Kumbe siasa ipo katika kila nyanja hapa tanzania- mgomo wa madereva ubungo | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kumbe siasa ipo katika kila nyanja hapa tanzania- mgomo wa madereva ubungo

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Jatropha, Aug 28, 2009.

 1. Jatropha

  Jatropha JF-Expert Member

  #1
  Aug 28, 2009
  Joined: Apr 9, 2009
  Messages: 1,152
  Likes Received: 144
  Trophy Points: 160
  RAIA MWEMA TOLEO NO 95

  19 AGOSTI 2009
  Mgomo wa madereva Ubungo: Abiria walikuwa silaha ya mapambano

  [​IMG]
  Mwandishi Maalum​
  Agosti 19, 2009[​IMG]
  [​IMG]Waliouandaa ni wahujumu wa maslahi ya madereva

  [​IMG]Ni mpambano wa makundi mawili yapinganayo ndani ya UWAMATA  MAELFU ya abiria waliokuwa wamekata tiketi kusafiri mikoa mbali mbali kwa mabasi kutoka Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo, Dar es Salaam, Ijumaa, Agosti 14, 2009 walitumiwa kama ngao au silaha ya mapambano na madereva wachache wakorofi wakiongozwa na kikundi cha watu wasio waadilifu ili kutimiza malengo na maslahi binafsi ambayo kwa kiwango kikubwa yanakinzana na sheria za nchi.
  Wengi wa abiria hao wakiwa ni akina mama na watoto, walijikuta katikati ya kundi kubwa la watu wasiokuwa abiria au kuwa na uhusiano wowote na shughuli za usafirishaji wa abiria kwa mujibu wa sheria.
  Kundi hilo lilikuwa limeandaliwa ipasavyo na kwa utaalamu mkubwa kukabiliana na vyombo vya dola endapo Serikali ingewashinikiza wamiliki wa mabasi kusafirisha abiria kwa mujibu wa tiketi walizokuwa nazo. Ni wazi kuwa waathirika wakubwa wa mpambano huo wangekuwa abiria wasiokuwa na hatia yoyote.
  Naipongeza Serikali, hasa Kaimu Mkuu wa Mkoa, Evans Balama, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana na Kamanda wa Kanda Maalumu Suleiman Kova, ambao walikuwa wepesi kubaini hatari iliyokuwa mbele ya maelfu ya abiria waliokuwa tayari wameingia ndani ya uzio wa kituo hicho.
  Badala ya kutumia sheria na kanuni, Serikali katika kile kinachoonekana ni kujali zaidi uhai na maisha ya binadamu, ilishikiliwa mateka na makundi ya kihuni na ikaamua kutumia majadiliano kumaliza tatizo hilo na ikaagiza kuwa mabasi hayo yasisimamishwe njiani ili abiria waweze kufika wanakokwenda mapema kadri inavyowezekana.
  Wasiokuwa na upeo na wasiothamini uhai na maisha ya binadamu, wanadhani kuwa siku ya mgomo walipata ushindi dhidi ya Serikali. Hasha. Serikali ilitimiza wajibu wake wa kulinda raia na mali zao.
  Kitendo cha Serikali yenye maguvu yote; askari, bunduki, mabomu ya machozi na magari ya kumwaga maji ya kuwasha, kujishusha na kukubali kujadiliana na waandaaji mgomo ambao kwa vigezo vyovyote hawakuwa na uhalali wowote kufanya walichokifanya au kuwapo ndani ya Kituo cha Ubungo kusitisha safari za mabasi siku ile, ni cha kupongezwa na kuigwa na wote wanaojifanya wanawatumikia wananchi katika nafasi mbali mbali ukiwamo uongozi wa asasi mbali mbali za kiraia kama ile iliyoandaa mgomo kwa kutumia binadamu kama silaha ya majadiliano yao.
  Lengo kuu la waandaaji mgomo ule ilikuwa ni kujichimbia katika uongozi wa asasi ambayo wamewapindua viongozi wake na mpaka sasa wameshindwa kukaa meza moja kumaliza tofauti zao.
  Mgomo huo uliandaliwa na kikundi cha watu wanaojiita madereva wa mabasi lakini kila siku hushinda Ubungo Stendi chini ya mti karibu na lango kuu, kutokana na kukosa sifa za kupata ajira katika basi lolote la abiria. Kikundi hiki kilifanikiwa kufanya mapinduzi ndani ya asasi iitwayo Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania (UWAMATA) mwanzoni mwa mwaka huu, kuifanya asasi hiyo kuwa na makundi mawili yanayokinzana yaani (UWAMATA-A) wale waliopinduliwa na (UWAMATA-B) wale waliofanya mapinduzi.
