Kuelekea 2025: Rais Samia kuvuna kura za vijana, wanawake, wapinzani

Mama Amon

JF-Expert Member
Mar 30, 2018
2,021
2,478

images

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

ZIPO
kila dalili kwamba Dkt. Samia Suluhu Hassan, atagombea nafasi ya urais anayoishikilia sasa katika uchaguzi mkuu ujao – miaka mitatu kutoka sasa.

Mbali na “kufokea” waliozusha kwamba hatagombea na yeye mwenyewe kueleza kwamba atawania nafasi hiyo katika uchaguzi ujao, tayari marais (wastaafu); Jakaya Kikwete na Ali Hassan Mwinyi wametamka mara kadhaa kwamba “hawaoni mtu wa kuchuana na Samia ndani ya chama na hata kwa wananchi.”

Ni kutokana na msingi huo, chama tawala - Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambamo yeye ni mwenyekiti wake, kimepata mgombea wake wa urais 2025.

Pamoja na kupata mgombea wake, CCM na serikali yake – na kupitia kwa Rais Samia mwenyewe, kuna mchakato wa kuhakikisha kwamba kura nyingi za ushindi wa kiti cha urais zinapatikana kutoka kwa wapigakura watakaokuwa na sifa za kushiriki uchaguzi huo.

Tayari Rais Samia na wasaidizi wake; ndani ya chama na serikali wamebaini eneo ambalo lina kura nyingi, eneo la vijana na wanawake, hasa wale walioko maeneo ya vijijini wenye ajira kubwa juu ya ardhi; kilimo.

Hawa ni vijana na wanawake na sasa Rais Samia, pamoja na kutimiza wajibu wake, amebaini fursa ya kuwapa “mbeleko” ili wamkumbuke na kumpa ridhaa ya kuongoza Tanzania, safari hiyo - akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyechaguliwa kwa sanduku la kura.

Rais Samia aliingia ikulu Machi, 2021 baada ya kufariki kwa rais aliyekuwa madarakani, John Pombe Magufuli. Wakati wa utawala wa Rais Magufuli, Samia alikuwa makamu wake.

Wachambuzi wa siasa na uchaguzi wanadai kwamba Rais Samia kuwekeza zaidi kwa vijana na wanawake, anajiwekea mazingira mazuri ya “kubeba” kura nyingi za kumpa nafasi ya kuendeea kuongoza Tanzania.

Dkt. Lenny Kasoga akizungumza na Pambazuko anaeleza kwamba Rais Samia ameona mbali na kwa hakika anapenda kuendelea kuongoza, ndiyo maana anafanya kila analoweza kuhakikisha kundi kubwa la wapigakura wanapewa kipaumbele kwanza.

“Uzuri wa Mama Samia, kwa kufanya hivyo anatekeleza wajibu wake, lakini pia anajenga uwanja utakaobeba hao anaoonekana kuwahudumia zaidi kwa kuwawezesha, sayansi ya siasa na uchaguzi, inaonekana anaicheza vyema sasa,” anaongeza Dkt. Kasoga ambaye ni mhadhiri mstaafu wa vyuo vikuu mbalimbalimbali ndsani na nje ya Tanzania.

Dkt. Kiondo Kalunga, mkurugenzi wa taasisi mpya ya Kivuli anaeleza kuwa Rais Samia “amechagua” fungu jema la kuhakikisha vijana, tena wasiokuwa na ajira za uhakika, wanaingia shambani na kupata ajira muhimu, hivyo hawawezi “kumsahau” kitakapokuja kipindi cha kupiga kura.

Anasema tatizo kubwa la ajira kwa Tanzania liko kwa vijana zaidi na kwamba walikikimbia kilimo kwa kuwa hakukuwa na kitu kinachowavutia na kwamba serikali ilionekana “kukitelekeza” kilimo kwa muda mrefu.

