Kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Barubaru, Jul 20, 2009.

 1. Barubaru

  Barubaru JF-Expert Member

  #1
  Jul 20, 2009
  Joined: Apr 6, 2009
  Messages: 7,162
  Likes Received: 27
  Trophy Points: 0
  Hili ni suala nimekuwa najiuliza sana huko Tanzania. Tunaelewa kuwa Mwaka huu mwezi Oct kuna chaguzi za Serikali za mitaa yaani kuchagua wenyeviti wa Serikali za mitaa na wajumbe wao.

  naona kuwa mpaka sasa hakuna msisimko wowote wa maandalizi kwa vyama vya siasa na hata Serikali kijumla kama maandalizi ya chini chini aliyoanza kwa uchaguzi mkuu mwakani october.

  Ukisoma Katiba ya Tanzania , Ibara ya 146 (1) inazungumzia madhumuni ya kuepo ka serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi.

  katiba inazungumzia vizuri sana umuhimu wa kuimarisha demokrasia hususan katika ngazi za mitaa na kuelekea kwenye serikali kuu.

  nauliza kwanini chaguzi zake hazina mashamsham?

  Nitapembua kutoka kwenye katiba ya tanzania umuhimu na uhalali wa Serikali za mitaa ukilinganisha na serikali kuu.

  Nasriyah Saleh Al-Nahdi.
   
 2. S

  S. S. Phares JF-Expert Member

  #2
  Jul 20, 2009
  Joined: Nov 27, 2006
  Messages: 2,141
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0

  Mkuu, hizi chaguzi ni muhimu sana. Tatizo liko pale pale, wanachi hawana mwamko wa kuchagua viongozi bora.

  Migogoro mingi ya arthi inachangiwa sana na tabia ya kula rushwa ya viongozi wa mitaa.
   
 3. Sipo

  Sipo JF-Expert Member

  #3
  Jul 20, 2009
  Joined: Jul 25, 2008
  Messages: 2,146
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 0
  Ni kweli kuwa chaguzi za serikali za mitaa ni muhimu sana kwenye maendeleo ya demokrasia na maendeleo ya nchi yetu. Lakini kumekuwa na tatizo la vyama vyetu kutotilia maanani uchaguzi huu. Lakini mwisho wa siku utakuta mwisho wa siku wanaishia kushindwa na hii inawaondolea ile bases ya kushinda hata ule uchaguzi wa Rais na Wabunge.

  Kimsingi ni kwamba huu uchaguzi umekuwa dominated sana na chama cha Mapinduzi (CCM), jaribu kupitia matokea ya nyuma. Na nafikiri hapa ndio vyama vya upinzani ndio vinapokosea kwa sababu haviwezi kupata wabunge wengi wakati huku chini wengi ya viongozi ni kutoka chama cha CCM.

  Na ilivyo kwa Tanzania ni kwamba CCM ina nguvu kubwa sana katika maeneo ya vijijini kuliko hata mijini. Kwa hyo ni wakati sasa wa vyama vya siasa kuanza kujijenga kwa kuwa na wenyeviti wengi wa vijiji na mitaa ili kujenga bases ya kuwa na wabunge wengi kwenye uchaguzi wa 2010. Wasipoweza kufanya haya ni ukweli ulio dhahiri kuwa kuwa na wabunge wengi kutoka kambi ya upinzani hapo 2010 ni ndoto za abunuwasi.
   
 4. I

  Interested Observer JF-Expert Member

  #4
  Jul 20, 2009
  Joined: Mar 27, 2006
  Messages: 1,400
  Likes Received: 432
  Trophy Points: 180
  MITAA hakuna Pesa
  SERIKALI KUU Ndiko kwenye pesa
  We go where money is!!!
   
 5. M

  Mfumwa JF-Expert Member

  #5
  Jul 20, 2009
  Joined: Aug 29, 2008
  Messages: 1,456
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135
  Hizi chaguzi ni muhimu, manake mipango ya Serikali za mitaa husimamiwa na Madiwani. Lakini vyama vinajikita zaidi katika Ubunge kutokana na mengineyo ni kwa ajili ya kupata Ruzuku. Ingekuwa pia uwingi wa Madiwani nk unaongeza ruzuku ungeona msisimko katika hizi chaguzi, manake vyama vingewekeza huko kama katika Ubunge.
   
