Kukata tamaa:je,ni hulka ya watanzania?

Technician

JF-Expert Member
Mar 30, 2010
841
222
“Sitaenda kwenye maandamano. Hata tukiandamana hakuna kitakachobadilika.” Iliuwa kauli ya kwanza ya Mtanzania mmoja. Mwingine naye, “Nendeni tu kwenye mkutano. Mtakalolizungumza lolote kwangu ni sawa tu. Hata hivyo hiyo mikutano haina maana yoyote.” Sasa iliyonishangaza na kunikera zaidi ilikuwa hii:

“Hii ni Tanzania bwana. Mtapiga kelele weeee ila hakuna kitakachofanyika. Kujihusisha kwenye mambo ya siasa ni kazi bure. Wewe fanya mambo yako. Tafuta chakula cha familia yako. Jitafutie maendeleo yako mwenyewe. Achana na mambo ya kitaifa. Acha kabisa kuongelea siasa za nchi.”

Hizi ni kauli za watu waliokata tamaa. Ni kauli za Watanzania wengi: vijana na hata wazee. Ni watu waliochoka. Mbele yao wanaona bahari na nyuma yao majeshi ya Farao. Wamefika mwisho. Hawana tumaini. Ila kauli hizi si za kupuuza hata kidogo. Hizi ni kauli-sumu kwa taifa ambalo linataka kupiga hatua ya kimaendeleo.

Ni kauli zenye nia ya kuzima dhamira za watu ambao wangependa kudai haki zao. Ni kauli ambazo viongozi wazembe, wavivu na wabadhirifu wangependa kuzisikia. Kibaya zaidi: hizi ni kauli ambazo zaweza kuleta kizazi cha watu waoga, wasiopenda kuhoji nchi yao inaendeshwaje. Ni mawazo-mgando. Mawazo hatari!

Mtanzania yeyote anayetoa kauli za hivyo usidhani kuna siku atamkemea mtoto wake asijihusishe na wizi wa mali za umma. Na wala sidhani kama watoto wa mtu mwenye mawazo kama haya wanaweza kufikiri kwamba wizi wa mali za umma ni jambo baya. Tutaleta Tanzania kizazi kisicho na maadili kwa sababu kizazi chetu kimekuwa ni chenye kupuuzia.

Shime Watanzania, tuamke! Zi wapi nyimbo zetu za kizalendo? Zi wapi kauli zetu za ukombozi? U wapi ujasiri wetu wa kale? Ni nini kimetupata?

SOURCE:Kukata tamaa: Je, ni hulka ya Watanzania? « Jicho la Kiongozi (The Leader's Eye) Tanzania
 
Ogopa watu waliokata tamaa, maana siku wakiamua wataangamiza kila kitu kwa sababu hawana cha kupoteza.
 
Back
Top Bottom