Kufuatia kibano cha DC (Igunga): Wabunge wa CHADEMA wakamatwa


• DK. SLAA, MBOWE KUZUNGUKA NCHI NZIMA

Na Waandishi wetu

WABUNGE wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Susan Kiwanga (Viti Maalum) na Sylivester Kasulumbai (Maswa Mashariki), wamehojiwa na Jeshi la Polisi Mkoani Tabora wakituhumiwa kushiriki kumvamia na kumpiga Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Fatma Kimario.


Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Igunga, jana, Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Makao Makuu ya Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi Issaya Mungulu, alisema wabunge hao walikamatwa na kuhojiwa kwa saa kadhaa kabla ya kuachiwa.

Akizungumzia kile kilichotokea, Mngulu alisema mkuu huyo wa wilaya alikwenda katika kijiji cha Isakamaliwa kufanya mkutano wa ndani na watendaji wa kijiji hali iliyowafanya wafuasi na viongozi wa CHADEMA kuchukizwa kwa madai kuwa wameingiliwa.


“Mkutano wa CHADEMA katika kijiji cha Isakamaliwa ulikuwa ufanyike kati ya saa nne na saa sita. Kikao cha mkuu wa wilaya kilifanyika kati ya saa 7:30 na saa 9:00 alasiri muda ambao CHADEMA hawakuwa na mkutano,” alisema.


Hata hivyo, kamanda huyo wa polisi alikiri kuwepo kwa malalamiko ya CHADEMA kuhusiana na kuingiliwa katika maeneo waliyotengewa kufanya kampeni na ukiukwaji wa maadili unaodaiwa kufanywa na mkuu huyo wa wilaya lakini akadai msemaji wa mambo hayo ni msimamizi wa maadili ambaye ni mkurugenzi wa uchaguzi.


Aidha alikiri kwamba askari wake walikuta hali ya amani na utulivu katika kijiji hicho, ndipo walipolazimika kuanza upelelezi kujua ukweli wa tukio hilo.


Aliongeza kuwa tuhuma zinazochunguzwa dhidi ya wabunge hao na wafuasi wengine watatu wa CHADEMA, ni kuvamia kikao cha mkuu wa wilaya.


Taarifa hizo zinadai kwamba katika tukio hilo mkuu wa wilaya alivuliwa hijabu, viatu, kukatiwa mkufu ambao thamani yake haijajulikana.


“Anadai kuwa simu yake ya mkononi aina ya Samsung yenye thamani ya sh 400,000 ilipotea na kumtukana matusi ya nguoni,” alisema na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi lilipokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa Ofisa Tawala wa Wilaya, Sumera Manoti.


Taarifa zimebainisha kuwa mkuu huyo wa wilaya amefungua jalada la shambulio la aibu namba IR/1115/2011, wakati CHADEMA wamefungua jalada namba IR/1115/2011 linalohusu kuingilia mkutano wa kampeni kwa mujibu wa ratiba ya msimamizi wa uchaguzi. Kwa sasa jeshi hilo linaendelea kukusanya ushahidi kuhusiana na kesi hizo.


Hata hivyo, Kamanda Mngulu alitoa wito kwa vyama, viongozi, wanachama, wapenzi na wafuasi wa vyama vya siasa kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi hususan kipindi hiki cha uchaguzi.


Juzi mkuu wa wilaya hiyo akiwa katika kijiji cha Isakamaliwa, tarafa ya Igunga alivamiwa na viongozi, wafuasi na mashabiki wa CHADEMA muda mfupi baada ya kumaliza kikao cha ndani na watendaji wa vijiji.


Mbowe, Dk Slaa kuzunguka nchi nzima

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema kuanzia sasa yeye na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, watazunguka nchi nzima kuwahamasisha watu waikatae CCM na kuichagua CHADEMA.

Kauli hiyo aliitoa jana wilayani Sikongo, mkoani Tabora, alipofanya mikutano ya hadhara pamoja na kuzindua kampeni za udiwani wa kata ya Kisanga.


