Kuelekea siku ya wanawake duniani

Asha Abdala

JF-Expert Member
Mar 21, 2007
1,130
44
MABADILIKO YA KWELI! UHURU WA KWELI!
KONGAMANO! KONGAMANO! KONGAMANO!


Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani,Wanawake wa CHADEMA wameandaa Kongamano Kubwa la kihistoria na la aina yake.

Wapi?: Ukumbi wa Urafiki Ubungo-Nyuma ya Maghorofa ya Urafiki

Lini? Jumamosi, 08 Machi 2008, saa 2:30 mpaka saa 8:30 mchana

Kunani? Kongamano la Wanawake-kujadili mustakabali wa wanawake
Tanzania
Mgeni nani? Mhe Freeman Mbowe-Mwenyekiti CHADEMA Taifa

Mada? Kutakuwa na mada nne siku hiyo, 1.Uwajibishwaji wa
watuhumiwa wa ufisadi,2.Uchambuzi wa Baraza Jipya la
Mawaziri, 3.Hali ya Wanawake Tanzania na 4.Haki na Wajibu
wa Wanawake katika Maendeleo


Watoa Mada ? Wanasiasa na Wanaharakati Wanawake ndani na nje ya CHADEMA

Kwa maelezo zaidi piga simu au tuma ujumbe kwenda 0713 760534 au 0754 598422 au 0756 007671


Wanawake! Chimbuko la Maendeleo!
 
Naomba niwatakie kongamano jema; ni wakati wakutambua nguvu yenu katika mapambano haya na mafisadi. Kina mama amkeni, mjenge Taifa lenu.
 
Dada Asha,

Hongera sana kwa Kina mama wote (Wanawake) kwa siku hii maalum kuhusu nafasi yao kwa jamii.

Naomba uwakilishe nasaha za Rev. Kishoka kwenye mkutano wenu hapo Urafiki; Je ni lini Wanawake wa Tanzania watafanya mapinduzi ya kuondokana na kutengewa nafasi maalumu katika uongozi na uwakilishi? Je hawaoni kuwa kuendelea kuwepo kwa upendeleo huu kunadhoofisha nguvu zao za kuwa sawa katika uongozi na uwakilishi? Je ni empowerment ya namna gani inapatikana ikiwa wengi wa kina mama wetu wataogopa kwenda kugombea nafasi za uwakilishi na kusubiri uwakilishi wa kuteuilwa na upendeleo?
 
Dada Asha,

Hongera sana kwa Kina mama wote (Wanawake) kwa siku hii maalum kuhusu nafasi yao kwa jamii.

Naomba uwakilishe nasaha za Rev. Kishoka kwenye mkutano wenu hapo Urafiki; Je ni lini Wanawake wa Tanzania watafanya mapinduzi ya kuondokana na kutengewa nafasi maalumu katika uongozi na uwakilishi? Je hawaoni kuwa kuendelea kuwepo kwa upendeleo huu kunadhoofisha nguvu zao za kuwa sawa katika uongozi na uwakilishi? Je ni empowerment ya namna gani inapatikana ikiwa wengi wa kina mama wetu wataogopa kwenda kugombea nafasi za uwakilishi na kusubiri uwakilishi wa kuteuilwa na upendeleo?

KONGAMANO LA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
MACHI 8, 2008.


MADA
VITA YA UFISADI NA MUSTAKABALI WA MAENDELEO YA MWANAMKE NCHINI.
Na
SUZAN LYMO (MB)

UTANGULIZI.
Kwanza niwashukuru wanawake wenzangu kwa mwitikio wenu kuja kuungana na wanawake wa CHADEMA katika Kongamano hili la kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Najua mpo mlio tayari wanachama wa CHADEMA lakini najua kuna wengine wanaweza kuwa wanachama wa CCM, CUF, TLP,NCCR-Mageuzi na vyama vingine, na hata wasio na vyama. Nawapongezeni kwakuwa mmeamua kusimama pamoja kama wanawake na kusahau itikadi zenu.

Nawapongeza kwakuwa mmefahamu kuwa maendeleo ya mwanamke hayana itikadi. Mmefahamu kuwa maendeleo ya mwanamke yataletwa na mshikamano wa wanawake. Mmefahamu kuwa ni wakati wa wanawake kusimama pamoja kuijenga nchi hii.

Wanawake wenzangu matatizo yanayowakabili wanawake nchini hayutupi muda kuendekeza malumbano au mabishano ya kisiasa kwa misingi ya Itikadi bali uzalendo. Matatizo yanayomwangamiza mwanamke sasa yanahitaji nguvu ya pamoja na uthubutu wa hali ya juu kwa wanawake bila kujali itikadi wanayotoka ilmradi maslahi ya Taifa yanalindwa kwani maslahi ya Taifa yanapaswa kuwa maslahi ya wanawake kutokana na wingi na nafasi yao kwa maendeleo.

