Kuelekea miaka 3 ya Rais Magufuli, TPA yataja hatua muhimu kumaliza bandari bubu

Sep 30, 2014
34
25
IMG_9385.jpg

Na Mesa Mahadhi
SERIKALI ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ina mpango wa kuzirasimisha Bandari Bubu zote nchini ili kutengeneza mazingira mazuri kwa watu wanaozunguka bandari hizo.

Bandari hizi ni zile zinazopakia na kupakua bidhaa bila kufuata utaratibu, wala fedha kufika katika mamlaka husika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko akiwa katika mahojiano maalumu na Jamvi la Habari ofisini kwake hivi karibuni alisema, Bandari Bubu si njia sahihi ya usafirishaji mizigo baharini na ziwani kwani inaikosesha mapato serikali na kuua ushindani wa viwanda vya ndani.

“Bandari Bubu zinaanzishwa na nchi jirani kwenda vijiji vyenye watu kidogo ili kupitisha bidhaa bila kulipia kodi, tunatambua katika maeneo hayo kunakuwa na biashara kubwa inayoleta mapato kwa wananchi waliozunguka.

“Ndiyo maana tuliamua kutembelea bandari zote bubu ili kuangalia namna ya kushirikiana nao kufanya kazi, bandari hizi zinatambulika ndiyo maana wakuu wa mikoa na wilaya walikiri kufika mara kwa mara kwa ajili ya ukaguzi,” alisema Mhandisi Kakoko.

Hata hivyo, alibainisha zipo hatari nyingi zinazoweza kuwapata wakazi wanaozunguka Bandari Bubu kwa sababu hakuna vifaa vya kuzimia moto, wala vifaa vya dharura pindi linapotokea janga lolote linalotokana na upakuaji na upakiaji mizigo.

“Kuna baadhi ya bidhaa zina mionzi mikali, hakuna vifaa vya kudhibiti mionzi hii. Hakuna huduma za afya lakini pia bandari hizi hutumika kupitisha nyara za serikali kama pembe za ndivu, faru na wanyama hai wakati mwingine,” alisema Kakoko.

Aliongeza kuwa wamefanya mikutano ya mara kwa mara na wakazi wanaozizunguka banadari hizo kwa kuwahsirikisha viongozi wa serikali za mitaa, kitu walichobaini hata viongozi wa serikali za mitaa huchukua baadhi ya malipo katika bandari hizo, maana yake wanazitambua. Lakini kinachotakiwa kwa sasa ni kutengeneza urafiki ili fedha hizi ziingie katika mikono halali.

Hata hivyo, alisisitiza zipo Bandari Bubu zisizofaa kuwepo kutokana na mazingira. Kwa sababu uanzishwaji wa bandari una namna yake. Lakini pia baadhi ya maeneo huwezi kuweka wafanyakazi ni gharama kubwa kulinganisha na kipato kinachopatikana, hivyo watahakikisha wanazifungia na atakayethubutu kwenda kinyume na utaratibu adhabu kali zitawakuta.

“Tulizunguka na wakuu wa mikoa na kufanya nao vikao vingi katika maeneo yanayotajwa kuwa na bandari hizi, bado tunaendelea na vikao ikifika Disemba mwaka huu itakuwa tumezifikia bandari zote bubu nchini na tutaamua zipi ziendelee na tutaziwekea mashine za EFD na vifaa vingine vya dharura na zipi tuzifungie,” alisema na kuongeza:

“Hadi kufikia mwaka 2020 hakutakuwa na Bandari Bubu nchini, kwa sasa tunazo boti tatu za ‘patrol’ upo mpango wa kuongeza nyingine tutakazozisambaza kwenye bahari na maziwa makuu. Lengo kudhibiti Bandari Bubu.”

Anasema alifanya ziara katika Bandari ya Nyamisati, akakuta shehena inashushwa lakini walipotokea boti iliyokuwa ikishushwa iliondolewa kwa haraka. Hali hiyo iliwafanya kupata wasaa wa kuzungumza na watendaji wa eneop lile ili kupata njia nzuri ya kuendesha banadari hiyo bubu.

Vilevile katika maelezo yake Mhandisi Kakoko, alibainisha kuna baadhi ya maeneo kwenye maziwa makuu alikuta baadhi ya matajiri wanamiliki Bandari Bubu kwa kuwatoza ushuru wanaopakia na kushusha mizigo.

“Tulifanya mazungumzo na baadhi ya matajiri wanaomiliki bandari hizo, tukawataka wawe karibu na sisi ili tuwape msaada na kuwaeleza namna ya kushirikiana nao tutengeneze mazingira mazuri ya kupata huduma na serikali ipate maparo,” alisema Mhandisi Kakoko.