Dk. Slaa alisema binafsi ameamua kuacha kukaa ofisini baada ya kutembelea maeneo mengi ya nchi na kuona watu wanavyoishi kwa umaskini ilhali wamezungukwa na rasilimali lukuki.


“Moto tunaouwasha sasa CCM hawajawahi kuuona. Sitakaa ofisini mpaka kieleweke, taifa linahitaji ukombozi na sisi tuko tayari kuwakomboa wananchi,” alisema.


Dk. Slaa aliongeza kuwa Watanzania wako katika hali mbaya kwa sababu CCM imeshindwa kuzitumia rasilimali zilizopo kwa manufaa ya walio wengi.


Alisema umaskini unaowakabili wananchi hivi sasa si laana kutoka kwa Mungu bali ni maamuzi mabovu ya wananchi kuwachagua viongozi wenye kuweka mbele ulaji na maslahi binafsi.


“Tumebarikiwa rasilimali lukuki lakini wananchi tunapumulia mashine kwa umaskini, watu wetu wanaishi kwenye nyumba za tembe, hawajui bati wala umeme, hili halikubaliki hata kidogo,” alisema.


Dk. Slaa alisema kama Watanzania wanataka ukombozi ni lazima waache woga wa kuwachagua viongozi wa CCM ambao hawana uchungu wa matatizo ya wananchi.


Naye mgombea udiwani wa kata ya Kisanga, Mgombozi Ntewi (CHADEMA), alisema mabadiliko ya kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa hayawezi kufanyika kama wananchi wataendelea kuwa waoga.


Alisema iwapo atachaguliwa kuwa diwani wa kata hiyo atahakikisha michango yote inayotolewa na wananchi inatumika kwa kazi zinazotakiwa.


“Maendeleo makubwa tutayapata iwapo mtanichagua kuwa diwani wenu; viongozi wetu wanatafuna fedha za miradi kwa manufaa yao, mimi nitawabana vilivyo,” alisema.


 
CHADEMA wasivyopenda hijab! Nadhani nayo ilichangia kwa kiasi kikubwa hilo sakata! Hawa wahuni wamepoteza imani hata ile ndogo tuliyokuwa nayo juu yao!
 
Mama anapambania ukuu wa mkoa,alishauriwa vibaya na nape kwa lengo la kuvuluga mkutano wa cdm mwisho wa siku kavulugwa yeye,hizo ndizo gharama za vyeo vya kupeana.
 
Hainingiii akilini hata kidogo kuwa mkuu wa wilaya hakutambua kama kuna mkutano hapo kijijini. na hata kama hakutambua je! alipofika kwa nini hakufahamishwa na hao aliokuwa nao?
 
Duu, jimama anatia huruma!
huyu mama sijawahi kuona nywele zakejifunika kichwa siku zote kumvua mwanamke wa imani hiyo hijab ni udhalilishaji wa hali ya juu!nawashangaa wanawake wanaoshangilia udhalilishaji huo!
 
Polisi wameshikwa pabaya kweli. Wao wanafahamu fika kuwa mama kachemsha, ila kwa kuwa ndiyo kishavuliwa nguo tena, wasipoonekana wanabweka na kufyata mkia mwenye mbwa atawashughulikia wao mbwa kwa kuwanyima chakula. Kinachoendelea ni sanaa ya kuonesha kuwa wanafanya kazi. CCM wanaviweka vyombo vya dola katika wakati mgumu sana na siasa zao za kutaka kubebwa hata kama hawabebeki.
 
CHADEMA wasivyopenda hijab! Nadhani nayo ilichangia kwa kiasi kikubwa hilo sakata! Hawa wahuni wamepoteza imani hata ile ndogo tuliyokuwa nayo juu yao!

Umetumwa na magamba, kuja kueneza propaganda za udini hapa JF? SHAME ON YOU.
 