 6. H

  Hofstede JF-Expert Member

  #6
  Jul 20, 2009
  Joined: Jul 15, 2007
  Messages: 3,584
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 0
  Tatizo haliko kwa wananchi kuwa na mwamko, tatizo lipo kwenye uchaguzi kuwa fair. CCM wanatumia chaguzi hizi strategically, kwanza ni kama training ground ya uchaguzi mkuu katika kuhakikisha mbinu zao chafu mpya walizobuni za kujitwalia ushindi kama zinafanya kazi (wizi wa kura). Pili wanahakikisha wapinzani wanashindwa vibaya ili next GE, waweze kuwa na sababu za kujipangia matokeo kuwa wananchi waliwachagua wao kwa kishindo last year, hivyo mwaka mmoja hauwezi kubadilisha mawazo hayo. Tatu uchaguzi huu hutumika kama "furnace ya kuwa suffocate" wapinzani kiuchumi, ili watumia resources zao hapa next year wawe hoi bin taaban kwenye fedha za kupigia campaign za uchaguzi mkuu. Na kubwa zaidi wananchi wameshajua kuwa CCM hata wasipochaguliwa watajitangaza washindi tu, sasa kuna haja gani ya kupoteza muda? (democracy imeshauwawa siku nyingi).

  Ushauri wangu kwa wapinzani, wasijiingize kichwa kichwa kwenye uchaguzi huu wataishiwa resources za uchaguzi mkuu wakati wenzao CCM kuna EPA, n.k. Watumie uchaguzi huu kudai katiba ibadilishwe yaani iwe ni strategy ya kuonesha kuwa hakuna fair playing ground inayowekwa na katiba. Vinginevyo waendelee kuwa washika pembe wa CCM kila uchaguzi unapowadia.
   
 7. K

  Kinyikani Member

  #7
  Jul 21, 2009
  Joined: Dec 5, 2006
  Messages: 65
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 0
  Mimi hushangaa sana humu netini kama kuna watu kweli wame kwenda shule angalau darasa la pili hapa hakutaki mwanasansi kuweza kutambua kama tanzania hakuna uchaguzi ni uhuni tu ulioko. Hivi kweli TUMe ya uchanguzi ya CCM (NEC)itawezaje imuwachie CUF au CHADEMA ???????????
   
 8. Barubaru

  Barubaru JF-Expert Member

  #8
  Jul 21, 2009
  Joined: Apr 6, 2009
  Messages: 7,162
  Likes Received: 27
  Trophy Points: 0
  Hakika ukiangalia katiba ya Tanzania Ibara ya 146 (2)(c) inasema malengo ya Serikali za mitaa ni kuimarisha demokrasia na kutumia demokrasia kuharakisha maendeleo ya wananchi.

  Sasa utaona hapa ni sehemu muhimu sana kwa Serikali ikiwa pamoja na vyama vya siasa kuanza kujikita ili kujihakikishia ushindi katika uchaguzi mkuu.

  Ingawa demokrasia yenyewe imepindishwa na Sheria namba 7 na namba 8 za mwaka 1982 zinazoipa Serikali kuu mamlaka ya kuunda au kuvunja serikali za mitaa bila kujadiliana na wananchi husika.

  Mtu anaepewa mamlaka kisheria kuvunja Serikali za mitaa ni waziri wa TAMISEMI. hapo utaona Serikali kuu ndio yenye mamlaka ya kuunda serikali za mitaa na sio wananchi.


  Sasa ni vizuri wabunge wetu huko Tanzania mkajikita katika kurekebisha katiba na kuupa uchaguzi huu wa serikali za mitaa chachu ja demokrasia na maendeleo ya nchi.

  Nasriyah saleh Al-Nahdi
   
 9. Lunyungu

  Lunyungu JF-Expert Member

  #9
  Jul 28, 2009
  Joined: Aug 7, 2006
  Messages: 8,836
  Likes Received: 75
  Trophy Points: 145
  Salaam toka maeneo ya huku Dodoma .
  Ndugu Watanzania na wapinzani mnao fika hapa JF napendwa kuwapa habari ya kuwasaidia ama ya kuwaondoa huko mjiandae kikamilifu kukabiliana na CCM uchaguzi ujao wa serikali za mitaa .

