Kuhesabu na Kujumlisha Kura Siku ya Uchaguzi

Mwakaboko King

JF-Expert Member
Apr 22, 2015
1,099
207
Ndugu wanajamvi ni vyema tukaendelea kuelimishana juu ya mambo yanayofanyika Siku ya Uchaguzi nchini Tanzania na hapa nazungumzia Uchaguzi Mkuu au Uchaguzi mdogo. Fuatana nami katika Mada hii ya utaratibu unaotumika kuhesabu na Kujumlisha Kura Siku ya Uchaguzi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 70A(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kura za Rais, Mbunge na Diwani zitahesabiwa katika kituo kilichotumika kupigia Kura.

Wakala wa kuhesabu Kura

Kwa kuzingatia kifungu cha 70 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 pamoja na kifungu cha 71 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kila Wakala wa chama au Mgombea aliyeteuliwa kuwa Wakala wa Upigaji Kura anaweza kuwa Wakala wa kuhesabu kura, au chama au mgombea wanaweza kuleta Wakala wa kuhesabu Kura na aliyekuwepo atapaswa kumpisha aliyeletwa kusimamia zoezi la kuhesabu Kura.

Wakala huyu atapaswa kula kiapo cha kutunza Siri.

Wakala au Mgombea Kuridhika au kutoridhika wakati wa kuhesabu Kura Kituoni

Kanuni ya 59 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015 na kanuni ya 53 ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani) za mwaka 2015, Wakala wa kuhesabu Kura au Mgombea atajaza Fomu Na. 16 kuonesha kuridhika au kutoridhika na utaratibu wa kuhesabu Kura.

Taratibu za kuhesabu Kura

Baada ya Upigaji Kura kukamilika na taratibu za kufunga Kituo kukamilika, Kituo cha Kupigia Kura hubadilika na kuwa Kituo cha Kuhesabu Kura. Kura za Rais huanza kuhesabiwa mwanzo, zikifuata Kura za Wabunge na mwisho Kura za Madiwani.

Kifungu cha 73 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 70B(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 kinaeleza kwamba Msimamizi Msaidizi wa kituo kabla hajaanza kuhesabu Kura mbele ya wanaostahili kuwepo kwenye Kituo atafanya yafuatayo:

(i) Atahakiki na kuandika idadi ya wapiga Kura wote waliopiga Kura katika Kituo husika.

(ii) Atahesabu na kuandika idadi ya karatasi za kura zote ambazo hazikutumika pamoja na zile zilizoharibika na kuzifunga katika bahasha maalum.

(iii) Atakagua lakiri iliyofungwa katika masanduku ya Kura ili kuhakikisha kama imefunguliwa au kuchezewa

(iv) Atafungua lakiri

(v) Atafungua sanduku la kupigia Kura.

Baada ya hapo atafanya yafuatayo mbele ya watu wote wanaoruhusiwa kuwepo ndani ya kituo cha kuhesabia Kura kwa kuanzia na Sanduku lenye Kura za Rais, kisha Sanduku lenye Kura za Mbunge na kwa kumalizia Sanduku lenye Kura za Diwani:

(i) Atamimina Kura zote juu ya meza na kuanza kuhesabu Kura moja baada ya nyingine kwa sauti inayosikika na kila mtu.

(ii) Iwapo zitakutwa Kura zisizokuwa za sanduku hilo atasisema na kuziweka katika sanduku husika.

(iii) Ataandika katika Daftari la kuandikia idadi ya Kura zote zilizopatikana katika kila Sanduku la Kura.

(iv) Baada ya hapo zoezi la kuhesabu Kura litaanza kwa sanduku la Kura za Rais, kisha Sanduku lenye Kura za Mbunge na kumalizia Sanduku lenye Kura za Diwani, kufanya yafuatayo;

(v) Atakunjua Kura moja baada ya nyingine kwa kuonesha upande wa juu wa picha za Wagombea na kutangaza kwa sauti inayosikika na kila mtu aliyepo ndani ya Kituo akitaja Mgombea aliyepigiwa Kura. Aidha, huonesha Karatasi ya Kura ambayo haina alama yoyote au iliyoharibika.

(vi) Atapanga karatasi za Kura kwa mafungu tofauti kwa kila Mgombea na upande wa picha ukiwa juu;

(vii) Atahesabu kwa sauti inayosikika na kila mtu na kuandika idadi ya Kura kwa kila fungu yaani Kura alizopata kila Mgombea, Kura zilizokataliwa, na Kura zenye mgogoro au Kura zilizoharibika.

Alama zinazokubaliwa katika Karatasi ya Kura

Kwa mujibu wa kipengele cha 9.17.1 cha Maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa Wasimamizi wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015, alama ya Vema ( √ ) ndiyo inayokubalika.

Kukataliwa kwa Kura

Kwa mujibu wa kifungu cha 74 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 pamoja na kifungu cha 77 cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292; karatasi za Kura zitachukuliwa kuwa zimekataliwa iwapo:

(i) Hazina mhuri wa kituo.

(ii) Itakuwa na kitu au alama yoyote yenye kumtambulisha mpiga Kura.

(iii) Haijawekwa alama zinazotambuliwa kuwa ni halali.

(iv) Kura yoyote itakayopigwa kwa mgombea aliyejitoa kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi.

(v) Alama imewekwa kwa wagombea zaidi ya mmoja.

(vi) Haina alama yoyote.

Ombi la Kurudiwa kuhesabiwa Kura

Kifungu cha 78 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na 79 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 vinatoa fursa kwa Mgombea au Wakala wa kuhesabu Kura waliokuwepo wakati wa kuesabu Kura katika kituo, kuomba Msimamizi wa Kituo kurudia kuhesabu kura mara moja au mara mbili na Msimamizi wa Kituo anaweza kukataa kurudia kuhesabu Kura kwa mara ya tatu iwapo matokeo ya kurudiwa mara mbili za mwisho yanalingana.

Uamuzi wa Uhalali wa Kura Kituoni

Kwa mujibu wa Kifungu cha 79 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, uamuzi wa mwisho kuhusu uhalali wa Kura itakayohesabiwa ni wa Msimamizi wa Kituo.

Iwapo Msimamzi wa kituo ataridhika kuwa Kura imeharibika na haiwezi kuhesabiwa ataikataa na haitahesabiwa na ataandika nyuma ya Kura hiyo “IMEKATALIWA”.

Endapo uamuzi wa kuikataa Kura hiyo umepingwa, Msimamizi wa Kituo ataandika nyuma ya Kura hiyo “UAMUZI UMEPINGWA NA” atataja jina la aliyepinga na Chama chake.


Nitaendelea na Mada hii, Nawatakia Siku njema.
 
Back
Top Bottom