“Kila mara tunaelezwa kilimo ni uti wa mgongo wa Tanzania, lakini serikali ni kama ilikuwa inadanganya, hakuna uwekezaji, hakuna miundombinu inayofaa, hasa huko kunakofanyika kilimo, hivyo hatua ya sasa kuonyesha Rais Samia, amekishikia bango kilimo, kutawavuta vijana wengi kufanya kazi za kilimo,” anaongeza dajtari huyo wa uchumi ambaye taasisi yake inajihusisha na utafiti.

Daktari huyo anapongeza hatua ya Rais Samia kuwaweka wanawake pia katika mipango ya kilimo na biashara zingine ndogondogo kwani kufanya hivyo kutawainua kiuchumi na kuwa na maana halisi ya “walezi wa familia.”

Katika mpango wake wa kuwanufaisha vijana na wanawake, Rais Samia ametangaza kwamba serikali itawawezesha vijana kupitia umiliki wa ardhi na kwamba mchakato huo ndiyo kipaumbele kikubwa cha serikali ya awamu ya sita.

Kwa ajili ya kufanikisha lengo hilo, tayari serikali imetenga hekta 680,000 kwa ajili ya wanawake na vijana, wenye nguvu za kuzalisha chakula cha kutosha na kuuza ziada nje ya nchi.

“Serikali imetenga hadi ekari 10 kwa kila kijana mwenye sifa ambapo baadaye watazimiliki,” amesema Rais Samia, ambaye anaonekana kuilenga nguvukazi ya vijana, wenye kuunda asilimia 45 ya watu wote, kama injini ya mabadiliko ya kiuchumi kupitia sekta ya kilimo.

Rais Samia anasema serikali iko katika mchakato wa kupokea maombi kwa kundi la kwanza la vijana watakaopata fursa ya kupata mafunzo ya miezi mitatu kuanzia katikati ya mwezi Februari halafu wagawiwe ardhi.

Katika kuipa nguvu na uhai zaidi ajenda ya Rais Samia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imekubali kuipatia Tanzania mkopo wa dola za Marekani milioni 120 ajili ya sekta ya kilimo ikiwemo umwagiliaji na kujenga kituo cha usafirishaji na usambazaji mboleo.

Sehemu ya mkopo huu itatumika kwa ajili ya kuanzisha “Mfuko wa Pembejeo kwa ajili ya Dhamana kwa Vijana na Wanawake,” yaani “Agricultural Input Trust Fund.”

Fedha katika mfuko huu zitatumika kuanzisha vituo atamizi kwa ajili ya mafunzo ya vijana, yaani “incubation centres.”

Pia zitatumika kuwawezezesha vijana na wanawake kupata mikopo kwa ajili ya mbolea, dawa za kuua magugu na wadudu.

Mpango wa BBT

Katika kuhakikisha kwamba malengo ya serikali yanatimia, serikali – kupitia Wizara ya Kilimo—imeyunganisha pamoja mawazo haya katika andiko ambalo ni mpango madhubuti unaolenga vijana na wanawake ujulikanao kwa jina la BBT, ambacho ni kifupi cha “Building Better Tomorrow,” yaani ‘Ujenzi wa Kesho Bora.

Ni kwa kuzingatia mpango huu, Rais Samia anasema Tanzania imeamua kuanzisha mpango huo kutokana na idadi kubwa ya vijana kukosa sifa zinazohitajika na taasisi za kifedha wanapoomba mikopo, hivyo kupitia mpango huo, wataweza kupata mikopo kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo.

Pambazuko lina taarifa kwamba tangu kuanzishwa kwa mpango huo wa BBT miezi sita iliyopita, tayari kumetengwa jumla ya hekta 680,000 kwa nchi nzima na shughuli ya kusafisha mashamba hayo imeanza.

Kwa mujibu wa andiko la mradi wa BBT, lililoko kwenye tovuti ya Wizara ya Kilimo, mradi huu utatekelezwa kwa miaka nane, tangu 2022 hadi 2030.

Andiko linataja nadharia ya mabadiliko, kaulimbiu, shabaha, malengo, madhumuni, majukumu, vigezo vya kupima kasi ya ufanisi, na limetaja rasilimali zinazohitajika.