Wanawake wenzangu. Leo nimepewa nafasi nizungumzie hatua wanazopaswa kuchukuliwa mafisadi wananyonya uchumi wan chi na kusababisha umasikini mkubwa kwa watanzania. Inagwa nimepewa fursa ya kujadili hatua ambazo wanapaswa kuchukuliwa mafisadi wanyonya uchumi wan chi hii, naomba hukumu hiyo nisiitoe mimi.

Badala yake nichokeze mjadala kuhusu hali ya wanawake nchini, ili kwa pamoja kama wanawake tutoke na azimio kuhusu hatua wanazopaswa kuchukuliwa mafisadi hawa. Nataka wanawake tujadili Tanzania bila mafisadi hali ya mwanamke ingekuwaje?. Ili kwa pamoja tupeane majukumu kuona kila mmoja ana nafasi gani katika vita hii dhidi ya mafisadi.

Kati ya malengo manane ya millennia(MDGs), Malengo matatu yanagusa moja kwa moja maisha ya kila siku ya mwanamke. Lengo Na5 la Millenia linazungumzia kuboresha afya za akina mama wajawazito, Lengo Na 6 kudhibiti maradhi ya Ukimwi,Malaria na magonjwa mengine, wakati lengo Na 4 linazungumzia kupunguza vifo vya watoto kufikia mwaka 2015. Mambo haya yanagusa maisha ya mwanamke moja kwa moja. Ni malengo mazuri na serikali siku zote imekuwa ikiahidi kuyatekeleza.

Ndugu zangu, Ili malengo hayo yatekelezwe yanahitaji uongozi dhabiti na wenye kupambana na ufisadi. Usio na simile kwa mafisadi. Serikali ya mafisadi haiwezi kupambana na ufisadi, Serikali inayoingia madarakani kwa rushwa za makampuni haiwezi kukusanya kodi kwenye makampuni, Serikali ya mafisadi haiwezi kutoa huduma za jamii.Na ndio maana ni vigumu kufikia malengo hayo.

Ufisadi sasa ni janga la kitaifa. Na Taifa linapoangamizwa na mafisadi mwathirika wa kwanza ni mwanamke. Leo hii serikali inashindwa kuboresha huduma za maji, Serikali inashindwa kusomesha madaktari, serikali inashindwa kutoa dawa zakutosha kwenye zahanati zetu, tunalea watoto waliothirika kwa utapia mlo, tunapoteza watoto kwa magonjwa yanayotibika kama maralia, wanawake wanahangaika vijijini kwa kilimo cha jembe la mkono, wanawake wanahangaika na biashara za uchuuzi, biashara za mamantilie, wanawake wanahangaika na kila aina ya dhiki na ufukara katika nchi hii, lakini kila tunapoihoji serikali bungeni serikali haina fedha.

Pamoja na utajiri mkubwa wa rasilimali tulio nao, bado miradi mingi ya maendeleo inadhaminiwa na wahisani. Serikali yetu imefika mahala haiwezi kutekeleza mradi wowote wa maendeleo bila pesa za wafadhili. Asilimia 100 ya bajeti ya maendeleo inatolewa na wafadhili.

Pamoja na madini, Maziwa, bahari, mbuga za wanyama, na kila aina ya utajiri ambao nchi hii imejaariwa lakini serikali yetu haina uwezo wa kuhudumia hata gharama za uendeshaji wa serikali(recurrent expenditure), ambapo mpaka sasa asilimia 60 zinatokana na misaada ya wahisani. Hii ina maana bila misaada ya wahisani hata serikali yenyewe haiwezi kuwepo maana haiwezi hata kumudu gharama za kujiendesha.

Watanzania kila wanauliza kulikoni hali hii? Wabunge tunahoji bungeni kwanini serikali inakuwa taabani kiasi hiki? Serikali haina majibu. Hata Mh Rais alipokuwa mwaka jana akiwa Ufaransa alipouzwa kwanini watanzania ni masikini licha ya utajiri mkubwa unaowazunguka, alisema hajui. Kumbe ilikuwa ni siri, sasa tumegundua kuwa ufiasadi ndio siri ya umasikini wa mtanzania. Ufisadi ndio umelifikisha Taifa hili ICU kiasi cha hata serikali yenyewe kushindwa kujiendesha.