  Kutokana na mapinduzi hayo fursa ya kukusanya shilingi 1,000 kutoka kila dereva wa basi la mkoani linalotoka Kituo cha Ubungo ikahamia kwa UWAMATA- B na ndiyo chanzo cha mgogoro uliosababisha abiria kucheleweshewa safari siku ile ya Agosti 14, 2009 .
  Katika jitihada za kujirejesha madarakani viongozi waliopinduliwa inaaminika walifanikiwa kujisogeza kwa Mkuu mpya wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, wakati akizindua utaratibu wa mistari ya rangi kwa teksi, mikataba ya ajira kwa madereva wa daladala na bajaj katika viwanja vya Mnazi Mmoja mwisho mwa Julai 2009 kupitia kwa kiongozi mmoja wa taasisi inayohusika na usimamizi wa usafiri, aliyemsogezea Lukuvi barua kutoka kwa viongozi waliopinduliwa (UWAMATA-A).
  Kwa nia njema kabisa, Lukuvi katika hutoba yake siku hiyo, wakati akisistiza umuhimu na faida za mikataba kwa madereva alitaja kuwa amepokea barua kutoka Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania (UWAMATA) inayoonyesha jinsi madereva wa mabasi ya mikoani walivyo na maslahi duni. Mafanikio ya UWAMATA-A kuwasilisha hoja ya madereva kukosa mikataba ya ajira kwa Mkuu wa Mkoa yaliwakera sana UWAMATA-B na hivyo wakaona maslahi yao yametishiwa. Kwa tafsiri yao waliona kuwa pengine Mkuu wa Mkoa anawaunga mkono UWAMATA-A. Sioni kosa kwa mtu mmoja mmoja au kikundi kumuandikia barua kiongozi wa Serikali kulalamikia jambo fulani.
  Kama Lukuvi alipewa barua hiyo pale pale uwanjani, aliyempatia barua hiyo atakuwa ni mmoja wa viongozi anayeufahamu vizuri mgogoro uliopo ndani ya UWAMATA, pamoja na malalamiko ya madereva wa mabasi ya mikoani ya muda mrefu dhidi ya viongozi wa asasi hiyo ya ufujaji wa zaidi shilingi milioni 20 kama michango wanayotoa kila siku wanapotoka stendi kwa ajili ya kuwasaida wakati wa kesi mahakamani. Na atakuwa alilenga kulibeba kundi moja dhidi ya jingine badala ya kutumia nafasi yake kuwasuluhisha.
  Hivyo hakumtendea haki Mkuu wa Mkoa Lukuvi, wala kuwatendea haki abiria ambao kabla ya kitendo hiki cha kufikisha kundi mojawapo kati ya yanayopingana kwa Mkuu wa Mkoa hapakuwahi kutokea usumbufu wala mateso ya aina yoyote kwa abiria kituoni Ubungo, japokuwa makundi haya yamekuwa yakipingana chini kwa chini kwa muda sasa .
  Baada ya kuona kuwa maslahi yao yametishiwa kwa mtaji wao wa kisiasa (madereva kukosa maslahi ya kueleweka) inashughulikiwa na viongozi waliopinduliwa, upande wa UWAMATA-B wakalazimika kubuni mikakati ya kuhakikisha kuwa wanabakia katika nafasi walizonazo.
  Moja ya mikakati hiyo ikawa ni kutoa matangazo, Agosti 5, 2009 kuwa UWAMATA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani watafanya ukaguzi maalumu wa mabasi kuanzia Septemba 1, 2009 ili kwamba mabasi ambayo wamiliki wake hawajaingia mikataba ya ajira na madereva wao hayataruhusiwa kupakia abiria tena.
  Tangazo liliendelea kuwatisha hadi wakatishaji tiketi kuwa watawajibika kuwarejeshea nauli abiria ambao mabasi yao hayataruhusiwa kutoka Kituo cha Ubungo Septemba 1, 2009. Kwa kitendo cha kujitwalia jukumu la kuwa wasemaji wa Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, UWAMATA-B wakafanikiwa kuteka mawazo ya madereva, wamiliki wa mabasi na kundi kubwa sana la wakatishaji tiketi na wapiga debe wao ambao kwa kiwango kikubwa ndio waliotumika kuwashurutisha madereva kushiriki mgomo wa Agosti 14, 2009.