Takwimu zinasema kuwa, asilimia 51 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi na wanaoshughulika na kilimo ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 24.

Hawa hulazimika kufanya kazi katika miradi ya wazazi wao, hasa mashambani, kutokana na changamoto ya kuanzisha miradi binafsi ya kilimobiashara kwa sababu kadhaa.

Sababu hizo ni pamoja na ukosefu wa ujuzi na stadi za kazi; ukosefu wa ardhi; ukosefu wa mtaji wa kifedha; ukosefu wa masoko; ukosefu wa hamasa ya kujiajiri katika kilimo kwa sababu ya fikra kwamba kazi ya kilimo sio mradi unaoweza kuleta tija stahiki kwa wakati mwafaka; na ukosefu wa mfumo wa kuratibu juhudi za vijana walio tayari kwa ajira karika sekta ya kilimo.

Bajeti ya mradi wa BBT

Bajeti kamili ya mradi iliyotajwa kwenye andiko ni Shilingi za Tanzania bilioni 356.199, sawa na dola za Marekani 148,416,167.

Asilimia 24 ya fedha hizo itatokana na bajeti ya Wizara ya Kilimo na TAMISEMI. Na asilimia baki 76 itatoka kwa wadau wa maendeleo, azaki, na makampuni ya sekta binafsi.

Mchanganuo wa jumla wa bajeti hii ni kama ifuatavyo: Eneo la kwanza, yaani kuhamasisha vijana na wanawake (“inspire”), limetengewa shilingi za Tanzania 7,645,000,000; sawa na asilimia 2.1 ya bajeti yote.

Eneo la pili, yaani kuwezesha upatikanaji wa ujuzi na ustadi wa kazi (“empower”), limetengewa shilingi za Tanzania 241,680,000,000; sawa na asilimia 67.8 ya bajeti yote.

Eneo la tatu, yaani kuwezesha upatikanaji wa mitaji na masoko (“engage”), limetengewa shilingi za Tanzania 86,694,000,000; sawa na asilimia 24.3 ya bajeti yote.

Eneo la nne, yaani kuwezesha utendaji kazi katika mazingira yaliyo rafiki kisera na kisheria (“enable”), limetengewa shilingi za Tanzania 1,368,000,000; sawa na asilimia 0.4 ya bajeti yote.

Na eneo la tano, yaani muundo wa usimamizi wa mradi (“coordinate”), limetengewa shilingi za Tanzania 18,811,800,000; sawa na asilimia 5.3 ya bajeti yote.

Samia kuvuna wapinzani

Mbali na nguvu inayowekezwa kwenye kilimo, hasa kupitia kwa vijana, wachambuzi wanaeleza kwamba upo uwezekano mkubwa kwa Rais Samia “kuzoa” kura nyingi kutoka kwa wanachama na mashabiki wa vyama vingine vya ushindani.

Kwamba kufungua milango na kupangua zuio la kukataza mikutano ya hadhara lililowekwa na mtangulizi wake, John Magufuli kwa kipindi cha miaka sa, kunampa fursa ya kupendwa na hata waliokuwa vyama vikubwa vya ushindani; hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo.

“Pamoja na kuonekana hana makeke wala mbwembwe za uongozi, Rais Samia kwa hatua anazochukua kuiweka nchi katika misingi ya usawa na haki kwa kila mmoja, anavuna idadi kubwa ya wapinzani wake, hawa nao watakuwa wapigakura wake kwenye uchaguzi mkuu ujao, “ anasema Obadia Kisonge, ambaye amejitambuisha kwa Pambazuko kuwa ni mwanachama wa ACT-Wazalendo. Anaongeza; “weka maneno haya benki na nikumbushe 2025.”

Muundo wa mradi wa BBT

Mradi wa BBT unayo nadharia ya mabadiliko, kaulimbiu, shabaha, malengo, madhumuni, majukumu, vigezo vya kupima kasi ya ufanisi.