HALI YA WANAWAKE NA UFISADI TANZANIA.
Wanawake wa Tanzania wanakabiliwa na umasikini uliokithiri unaosababishwa na usimamizi mbovu wa rasilimali za taifa. Matatizo mengi yanayogharimu maisha ya wanawake yanatokana na uwezeshaji mdogo wa serikali unaosababisha umasikini mkubwa kwa wanawake.Leo kuna vijana wengi wa kike wanaojiuza miili yao ili kukabiliana na maisha, kuna wakina mama wengi wanakufa hospitali kutokana na kukosa huduma za afya ya uzazi, kuna watoto wengi ambao kina mama ndio sauti yao wanakufa kwa magonjwa ya malalia, kifua kikuu,….ambayo ni magonjwa yenye kutibika. Hali ya huduma nchini ni mbaya mno na akina mama ndio wahanga wakuu.

Pamoja na upole wa akina wa wananchi hasa akina mama. Serikali bado imeshindwa kutumia rasilimali zake kuwahudumia. Hali ya umasikini nchi hii inatisha. Serikali inapoteza mabilioni ya fedha kwa rushwa na ufisadi uliokithiri huku ikishindwa kutoa pesa kiduchu kuwahudumia wananchi wake.

Leo hii Tanzania ni miongoni mwa nchi kumi zina vifo vingi zaidi vya uzazi duniani. Zaidi ya wanawake 800(wanawake22kwa siku) wanakufa kutokana na huduma mbovu kwa wazazi, Kwa uduni wa huduma za afya, takribani asilimia 60 ya wanawake wanajifungulia nyumbani kutokana na uahaba na uduni wa huduma ya afya.

Kila mwaka akina mama tunafisha wototo 183,800 sawa na watoto 20 kwa saa moja kutokana na magonjwa ya ya malalia, utapiamlo, upungufu mkubwa wa damu, nimonia, kuharisha na ukimwi. Yote haya kwa kiasi kikubwa yanatokana na umasikini uliokithiri wa wananchi pamoja na huduma duni za afya.

Katika mwaka wa fedha 2006/07 serikali ilishindwa kutoa bajeti iliyoahidi ya milioni540 kwa kwa hospitali ya Mwananyamala kwa mwaka na kupeleka milioni200 tu kwa hoja kuwa serikali haina pesa. Wakati serikali inasema haina fedha hizo, inakubali kupoteza billioni260 kwa ufisadi wa mkataba wa RICHMOND . Kama fedha za RICHMOND zinge elekezwa kwenye huduma za afya ingeweza kuendesha hospitali ya Mwananyamala kwa miaka 520 kama ingekuwa inatengewa sh 540milioni. Na kwa kiasi cha milioni200 wanazopewa, fedha za RICHMOND zingeweza kuendesha hospitali ya Mwananyamala kwa miaka1300.Wanawake wa Dar es Salaam hiyo ndio tafsiri ya pesa zilizopotea kwenye RICHMOND peke yake.

Wanawake wenzangu kiasi cha bilioni 260 zilizoporwa na genge la mafisadi zingetosha kuendesha hospitali ya Temeke kwa miaka 370. Au zingeweza kuendesha hospitali 370 zenye viwango sawa na ile ya Temeke. Jiulize wewe mwanamke unayehangaika na huduma mbovu Temeke, Mwananyamala kwasababu tu serikali haina pesa, lakini serikali hiyohiyo inakuwa tayari kupoteza pesa ambazo zingeweza kuendesha hospitali ya Temeke kwa miaka 370(karne moja na miaka70) au ambazo zinaweza kuendesha hospitali ya Mwananyamala kwa miaka1300(karne 13).Nawaomba mtafakari na muamua wenyewe kuhuau watu wa aina hii wanastahiki adhabu gani?

Ukija Benki kuu huko ndiko watu kuna makampuni ya kunyonya damu watanzania. Kwa mujibu wa hoja ya Dk Slaa, jumla ya trilioni1.3 zimepotea katika maeneo mbalimbali ndani ya Benki Kuu.Uchunguzi uliofanywa ulihusu bilioni133 za akaunti ya madeni ya nje ambazo ni sawa na asilimia 10 tu pesa zilizopotea. Bado uchunguzi haujafanyika kwenye ujenzi wa minara pacha iliyogharimu takribani bilioni600, bado uchunguzi haujafanyika kwenye kampuni za DeepGreen financial Ltd, Meremeta Co, Mwananchi, Import Support,nk.

Wakati akina mama vijijini wanahangaika na jembe la mkono, na kila wanapolia serikali iwakumbuke serikali inasema haina fedha, pesa ambazo serikali imepoteza Benki kuu ni Trilioni 1.3 ambazo kama serikali ingekuwa na dhamila ya kupunguza umasikini, pesa hizo zingetosha kununua matrekta 65000, ambayo ni wastani wa matrekta 7 ya thamani ya milioni20 kwa kila kijiji.