Tuwe wakweli chadema ni wavunjaji wa sheria, hapa wamefanya kosa kubwa kuchukua sheria mkononi na kumdharirisha mteule wa rais ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani
 
Hainingiii akilini hata kidogo kuwa mkuu wa wilaya hakutambua kama kuna mkutano hapo kijijini. na hata kama hakutambua je! alipofika kwa nini hakufahamishwa na hao aliokuwa nao?

Hata watendaji wa kijiji walikuwa pamoja na huyu mama.
 
SERIKALI imesikitishwa na udhalilishaji uliofanywa na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Fatma Kimario juzi.

Imesema kwa kuwa nchi inafuata utawala wa sheria, inaviachia vyombo vya Dola vifanye uchunguzi wake.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika, alipozungumza na gazeti hili akiwa Newala mkoani
Mtwara.

“Serikali imesikitishwa na udhalilishaji uliofanywa kwa DC wa Igunga. Nchi ina taratibu, kanuni na sheria kwa hiyo unaviachia vyombo vya Dola kufanya kazi yake. “Lakini tumesikitishwa na tukio lile kwa sababu DC alikuwa tayari kusema nao, alikuwa eneo lake la utawala akifanya kazi. Kwa nini wamkamate na kumtoa nje kwa udhalilishaji ule,” alisema Mkuchika.

Alisema haikuwa vyema kwa wahusika kufanya udhalilishaji huo hasa baada ya Mkuu huyo wa wilaya kuwa tayari kuzungumza nao; hivyo wangeweza kuzungumza naye ofisini katika mazingira ya ustaarabu.

DC Kimario alifanyiwa vurugu na vijana wa Chadema juzi akiwa katika shughuli zake za kikazi.

Vijana hao walidai DC alikuwa akifanya kampeni za kisiasa katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Igunga utakaofanyika Oktoba 2, mwaka huu.

Katika taarifa yake jana, Polisi ilisema DC huyo amefanyiwa shambulio la kudhalilisha kinyume cha maadili, ikiwemo kuvuliwa vazi lake la hijab ambalo humsitiri mwanamke wa Kiislamu hasa kichwani.

Akizungumza jana wilayani Igunga, Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimini wa Polisi, Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya Mngulu, alisema mbali na kuvuliwa hijab, pia DC alidai alivuliwa viatu na kukatiwa mkufu.

"Pia simu yake ya mkononi aina ya Samsung ilipotea na alitukanwa matusi ya nguoni ya kumdhalilisha …(hatuwezi kuyaandika hapa)," alisema Mngulu akielezea madai hayo ya DC Kimario.

Alisema wakati Mkuu huyo wa Wilaya akifanyiwa vitendo hivyo na vijana hao wa Chadema, Ofisa Tawala wa Wilaya ya Igunga, Sunera Manoti, alikwenda Polisi kutoa taarifa.

Hata hivyo, baada ya Polisi kupata taarifa hiyo, kwa mujibu wa Mngulu, walikwenda eneo la tukio na kukuta hali ni shwari na kuanza upelelezi baada ya majalada ya tuhuma; la kwanza la DC akilalamika kufanyiwa shambulio la aibu na la pili la Chadema wakilalamikia kuingiliwa katika mkutano wa kampeni.

Kwa mujibu wa taarifa za Chadema, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Kiwanga, Mbunge wa Maswa Mashariki, Kasulumba Sylvester pamoja na shabiki wao ambaye jina lake halikupatikana waliitwa Polisi na kuhojiwa saa moja na kuachiwa kwa dhamana.

Madai ya Chadema Awali, kabla ya Polisi kuzungumzia hilo, Chadema iliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuelezea makosa 15 ya DC huyo, likiwemo la kuitisha mkutano waliodai kuwa ni wa hadhara na kinyume cha sheria.