  Kwa uzoefu wangu shughuli nyingi zinazofanywa na Kikosi cha Usalama Barabarani, hasa ukaguzi, hufanywa kwa ushirikiano wa karibu na SUMATRA. Lakini Tangazo la UWAMATA-B la Agosti 5, 2009 kwa namna yoyote halikuitaja SUMATRA kwa madai kuwa ndio wanawabeba viongozi waliopinduliwa yaani UWAMATA-A.
  Baada ya tangazo hilo batili la UWAMATA-B kuleta taharuki ya aina yake Kituo Kikuu cha Ubungo, uongozi wa UWAMATA-B ukatumia mbinu za kichochezi kuwachochea madereva dhidi ya sheria za usalama barabarani. Hii ilifanyika kusubiri fursa ya tendo lolote litakaloweza kutumiwa kuleta fujo walizofanya Agosti 14, 2009. Fursa waliyokuwa wakiisubiri ilipatikana baada ya Mahakama mkoani Tabora kutoa hukumu dhidi ya dereva wa basi la Mohamed Trans aliyesababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine sita.
  Dereva huyu alihukumiwa kwenda jela miaka 30 na ilivyo ada kwa makosa ya barabarani adhabu zake hutumikiwa kwa pamoja kwa kuwa makosa hayo hufanyika kwa pamoja, dereva huyo atatakiwa kukaa jela kati ya miaka 3 au 4. Uongozi wa UWAMATA-B ukawachochea madereva kuwa mwenzao kahukumiwa miaka 30 na anatakiwa kutumikia miaka yote 30 kwa sababu ni hivi karibuni tu Rais Jakaya Kikwete alizitaka mahakama kutoa adhabu kali kwa madereva wanaosababisha ajali na vifo kwa kukiuka sheria za usalama barabarani.
  Mimi si mwanasheria lakini naamini kuwa kupotosha hotuba ya Rais kwa makusudi ni kosa la jinai. Katika uchochezi wao uongozi wa UWAMATA-B walifikia hatua ya kuwapotosha madereva kuwa Rais ametaka madereva kufungwa maisha.
  Hayo yalifanyika ili kulinda maslahi yao binafsi na si kuwatetea madereva, kwani kwa mtu yoyote mwenye busara anatambua kutokana na mgomo ule madereva walionyesha dharau kwa vyombo mbali mbali vinavyowajibika kuwasimamia kutekeleza wajibu wao wawapo barabarani, mara nyingi madereva hunusurika kuchukuliwa hatua za kisheria na hata kukuhukumiwa adhabu kali kutokana busara, huruma na hisani ya askari wa Usalama Barabarani na Mahakimu.
  Kutokana na watendaji wa vyombo vilivyotajwa hapo nao kuwa binadamu wenye hisia kama walivyokuwa madereva, ni lazima watakuwa wameguswa na dharau na unyanyasaji waliouonyesha watu wanaojiita madereva siku ya Agosti 14, 2009. Na kila binadamu ana namna ya kupokea na kutawala hisia zake awapo wenye uwezo wa kusamehe; wapo wenye shauku ya kulipa visasi.
  Mara kadhaa tumeona watendaji wa fani mbali mbali, kama waandishi wa habari, wakiungana kuchukua hatua dhidi ya dharau au unyanyasaji wa mtendaji mwenzao. Kutokana na madereva kuonyesha dharau kwa mahakimu, wanaweza kabisa kuanza kutoa adhabu za juu zinazotamkwa na sheria zikiwamo vifungo vya mara kwa mara badala ya faini ama hukumu zote mbili yaani vifungo na faini, tofauti na hali ilivyo sasa.
  Kutokana na pande zote mbili yaani UWAMATA-A na UWAMATA-B kugubikwa na ubinafsi na tamaa ya maslahi binafsi, walikwamisha wakashindwa kuiheshimu Serikali na jitihada za kuingila kati kuepusha adha na mahangaiko kwa binadamu (abiria).
  Kwa mujibu wa gazeti moja la kla siku la Agosti 15, 2009 mtu aliyejitambulisha kama Katibu Mkuu wa UWAMATA, Salum Abdallah (tofauti na Katibu Mkuu aliyehusika na majadiliano na viongozi wa Serikali siku ya mgomo) alinukuliwa akidai kwamba “haungi mkono mgomo huu aliodao unaongozwa na wahuni”. Abdallah alisema malalamiko ya madereva waliyawasilisha kwa Lukuvi (Mkuu wa Mkoa) mapema na aliwataka wayaweke kwenye maandishi na walikwisha kufanya hivyo.