Nadharia ya mabadiliko (“theory of change”) inayoongoza mradi wa BBT ni kama ifuatavyo: Serikali inaamini kuwa, mradi huu utafanikiwa kwa kuzingatia nadharia ya mabadiliko ifuatayo:

Takwimu zinasema kuwa, asilimia 51 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi na wanaoshughulika na kilimo ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 24. Hawa hulazimika kufanya kazi katika miradi ya wazazi wao, hasa mashambani, kutokana na changamoto ya kuanzisha miradi binafsi ya kilimobiashara kwa sababu kadhaa.

Sababu hizo ni pamoja na ukosefu wa ujuzi na stadi za kazi; ukosefu wa ardhi; ukosefu wa mtaji wa kifedha; ukosefu wa masoko; ukosefu wa hamasa ya kujiajiri katika kilimo kwa sababu ya fikra kwamba kazi ya kilimo sio mradi unaoweza kuleta tija stahiki kwa wakati mwafaka; na ukosefu wa mfumo wa kuratibu juhudi za vijana walio tayari kwa ajira karika sekta ya kilimo.

Kwa hiyo, serikali inapendekeza kwamba, kama vijana hawa watahamasishwa kifikra, kuwezeshwa kimitaji, kushirikishwa katika kuanzisha miradi ya kilimobiashara, kupewa ujasiri wa kibiashara, na kuongozwa katika namna ya kusimamia miradi ya kilimobiashara, basi, ajira nyingi zitazaliwa.

Lengo kuu (“impact”) la mradi wa BBT ni kukuza ushiriki wa vijana na wanawake katika kilimobiashara kwa ajili ya kuwawezesha kuwa na kipato endelevu. Kaulimbiu ya mradi huu ni “Kijana Janjika! Kilimo Biashara ndo Mchongo wa Kitaa”.

Malengo ya muda mrefu (“outcomes”) katika mradi wa BBT ni sita. Mosi, ni kuanzisha miradi ya kilimobisahara 2,000 kila mwaka, ili ipatikane miradi 12,000 ndani ya miaka nane ijayo, sawa na mradi mmoja katika kila kijiji cha Tanzania.

Pili, ni kuongeza ajira hadi waajiriwa watano (5) kwa kila kituo cha kilimobiashara, sawa na ajira 60,000 katika miradi yote 12,000.

Tatu, ni kuongeza tija katika sekta ya kilimobiashara. Nne, ni kuongeza kipato cha vijana na wanawake. Tano, ni kuongeza usalama wa kipato.

Na sita, ni kuajiri vijana na wanawake 60,000 katika miradi ya kilimobiashara inayoendeshwa vijijini ili wawe mifano ya kuigwa na vijana baki wapatao milioni 16.

Malengo ya muda mfupi (“outputs”) katika mradi wa BBT yamegawanywa kwenye “maeneo mahsusi ya kimatokeo (key output areas-KOAs)” matano.

Eneo la kwanza ni kuhamasisha vijana (“inspiration”): Dhamira ni kuhamasisha vijana ili wapende kilimobiashara kupitia mawasiliano chanya kuhusu kilimobiashara yanayolenga mabadiliko katika mtazamo na tabia zao.

Eneo la pili ni kuwezesha upatikanaji wa ujuzi na ustadi wa kazi (“empowerment”): Dhamira ni kuwajengea vijana uwezo wa kutumia tekinolojia stahiki na kuwapa ustadi wa ujasiriamali, kwa kutoa mafunzo ya umahiri wa kihasibu, mafunzo kwa vitendo kuhusu ustadi wa kazi, na kuwafanyia ukocha na umenta kupitia program atamizi.

Eneo la tatu ni kuwezesha upatikanaji wa mitaji na masoko (“engagement”): Dhamira ni kuwajengea vijana uwezo wa kupata vitendea kazi, ardhi, huduma za kifedha, mtaji wa kuanzisha biashara, na masoko.

Eneo la nne ni kuwezesha utendaji kazi katika mazingira yaliyo rafiki kisera na kisheria (“enablement”). Dhamira ni kuwawezesha vijana kuanzisha na kuendeleza miradi ya kilimobiashara kwa kuwajengea mazingira bora ya kisera na kisheria, kwa kurekebisha sera na sheria kandamizi kuhusiana na mkakati wa kuwawezesha vijana katika kilimo, kilimo cha mkataba, kukodi ardhi, usalama wa ardhi na maji, na matumizi ya mali zinazohamishika kama dhamana ya mkopo.

