The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 613
- 1,776
Mwalimu ana jukumu muhimu katika kuunda haiba ya vijana na kuwatayarisha kuwa raia wazalendo na wanaowajibika. Kando na kazi za kufundisha darasani, mwalimu pia anatarajiwa kuchukua nafasi ya mshauri, kiongozi na mlezi kwa wanafunzi. Lakini pamoja na umuhimu huo, bado kuna mtazamo hasi dhidi walimu katika jamii.
Ualimu hauchukuliwi kama taaluma inayoheshimika. Kwa siku hizi ni nadra kuona kijana yeyote akitazama ualimu kama chaguo lake la kwanza la taaluma. Hii ni kwakuwa kuna changamoto mbalimbali zinazosababisha taaluma ya ualimu kutoheshimika na wengi nchini Tanzania.
Kwanza, ni kwa sababu ya mishahara midogo ukilinganisha na taaluma nyingine kama vile sheria na udaktari. Aidha, malalamiko ya walimu kuhusu mazingira duni ya kufundishia na kujifunzia, uhaba wa vitendea kazi na ukubwa wa madarasa hayawavutii wengi kuingia katika taaluma hiyo. Hata hivyo, vijana wanaojiunga na taaluma hii ni kwa sababu hawana njia mbadala.
Sababu nyingine ni kwamba vijana wanaona taaluma ya ualimu kama ni kwa ajili ya wale ambao hawakufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.
Hivyo, inaweza kuwa elimu ni sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo ya serikali ya Tanzania, lakini haijawavutia vijana kujiunga na taaluma ya ualimu kwa moyo mmoja kwasababu kila mara inaonekana hasi ikilinganishwa na taaluma nyingine.
Tufanye nini?
Tuboreshe vipato
Ili kuwavutia vijana kwenye taaluma ya ualimu, kuwe na mishahara inayoendana na maisha ya sasa. Serikali inapaswa pia kuunda sera bora za taaluma hii na kutoa motisha kwa kazi za ziada. Hii isiwe tu kwa shule za umma; shule za binafsi pia zina jukumu la kufanya kazi ya ualimu kuvutia. Baadhi ya shule za binafsi pia zinashutumiwa kutotoa mikataba kwa walimu hata baada ya miaka kadhaa. Hili linapaswa kurekebishwa ili kuongeza hamu ya vijana kufundisha.
Mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia
Baadhi ya majengo ya shule yana paa zinazovuja, madarasa yenye vumbi, madawati na meza mbovu au kutokuwepo kabisa na vifaa vya kufundishia. Njia rahisi ya kufanya taaluma ya ualimu ivutie vijana ni kujenga majengo mazuri, ofisi na madarasa kwa waelimishaji. Hii itasababisha kuwa na mazingira rafiki kwa wote – wanafunzi na walimu.
Mazingira ya mwanadamu yanaweza kuathiri sana uzalishaji. Ili kuwafanya walimu kuzingatia majukumu yao na wanafunzi kujifunza vizuri, lazima mazingira yawe ya kuvutia. Shule nyingi za binafsi zinaonekana kuzingatia sana kipengele hiki, ila serikali bado inahitaji nguvu kubwa kuboresha mazingira pamoja viwango vya ufundishaji katika shule za umma.
Teknolojia katika sekta ya elimu
Vijana wa karne ya 21 wanaweza kufanya kazi vizuri katika sehemu za kazi ambazo zinahimiza matumizi ya teknolojia na ubunifu. Mbinu za kizamani za ufundishaji sasa haziendani na wakati tuliomo. Matumizi ya teknolojia yanaweza kuwavutia vijana wengi kwani pia unawapatia fursa ya kukua na maendeleo ya kiteknolojia lakini pia kunaweza kuwasaidia kupunguza mzigo wa kazi. Shule nyingi za umma zina changamoto ya umeme, hivyo ni wakati sasa wa serikali kuona umuhimu wa kuzifanya shule zetu kuwa za kisasa na zinazotoa fursa ya vijana kupata elimu inayoendana na teknolojia ya sasa.
Huduma za msingi kwa walimu
Walimu wa shule za umma zilizopo katika maeneo ya vijijini wanakumbana na changamoto za kila aina: maji, umeme, usafiri na huduma nyingine za kijamii. Wengine kuna wakati wanatumia karibu nusu ya mshahara kama nauli ya kwenda ofisi za halmashauri au kufanya manunuzi ya msingi. Haya si mazingira ambayo vijana wengi wa leo wapo tayari kuyaishi. Ni vyema serikali iangalie utaratibu wa kuwawezesha walimu wanaoishi katika maeneo hayo kuishi vizuri kwa kuwapatia makazi, posho maalum, chakula na kuhakikisha wanapata huduma nyingine za msingi.
Ualimu ni kazi ya muhimu, na pengine ya lazima katika jamii. Ili jamii kuyaona na kuyafurahia matunda yake inapaswa kuwa na mikakati endelevu ambayo itawanufaisha walimu na wanafunzi. Serikali ina jukumu, sisi pia tunapaswa kuondokana na dharau tuliyonayo kuhusu taaluma ya ualimu. Kufanya ualimu kuvutia huanza na jinsi tunavyouchukulia na jinsi tunavyoelewa umuhimu wake.
Ikiwa leo ni Oktoba 5, ambayo ni Siku ya Walimu Duniani, nimeona ni vyema tukumbushane mambo machache kwa manufaa ya walimu wetu.