  Cha kushangaza siku ya Agosti 14, 2009 wakati wa mkutano wa madereva na viongozi wa Serikali mtu aliyekuwa akijiita mlezi wa UWAMATA-B, Awadh, alitoa amri kuwa Salum Abdallah afukuzwe kwenye mkutano huo mbele ya viongozi wa Serikali, na amri hiyo ikatekelezwa na wafuasi wake. Kitendo hiki kinashiria ukubwa wa tofauti na uhasama uliopo baina ya pande hizi mbili. Hivyo isingewezekana kwa pande hizi hasimu kukaa pamoja kushirikiana kuandaa na kuwasilisha malalamiko ya madereva kwa Mkuu wa Mkoa kama alivyoagiza Agosti 13, 2009 ili mgomo usiwepo.
  Kama alivyonukuliwa Salum Abdallah wa UWAMATA-A na gazeti hilo ya kuwa tayari agizo la Mkuu wa Mkoa lilikwisha kutekelezwa, na hapakuwepo haja ya mgomo, ni wazi kuwa ni upande wake ndio ulikuwa ukifanya mawasiliano na Serikali kuepusha mgomo ambo ulikuwa ukiandaliwa na upande wa UWAMATA-B.
  Kama hivi ndivyo, kitendo cha Salum Abdallah wa UWAMATA-A kushindwa kutoa taarifa sahihi kwa Serikali kuwa si kundi lake linaloandaa mgomo ili Serikali iweze kufanya mazungumzo na waandaaji halisi wa mgomo kilikuwa ni cha kibinafsi na kuvunja sheria na kingeweza kusababisha maafa endapo fujo zingezuka siku ya mgomo.
  Kulingana na uzito wa suala lenyewe, Salum Abdallah na kundi lake la UWAMATA-A walitakiwa kuweka maslahi binafsi pembeni na kuipatia Serikali taarifa sahihi (volunteer correct information) kwa nia ya kuepusha adha, mahangaiko, majeruhi na hata vifo vya wananchi (abiria) wasio na hatia endapo fujo zingezuka.
  Lakini walihofia ya kuwa kuwatangaza wenzao kwa Serikali kitaujenga upande wa UWAMATA-B hivyo walikuwa tayari watu waumie na hata kufa siku ya mgomo lakini upande wa UWAMATA- B wasipande chati.
  Ni imani yangu pia katika majadiliano kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam yaliyolenga kuepusha mgomo siku ya Agosti 13, 2009, ni lazima taasisi ya SUMATRA ilihusika kwa kiwango kikubwa. Na kama ni kweli ni upande wa Salum Abdallah na upande wa UWAMATA-A ndio waliofanya mazungumzo na Serikali pasipo kuwapo upande wa UWAMATA-B, ni wazi kuwa watendaji wa SUMATRA watakuwa walifanya kosa kubwa sana kutoipatia Serikali ushauri sahihi na wa kweli kuhusu hali ilivyo ndani ya stendi ya Ubungo.
  Lukuvi na na Wakuu wake wa Wilaya za Dar es Salaam wote ni wageni. Haikuwa rahisi kufahamu kuwa kuna UWAMATA-A na UWAMATA-B. Lakini watendaji wa SUMATRA wanalifahamu hilo vizuri sana na kulingana na uzito wa suala lenyewe walitakiwa kuiarifu Serikali hali hiyo kwa nia ya kuepusha adha, mahangaiko, majeruhi na hata vifo vya wananchi (abiria) wasio na hatia endapo fujo zingezuka.
  Kama walishindwa kufanya hivyo na kuruhusu Serikali iendelee kufanya majadiliano ya kuepusha mgomo na upande ambao haukuandaa wala kwa sasa hauna uwezo wa kuandaa mgomo, kitendo hicho kinaweza kutafsiriwa kuwa ni cha kukumbatia upande mmoja kati ya makundi yanayohasimiana ndani ya UWAMATA.
  Laiti kama UWAMATA-A ya Salum Abdallah na UWAMATA-B ya Maulidi Lubuva zingekutanishwa katika jitihada za kuepusha mgomo huo ni imani yangu kuwa mgomo usingekuwepo na abiria wasingepata adha na mateso waliyopata, na Serikali ingekuwa na uhakika kuwa hali hiyo haitarejewa siku za karibuni baada ya mgogoro ndani ya UWAMATA kumalizwa. Endapo hali itaachwa kuendelea kama ilivyo sasa kwa makundi ndani ya UWAMATA kuhasimiana, ni uhakika kabisa kuwa tatizo bado ni kubwa na madereva na abiria wataendelea kutumiwa kama ngao au silaha ya mapambano baina ya kufanikisha malengo ya watu binafsi ndani ya UWAMATA-A na UWAMATA-B.