Na eneo la tano ni muundo wa usimamizi wa mradi (“coordination”). Dhamira ni kuunda mfumo wa kuratibu, kufuatilia na kutathmini maendeleo ya miradi ya kilimobiashara, wenye kushirikisha azaki na taasisi baki zinazounga mkono kilimobiashara.

Majukumu yatakayotekelezwa chini ya mradi wa BBT (activities) ni kama ifuatavyo, yakiwa yametofautishwa kwa kuzingatia maeneo mahsusi ya kimatokeo (KOAs):

Katika eneo la kwanza, yaani kuhamasisha vijana na wanawake (“inspiration”), kuna majukumu ya aina mbili.

Jukumu la kwanza ni kumsajili mtaalam mshauri wa kuzalisha na kusambaza taarifa zitakazosaidia kuleta mabadiliko ya kimtazamo katika akili za vijana na wanawake ili wapende kilimobiashara.

Na Jukumu la pili, ni kuanzisha mtandao wa mawasiliano utakaojumuisha chama cha vijana wajasiriakilimo Tanzania, na kuutumia mtandao huu kuendesha mijadala ya kubadilisha fikra za vijana na wanawake.

Katika eneo la pili, yaani kuwezesha upatikanaji wa ujuzi na ustadi wa kazi (“empowerment”), kuna majukumu ya aina mbili pia.

Jukumu la kwanza, ni kuendesha mafunzo nje ya kazi, mafunzi kazini katika mashamba ya kibiashara, na mafunzo kupiti vituo atamizi.

Na Jukumu la pili ni kuwaunganisha vijana pamona na mtandao wa wasambazaji wa pembejeo na tekinolojia za kilimo ili waweze kuzipata kwa njia ya kuazima au kukopeshwa.

Katika eneo la tatu, yaani kuwezesha upatikanaji wa mitaji na masoko (“engagement”), kuna majukumu ya aina nne.

Jukumu la kwanza, ni kuwapatia vijana ardhi ya kilimo, na kasha kuwamilikisha rasmi ardhi hiyo, ama mmoja mmoja au katika vikundi.

Jukumu la pili, ni kuwaunganisha vijana na taasisi za kifedha ili wapate mitaji ya kifedha kwa ajili ya kuanzisha biashara pamoja na huduma za kifedha zinazoambatana na mitaji hiyo.

Jukumu la tatu, ni kuwaunganisha vijana na masoko ya ndani nan je ya nchi kwa njia ya mafunzo, kukusanya na kusambaza taarifa za masoko, upatikanaji wa mghala na vifungashio.

Na jukumu la nne, ni kuwaunganisha vijana na mtandao wa huduma za ushauri, ukocha na umenta katika sekta ya kilimobiashara

Katika eneo la nne, yaani kuwezesha utendaji kazi katika mazingira yaliyo rafiki kisera na kisheria (“enablement”), kuna majukumu yanayohusiana na utafiti na marekebisho ya sera na sheria zisizo rafiki kwa vijana; na mafunzo kwa vijana kuhusiana na mabadiliko hayo.

Na katika eneo la tano, yaani muundo wa usimamizi wa mradi (“coordination”), kuna majukumu ya aina mbili.

Jukumu la kwanza ni kuunda mfumo wa kufuatilia na kutathmini utendaji kazi wa miradi ya vijana, utakaohusisha azaki, wafanyabiashara na wadau baki katika sekta binafsi.

Na jukumu la pili ni kusimamia na kuratibu uendeshaji wa miradi ya kilimobiashara inayoendeshwa na vijana.

Walengwa wa mradi wa BBT

Mradi wa BBT umelenga kuwanufaisha vijana wa kike na kiume wapatao miliono 16. Kati yao, vijana milioni 10 wana umri kati ya miaka 15 hadi 24; na vijana milioni sita wana umri kati ya miaka 25 hadi 34.

