Kulikoni matumaini ya Zanzibar?/Raia Mwema, Julai 24, 2019

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
BARAZANI

Na Ahmed Rajab

MIAKA 55 tangu Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iunganishwe na Jamhuri ya Tanganyika kuunda Muungano wa Tanzania bado kuna utata mkubwa kuhusu muungano huo. Hili si geni. Wala halifichiki.

Wakati zilipoungana, Jamhuri hizo mbili zilikuwa tofauti kiitikadi. Tofauti hiyo iliashiriwa katika majina rasmi ya jamhuri hizo mbili. Tanganyika ikiitwa jamhuri tu lakini Zanzibar kwa kujiita “Jamhuri ya Watu” ilikuwa ikitaka itambuliwe kwa mengine yaliyoizidi jamhuri ya kawaida. Ikijigamba kuwa ni taifa lenye mrengo wa kisoshalisti.

Mrengo huo ndio uliokuwa msingi wa sera za Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kabla ya Rais Julius Nyerere wa Tanganyika kuanzisha Ujamaa 1967. Tanganyika ilikuwa ikifuata sera za kibepari na siku hizo hata Nyerere alikuwa kipenzi cha nchi za Magharibi.

Barani Afrika, tukiicha Zanzibar nchi pekee nyingine iliyokuwa na maneno “Jamhuri ya Watu” katika jina lake rasmi ilikuwa Algeria. Ziliibuka nyingine kama Angola, Congo-Brazzaville, Ethiopia na Msumbiji, lakini miaka kadhaa baadaye.

Mnamo 1964, Zanzibar ikijitofautisha kuwa ni taifa lenye kutaka kuleta usawa kwa wananchi wake wote. Na ni kweli kwamba miezi ya mwanzo baada ya Mapinduzi hapakuwa na mambo ya kijinga ya ubaguzi.

Wananchi wote walikuwa na fursa sawa za kujiendeleza na dola halikuwa likibagua kwa misingi ya kikabila au ya kidini. Watoto walipelekwa nchi za nje kwa masomo ya juu bila ya kujali kabila zao. Kwa wengi wa wakaazi wa Zanzibar huo ulikuwa wakati wa matumaini makubwa.

Katika miezi mitatu ya mwanzo serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ilikuwa mbioni kutunga miradi yake ya maendeleo yaliyokuwa na lengo la kuzinyanyua hali za maisha ya wananchi. Misaada au ahadi za misaada zilikuwa zikimiminika kutoka mataifa ya kisoshalisti yakiwemo China, Urussi na iliyokuwa Ujerumani ya Mashariki. Zanzibar pia ilikuwa ikisaka masoko mepya ya karafuu na mbata zake na kuanzisha maingiliano na nchi za Asia, zikiwa pamoja na Pakistani na Indonesia.

Salim Rashid aliyekuwa katibu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi anakumbuka jinsi serikali yao ilivyokuwa imejawa na matumaini ya kuifanya Zanzibar iwe mfano kwa nchi nyingine za Afrika ya Mashariki. Iliyokuwa Ujerumani ya Mashariki ilipeleka Zanzibar wataalamu na mastadi wa mambo ya uchumi kuisaidia Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kuandaa Mpango wake wa kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitatu.

Mpango huo ulitilia mkazo ukuzaji wa sekta ya kilimo, uvuvi na ujenzi wa miundombinu visiwani Unguja na Pemba.

Kwa vile wakati huo Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ilikuwa imesusiwa na nchi za Magharibi, Zanzibar ikitegemea kupata ruzuku na misaada isiyo na masharti kutoka nchi za Kikomunisti. Yote hayo yaliwafanya viongozi wa Zanzibar wawe na matumaini makubwa ya kuzidi kuvinyanyua visiwa vyao.

Ni matumaini hayo yaliyozitia hofu nchi za Magharibi, hususan Marekani na Uingereza. Hazikutaka Zanzibar iliyotangaza kwamba inafuata sera za kisoshalisti ifanikiwe na kuwa nchi ya kupigiwa mfano katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Ndio maana Marekani ikaanza kuisema Zanzibar kuwa ni “Cuba ya Afrika”. Nia yake ilikuwa kuzitia hofu nchi jirani ya Zanzibar ziione kuwa ni ya kikomunisti. Marekani ikiamini kwamba lau Zanzibar ingefanikiwa basi ingekuwa mfano mbaya kwa nchi jirani za Kiafrika.