  Kama UWAMATA-B kwa upande wao hawakuwa wamefanya majadiliano yoyote na Serikali kabla ya kupanga mgomo wa Agosti 14, 2009 nalo ni kosa. Ilitakiwa iwapo wanahisi hawapati haki yao na ya wanachama wao (madereva) wilayani, waende mkoani, kama hawapati haki mkoani waende ngazi ya taifa, lakini kitendo cha kuwatumia binadamu (abiria) kama ngao na silaha ya mapambano ya kudai maslahi ya madereva au kufanikisha mapambano dhidi mahasimu wao hakikubaliki.
  Walichotakiwa kufanya ni kutoa taarifa ya siku kadhaa ili abiria wasikate tiketi na wao waendelee na mgomo wao kama kweli wana amini kuwa mgomo ule ulikuwa ndani ya mawazo na mioyo ya madereva kama walivyofanya waalimu. Huo ndio utaratibu wa kistaarabu na tunapaswa kuzingatia sheria kwani ni kutokana na sheria hizio ndiyo maana wanajiita UWAMATA na si majina yao binafsi.
  Kwa mtiririko huo, wakati Serikali ikihangaika kunusuru mgomo Alhamisi Agosti 13, 2009, uongozi wa UWAMATA-B ulikuwa wakichapisha vipeperushi na kuwasambazia madereva wa mabasi yaliyokuwa yakiingia kutoka mikoani kuwa mkutano wa madereva utafanyika saa 11.00 alfajiri kesho yake, hivyo madereva waache kutimiza wajibu wao wa kuendesha mabasi na wahudhurie mkutano huo.
  Viongozi na wanachama wa UWAMATA-A na UWAMATA-B ni watu wa muda mrefu stendi Ubungo, wanafahamu vizuri wingi wa watu ambao hufurika stendi kila asubuhi kupata usafiri wa mikoani. Kitendo cha pande zote mbili, waliounga mkono na kushiriki mgomo huo kushindwa kuchukua hatua zozote kuipatia Serikali taarifa sahihi kuhusu kuwapo kwa mgomo huo au kuwatahadharisha wananchi (abiria) kuwa wasisogee eneo la stendi ambapo pangeweza kuzuka fujo na mapambano makali kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kutumika, kinaashiria kuwa zilikuwapo njama za kuwatoa kafara binadamu (abiria) wasio na hatia hasa ikizingatiwa kuwa ilikuwapo idadi kubwa ya wahuni waliokuwa wametayarishwa kwa ajili ya makabiliano na Serikali.
  Kitendo hiki cha kula njama ya kuwatoa binadamu (abiria) kafara kimetoa mwanga ni kwa kiwango gani madereva wa mabasi ya abiria bila ya kujali yuko upande gani kati ya pande zinazohasimiana, wanavyothamini uhai na maisha ya binadamu wenzao.
  Kimeweza pia kutoa picha ya namna madereva wa mabasi ya abiria wanavyofikiri na kuchukua maamuzi katika mambo yanayohusu uhai na maisha ya binadamu ambayo hulazimika kuyafanya kila siku wawapo kazini, kama kuamua kasi ya uendeshaji, uamuzi wa kulipita gari jingine katika kona, kilima au daraja na hatari nyinginezo zilizopo barabarani wakiwa wamebeba abiria. Takwimu kutoka Jeshi la Polisi zinaoonyesha kuwa mwaka 2007 peke yake watu 2594 walipoteza maisha na wengine 16,308 walijeruhiwa; na idadi ya waliopoteza maisha kuongezeka mwaka 2008 kufikia watu 2905 na wengine 17,861 kujeruhiwa.
  Madereva wa mabasi kushindwa kufanya maamuzi sahihi yanayohusu usalama wa abiria siku ya mgomo wao Agosti 14, 2009 wanaweza kujitetea kuwa ilitokana na kukumbwa na hali ngumu ya kimaisha kwa muda mrefu.
  Sijui watendaji wa SUMATRA endapo itafahamika kuwa walishindwa kutoa ushauri muafaka kwa Serikali kuhusu makundi yanayopingana ndani ya UWAMATA na hivyo kusababisha uhai na usalama wa abira kuwa hatarini siku ya Agosti 14, 2009 watajitetea nini kwa kuwa wanalipwa mishahara, posho, marupurupu na stahili nyingne.
