IslamTZ
JF-Expert Member
- Nov 22, 2010
- 309
- 182
Tukio la kawaida la mkusanyiko wa watu kumkumbuka mpendwa wao limenifumbua akili na kuyajua mambo mengi kuhusu siasa za nchi hii na asili ya uhusiano wa karibu wa baadhi ya watu.
Nazungumzia kumbukizi ya miaka 20 tangu kufariki kwa mmoja wa viongozi mahiri wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Brigedia Jenerali Moses Nnauye, ambaye, kama cheo kinavyojieleza, pia aliwahi kuhudumu serikalini, jeshini huku akikumbukwa zaidi kwa kipawa chake cha muziki.
Ukiacha familia ya Nnauye mwenyewe (mjane na watoto), walikuwepo pia Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, na Makatibu wakuu wa CCM wastaafu Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba.
Orodha hii ikanikumbusha tukio lile enzi ya awamu ya tano ziliponaswa sauti zikimsema vibaya marehemu Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli. Ni wazee hawa, (ukimuondoa Kikwete) ndio waliosikika wakimsema vibaya marehemu. Pia alikuwemo Nape, ambaye katika mazungumzo na Mzee Makamba alisikika akimuita ‘baba’ kwa heshima zote.
Hawa jamaa pamoja na marehemu ambaye walijikusanya kumkumbuka, wametoka mbali na sio ajabu kwamba wanazeeka wakiwa na ukaribu mkubwa, sio wao tu bali hata familia zao! Naamini wapo sahihi watu waliosema kuwa kuna ‘family coalition’ (muungano wa familia) unaosaidiana kuhakikisha wanatawala nchi hii.
Wote watatu niliowataja licha ya kulelewa ndani ya chama, pia walikuwa wanajeshi mahiri, enzi hizo wakati chama kimeshika utamu na hatamu zikiitangulia sio tu serikali bali hata jeshi. Kikwete, hadi anatoka jeshini alikuwa Luteni., Kinana alikuwa Kanali na Makamba alikuwa Luteni huku marehemu waliyekuwa wakimuadhimisha akiwa Brigedia Jenerali. Hii inaelezea hisia za kujiona wanastahili zaidi kukamata uongozi wa nchi wanayoona kuwa wameipigania chamani, jeshini na serikalini.
Ukiangalia historia zao, walianza kwenye chama pamoja,wakahudumua tena pamoja jeshini na kisha serikalini. Nnauye na Makamba walikuwa na mengine ya kuwaunganisha: sanaa. Wote walikuwa waimbaji enzi hizo. Kwa kweli, sikuwa najua kuwa Nnauye alikuwa ndio John Komba wa kwanza!
Hotuba ya Makamba ilifichua siri nyingi, ambapo alielezea ukaribu wake mkubwa na Nnauye kiasi kwamba bosi wake huyo wa zamani alimfia mkononi, akimsaidia kumtamkisha neno muhimu kwa Muislamu kulitamka kabla ya kifo: Laa Ilaaha Illa llah (Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu).
Kinana alisema katika hotuba yake kuwa Nnauye aliacha mafunzo mawili makubwa: Kwanza kiongozi huandaliwa na pilli, mafanikio huja kwa kuwa na ‘organization’ nzuri katika taasisi. Kwangu, kauli hizi ni dongo kwa marehemu JPM ambaye anajulikana kama kiongozi aliyekosa malezi ya chama na ambaye hakuna na weledi katika organization ya chama na badala yake alikuwa mtu wa ‘matamko’.
Wapo watu waliotafsiri kusanyiko lile kuwa sio tu ni maadhimisho ya kumbumbuka Mzee Nnauye bali pia shukrani kwa kundi lile kwa Mwenyezi Mungu wao kwa kuwatoa kifungoni baada ya kuwekewa alama ya X na JPM. Sio siri kuondoka kwa JPM kumewapa ahueni Mzee Makamba na Kinana ya walau kufurahia uhuru na kutoishi kwa wasiwasi tena! Sio siri pia kuwa kuondoka kwa JPM kumefufua matumaini ya kupanda kisiasa kwa wakina Nape, Ridhwani na Januari.
Ninachokiona ni kuwa hizi familia ziko ‘connected’ mno na kuna makubaliano mengi ya kifamilia. Nani alijua kuwa kumbe wakina Nape walikabidhiwa kwa Makamba awalee baada ya kufariki kwa mzee wao? Nani hajui kuwa Kikwete kambeba sana Januari na kumlea kisiasa? Kinana naye akawa karibu na Nape enzi zao chamani akimpa madini ya ‘organization’ ambayo naye alijifunza kwa Mzee Nnauye? Yapi mengine hatuyajui katika mikataba hii ya kifamilia?
Nikiangalia mustakbali wa nchi, nikirejea sauti zile zilizovuja za kumponda JPM hasira zao sitashangaa hawa wababe wakiichukua nchi baada ya Rais Samia kustaafu. Tayari kuna tetesi kuwa Rais Samia anapokea ushauri kutoka Mzee wa Chalinze, ambaye ndiye mzee wa hawa vijana.
Halafu vijana wako vizuri na wamejipanga hasa Januari ambaye anajulikana kama kipenzi cha watu wa mitandaoni hasa Twitter (Twitter darling), ingawa kwa upande mwingine sio siri rekodi yake ya utendaji haivutii, haishtui.
Bila vikwazo vingine njiani, naiona serikali huko mbele ya Rais Januari, Waziri Mkuu Nape huku wakina Ridhwan, Bashe wakipewa majukumu kubwa katika Baraza la Mawaziri.
Tusubiri na tuone