Akifafanua madai hayo, Mkurugenzi wa Chadema wa Oganaizesheni na Mafunzo, Benson Singo, alidai kuwa mtu ye yote akitaka kufanya mkutano, lazima atoe taarifa kwa Polisi na kwa kuwa polisi walikuwa wakifahamu kuwepo kwa mkutano wa Chadema, wasingemruhusu DC kufanya wa kwake.

Hata hivyo, Mngulu alisema DC Kimario alikuwa katika kikao cha ndani na sio mkutano wa hadhara kama Chadema walivyodai, ambacho kisingehitilafiana na mkutano huo wa Chadema, lakini hata muda wa tukio la kushambuliwa Mkuu huyo wa Wilaya na mkutano wa Chadema vilikuwa tofauti.

Kwa mujibu wa ratiba ya mikutano ya hadhara ya kampeni iliyooneshwa na Mngulu, Chadema ilipaswa kufanya mkutano wao wa hadhara katika eneo hilo la Kijiji cha Isakamaliwa saa 4 asubuhi hadi saa 6 mchana na tukio hilo, lilitokea kati ya saa 8:30 na saa 9.

Mngulu alisema hata polisi walikwenda eneo la mkutano huo kulinda amani saa 4 mpaka saa 6, lakini waliondoka kwa kuwa Chadema hawakwenda katika mkutano huo kwa mujibu wa ratiba.

Chadema pia walilalamika kuwa katika kikao hicho, DC huyo alikusanya na kujadili barua za maombi ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura na waelekezaji wa vituo kinyume cha sheria.

Hata hivyo, DC Kimario alipozungumza na waandishi na kuhojiwa kuhusu kukutwa na baadhi ya barua za maombi ya wasimamizi wa vituo vya kupiga kura, alisema alipewa na wasimamizi wa uchaguzi vijijini ili awasaidie kuzipeleka kwa msimamizi wa uchaguzi.

DC katika maelezo hayo, alisema anajua Chadema watasema kuwa alikuwa na hizo barua, lakini kwa maelezo yake ni kwamba yeye alitoa msaada tu wa kuzifikisha kwa msimamizi wa uchaguzi.

Waandishi wagawanyika Katika tukio lingine, waandishi wa habari waliokutana Kituo cha Polisi muda mfupi baada ya kumalizika kikao cha Chadema na waandishi, waligawanyika, baadhi wakimtuhumu DC kuwa ndiye mwenye makosa; wengine wakiituhumu Chadema ndiyo chenye makosa.

Waliomtuhumu DC Kimario kuwa ndiye mwenye makosa, walidai ameitisha mkutano huo kinyume cha sheria na walipopewa sheria hiyo na kutakiwa kuisoma, walibadilika huku wakisahihishana kuwa, hakukiuka sheria, bali maadili ya uchaguzi.

Waliokuwa wakituhumu kuwa Chadema ina makosa; walitaka kujua Polisi imechukua hatua gani; kama inawashikilia watuhumiwa ni wangapi, akina nani na lini watapelekwa mahakamani.

Akijibu hoja hizo, Mngulu alisema suala la kukiuka maadili ya uchaguzi ni la Msimamizi wa Uchaguzi, Protas Magayane, lakini suala la shambulio ni la Polisi.

Alisema mpaka sasa wameshawahoji watu watatu, lakini akakataa kuwataja majina kwa maelezo kuwa uchunguzi bado unaendelea. Hata hivyo katika mkutano na waandishi wa habari na Chadema, Mkurugenzi wa Chadema wa Oganaizesheni na Mafunzo, Singo alisema waliohojiwa ni pamoja na wabunge hao wa Chadema.

Gazeti hili liliwasiliana na Msimamizi wa Uchaguzi, Magayane kwa simu ambaye alijibu kuwa yupo Dar es Salaam akishughulikia picha za wagombea.