  CCM na baada ya kuona watu wameamka wameamua kuwaita madiwani wao na kuwauliza kuna shida gani maeneo yao.Madiwani wao na mabalozi wa nyumba kumi wameibua miradi na CCM imeipeleka rasmi kwenye Halmashauri za Wilaya ili pesa zitoke ziende kwenye miradi hiyo haraka wananchi waone na waichague CCM tena serikali za mitaa .Inawezekana habari hii ni nzee lakini kwa kuwa nimepata leo na nilikuwa sijaisoma hapa basi nimeona pamoja na matusi ya wana jamvi nisikate tamaa.

  Kuanzia sasa mtaona miradi inatekelezwa haraka haraka na vikundi katika kata na mitaa vitashamiri na pesa zinatoka huko huko Local government ku fund move zote na baada ya uchaguzi watu wanarudia maisha ya kawaida .Nitajua baadhi ya miradi baadaye kama nitaipata toka kokote TZ kwenye halmashauri kata ama mitaa ambao jambo limeibuliwa nitalileta hapa ili limulikwe .

  Mikutano ndani ya halmashauri na CCM haishi na kazi ni moja kushinda tu na kuweka ngoma chini.

  Natoka sasa
   
 10. M

  Mfumwa JF-Expert Member

  #10
  Jul 28, 2009
  Joined: Aug 29, 2008
  Messages: 1,456
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135
  Kuiondoa CCM madarakani tuna kazi kubwa Wananchi. Manake wanatumia kila mbinu (fedha, danganya toto, tume za uchaguzi nk) kubaki madarakani.
   
 11. Chechetuka

  Chechetuka JF-Expert Member

  #11
  Jul 28, 2009
  Joined: May 28, 2009
  Messages: 549
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Kama CCM haitajirekebisha itaondolewa madarakani. Uchaguzi ujao kwa kiasi kikubwa watakaopigiwa kura ni watu na sio Chama kama ilivyokuwa hapo awali. CCM inapoteza imani yake kwa wananchi kwa kasi kubwa sana. Matatizo ya Ufisadi na kukaa mbali na wananchi kunakikosesha chama hicho hadhi kiliyoijenga kwa miaka mingi sana.
   
 12. Chechetuka

  Chechetuka JF-Expert Member

  #12
  Jul 28, 2009
  Joined: May 28, 2009
  Messages: 549
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Hakuna ubishi kuwa CCM ndio chama pekee chenye mtandao mkubwa zaidi kuliko chama kingine, na wapiga kura wangependa kukipigia kura ili kitawale, lakini kwa ubabaishaji unaofanywa na mawaziri wake, chama kinahitaji nguvu ya ziada kurudi madarakani kwa kishindo. Kama watawasimamisha Mafisadi kugombea nafasi mbali mbali, basi huo ndio utakuwa mwanzo wa mwisho wa Chama dola hiki.
   
 13. H

  Hussein Abdallah Member

  #13
  Jul 29, 2009
  Joined: Nov 1, 2006
  Messages: 70
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Ama kweli CCM n uma uma.Wanawafanya wananchi kama watot wadogo ? Lunyungu shukrani .Zitto , Slaa, NCCR mmesikia mbinu hizo ? Amkeni
   
 14. Barubaru

  Barubaru JF-Expert Member

  #14
  Jul 29, 2009
  Joined: Apr 6, 2009
  Messages: 7,162
  Likes Received: 27
  Trophy Points: 0
  Kuna kazi kubwa sana na nguvu za ziada zinahitajika kuipiku CCM.

  Bila kubadili KATIBA basi Labda baada ya miaka 20 ndio wapinzani wanaweza kukishinda CCM
   
 15. John Mnyika

  John Mnyika Verified User

  #15
  Jul 29, 2009
  Joined: Jun 16, 2006
  Messages: 715
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 0
  Pinda kupindisha kanuni za Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa?

  Na John Mnyika

  Katika mchezo wowote haiyumkiniki refa kuwa mchezaji wa moja ya timu zinazoshindana. Wala haifikiriki wakati huo huo refa huyo huyo akawa kocha, mchezaji na mtungaji wa kanuni za mchezo. Lakini maajabu hayo ni jambo la kawaida katika sheria zetu kuhusu chaguzi za vitongoji, vijiji na mitaa.

