafasi ya kuzungumza na wapo kati yao waliofunguka kwa namna moja au nyingine. Wapo watu ambao walikuwa ni wahasibu lakini leo wanazunguka dunia kufanya motivational speaking na mmoja wa watu hao ni rafiki yangu Azim Jamal.

AzimJamal anasema alianza motivational speaking akiwa na miaka 43 baada ya kuamua kuacha kazi yake kama mhasibu nchini Uingereza. Azim anasema haikuwa rahisi na kuna kipindi ilimlazimu agawe vitabu vyake bure na kuna kipindi ilimlazimu aongee bure lakini leo Azim anapata mpaka milioni 50 kwa siku kutokana na motivational speaking. Amezunguka nchi nyingi sana duniani na mara ya mwisho nimekutana naye kama wiki 3 zilizopita alikuwa ametokea Cuba.

Motivational Speakers wanakuwa kama wanavyokuwa wanataaluma wengine. Lazima ujifunze na ubadilike kila siku. Uzoefu unaonyesha kuwa Motivational Speakers waliofanikiwa ni wale walioamua kujikita katika eneo fulani. Mfano kuna watu wanazungumzia biashara tu, uchumi tu, mahusiano tu, ujasiriamali tu, fedha tu nk.

Hii inakutambulisha vyema katika soko.Mfano Azim Jamal amejikita katika 'Business Balance and Beyond' Deepak Chopra amejikita katika 'Health and Spirituality' Robin Sharma amejikita katika "Leadership' Dr. Chris Mauki amejikita katika 'saikolojia na mahusiano' Liz Wachuka amejikita katika 'kazi na ajira' Paul Mashauri amejikita katika 'ujasiriamali' , James Mwang'samba amejikita katika bisahara nk. Pili ni lazima ubadilike katika ujumbe wako.

Huwezi kuwa motivational speaker ambaye unaongea kitu kilekile miaka nenda rudi, hauna jipya. Ukifanya hivyo unachosha watu na unakosa kazi au kupata mialiko ya kuzungumza. Lakini zaidi ya hapo ili uwe Motivational Speaker mzuri lazima ujue vitu vingi zaidi ya kile unachokizungumzia. Mfano unaweza ukatumia mifano ya kibailojia kuzungumzia biashara. Chukulia mfano mmea unavyokua, unavyopanda mbegu, unavyolima na unavyovuna, hii inatofauti gani na biashara? Kwa mtu anayewaza au kutaka kuwa Motivational Speaker inawezekana kabisa.

Lakini cha kwanza lazima ujue unataka nini hasa na kwanini motivational speaking. je unapenda tu kuzungumza, je unataka pesa? je unakipaji na unahisi haujakitumia? je unamuiga mtu? je umekosa kazi nyingine ya kufanya? je unataka umaarufu? je ni njia ya kupata kitu kingine kama uongozi nk? hivyo lazima ujue nini unataka.

Pili lazima uanze mahala. Unaweza ukaanza kwa kujifunza kuzungumza mbele za watu. Mfano kwenye vikao vya familia, kwenye harusi, kwenye misiba, hata kwenye makongamano usisite kuzungumza ili ujenge kujiamini (confidence). Cha pili kuna kozi maalum za public speaking, unaweza ukaenda kujifunza jinsi ya kuzungumza mbele za watu.

Tatu fanya mazoezi hata ukiwa mwenyewe nyumbani, mbele ya familia yako au mbele ya kioo.

Nne omba kuzungumza bure (volunteer speakers) ili upate nafasi ya kujifunza na kufahamika. Unaweza ukajiunga na baadhi ya taasisi ili kupata fursa hizi mfano Lotary na Toastmasters Club.

Tano soma sana vitabu na wasikilize wazungumzaji wengine. Ikiwezekana tafuta mentor au coach ambaye yeye anafanya vizuri katika fani hii ili aweze kukusaidia. Haitakuwa rahisi lakini usikate tamaa. Sehemu nzuri unayoweza kuangalia namna wenzake wanavozungumza ni kupitia website au tovuti ya TED. (TED Talks)

Ili uweze kuwa mzungumzaji mzuri lazima uwe 'natural'. usimuige mtu, usiige uzungumzaji wa mtu mwingine. Hauwezi kumpita mwingine kwa sababu wewe sio mwingine. Ukimuiga mtu utafanya vizuri lakini sio vizuri sana.Pia lazima ujue unazungumza na nani. Usikariri hotuba yako.