Kampeni za Uchaguzi Mdogo wa Igunga tayari zimekumbwa na matukio ya vurugu huku yakihusishwa na Chadema ikiwemo mtu mmoja kumwagiwa tindikali na wengine kukatwa mapanga.

GAZETI LA HABARI LEO, Septemba 17, 2011
 
Tuwe wakweli chadema ni wavunjaji wa sheria, hapa wamefanya kosa kubwa kuchukua sheria mkononi na kumdharirisha mteule wa rais ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa ccm, na si usalama wa wananchi, ambae hajui kuna nini kinaendelea katika wilaya yake? na kwa taharifa yako hakuna sheria iliyovunjwa.
 
Lakini mkuu wa Wilaya ni boss wa mapolisi kama sikosei.!!
Kuna haki hapo kweli?
 
Wamezoea kuvuruga uchaguzi hawa watendaji wa serikali halafu kutupia lawama vyama vya upinzani,hiyo ndo dawa yao! Igunga songeni mbele
 
Taarifa zimebainisha kuwa mkuu huyo wa wilaya amefungua jalada la shambulio la aibu namba IR/1115/2011, wakati CHADEMA wamefungua jalada namba IR/1115/2011 linalohusu kuingilia mkutano wa kampeni kwa mujibu wa ratiba ya msimamizi wa uchaguzi. Kwa sasa jeshi hilo linaendelea kukusanya ushahidi kuhusiana na kesi hizo. Hata hivyo, Kamanda Mngulu alitoa wito kwa vyama, viongozi, wanachama, wapenzi na wafuasi wa vyama vya siasa kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi hususan kipindi hiki cha uchaguzi.


Tanzania daima

haiwezekani kesi mbili zikawa na IR-Inestigation Register zinazofanana. rejea taarifa zako
 
Lakini mkuu wa Wilaya ni boss wa mapolisi kama sikosei.!!
Kuna haki hapo kweli?

DC ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wakati OCD ni mjumbe. Hata hivyo, DC ni ofisi ya Rais hivyo OCD akipewa amri, sharti aitekeleze kwani kukataa anaweza akachongewa kunyang'anywa madaraka yake.

Ndo maana tunatakiwa kupambana kuzibiti nguvu ya wanasiasa kuwa na power kikatiba ya kuteua watendaji kwani mwisho wa siku watafanya siasa kinyume na sheria. na huwezi zuia DC au RC asifanye siasa kwani sifa yao namba moja ni kuwa makada wazuri wa CCM
 
Hili nalo litapita. Baada ya uchaguzi huu hatutasikia tena habari ya dc kudhalilishwa na kesi zitafia polisi.

Sikumbuki kama matukio kama haya huwa yanapelekwa mahakamani, polisi wenyewe tu ndo wanajigeuza kuwa mahakama na kutoa hukumu!
 
Nami nashangaa namba za majalada waliofungulia zote ni zinafanana, sijui ni typing error ama lah!
 
Mpanda hila huvuna Aibu ndo yaliyompata huyo mama. Pole zake alikuwa anatetea nafasi ili asije sahaulika kwenye list ya wakuu wa wilaya wapya.
 
yaani bado najiuliza ,ina maana mkuu wa wilaya hakwenda mkutanoni hata na afisa usalama wa wilaya?basi huo mkutano ulikuwa wa kimagumashi acha wamtie adabu kwa sababu hakuheshimu cheo chake in the first place.



9-17-2011 7-51-25 AM.jpg


9-17-2011 7-54-22 AM.jpg


9-17-2011 7-52-29 AM.jpg







9-17-2011 7-51-54 AM.jpg


Hipo kazi,mtoto kaiga matendo ya baba nani,ananguvu zaidi ni mtoto au ni baba ambae ameona mengi lakini hana nguvu ya kupambana na mahitaji na mbinu za kisasa.
 

Attachments

  • 9-17-2011 7-52-52 AM.jpg
    9-17-2011 7-52-52 AM.jpg
    38.5 KB · Views: 30
Back
Top Bottom