  Chini ya sheria zetu, kanuni za chaguzi hizo hutungwa na Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI). Na kwa mujibu wa muundo wa sasa wa utawala wa Tanzania pamoja na kuwa na waziri wa nchi anayehusika na TAMISEMI, mwisho wa siku mwenye dhamana kamili ya “Wizara” hii ni Waziri Mkuu, ambaye kwa sasa ni Mheshimiwa Mizengo Pinda.

  Izingatiwe kuwa mfumo wa utawala wa nchi yetu unaanzia katika vitongoji, vijiji na mitaa ambayo ina mamlaka kadhaa ya kiutendaji na kimaamuzi.

  Uchaguzi wa ngazi hii umekuwa ukifanyika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu hivyo hutumika kama msingi wa vyama vya siasa katika uchaguzi mkuu na kuandaa mfumo wa chama kutawala kuanzia ngazi ya chini.

  Ama kwa hakika Waziri Mkuu yuko katika majaribu makubwa mwezi huu wakati ambapo watanzania wanasubiri mwezi ujao wa Agosti atangaze rasmi katika gazeti la serikali kanuni za uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa sheria, kanuni hizi kwa sasa zinatungwa na Waziri mwenye dhamana ya tawala za mikaoa na serikali za mitaa.

  Mtihani huu unakuwa mgumu kwa kuwa miezi michache iliyopita mnamo tarehe 20 Februari 2009, wadau mbalimbali ikiwemo ofisi yake, vyama vya siasa, asasi za kiraia na msajili wa vyama vya siasa walifikia makubaliano kuhusu masuala ambayo yanapaswa kuingizwa kwenye kanuni husika.

  Wahenga walisema kinyozi hajinyoi; lakini hapa Waziri Mkuu Pinda amepewa mtihani wa kujinyoa kwa kupewa jukumu la kutunga kanuni za uchaguzi ambazo yeye na chama chake ni sehemu ya washiriki.

  Wadau wanasubiri kuona kama atatekeleza makubaliano ya wadau na kutunga kanuni zenye kusimamia misingi ya uchaguzi huru na haki. Ama Waziri Mizengo atafanya mizengwe na kutunga kanuni za uchaguzi zisizoweka uwanja sawa wa kisiasa na hatimaye kuleta uchafuzi badala ya uchaguzi?

  Kujiuliza huku kwa wadau kunasababishwa na kumbukumbu za mwaka 2004, ambapo kama ilivyo sasa kanuni za uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa zilitungwa na Waziri mwenye dhamana badala ya chombo huru cha kusimamia uchaguzi mathalani tume ya uchaguzi.

  Mwanya huu wa kisheria wa mchezaji kujitungia mwenyewe kanuni za mchezo ulifanya kanuni hizo kutungwa kupendelea chama kinachotawala kwa kuweka mianya ya hujuma za kiuchaguzi. Matokeo yake ni uchaguzi uliopita wa vitongoji, vijiji na mitaa kutokuwa huru na haki kutokana na mapungufu mengi ambayo hata serikali yenyewe iliyakiri.

  Mathalani upigaji kura kutokuwa wa siri, fujo katika mikutano ya uchaguzi, matayarisho kuwa hafifu, kuinguliwa na maafisa na watendaji wa kata na vijiji ambao walifikia hatua ya kuwatisha wananchi na kutotoa taarifa za muhimu za uchaguzi, kukosekana kwa daftari la wapiga kura na uchaguzi kusimamiwa na chombo kisicho huru cha kiserikali moja kwa moja(Wizara ya TAMISEMI).

  Wakati mchakato wa uchaguzi huo ukiendelea vyama vya upinzani vikaenda mahakamani, baadhi ya taratibu za uchaguzi huo zikazuiwa lakini uchaguzi wenyewe haukuzuiwa. Mahakama ikaamua uchaguzi uendelee wakati kesi ya msingi inaendelea kusikilizwa kwa maelezo kuwa serikali tayari ilishaingia gharama za maandalizi ya uchaguzi!

  Kutokana na mapungufu hayo CCM ilishinda kwa asilimia 96 na kupata mtaji haramu wa kisiasa ambao ilianza nao kama hujuma katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na kufanya uwanja wa ushindani wa kisiasa usiwe sawa. Na hivyo, CCM ikashinda kwa takribani asilimia 80 katika uchaguzi mkuu mwaka mmoja baadaye.