Vitu vya kuangalia unapozungumza na watu kwanza ni tamaduni zao, historia zao, matarajio yao, umri wao, misingi yao (values), upeo wao, elimu yao, mahala walipo, mazingira uyao nk. Lazima uongee lugha wanayoielewa. Ndiyo sababu hata mimi napoenda kuzungumza huwa nachunguza kwanza naongea na nani.

Ninapoongea na wazee najua nini cha kuwaambia, ninapoongea na vijana najua lugha ya vijana, ninapoongea na CEOs najua nini wanategemea. Hivyo lazima ujue unazungumza na nani. Pili lazima uzungumze kitu kinachowafanya wao waone mahusiano kati ya maneno yako na mazingira yao.

Tatizo wazungumzaji wengi wanachukua mawazo ya wazungumzaji wengine You Tube. Matokeo yake wanaongea vitu vya Marekani kwa Mtanzania (tamaduni tofauti, mazingira tofauti, watu tofauti) badala ya kuhamisha hotuba za Ulaya kuzileta Dar es Salaam kwanini usitengeneze hotuba za kwako za Dar es Salaam? Hizi ni baadhi ya chagamoto.

Nimeandika makala hii ili kuweza kueleza japo kwa kifupi motivational speaking ni nini, fursa na changamoto zake ili kuweza kutoa ufafanuzi wa maswali mengi ambayo watu wanayo kuhusu Motivational Speakers. Hivyo inawezekana kweli kukawa na Motivational Speakers waganga njaa kama walivyo wanasheria waganga njaa na kama walivyo madaktari waganga njaa.

Waganga njaa wako kila sehemu, hata kwenye siasa wapo waganga njjaa, hata kwenye bongo movie wapo waganga njaa. Waganga njaa wapo kila sehemu hata kwenye bunge la Marekani wapo waganga njaa. Sekta ya Motivational Speaking bado ni changa sana Tanzania, hivyo inahitaji juhudi za pamoja kuikuza. Huwezi kulinganisha Motivational Speakers wa Tanzania na wa Marekani.

Kufanya hivyo ni sawa na kulinganisha Yanga Sports Club na Real Madril. Lakini ili sekta yoyote ikue lazima watu wawe na udiriki na uthubutu na lazima watunze viwango. Hata Marekani sekta hii haikujengwa na Trump na Ben Carson peke yake. Wapo ambao hawana mafanikio au pesa nyingi kama Trump lakini impact au athari waliyoileta Marekani kutokana na motivational speaking ni kubwa kuliko impact iliyoletwa na wazungumzaji matajiri.

Mfano wa watu hao ni Nicholas James Vujicic (Evangelist and Motivational Speaker) . Huyu ni mAustralia aliyezaliwa pasipo miguu lakini mmoja kati ya watu waliowabadilisha watu wengi sana duniani. Watu hawamsikilizi Nicholas James Vujicic kwa sababu ana pesa. Wanamsikiliza kwa sababu kwa mazingira yake na jinsi alivyo alitakiwa awe ombaomba barabarani. Badala yake anamtumikia Mungu na kuhamasisha wengine. Ana mke na watoto wazuri.

Sekta ya Motivational Speaking Tanzania haieleweki kwa sababu ni ngeni. Hivyo Inahitaji ufafanuzi na utetezi. Haina tofauti na bongo fleva ilivyoanza. Wakati Salehe Jabri anaanza kurap kiswahili alikuwa anachukua rap za Ulaya anabadilisha maneno yanakuwa ya kiswahili. Nakumbuka wimbo wake wa kwanza wa Ice Ice baby ulikuwa na vionjo vya FUNK.

Kipindi hicho FUNK ilikuwa inasikilizwa sambamba na mziki wa POP. Baadaye wakaja akina Kwanza Unit, Mr. Paul, II Proud, Hard Blasters na leo hii Bongo Fleva ni kitu kingine kabisa. Iinawezekana leo hii Motivational Speakers wanaiga hotuba za Ulaya. Mimi sisangai, hii ni kwa sababu ya uchanga wa sekta, ni kama Bongo Fleva ilivyoanza, naamini ipo siku sekta itakuwa kubwa na wote tutatambua mchango wake.