Hofu hiyo pia iliipa Marekani kisingizio cha kuandaa mkakati wa kuisambaratisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar isiweze kufanikiwa kutekeleza malengo yake ya kuondosha matabaka ya kijamii kwa kujenga jamii ya usawa, isiyo na ubaguzi na iliyojitolea kuwanyanyua wakaazi wake.

Mambo yalianza kwenda kombo Zanzibar ilipopoteza dira. Iliipoteza ilipounganishwa na Tanganyika miezi minne baada ya Mapinduzi. Ule Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitatu ulitupiliwa mbali.

Si kwamba nia ya kuungana ilikuwa mbaya. Lakini Muungano uliingia nuksi kwa namna ulivyoasisiwa bila ya ridhaa ya wananchi wa Tanganyika na wa Zanzibar.

Pia Nyerere hakuwa na insafu aliposhauri pawepo huo Muungano. Nia yake ilikuwa nchi hizo mbili ziungane kila moja ikiwa na serikali yake na baadaye serikali ya Zanzibar iyayuke na pabaki serikali moja tu ya Muungano. Wazanzibari wanaiona dhana hiyo kuwa ni njama ya kuimeza nchi yao na kuigeuza iwe mkoa. Ni dhana inayowachochea Wazanzibari.

Nyerere alikuwa hodari kwa vile hakuwa na papara kutimiza lengo lake. Aliwavumilia Wazanzibari huku taratibu akiyadokoa mamlaka yao na kuyaingiza katika orodha ya yale yaitwayo “mambo ya Muungano”.

Kwa ufupi, katika kipindi cha miaka 55 Zanzibar iliyokuwa na mamlaka yake kamili ilipokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar hivi sasa imebaki kama kifuu. Haina lake inaloweza kulifanya ikiwa halitakiwi na serikali ya Tanganyika inayojivisha koti la serikali ya Muungano.

Miaka yote hii hajachomoza Rais yeyote wa Muungano aliyejitolea kwa dhati kuufanya Muungano wa Tanzania uonekana kuwa ni Muungano uliojengeka juu ya msingi wa usawa baina ya nchi mbili zilizokuwa huru na zilizowahi kuwa na mamlaka kamili.

Zanzibar yenyewe hivi ilivyo ni taifa lililodumaa. Haina maendeleo ya maana ambayo serikali inaweza kujivunia. Ilishangaza hivi karibuni kumsikia Rais wa Zanzibar , Dkt. Ali Mohamed Shein, akilalamika kwamba Zanzibar ikilingalishwa na jiji la Dar es Salaam iko nyuma sana hasa kwa miundombinu.

Bila ya kulitaja kwa jina Shein alililaumu Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kwa kuutangaza Mji Mkongwe kuwa Turathi ya Ulimwengu na hivyo kuuwekea masharti ya kuuzuia usiweze kujengwa upya. Hotuba aliyoitoa akiyataja manung’uniko yake kwa Zanzibar kutopata maendeleo imekuwa ikisambazwa siku mbili hizi na kuwashangaza wenye kuisikiliza.

Wanashangaa kumsikia mkuu wa serikali yenye dhamana ya kuipatia Zanzibar maendeleo akiwalaumu wengine kwa kasoro za utendaji wa serikali yake.

Shein si Mzanzibari pekee aliyetukumbusha ilipotumbukia Zanzibar katika maendeleo. Wapo wengine pia. Lakini wao wanaulaumu utawala wake na tawala alizozirithi. Zote zikiwa chini ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kinyume na Shein Wazanzibari hao wengine wamekuwa wakilenga ndipo wanapoulaumu uonevu unaofanyiwa Zanzibar na serikali ya Muungano pamoja na udhaifu wa serikali ya Shein katika kupigania maslahi ya Zanzibar.

Leo nitawataja wawili tu miongoni mwa Wazanzibari hao. Wa kwanza ni Juma Duni Haji (“Babu Duni”), naibu kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo. Na wa pili ni Salim Rashid, niliyekwishamdhukuru.

Hivi karibuni Duni alisema lililo wazi alipokuwa akitoa maoni yake kuhusu hotuba ya bajeti iliyosomwa kwenye Baraza la Wawakilishi na waziri wa fedha wa Zanzibar, Balozi Mohamed Ramia.