  Ilitarajiwa kwamba marekebisho ya haraka yangefanyika, hata hivyo hakuna hatua za maana zilizochukuliwa kati ya mwaka 2005 mpaka 2008. Kesi iliyofunguliwa na vyama vya upinzani mwaka 2004 mpaka sasa bado ni kizungumkuti. Kwa upande mwingine, Serikali ilikuwa ikiitisha mikutano na vyama na kuiahirisha bila maamuzi ya msingi kufikiwa kuhusu marekebisho yanayostahili kufanywa katika sheria na kanuni zinazosimamia chaguzi husika. Mithili ya mbinu ya timu iliyoshinda kupoteza muda ili mpira umalizike; lakini kwa kuwa refa ni kocha mchezaji, hakukuwa na wa kupuliza filimbi wala kutoa kadi!

  Mwaka 2009, mwezi Februari ndipo serikali imesaini makubaliano na wadau kuhusu uchaguzi huu. Kwa kisingizio cha ufinyu wa muda, masuala ya msingi yaliyopaswa kufanyiwa marekebisho mengi hayapo kama sehemu ya makubaliano hayo. Kwa mara nyingine tena, serikali imechelewesha muda na baadaye kutumia kisingizio cha muda kukwepa kufanya mabadiliko ya msingi ya kisheria ya kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa huru na wa haki.

  Shabaha ya makala hii ni kuibua mjadala wa kukumbusha makubaliano haya ili wadau waweze kufuatilia kwa karibu kuhakikisha kwamba walau makubaliano hayo yanazingatiwa na Waziri Mkuu Pinda katika kutunga kanuni.

  Kama mchakato wa utungaji wa kanuni utaendelea kufanyika kimya kimya bila rasimu ya kanuni kupelekwa kwa wadau ikiwemo vyama vya siasa kupitiwa kabla ya kuchapwa kwenye gazeti la serikali makubaliano hayo yanaweza kupindishwa.

  Kwa mujibu wa makubaliano hayo; yafuatayo hayatafanyiwa marekebisho: umri wa kugombea; utabaki miaka 21 badala ya kushuka mpaka 18. Wagombea binafsi;hawataruhusiwa.

  Kuhusu kilio cha miaka mingi cha wadau cha kutaka Uchaguzi usimamiwe na Tume ya uchaguzi kama ilivyo katika baadhi ya nchi nyingine duniani; makubaliano yameweka bayana kuwa uchaguzi utaendelea kusimamiwa na serikali kupitia waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa. Kwa mantiki hiyo basi hata hoja ya kutaka kanuni za uchaguzi zitungwe na chombo huru haitazingatiwa.

  Mwito wa Vyama vya siasa kutaka viwezeshwe kutoa elimu ya uraia nao hautazingatiwa. Serikali ilishaweka msimamo kuwa jukumu la kutoa elimu ya uraia litaendelea kuwa la serikali, vyama vya siasa vinaweza kutoa kwa kutumia rasilimali zao.

  Hoja ya kutaka uchaguzi wa madiwani uende sambamba na chaguzi zingine za mitaa nayo haitarajiwi kuwepo katika kanuni zitakazotolewa na Waziri Mkuu Pinda. Uchaguzi wa madiwani utaendelea kuwa na uchaguzi mkuu mwaka 2010; hii ni kwa sababu suala hili linahitaji marekebisho ya kisheria na serikali imeshatamka wazi kwamba muda umeshakwisha wa kufanya marekebisho husika.

  Haya ni masuala nyeti ambayo wadau wengi wangependa yafanyiwe marekebisho lakini hakuna mabadiliko yoyote ambayo Serikali itayafanya kuhusu masuala hayo katika kanuni zinazotungwa ambazo Waziri Mkuu Pinda atazitangaza siku za usoni.

  Mtiririko wa masuala haya kwa ujumla unadhihirisha kwamba serikali haikupanga kufanya mabadiliko ya msingi na kutoa uzito unaostahili kwa uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa. Kirasilimali makubaliano yalilenga tu kwamba katika bajeti ya mwaka wa fedha 2009/10 serikali itatenga bilioni nane(8) tu zitakazotumika kusimamia na kuratibu uchaguzi wenyewe ngazi ya halmashauri ifikapo Oktoba 2009.