Imeandikwa na Paul R.K Mashauri, CEO, Masterclass Worldwide (www.masterclassworldwide.net) (www.mashauri.net) Paul is a serial entrepreneur, inspirational story teller, trainer, coach, producer and actor.Ukiona makala hii ina jambo lenye manufaa kwa jamii, usisite kucopy na kushare na ndugu, jamaa na marafiki zako kupitia facebook na whatsapp. Mungu akubariki.
 
Aksante sana Kaka, nimetambua kuwa wewe sio mchoyo wa maarifa, unapenda sote tupige hatua. Mimi binafsi napenda sana kuwa motivational speaker lakini na kuwa sijui nianzie wapi hivyo natakata tamaa ya kuendelea.
 
Motivation speaker wote hufanya Biashara na lmsi vinginevyo yaani ile kuongea kwao ndo biashara yao na hulipwa pesa kwa kazi hiyo.

Unavyo sema Wa Tanzania ni waganga njaa una manisha nini?

Hata wao wanafanya yale wanao fanya hao wa nje,

Ni sawa na Bidhaa labda ya Simu kutoka China useme hii ndo simu na iliyo tengenezwa Tanzani useme hawa wanaganga njaa tu simu yao sio nzuri.

Wewe hapo umeajiriwa unaganga njaa pia, kila mtu ana ganga njaa
 
Kwa Tanzania huyo dogo ONTARIO akiendelea atafika mbali sana, anajua kujenga hoja na kuitetea, anajua kuhamasisha.

Hayo akina Shigongo ni wasimuliaji tu
 
Kwa Tanzania huyo dogo ONTARIO akiendelea atafika mbali sana, anajua kujenga hoja na kuitetea, anajua kuhamasisha.

Hayo akina Shigongo ni wasimuliaji tu
Kuhamasisha kunaendana na Physical things, Mtu kama Shigongo anakuwa na Advantage ya kwamba ana kitu kinacho onekana.

Kwamba watu wana kitu cha kurefer, wanaweza piga picha ya magazeti yake ya Udaku na kadhalika.

Kuna mmoja Cris Mulubi Yuko kenya yue naye ni Motivator mkubwa sana ila ana Biashara nyingi sana Kenya na Ni Bilionare kwa maana kwamba ana Real estate, ana mashamba ya Kahawa na biashara zingine.

Sasa anavyo kuwa ana Motivate watu, huwa wanamuelewa kwa sababu ana mifano hai kutoka kwake yeye mwenyewe.

Sio una motivate watu halafu mfano unamtolea Bilgate au Mengi
 
Kuhamasisha kunaendana na Physical things, Mtu kama Shigongo anakuwa na Advantage ya kwamba ana kitu kinacho onekana.

Kwamba watu wana kitu cha kurefer, wanaweza piga picha ya magazeti yake ya Udaku na kadhalika.

Kuna mmoja Cris Mulubi Yuko kenya yue naye ni Motivator mkubwa sana ila ana Biashara nyingi sana Kenya na Ni Bilionare kwa maana kwamba ana Real estate, ana mashamba ya Kahawa na biashara zingine.

Sasa anavyo kuwa ana Motivate watu, huwa wanamuelewa kwa sababu ana mifano hai kutoka kwake yeye mwenyewe.

Sio una motivate watu halafu mfano unamtolea Bilgate au Mengi
At his age he has alot of things to show.. Na yeye pia ni mzuri kwa vijana kuwaonyesha kuwa wanaweza..

Ngoja nitajaribu kumfuatilia na huyo Mkenya.. Lakini hawa akina Shigongo na story zao eti kutoka kulala barabarani then after a short period yupo na Magazeti huwa hainiingii akilini. Lazima kuna vitu anaficha
 
Motivation speaker wote hufanya Biashara na lmsi vinginevyo yaani ile kuongea kwao ndo biashara yao na hulipwa pesa kwa kazi hiyo.

Unavyo sema Wa Tanzania ni waganga njaa una manisha nini?

Hata wao wanafanya yale wanao fanya hao wa nje,

Ni sawa na Bidhaa labda ya Simu kutoka China useme hii ndo simu na iliyo tengenezwa Tanzani useme hawa wanaganga njaa tu simu yao sio nzuri.

Wewe hapo umeajiriwa unaganga njaa pia, kila mtu ana ganga njaa
motivation speaker wengi wa bongo miyeyusho
 
Back
Top Bottom