Ramadhan Saleh, mdau wa wakala wa forodha anasema: “Bandari Bubu ni tatizo kwa sisi tunaofuata utaratibu kwenye kutoa mizigo bandarini, tunatumia muda mwingi na fedha katika kutoa mizigo lakini kuna watu wanafanya kazi nyuma ya pazia.

“Hili linatuathiri kwa kiasi kikubwa kwa sababu hakuna ushindani, wateja wangu wanaoshusha mizigo Zanzibar wanapotaka kuleta mizigo yao Dar es Salaam wanajishauri sana kwa sababu zipo Bandari Bubu maeneo ya Bagamoyo, Kigombe huko Tanga na maeneo mengine pembezoni mwa bahari ya Hindi zinatumiwa na watu wasio waaminifu kwa kutoa fedha kidogo, lakini kwa kiasi kikubwa usafiri wake si salama.”

Alibainisha Saleh, serikali inakosa mapato lakini pia wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa Bandari Bubu wapo katika hati hati ya kuathirika afya zao kwa sababu wanatumia bidhaa za vyakula kama sukari na siagi ambavyo havijathibitishwa na mamalaka zinazohusika ikiwa ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Akizungumzia tofauti kati ya huduma za bandari katika miaka ya nyuma na sasa, Saleh anasema: “Kiukweli kwa sasa huduma ni nzuri, ingawa sisi kuna vitu tunaona vimepungua kama rushwa na kutoa mizigo kwa mlango wa nyuma lakini kwa kiasi kikubwa ni salama kwetu. Zamani ukileta gari kutoka Japan, kila kitu kinachomolewa lakini kwa sasa hata pini haichukuliwi. Mizigo inatoka kwa wakati hakuna foleni na hata eneo la kuegesha magari limekuwa kubwa.”

Katika Tanzania ya Viwanda, Bandari Bubu imekuwa tishio kwa wawekezaji kutokana na wafanyabishara wasio waaminifu kuzitumia kuingia bidhaa kutoka nje na kuua ushindani kutokana na bidhaa hizo kuuzwa kwa bei ya chini.

Mathalan, Mkoa wa Tanga pekee una Bandari Bubu zinazofikia 45, mikoa mingine yenye bahari ni Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara. Huku maziwa makuu ya Victoria, Nyasa na Tanganyika ambayo yanapakana na nchi jirani yakiwa na Bandari Bubu nyingi ambapo kwa pamoja zinaweza kufikia 130 ambazo ni zile zilizotambuliwa na serikali huku nyingine bado zikiendelea kuwa mafichoni.

Awali, Mhandisi Kakoko akizungumzia mafanikio ya Mamlaka ya Bandari Tanzania, alisema wakati TPA inaanzishwa kwa sheria ya mwaka 2004 ilikabidhiwa dhamana ya kusimamia bandari zote nchini zinazofikia 91 baharini na maziwa makuu.

Hivyo, nchi imezaliwa upya kwa kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano, ambapo upakuaji na upakiaji mizigo utafanyika kwa ufanisi mkubwa ili kukifanya chombo hicho kuwa sehemu ya mafanikio ya Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati kufikia 2025.

“Kumefanyika kazi kubwa katika kipindi hiki cha kuanzia mwaka 2015, shehena za mizigo imeongezeka kuliko wakati wowote wa uendeshaji Bandari, pengine kabla ya kuvunjwa Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika Serikali ya Awamu ya Kwanza,” alisema Mhandisi Kakoko.

Alibainisha, ziara ya kushitukiza ya Rais Dk. John Magufuli katika bandari hiyo mapema baada ya kuapishwa Novemba, 2015 ilikuwa ni uzinduzi wa mwendo kasi bandarini.

“Rais aliondoa uozo mwingi hadi meli zikaanza kukimbia, lakini alishikilia msimamo wake akasema bora tuhudumie meli moja lakini kwa ufanisi kuliko kuhudumia meli nyingi halafu mapato hayaonekani. Lakini watu wameshaanza kuvutiwa na huduma zetu meli zinamiminika, tulikuwa tunapokea tani milioni 13.7 kwa mwaka katika miaka mitatu iliyopita lakini kwa sasa tunapokea tani milioni 16.2 na tunatarajia zitaongezeka hadi kufikia tani milioni 25 ifikapo mwaka 2025, yaan kuanzia mwaka huu wa 2018 tutakuwa tunaongeza tani milioni moja kila mwaka,” alisema Mhandisi Kakoko.

Kwa sasa sekta ya Bandari ndiyo inayochangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa ambapo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inatoa asilimia 50 ya fedha zinazoingia katika Bajeti ya taifa, katika miaka hii mitatu ya mwanzo katika uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, ambapo katika asilimia 100 ya mapato ya TPA, asilimia 40 inatokana na idara ya forodha.
 

Attachments

  • JPM.jpg
    JPM.jpg
    18.8 KB · Views: 16
Back
Top Bottom