Vijana hawa wametawanyika kwenye kaya zipatazo milioni nane, zilizoko kwenye vijiji 12,345; sawa na wastani wa kaya 667 kila kijiji.

Kikanda, mradi huu unalenga kuvinufaisha vijiji vifuatavyo: Kanda ya Kati, vijiji 1,021; Kanda ya Mashariki, vijiji 1,089; Kanda ya Ziwa, vijiji 3,118; Kanda ya Kaskazini, vijiji 2,132; Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, vijiji 2,644; Kanda ya Kusini, vijiji 1,309; na Kanda ya Magharibi, vijiji 1,032.

Staili ya utekelezaji wa BBT

Utekelezaji wa mradi wa BBT utatumia staili (“approach”) ifuatayo: Kwanza ni usajili wa idadi kubwa ya vijana, angalau 200,000. Vijana hawa watagawanywa kwenye makundi manne tofauti.

Kundi la kwanza ni vijana walio katika miradi ya kilimobiashara iliyopo tayari. Kundi la pili ni vijana wasio katika miradi ya kilimobiashara. Kundi la tatu ni vijana wenye mafunzo rasmi ya kilimobiashara. Na kundi la nne ni vijana wasiopenda kilimobiashara.

Baada ya uhamasishaji na uwezeshaji stahiki idadi ya vijana 200,000 itachujwa taratibu hadi kufikia lengo la vijana 60,000 watakaokuwa wanaendesha miradi 12,000 ya kilimobiashara vijijini.

Hatimaye, vijana hawa 60,00 wataambukiza hamasa, ujuzi na ustadi kwa vijana wenzao wapatao milioni 16.

Minyororo ya thamani inayokusudiwa

Mradi wa BBT utatekelezwa kwa kuelekez nguvu za serikali katika minyororo ya thamani katika kilimo (agricultural value-chains) yenye kuhusisha mazao yenye soko, ama ndani au nje ya nchi.

Andiko la mradi linataja minyororo ya thamani ya aina kuu mbili.

Kwanza, kuna minyororo ya thamani inayohusisha mazao ya “horticulture,” yaani: mboga, matunda, na viungo.

Na pili, kuna minyororo ya thamani inayohusisha mazao ya nafaka. Katika kila mnyororo ya thamani serikali inapanga kuhakikisha kwamba mazo husika yanaongezewa thamani kupitia usindikaji stahiki, utakaofanyika kwa msaada wa tekinolojia za kisasa katika sekta ya kilimo.

Mfumo wa utekelelzaji wa mradi

Mradi wa BBT utasimamiwa na Wizara ya Kilimo na kutekelezwa katika vijiji vilivyo chini ya TAMISEMI.

Aidha, Wizara ya Fedha; Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu; pamoja na Wizara ya Sayansi, Tekinolojia na Elimu ya juu zinahusika katika mradi huu.

Kadhalika, azaki, makampuni ya sekta binafsi, taasisi za kifedha, na taasisi baki zilizo rafiki wa sekta ya kilimo kupitia usambazaji wa pembejeo, tekinolojia na ushauri zitashiriki pia.

BBT na mazingira yake ya kimkakati

Utekelezaji wa mradi wa BBT, ni sehemu ya mikakati kadhaa inayotekelezwa na Wizara ya Kilimo. Mikakati hiyo imetajwa kwenye Dira ya Taifa Kuelekea mwaka 2025; Mpango wa tatu wa maendeleo ya taifa wa miaka mitano (2020-2025); na Mkakati w a Pili wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo, yaani ASDP-II (2016–2025).

Hivyo, kwa sehemu fulani, ufanisi wa mradi wa BBT utategemea umakini wa serikali katika kuhakikisha kwamba mradi huu unasikilizana na mazingira mapana ya kimkakati yaliyopo.

Chanzo: Pambazuko, Toleo Namba 029
 
Kutakuwa na katiba mpya na tume huru ya uchaguzi?
 