  Siku ya mgomo mwandishi wa makala hii aliweza kushuhudia matangazo yaliyotolewa na UWAMATA-B na kubandikwa sehemu mbali mbali katika Kituo cha Ubungo yakiwa na jina na sahihi za Maulidi A Lubuva kama Katibu Mkuu. Matangazo hayo yalikuwa yakiwatisha wamiliki, madereva na wakata tiketi kuwa Jeshi la Polisi litasitisha safari za mabasi ya abiria kuanzia Septemba 1, 2009 ikiwa wamiliki hawatakuwa na mikataba ya ajira na madereva wao.
  Inadhaniwa kuwa vitisho vya aina hii vilivyotumiwa na waandaaji mgomo ndivyo vilivyoshawishi idadi kubwa ya madereva kuunga mkono mgomo huu, na idadi kubwa ya wakatishaji tiketi kutumia nguvu kuwashurutisha madereva wasiounga mkono mgomo huu. Magazeti ya Nipashe na Uhuru ya Agosti 15, 2009 yaliripoti kuwa idadi kubwa ya madereva, wamiliki na mawakala wa mabasi yakiwamo Dar Express, Meridian na Master City walikuwa tayari kuendelea kutimiza wajibu wao pasipo tatizo lolote.
  Lakini watu waliokuwa wameandaliwa waliwateremsha madereva hao kinguvu kutoka kwenye magari (sehemu zao za ajira) na hata baadhi yao kufikia kuchaniwa nguo. Vile vile silaha kama mawe zilitumika kuhakikisha kuwa hakuna gari linasafirisha abiria, hali iliyowafanya wamiliki na madereva kusalimu amri.
  Staili nyingine iliyotumiwa na kikundi hiki kutekeleza mgomo huo ni madereva wakorofi kutumika kuziba barabara za ndani ya stendi kwa kuegesha mabasi yao barabarani. Hii iliwafanya madereva waliokuwa tayari kusafirisha abiria kukosa njia za kupitisha mabasi yao kutoka nje ya kituo. Ibara ya 19 c ya Kanuni za Usafirishaji Abiria za 2007 zilizopitishwa na SUMATRA, katika Mwenendo Unaokatazwa (Prohibited Conduct) inasema ni marufuku kwa mtumishi wa gari la abiria kumzuia/ kulizibia njia basi jingine. Na katika ibara g inasema ni marufuku kuwanyanysa au kuwatesa abiria.
  Kwa mujibu wa Kanuni hizi mtu yeyote akipatikana na hatia ataweza kupigwa faini ya isiyopungua shilingi laki mbili na isiyozidi laki tano. Hii ina maana wakati madereva wakilalamikia faini kubwa za laki moja tayari walikuwa wakifanya makosa mengine yanayostahili faini ya shilingi laki tano.
  Ibara ya 18 ya Kanuni za Usafirishaji Abiria za 2007 zilizopitishwa na SUMATRA, Masharti ya Leseni (1) aliyepatiwa leseni ya usafirishai wa abiria (mmiliki) anawajibika kuhakikisha kuwa watumishi wake akiwemo dereva wanatimiza masharti ya leseni, ikiwamo kutozuia mabasi mengine kutumia barabara. Vifungu vya 30 na 31 vinaipa nguvu SUMATRA kuweza kusimamisha au kufuta leseni za wasafirishaji ambao wanashindwa kutimiza masharti ya leseni ikiwamo kuwadhibiti madereva wao wasizuie barabara au mabasi mengine.
  Napenda kuwapongeza baadhi ya wamiliki wa mabasi kwa kujaribu kuhakikisha kuwa madereva wao wanatimiza wajibu wao wa kuwasafirisha abiria kwa mujibu wa tiketi walizo nazo. Ni imani ya abiria walionyanyasika na kuteseka siku ya mgomo kuwa kwa kutumia picha za video na mnato SUMATRA itaweza kubaini ni madereva gani wa mabasi waliziba barabara za stendi kwa makusudi na kuwachukulia hatua za kufaa ili kuepusha hali hii kurejewa siku za usoni.
  Ni vyema watumishi wote nchini wakaelewa kuwa mtumishi akiamua kutumia uhuru wake na kugoma, uhuru huo huishia pale uhuru wa watu wengine unapoanzia. Uhuru wa mtu aliyeamua kugoma unapopitiliza na kuingilia na kuathiri uhuru wa watu wengine ni kuvunja sheria na haki za biandamu za watu wengine.
