Kubaki CCM ndiyo gamba, kuondoka ni kulivua | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kubaki CCM ndiyo gamba, kuondoka ni kulivua

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Molemo, Apr 19, 2012.

 1. M

  Molemo JF-Expert Member

  #1
  Apr 19, 2012
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 13,287
  Likes Received: 580
  Trophy Points: 280
  SUALA LA OLE MILLYA

  UAMUZI wa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James ole Millya, kuondoka CCM na kujiunga na CHADEMA ndilo gumzo la wiki hii.
  Uamzi huo wa Mwenyekiti huyo wa zamani wa UVCCM Mkoa wa Arusha umewashtua watu wengi na katika mshtuko huo, wengi wamejikuta wakisema maneno yanayoonyesha kuchanganyikiwa.
  Yeye mwenyewe amesema amechoka kuishi kwa matumaini; amechoka kupanda gari lenye pancha na mengine ya kawaida kwa wanaohama vyama. Makala hii ingependa kujishughulisha zaidi ya tafsiri ya viongozi wa CCM kuhusu kuondoka kwa James ole Millya.
  Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa alipoulizwa na Waziri Mkuu wa sasa Mizengo Pinda kuhusu kuondoka kwa Millya, alimjibu kwa maneno mafupi tu kuwa "hayo ndiyo mambo ya vijana".
  Kwangu mimi, nayaona majibu hayo kama ni mwendelezo wa msimamo wa siku nyingi wa Edward Lowassa, kuwa CCM isiwaingilie vijana, iwaache wafanye kazi ya siasa kwa uhuru na ikilazimika iwashauri pasipo kuwatisha. Msimamo huo unajidhihirisha katika majibu aliyompa Pinda katika uwanja wa ndege wa Arusha kabla ya kurejea Dodoma, Jumatatu alasiri.
  Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM Benno Malisa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Arusha Ole Nan'gole walikuwa waangalifu na kusema kuwa wameshtushwa na uamuzi wa James Millya. Haihitaji akili nyingi kujua kuwa watu hawa wawili wameguswa sana na uamuzi wa Millya kwa sababu unakigusa na kukitikisa chama wanachokiongoza.
  Walionishtua kwa kauli zao ni Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye, na Katibu Mkuu wa UVCCM Martin Shigella. Hawa walidai Millya alikuwa ni mzigo kwa chama, na kuwa kwa kujiondoa mwenyewe kwenye chama ametekeleza uamuzi wa NEC wa kujivua gamba.
  Mapema mwaka jana, NEC ya CCM ilifanya maamuzi tata yaliyozua mjadala kuwa viongozi na wanachama wa CCM ambao ni mzigo kwa chama wajitathmini na kufanya maamuzi ya kujiondoa wenyewe kabla chama hakijawaondoa.
  Kwa mantiki hiyo, Shigella na Nape Nnauye wanaona ole Millya amejivua gamba, na ndivyo baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti tukio hilo. Napenda nikubaliane nao kwa sehemu lakini nitoe maelezo.
  NEC ya CCM ilifikia uamuzi kuwa kuna viongozi na wanachama ni mzigo wa chama. Ikaagiza viongozi hao na wanachama wajiondoe (wajivue gamba). Kwa maana nyingine, kuondoka ndiko kujivua gamba, na kubaki ndani ya CCM ni kubaki na gamba. Hii ni mantiki inayotokana na matamko mepesi ya viongozi wa CCM.
  Nayaita matamko mepesi kwa sababu haiingii akilini kuwa mtu aliyekuwa kiongozi ndani ya chama kwa ngazi ya juu kama ole Millya, ghafla aambiwe ni gamba, tena mara baada ya kutangaza uamuzi wa kujiondoa katika chama.
  Ikiwa alikuwa ni mzigo ni kitu gani kilikuwa kinakizuia chama kumuondoa mpaka kifikie hatua ya kumbembeleza aondoke mwenyewe, na akiishakuondoka ndipo chama kipate "mshipa" wa kusema alikuwa ni gamba!
  Kinachoonekana wazi katika mnyukano huu wa kimaslahi ni kuwa, NEC ilibaini kuwa "umagamba" (rushwa, ufisadi, uzembe, wizi, fitna, makundi, himaya, n.k) umekilemea chama, na hakuna mtu aliye na uthubutu wa kumwambia mwenzake aondoke, na ndiyo maana wakaamua sasa aliyechoka aondoke mwenyewe!
  Ikiwa fikra zangu hizi na tafsiri zangu zisizo rasmi katika vikao vya CCM zina ukweli wowote, basi wale wanaoondoka ndio wanaovua gamba la rushwa, ufisadi, uzembe, fitna, himaya, makundi na wizi wa mali ya umma. Kwa mantiki hiyo hiyo, wanaobaki ndani ya CCM ndiyo bado wamevaa magamba ikiwa kuondoka ndani ya CCM maana yake ni kujivua gamba.
  Niliwahi kuandika nikashutumiwa na kutishiwa uhai wangu niliposema hata Mwenyekiti wa chama hicho ni gamba, kama CCM yenyewe ilivyo gamba kwa Taifa letu.
  Ole Millya bila kumung'unya maneno amesema wazi kuwa chini ya CCM, umasikini umeongezeka, rushwa imeongezeka, vijana hawana ajira na Watanzania hawana matumaini.
  Kilichobaki ndani ya CCM ni makada wanaoishi kwa matumaini ya kuteuliwa kuwa wakuu wa wilaya, mikoa, wakurugenzi na kuingia katika bodi za ulaji katika makampuni tuliyowakabidhi wageni.
  Ole Millya anaweza kuwa amefanya mahesabu mabaya kisiasa, hilo si langu kwa sasa. Lakini kwamba kwa hatua ya kujiondoa CCM na kujiunga na CHADEMA kutafsirika kuwa ni kujivua gamba, hilo naliunga mkono, kwa kadri ya kwamba kubaki CCM ni sawa na kuendelea kung'ang'ania gamba. Mashiko ya hoja yangu ni pale ambapo gamba linamaanisha madhambi niliyoorodhesha hapo juu, likiwamo baba la madhambi hayo-ufisadi. Si siri tena kuwa, kuwa mwana CCM katika enzi hizi kunamaanisha kuwa muumini wa ufisadi na madhambi ya namna hiyo.
  Watu safi wachache walio katika chama hicho wanapata taabu sana kujitetea mbele ya watu na kueleweka. Kwa hatua ya mtu mmoja kama ole Millya kuchukua hatua ya kuondoka ndani ya CCM ameweka mfano uliowashinda wengi, tena ambao wameendelea kudhalilika kila kukicha na hata kuteswa dhamiri zao kwa ajili ya chama kinachokumbatia ufisadi.
  Ole Millya amekubaliana na kada mmoja wa CHADEMA ambaye huwa anasema na kuamini kuwa ni "heri ya kufa umesimama, kuliko kuishi umepiga magoti".
  Kuondoka CCM au kubaki ndani ya CCM, kwa sasa ni suala la kuchagua hasara iliyo ndogo. CCM kimekuwa chama kisicholeta matumaini kwa wapenzi na maadui wake. Viongozi wa CCM hawana furaha nacho, na hata wale vinara wake kitaifa wanaishia kutoa mawazo yao kupitia mitandao ya kijamii kuliko kuzungumzia ndani ya chama.
  Viongozi hawa wamefikia hatua ya kujificha nyuma ya majina ya bandia kama mimi "Msomaji Raia" na kutisha watu, kukibomoa chama na kufanya fitna mbalimbali wakati wana nafasi ya kutoa maoni yao ndani ya CCM wakasikilizwa.
  Kwa ole Millya kuondoka CCM ni hatua ya ujasiri uliokuwa chanzo cha kukua na kukomaa kwa TANU, ASP na baadaye CCM. Viongozi watangulizi wa vyama hivyo walifanya maamuzi magumu, yaliyohatarisha mistakabali yao kisiasa.
  Walihesabu mafao ya baadaye kuliko mafao ya wakati huo. Mwalimu Julius Nyerere alijiuzulu ualimu kuingia siasa, alijiuzulu uwaziri mkuu ili kuimarisha TANU, alijiuzulu urais akabakia Mwenyekiti wa CCM ili kuimarisha chama.
  Alistaafu akaenda kukaa kijijini ili kuthibitisha kuwa aliyokuwa akiyasimamia na kuyafundisha yanatekelezeka. Katika medani ya kimataifa, Mwalimu alivunja uhusiano wa kibalozi na Uingereza ili kuweka wazi msimamo wa Taifa letu katika masuala ya heshima ya mtu Mweusi.
  Kwa kufanya hivyo alihatarisha maslahi ya Taifa letu changa wakati huo. Hali kadhalika, Mzee Karume wa Zanzibar alikubali kwa hiari yake kuingia katika Muungano na Tanganyika. Kwa njia hiyo akahatarisha maisha yake na maslahi binafsi ya Visiwa vile ili kujenga eneo imara machoni mwa mataifa ya kibeberu wakati huo.
  Nayasema haya ili kuonyesha kuwa alichokifanya ole Millya ni kuendeleza utamaduni wa kujitoa mhanga na kupoteza mafao ya muda kwa ajili ya manufaa ya wengi kwa baadaye. Manufaa hayo yanaweza kuchelewa na kuwafanya wapinzani wa ole Millya wamcheke, lakini kamwe manufaa ya umma hayawezi kupotea.
  Kigugumizi walicho nacho wengi wa makada wa CCM kuondoka ndani ya CCM ni cha woga usio na maana. Aidha, kigugumizi walicho nacho makada hao kukikosoa chama chao wazi wazi au ndani ya vikao vya chama, ni dalili ya wao kukubaliana na uozo unaoendelea. Kwa yote mawili, CCM ikizama wakiwa bado na kigugumizi hicho, watazama nacho maana wakati huo, hata kuaminika mbele ya jamii kutakuwa kumepungua sana.