Nimesoma kwa umakini sana na nimegundua kuwa hili ni eneo jingine ambalo fedha nyingi zinaenda kupigwa bila mafanikio yoyote. Ukiangalia empowerment imechukua bajeti kubwa sana kiasi cha tzs 241,680,000,000/= fedha hizi zinaenda kuliwa na maafisa kilimo pamoja na watu wa wizara husika.

Hizi zitatumika kwenye mafunzo ya hawa vijana ambayo ni asilimia 67.8 ya bajeti yote.swali langu je ni taasisi ambayo itaweka pesa zao kwenye kilimo cha kubahatisha?

Mimi nilidhani labda wataanza na mabwawa ya umwagiliaji,mafunzo na mwisho hiyo engagement.tunaambiwa hiyo engagement nayo itatafuna tzs 86,694,000,000. Hizo zote nazo zitaingia kwenye mifuko ya watu. Huu mradi hautofautiani sana na mabilioni ya JK na zile fedha zinazotengwa na halmashauri kwa ajili ya makundi mbali mbali.

Huna mambo mengi ktk huu mradi ambayo ni kufikirisha zaidi kama masoko, mitaji, implementts,mbolea pia implementation ya mradi mzima ijapokuwa kuna bra bra nyingi kwenye andiko lenyewe.in short huo mradi hautakuwa feasible.

Tusubiri tuone tutakutana humu ndani.
 
Vijana na wanawake? Wanaume mnawaacha wapi. Mzungumzieni Rais kwa kwa kazi anazofanya kwa watanzania. Wanawake wenyewe ndio sisi wengi tunaoamini akili na fikra za waume zetu ni bora zaidi,mnatusemea? Rais analenga makundi yote,acheni ubaguzi hadi kwenye target ya kura or keep it to yourself.
 
Samia anaweza kuwa Rais wa kwanza kuungwa mkono na vyama vyote
Chadema wanamkubali, ACT wanamkubali, CUF
Wameachiwa kufanya mikutano ila unoana wanavyompngeza
 
Mwaka 2015 nilimpigia kura Mwendazake. Mwaka 2020 nikampigia Tundu Lisu. Mimi ni CCM haswaaa na nafasi chamani ninayo. Mwaka 2025, hata iweje nitampigia Samia.

Ulichokwishafanya kuhusu kuimarisha demokrasia kwangu inatosha sana sana sana sana sana sana! Samia wewe ni mwanaume zaidi hata hata ya Mwendazake - Mwanaume wa kweli ni yule asiyetumia ubabe.

Mwanaume wa kweli ni yule anayekubali ngumi ya mpinzani wake imguse, apate hasira, ajipange, aandae ngumi yake then ampige vizuri mpinzani wake. Mama wewe ni MWANAUME!
 
Mwaka 2015 nilimpigia kura Mwendazake. Mwaka 2020 nikampigia Tundu Lisu. Mimi ni CCM haswaaa na nafasi chamani ninayo. Mwaka 2025, hata iweje nitampigia Samia...
Kalelewa kwenye jamii ya wasitarabu sio kama yule jama wenu wa kule
 
Kipimo cha haya uliyoandika ni wakati wa uchaguzi, pale ambapo patakuwepo na mchakato wa haki kwenye zoezi zima, kuanzia kupiga kura, kuhesabu, mpaka kutangaza matokeo, aliyeshinda kihalali apewe ushindi.

Sio kudanganyika kirahisi wakati huu ambao hana chakupoteza, anajua kila eneo muhimu lipo chini ya chama chake, hasa kule bungeni, tusubiri tuone kama matokeo ya uchaguzi yakiwa magumu kwa chama chake atakuwa jasiri ayaache kama yalivyo.
 
Mwaka 2015 nilimpigia kura Mwendazake. Mwaka 2020 nikampigia Tundu Lisu. Mimi ni CCM haswaaa na nafasi chamani ninayo. Mwaka 2025, hata iweje nitampigia Samia...
Nafikiri ni issue binafsi wewe na Mheshimiwa, jaribu kumfikishia taarifa, sisi hatuhusiki
 
Back
Top Bottom