Katika hotuba yake Ramia alibaini kwamba Zanzibar imeshindwa kutekeleza miradi yake mitatu mikubwa baada ya kukwamishwa na Serikali ya Muungano. Miradi yenyewe ni uwanja wa ndege wa Zanzibar, bandari ya Mpigaduri na barabara ya Mkoani Chake Chake, Pemba.

Ramia ni kiongozi mwenye uweledi na uzoefu mkubwa katika mambo ya utawala yakiwa pamoja na shughuli za Muungano. Kwa hivyo, anapotamka kauli rasmi hawi anaropokwa. Kwa mujibu wa Ramia, miradi hiyo haikuanza kwa sababu ikihitaji kusainiwa na serikali ya Muungano lakini serikali hiyo ilikataa kusaini.

Huo ndio mtindo wa serikali ya Muungano. Mara nyingi imekuwa ikijifanyia mambo kana kwamba Zanzibar inapaswa kudhibitiwa au ni “koloni” la Tanganyika.

Kuhusu kadhia aliyoitaja Ramia, Duni alisema haya: “Sasa ni nchi gani inataka kutekeleza miradi yake mpaka ruhusa itoke nchi nyingine ndio itekelezwe? Jee, wananchi wa Zanzibar mna nchi na serikali?”

Hayo ni maswali mazito aliyoyauliza Duni. Ni maswali yenye kuulizwa na Wazanzibari wengi.

Duni amewataka Wazanzibari wazidi kuzindukana na kuwa wamoja kupigania maslahi yao. Akisema kwamba “saa ya ukombozi” ni sasa, Duni amewataka Wazanzibari wajikwamue kutoka utumwa wa kiakili.

Wito wa kuwataka Wazanzibari wazidi kuungana kudai haki zao pia umetolewa na Salim Rashid. Kuna kanda ya video ambayo kama sikosei ilitolewa mwanzo kama miaka mitano iliyopita na inayosambazwa tena sasa mitandaoni. Ni yake Rashid akieleza yaliyoikumba Zanzibar tangu uasisiwe Muungano na yaliyovifanya visiwa hivyo viwe, kama asemavyo, “taifa la njaa na umasikini”.

Anasema kila sekta visiwani humo imeathirika. Zanzibar iliyokuwa ya kwanza duniani katika usafirishaji karafuu sasa imepitwa na Singapore. Hakuna kinachoendelea bila ya ufisadi ilimradi Zanzibar imerudi nyuma kila upande, katika uchumi, elimu, afya na katika ustawi wa kijamii.

Akisema kwamba Shein hana uhalali wa kusema kwamba anaongoza serikali ya umoja wa kitaifa kwa sababu haongozi serikali ya aina hiyo na hata hapo alipokuwa nayo serikali hiyo hakuwa akimshirikisha Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad, katika maamuzi makuu ya serikali.

Rashid amemshauri Shein aitishe kura ya maoni kuwauliza Wazanzibari iwapo wanataka Zanzibar iwe dola huru yenye mamlaka yake kamili au iendelee na Muungano kama ulivyo sasa. Anaamini kwamba Muungano ni sababu ya mapungufu yote tunayoyashuhudia Zanzibar.

Iwapo serikali itashindwa kuendesha kura hiyo ya maoni basi Wazanzibari anaoshirikiana nao wanapanga kwenda Umoja wa Mataifa na kudai Zanzibar irejeshewe kiti chake katika Umoja huo. Hamu ya Wazanzibari, anasema, ni kutaka nchi yao iwe na mamlaka kamili ili iweze kuendelea.

Rashid ametoa wito muhimu kwa Wazanzibari akisema: “Tusikubali kubaguliwa kwa misingi yoyote ya kisiasa, kikabila au kidini.”



Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab
 
Mkuu, kuhusu siasa za Zanzibar wakulaumiwa ni Wazanzibari wenyewe, katiba ya Zanzibar inaruhusu mambo mengi lakini kwa sababu ya Woga wa wanasiasa wa Zanzibar ndio inaifanya Zanzibar iwe hapo ilipo..

Wanasiasa wa Zanzibar ni wachumia tumbo wanajali sana masilahi yao kuliko masilahi ya Taifa la Zanzibar..

Wanasiasa wa Zanzibar wajazwa Propaganda za "Mwarabu atarudi" na zimewangia kweli kweli..
 
Back
Top Bottom