  Na Mwandishi:Msomaji Raia wa RAIA MWEMA
   
 2. M

  Molemo JF-Expert Member

  #2
  Apr 19, 2012
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 13,287
  Likes Received: 580
  Trophy Points: 280
  Hakika hii habari imetulia mno.
   
 3. Lyimo

  Lyimo JF-Expert Member

  #3
  Apr 19, 2012
  Joined: Mar 7, 2006
  Messages: 3,828
  Likes Received: 33
  Trophy Points: 145
  Kama GAMBA limegoma kuvuka ukalitupa huko, basi ni wewe kuchomoka kwenye gamba na kuwa safi.
   
 4. N

  Nali JF-Expert Member

  #4
  Apr 19, 2012
  Joined: Mar 31, 2010
  Messages: 825
  Likes Received: 248
  Trophy Points: 60
  UKo juu, Ole Millya ni Mkombozi na chachu kwa mabadiliko ya kweli na historia nzuri katika Nchi!
   
 5. Ngalikivembu

  Ngalikivembu JF-Expert Member

  #5
  Apr 19, 2012
  Joined: Oct 6, 2010
  Messages: 1,908
  Likes Received: 355
  Trophy Points: 180
  Namkubali sana Msomaji Raia huwa napenda kwanza kuisoma habari yake ndipo niwatafute wengine.Huyu naona ni mtu wa jikoni haswa anayeyajua mambo ya huko.taarifa zake nyingi zina uhakika.
   
Loading...