Kuelekea awamu ya pili ya Bunge la katiba, wabunge wa CCM mmbadilike

the ultimatum

JF-Expert Member
Dec 16, 2012
402
114
Ikiwa imebaki takribani mwezi mmoja na nusu kabla ya kuanza kwa awamu ya pili ya mikutano ya Bunge maalumu la katiba.

Kuna mambo kadhaa ambayo nilijifunza kutoka kwenye mikutano iliyopita ya bunge la katiba lililosimamishwa ili kupisha bunge la bajeti. Kwa ufupi kabisa, mambo hayo ni Kama yafuatayo:-

1.Udhaifu wa mwenyekiti wa bunge maalumu Mheshimiwa Samwel Sitta katika kuliongoza bunge lile. Ambapo kwangu mimi Sitta alikuwa na sura zaidi ya moja katika bunge lile. Alikuwa Kama mwenyekiti, lakini pia alikuwa na sura ya kujisafishia njia ya mbio za urais mwaka 2015. Sitta alitumia muda mwingi kuwapiga vijembe wabunge wanaotoka upinzani, hasa Ukawa. Kwa mashinikizo kutoka mamlaka za nje ya bunge aliweza kupindisha kanuni mbalimbali walizojitungia wenyewe ilimradi tu awaridhishe wale aidha waliomuahidi nafasi ya kugombea urais kama tu ataliendesha bunge katika misingi wanaoitaka wao, au kujipalilia njia yeye mwenyewe akiamini anawaridhisha watu fulani wenye mlengwa mmoja nayeye ili ajiandalie mazingira mazuri mbele ya safari.

2. Wabunge wa CCM kutumia muda mwingi kujadili watu badala ya hoja. Mfano Mwigulu kuwatusi Jussa na Mbowe 'eti wanataka kuleta ushoga kwa kura za siri' badala ya kujadili kwanini anataka kura za wazi. Lakini pia hata katika kujadili hasa katika sura ya kwanza na ya sita ambazo ndizo zilichaguliwa katika kufungua mijadala ya rasimu. Wabunge wengi wa upande wa CCM walionekana kama watu waliokaririshwa maneno ya kusema, wengine walidiriki hata kusoma baadhi maelezo yao kutoka kwenye karatasi. Hii inaonyesha ni namna gani wabunge wa CCM wamekaririshwa maneno ya kuzungumza kutoka katika mamlaka za nje ya bunge. Kwa kiasi kikubwa hali hii ilipelekea mijadala ya bunge kutokuwa na uhalisia wake kwani wengi wao kuishia kusema naunga mkono maoni ya wengi ya serikali mbili kisha kuacha kueleza kwanini serikali mbili badala yake kuanza kuwashambulia wapinzani kwa matusi. Na hata walipojaribu kutetea hoja zao zilikuwa ni zile zile za kufanana. Mfano serikali mbili zitaleta umoja bila kueleza kikamilifu serikali tatu zitavunja vipi umoja. Kuenzi mawazo ya waasisi wa muungano kwa kuacha muundo wa serikali mbili nk. Lakini hoja zote walizokuwa wakiziongelea kuhusu muundo wa serikali zilikuwa ni zile zile. Yaani akiongea mbunge huyu wa CCM tegemea kuwa ataongea vile vile mbunge mwengine wa CCM nakadhalika.

Wajumbe 201 walio wengi kutumiwa na chama tawala kwenye kutetea mawazo ya CCM. Jambo hili lilidhihiri bila ubishi, nakumbuka hata wajumbe wa Ukawa waliposusia vikao na wakati mijadala inaendelea alisimama mama mmoja, simfahamu kwa jina ila alitoka katika kundi la 201. Yeye alisema wazi kabisa, bora wametoka wapinzani tumebaki sisi CCM tujadili kwa utulivu sasa!!

Lakini inatosha kabisa kusema haya yote yaliyokuwa yakiendelea kwa wabunge wa CCM ni kukosa uzalendo. Mimi najiuliza hawa wabunge wa CCM wametokea wapi?? Au ni wa kimbizi, nini uzalendo kwao!!

Uzalendo kwao ni kutetea maslahi ya wakina mzee Mkapa na kuacha historia ya taifa lao ikiangamia. Uzalendo kwao ni kupumbaza hoja ya nchi yetu kukosa mwelekeo wa kikatiba pamoja na migongano kati ya katiba ya Zanzibar na Tanzania bara (Tanganyika).

Nini maana ya uzalendo kwao kama wanapuuza mawazo ya wasomi mbali mbali juu ya muundo wa muungano uliowahi kuzungumzwa hata kabla ya tume ya Warioba!! Wabunge wa CCM wamejaa woga kweli kweli katika kutetea maslahi mapana ya nchi hii. Wengi wao wamekuwa wakitishwa na wakubwa wao kama tu wakienda kinyume na maelekezo yao, akili zao zimeshikiliwa na wakubwa zao.

Nawapongeza sana wabunge wa Zanzibar tena wote kutoka CUF na CCM. Wao walishiriki kuitengeneza katiba mpya ya Zanzibar ambayo iliitambua Zanzibar kama nchi, ikaipa wimbo wa Taifa la Zanzibar pamoja na bendera yake. Wote walisimama katika kuitetea Zanzibar bila kujali wametoka vyama tofauti. Na katika hili naamini kama kungekuwa na uhuru wa kimawazo kama ule ambao walikuwa nao katika kutengeneza katiba yao, wabunge wa Zanzibar wangeungana kama walivyoungana mwanzo katika kuitetea Zanzibar. Lakini katakana na vitisho kutoka kwa wanaowaita wakubwa wameacha misingi na ari ya uzalendo waliokuwa nayo tangu awali.

Jambo la kujiuliza kwanini ari hii ya uzalendo inakosekana kwa wabunge wa huku bara hasa wabunge wa CCM. Hivi kwa wingi wao na wakaamua kusimamia misingi ya rasimu ya katiba na wakaamua kulitetea taifa letu lililozikwa kwa miaka hamsini sasa ni mkubwa gani atawatisha. Wabunge wa CCM ni wengi sana ambao wanaweza kuondoa hali ya kutishana ndani ya chama na kuungana kama wabunge ili kutetea maslahi ya nchi yetu kama ambavyo wanafanya wazanzibari. Kama wataamua kuungana na kuepuka makundi yaliyogawanywa ndani ya chama chao ili kuuvunja umoja wao kwa namna moja au nyingine wataweza kulipigania taifa hili kikamilifu na hakika hakuna atakao watisha tena badala yake italeta hali ya mazungumzo ya namna gani ya kuboresha mawazo yao ya kimapinduzi.

Wito wangu kwa wabunge wa CCM tuamue sasa kulipigania taifa hili, tuamue sasa kuepukana na vitisho ndani ya CCM tulipiganie taifa hili. Huu ndio uzalendo na historia itawakumbuka milele na milele. Tujiulize kama wazanzibari wameweza sisi watanganyika tunashindwa nini!!

Mungu ibariki Tanzania. Wabariki wabunge wote wa Tanzania na uwajaze moyo wa kizalendo. Amen!
 
Back
Top Bottom