  Kazi ya asasi kama UWAMATA ni kuwaelimisha wanachama wake (madereva) umuhimu wa kujua na kuzingatia sheria. Kwani wakijua sheria wanakuwa katika nafasi nzuri ya kufikia malengo yao kwa kuepuka kuvunja sheria na wanakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kujitetea.
  Abiria walioteseka siku ya mgomo wanawafahamu wasemaji wa Jeshi la Polisi na Kikosi cha Usalma barabarani wakiwamo makamanda Abdallah Mssika na James Kombe, inastajaabisha kuona taarifa nyeti inayowahusu wamiliki wa mabasi ya abira, na madereva iliyosababisha athari kubwa kwa Taifa kiasi kile ilipitishwa kwa asasi ya kiraia, tena ambayo dalili zote zinaonyesha kuwa imo ndani ya mgogoro mkubwa wa uongozi kutokana na kuwa na wenyeviti, makatibu wakuu wawili wanaopingana.
  Hapa naamini Jeshi la Polisi litaufahamisha umma nani msemaji wake UWAMATA. Abiria walioteseka siku ya mgomo wanatarajia kusikia kutoka kwa wasemaji halali wa Jeshi la Polisi kuwa wanahusika vipi na taarifa hiyo? Ikiwa Jeshi la Polisi halihusiki kabisa na taarifa iliyotolewa na upande mmoja wa mgogoro ndani ya UWAMATA; wanatarajia kuona hatua za kufaa dhidi ya wote wanaotumia jina la Jeshi la Polisi kuwajenga hofu watu mbali mbali kwa maslahi yao binafsi na hatimaye kuwaathiri wananchi. Hii itasaidia kuepusha kurejewa kwa hali hiyo tena siku za usoni.
  Mwandishi wa makala hii ambaye alikuwapo katika majadiliano kati ya Serikali na madereva siku ya mgomo, alishuhudia waandaaji mgomo huo wakishindwa kuwasilisha hoja zao kwa viongozi wa Serikali kwa mpangilio unaothibitisha hoja zilizokuwa zimejadiliwa na vikao vyovyote vya asasi hiyo. Hilo liliwalazimu Serikali kuwaomba wakae wapate kutayarisha hoja zao ndipo waziwasilishe. Hii ni dalili ya kukosekana kwa vikao halali ndani ya asasi husika kujadili kero na malalamiko ya wanachama (madereva).
  Hata pale walipokuwa wamejitayarisha hoja nyingi zililenga kutumia mgomo huu kubadili sheria mbali mbali ikiwemo ya viwango vya mwendo wa magari ya abiria, viwango vya faini n.k., kazi ambayo ni ya Bunge.
  Awali waandaaji mgomo huo walishindwa kuwasilisha nakala ya hukumu ya dereva mwenzao waliyokuwa wanailalamikia, walitakiwa kufanya hivyo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni. Hii ilithibitisha kuwa walikuwa wakilalamikia kitu wasichokijua na ambacho hawajakisoma.
  Baada ya kushindwa kuwasilisha hukumu hiyo Serikali iliwashauri kuwa sheria zinaelekeza kuwa kama mtu/watu hawakubalina na hukumu iliyotolewa wana haki ya kukata rufaa kwa Mahakama ya juu kuzidi ile iliyotoa hukumu husika. Je, ni kweli viongozi walioandaa mgomo huu hawalijui hilo? Kama wanafahamu utaratibu wa kukata rufaa ni hatua zipi wanachukua kukata rufaa wanachama wao wanapohukumiwa?
  Baadhi ya madereva ambao ni wanachama wa UWAMATA na ambao walikuwa wakipinga kitendo cha wenzao wachache kutumia njia zisizokubalika (mabavu) kuchelewesha safari za abiria siku hiyo, walidai kuwa mgomo huu umepangwa na kutekelezwa na kikundi cha watu wanaojiita madereva kwa kuwa na leseni za udereva, lakini kutokana na kukosa maadili mema ya udereva, wamiliki wa mabasi wanashindwa kuwaamini na kuwapatia mabasi ya kusafirisha abiria.
  Wengi wa hao ndio wamekuwa wakihusika na ajali za mara kwa mara. Watu hao huingia na kushinda Kituo cha Ubungo kusubiri posho kutoka kwa madereva wanaosafiri. Walidai inapotokea dereva aliyeajiriwa kukataa kuendesha basi kutokana na ubovu, watu kutoka kikundi hiki haraka haraka hukubali kuendesha basi husika pasipo matengenezo yoyote, hivyo madereva waadilifu kuonekana wakaidi na wenye viburi mbele ya wamiliki wa mabasi.