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA VITA DHIDI YA UFISADI.
Ni wazi sasa serikali ipo kwenye kikaango cha vita dhidi ya ufisadi. Kama wanawake lazima tujiulize nafasi yetu ni ipi katika vita hii?lazima tujiulize sisi ni wasafi kiasi gani kuweza kuwa viongozi wa mfano. Ni wazi kuwa ifike wakati kila anayehusika na ufisadi achukuliwe hatua kali za kisheria.Na kama wanawake lazima tuwe mstari wa mbele kupaza sauti mafisadi washughulikiwe haka kama watakuwa mashoga zetu.

Ni wakati sasa wanawake tutumie nafasi yetu kujenga uzalendo ambapo kiongozi anapohusishwa na ufisadi anajiondoa kwa hiari yake badala ya kusubiri kufukuzwa.Ni wazi kuwa wimbi la ufisadi halijawagusa wanawake wengi. Na hii ni jambo la kujivunia kuwa wanawake wengi ni watu safi . Lakini kwa wachache waliohusishwa na ufisadi ni wazi kuwa walipaswa kujiuzulu kabla ya kung’olewa. Leo hii tuna viongozi wamehusishwa na ufisadi wa mabiloni ya fedha za wananchi lakini bado ni mawaziri na wengine ni viongozi wa juu kabisa serikalini.Mpaka sasa sielewi kwanini Mwanasheria Mkuu bado hajajiuzulu pamoja na kutakiwa wajibishwe.

Mpaka leo sijui Andrew Chenge ambaye ni waziri wa Miundombinu anasubiri nini ilhali yumo kwenye orodha ya mafisadi. Nivema hata wale wasio na madaraka serikalini wanapohusishwa na ufisadi watoke hadharani na kufafanua namna wanavyohusika au wasivyohusika kuliko kukaa kimya. Na hapa lazima niweke wazi kuwa kama mwanamke ninasikitishwa sana na hatua ya Getrude Mongera ambaye alipaswa kuwa mwanamke wa mfano kwetu alivyohusishwa na ufisadi katika bunge la Afrika lakini mpaka sasa yupo kimya. Huu ni mfano mbaya sana kwa wanawake viongozi.

Imefika wakati wanawake tusikubali mambo haya yaishe kwa ujanja ujanja. Ni lazima tupaze sauti kutaka wahusika wa ufisadi wachuliwe hatua ili haki ionekane inatendeka katika nchi yetu. Sote tunakumbuka kuwa mwaka jana wanawake wafanya biashara ndogo ndogo walikuwa wanapigwa na polisi, wanabomolewa vibanda vyao kwa kosa la kujitafutia riziki kupata hela ya sabuni na mafuta. Mtakumbuka ni serikali hii iliyovunja vibanda vya watu wenye ulemavu kwa madai kuwa ni uchafu, walemavu wakalia na kunyanyasisika, vijana wetu wakapigwa hata wengine kupoteza maisha ilhali hawajaiba cha mtu wala cha serikali. Tuwaulize serikali kulikoni walioiba mabilioni ya shilingi kubembelezwa? Inakuwaje serikali inapokea fedha kutoka kwa wezi bila kuwakamata?.Ni lazima wanawake masikini tupaze sauti kwa nguvu. Tuulize haki iko wapi?

HITIMISHO.
Wanawake wenzangu. umasikini, ufisadi na ubabaishaji katika nchi hii ni mkubwa mno. Tunahitaji kufanya mabadiliko makubwa kulinusuru Taifa hili. Na wanawake lazima tuwe mstari wa mbele. Nchi zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo duniani ni zile ambazo wanawake wako mstari wa mbele. Wanajua haki na wajibu wao sio wanaosubiri huruma ya watawala. Leo hii katika nchi za scandnavia ambazo zinaongoza kwa hali bora ya maisha duniani asilimia, 60 ya viongozi wake ni wanawake.Ni lazima sasa wanawake tupambane kushiriki uongozi wa nchi yetu ili kurejesha matumaini kwa watanzania.

Matatizo ya ufisadi chimbuko lake ni uongozi mbovu. Hivyo wanawake kwa wingi wetu tuna nafasi kubwa ya kuamua uongozi bora katika nchi yetu. Uongozi utakaotuhakikishia huduma bora za afya, utakaopunguza vifo vya akina mama wajawazito, utakao tokomeza ufisadi na mafisadi ili kunusuru maisha yetu na watoto wetu.Mwisho niwaulize tena wanawake wenzangu, kwa vifo vya watoto wetu, yatima, wajane,walioshindwa kuyanusuru maisha yao kwa kukosa huduma huku mabilioni yanaishia kwenye ufisadi, Tuchukue hatua gani dhidi ya mafisadi hawa?

Ahsanteni sana .
Nawakaribisha Chama Mbadala! Tutoe Uongozi Mbadala!Kwa Tanzania Mbadala!
CHADEMA; Vema! Wanawake;Chimbuko la Maendeleo.
 
Back
Top Bottom