  Wakati serikali ikipanga kutenga fedha kiasi kidogo kama hicho kwa ajili ya kuendesha uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa nchi nzima, tume ya uchaguzi kwa upande wake inatarajia kutumia bilioni 42.9 kama gharama za kuboresha daftari la wapiga kura pekee kuanzia mwaka 2009. Tume hiyo hiyo inakadiria kutumia bilioni 64.5 kuendesha uchaguzi wa mwaka 2010. Itakumbukwa kuwa mwaka 2005, Tume ya uchaguzi ilitumia bilioni 62.5 katika uchaguzi mkuu.

  Hata wadau wengine wa maendeleo hawajaweka mkazo wa kutosha kuhusiana na uchaguzi huu, mathalani miradi ya Shirika la Umoja wa Mataifa na michango ya washirika wa kimaendeleo kuhusu uchaguzi, imeelekezwa katika uchaguzi wa mwaka 2010 pekee.  Hata hivyo, kwa mujibu wa makubaliano; marekebisho yafuatayo yatafanyika na kuzingatiwa katika kanuni zinazotarajiwa kutolewa mwezi Agosti mwaka 2009. Hivyo wadau wanapaswa kujadili na kufuatilia kuhakikisha kwamba Waziri Mkuu Pinda hapindishi maamuzi hayo.

  Kanuni zinapaswa kuelekeza kwamba kutakuwa na karatasi maalum za kura zenye nembo ya halmashauri husika; karatasi hazitakuwa na majina ya wagombea, majina yatabandikwa sehemu ya wazi baada ya uteuzi. Ndoo maalum za plastiki zenye kuonyesha(transparent) zitatumika kupigia kura badala ya masanduku ya kura.

  Uchaguzi utafanyika kwenye majengo ya umma, kama hakuna msimamizi atashirikiana na vyama kupata sehemu muafaka. Kanuni zinapaswa zieleze kuwa uchaguzi wa Wenyeviti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri za Kijiji na Wenyeviti wa Vitongoji utafanyika katika kitongoji ili kuwafanya wapiga kura wengi kuweza kufika na kupiga kura zao; Kampeni zitafanyika kwa muda wa siku saba kama ilivyo kwa kanuni za 2004. Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mitaa na wajumbe wa Kamati za Mitaa utafanyika katika mitaa husika, vituo vitakuwa zaidi ya kimoja kulingana na wakazi wa mtaa.

  Kwa mujibu wa makubaliano Orodha ya wapiga kura(Local Voter register) itaandaliwa siku 21 kabla ya uchaguzi ili kutoa nafasi kwa wapiga kura kukagua orodha na kuweka pingamizi. Orodha itaandaliwa na watumishi wa umma lakini wasiwe watendaji wa vijiji, mitaa au kata. Uthibitisho wa mpiga kura utatokana na jina lake kuwepo katika orodha ya wapiga kura, vitambulisho vitavyotumika kumtambulisha chochote kati ya vifuatavyo- kadi ya mpiga kura, kitambulisho cha kazi, hati ya kusafiria, kadi ya benki, kadi ya bima ya afya, kitambulisho cha chuo/shule, leseni ya uderava au wakazi kama mpiga kura hana kitambulisho chochote.

  Kanuni zinapaswa kuwa na kifungu cha kamati ya rufaa ambayo wajumbe wake watateuliwa kutokana na hali ya eneo husika ila hawatakuwa kati ya wafuatao; afisa anayehusika na uteuzi wa wagombea, msimamizi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi, kiongozi wa ngazi yoyote wa chama cha siasa, mtumishi wa halmashauri, kiongozi yoyote wa dini. Masuala haya na mengine yako mikononi mwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wadau wanajiuliza; atatunga kanuni za uchaguzi zenye kuzingatia haki na demokrasia au ataleta mizengwe ya kupindisha makubaliano? Tunasubiri!