  Walidai kutokana na kikundii hiki kuwa ni idadi kubwa ya madereva wasio kuwa na ajira imekuwa vigumu kwa madereva kudai nyongeza za mishahara na marupurupu mengine kutoka kwa wamiliki wa mabasi kutoka na kikundi hiki kuwa tayari kuchukua ajira za muda mfupi wakati madereva wanapodai nyongeza.
  Wadereva wengine waliohojiwa siku ya mgomo walidai kuwa kikundi hiki ndicho kinahusika na madereva kufungwa kutokana na kutegemea kuishi kutokana na michango ya madereva ambayo hutoa kwa ajili ya kuwasiadia wakati wa kesi mahakamani. Walidai kila dereva wa basi hutozwa Shilingi 1,000 na UWAMATA kwa kushirikiana na kikundi hiki kila siku.
  Michango hii ya madereva ndiyo inafanya kikundi kufurika kila siku stendi ya Ubungo. Cha ajabu madereva wa mabasi wakipata ajali hakuna msaada wowote wanaopatiwa na UWAMATA unaolingana na michango waliyotoa.
  Walidai kuwa kutokana na kesi mahakamani kuchukua muda mrefu madereva wengi wanaoshitakiwa hushindwa kuhudhuria mahakamani kutokana na kukosa fedha za kujikimu katika mikoa mbali mbali walikoshitakiwa. Kutokana na hali hii madereva huchukuliwa na mahakimu kuwa wanadharau mahakama na kupatiwa adhabu za vifungo. Laiti kama michango ya madereva ingefanya kazi inayotakiwa ya kuwapatia misaada ya kisheria walidai kuwa idadi ya madereva wanaofungwa ingepungua sana.

  Madereva hao wanasema ya kuwa mwanzoni mwa mwaka huu viongozi waliotayarisha mgomo wa wiki iliyopita walifanya mapinduzi ndani ya UWAMATA baada ya mwenyekiti wa sasa waliyemtaja kwa jina moja la Machevu kufukuzwa kutoka Chama cha Madereva Tanzania (TDA). Baada ya mapinduzi hayo madereva walipata imani kuwa sasa watapata misaada ya kisheria kutokana na michango wanayotoa kila siku. Lakini hali imendelea kuwa ile ile, kwa madereva kukosa misaada ya kisheria na kushindwa kuhudhuria mahakamani kwa kukosa fedha za kujikimu katika mikoa waliyofunguliwa mashataka.
  Walimtaja dereva mwenzao aitwaye Issa aliyekuwa akiendesha katika kampuni moja yenye basi la kwenda Tunduma aliyefikia hatua ya kushindwa kufika mahakamani na hivyo akahukumiwa kifungo. Baada ya Issa kufungwa uongozi ulioandaa mgomo huu ulipitisha daftari kwa ajili ya kuchangisha fedha za gharama za wakili ili kumkatia rufaa. Lakini walidai fedha hizo zilizochangishwa maalumu kwa rufaa ya Issa hazikufanya kazi hiyo na haijulikani hadi leo zimetumikaje?
  Madereva hao ambao wanapinga kuwepo kwa mgomo walidai kuwa ni kutokana na manung’uniko ya chini chini kuhusu kuliwa kwa fedha za rufaa ya dereva Issa, ndiyo maana wanahisi upande wa uongozi wa UWAMATA unaoshirikiana na kikundi cha chini ya mti kwa pamoja, waliamua kupotosha kwa makusudi hukumu ya dereva aliyehukumiwa kifungo mkoani Tabora. Madereva hao walidai kuwa hata dereva wa Tabora alikumbwa na ukata na kushindwa kumudu gharama za kuhudhuria mahakamani mara kadhaa, na wanaamini kuwa hali hiyo ndiyo iliyochangia ukali wa hukumu yake japokuwa si kwa kutumikia miaka 30 kama uongozi wa UWAMATA na kikundi cha chini ya mti unavyodai na kutaka umma wa Watanzania waamini hivyo.

  Ushauri wa bure kwa madereva ni kuwa wanajikaanga kwa mafuta yao wenyewe. Wanatakiwa kusimamisha michango ya shilingi 1,000 kila siku wanayotoa pale getini kwa kuwa hiyo ndiyo inayofuga kundi kubwa la watu wasio na ajira ambao wanawahujumu wasiweze kudai maslahi bora zaidi kutoka kwa matajiri wao.
  [​IMG]
   
Loading...