  Mwandishi wa makala hii ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA anayepatikana kupitia 0754694553, mnyika@yahoo.com na JJ
   
 16. H

  Hussein Abdallah Member

  #16
  Jul 29, 2009
  Joined: Nov 1, 2006
  Messages: 70
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Diwani anani habarisha kwamba kata za Mburahati,Kibamba ,Makuburi, na Tandale mradi wao una anza soon so ina maana Lunyungu uko kwenye line sasa .CCM hao
   
 17. T

  T_Tonga Member

  #17
  Jul 30, 2009
  Joined: Jul 24, 2007
  Messages: 64
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  ccm kiboko yao ni wapemba tu hata watoe nini itabaki kutumia nguvu na wizi watafanya kampeni pemba na wapemba walivyo watakwenda kwa wingi katika mikutano ya ccm lakini kura kwa cuf watawadanganya watu wa bara na unguja tu wao hawajui nini wanataka
   
 18. John Mnyika

  John Mnyika Verified User

  #18
  Aug 1, 2009
  Joined: Jun 16, 2006
  Messages: 715
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 0
  Jana, Julai 31 Bunge limepitisha marekebisho ya sheria ili kurusu uchaguzi wa vijiji kura kupigwa vitongojini badala ya kwenye Mkutano Mkuu wa Kijiji. Baada ya Marekebisho hayo madogo, sana ni wakati wa Waziri Mkuu Pinda kutoa kanuni. Mjadala uendelee..
   
 19. Barubaru

  Barubaru JF-Expert Member

  #19
  Aug 1, 2009
  Joined: Apr 6, 2009
  Messages: 7,162
  Likes Received: 27
  Trophy Points: 0
  mengi nilishabainisha hapo awali lakini Bwana Mnyika nitaendelea kuzipembua sheria hizo za Serikali za Mitaa na kuwataka wabunge wetu wawe makini na kudai mabadiliko yake ili kuupa hadhi chaguzi hizi za ngazi za vitongoji.

  Nasriyah Saleh Al-Nahdi.
  Doha
   
 20. MwanaHaki

  MwanaHaki R I P

  #20
  Aug 23, 2009
  Joined: Oct 17, 2006
  Messages: 2,403
  Likes Received: 122
  Trophy Points: 145
  Asalaam Aleikum. Ramadhan Kareem.

  Waungwana, usiku wa leo, baada ya kutoka Salat Taraweh, nikapitia kwenye kijiwe chetu mtaani, nikawakuta watu wameketi, kukiwa na mabishano makali. Walikuwa wakijadili matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mtaani kwetu.

  Iliwastaajabisha kwamba mtu aliyetarajiwa (kutokana na ukweli kwamba yeye ni mkaazi wa mtaa wetu, kwa miaka zaidi ya ishirini) kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mtaa, hakuchaguliwa. Badala yake alichaguliwa mgeni, tena asiyefahamika. Likaulizwa swali, kwa sababu gani achaguliwe mgeni na mwenyeji asipewe kura, tena na wanachama wenza? Likajibiwa: Hana pesa!

  Nikagundua kwamba kweli hiki Chama sasa kimefika mwisho wake, maana, mfa maji heshi kutapatapa.

  Wanachama wa Chama Tawala - CCM - sasa wanageukana wenyewe. Badala ya kuchaguliwa mtu mwenye fikra mbadala, mwenye uwezo, mwenye ufahamu wa matatizo ya wenzake, anachaguliwa mgeni, kisa, ametoa dau kubwa. Kwani kura ni bidhaa inayouzwa sokoni, ndipo ipangiwe bei, mwenye kutoa rushwa apite, achaguliwe, na yule muadilifu asichaguliwe?

  Kiko wapi kiapo cha Chama "Rushwa kwangu ni mwiko, sitatoa wala kupokea rushwa"?

  Asthghafirullah!

  Kama huu ndio mwelekeo - tena kwenye ngazi ya mtaa - wa Chama, ifikapo 2010, asokuwa na ngawira asijipendekeze kugombea kura. Tuwaache mafisadi wachukuwe.

  Lakini cha ajabu zaidi, MBONA UCHAGUZI HUU haukutangazwa - kama ipasavyo - na Tume ya Taifa ya Uchaguzi? Au lilikuwa jukumu la nani kufanya hivyo? Sikuona tangazo lolote kwenye vyombo vya habari, si kusoma gazetini wala kusikia kwenye radio au kutazama kwenye luninga!

  Mheshimiwa Spika (kama yupo), napenda kuwasilisha hoja.

  Wabillah Tawfiq.

  ./Mwana wa Haki
   
Loading...