Kuanzia utawala wa Nyerere hadi Kikwete, Watanzania tunakwenda wapi?

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,112
0001kikwete.jpg

Na Mwandishi Wetu
MIAKA 50 ya uhuru wa Tanganyika imetimia huku Tanzania ikiwa bado haijatimiza malengo ya kudai uhuru yaliyokuwa na kibwagizo cha ‘Uhuru na Kazi’, au hata kuwashinda maadui watatu wakuu yaani, umaskini, ujinga na maradhi.

Licha ya nia njema ya rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere ya kupunguza umaskini na kuimarisha hali za jamii, lakini alishindwa kuinua uchumi na kuipeleka nchi yake katika anguko la uchumi.

Miaka ya 1980, Tanzania ilianza kulegeza masharti ya uchuni na kutokana na anguko la ukomunisiti katika miaka 1990, nchi ikaingia kwenye mfumo wa vyama vingi.

Kwa miongo miwili iliyopita, Tanzania imekuwa ikikua kiuchumi na kisiasa, lakini wakati huo huo, kiwango kikubwa cha umaskini, rushwa na utendaji hafifu wa serikali vinaendeleza changamoto katika kuleta maendeleo na demokrasia ya kweli.

Mchakato wa kuandikwa upya kwa katiba unatoa fursa mpya kwa kwa Watanzania kujenga msingi mpya wa kufikia malengo ya uhuru kwa kuondoa umaskini na na uhuru wa kisiasa.

Historia ya Tanzania

Historia ya Tanzania inaanzia mbali, kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni na baada ya kupata uhuru.

Mbali na mwingiliano wa mataifa mengine kama vile ya kirabau nay a Ulaya, Tanganyika ilianza kutawaliwa rasmi na Wajerumani mwaka 1885 ambao walitawala hadi mwaka 1918 wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia. Katika vita hiyo, Ujerumani iliyokuwa ikitawaliwa na dikteta Adolf Hitler ilishindwa na kunyang’anywa makoloni yake ya Afrika ikiwamo Tanganyika.

Mwaka 1919, Uingereza iliichukua Tanganyika na kuifanya kuwa kama mdhamini wake (Protectorate) hadi itakapopata uhuru. Hata hivyo, Uingereza iliendelea kuitawala Tanganyika kiuchumi, kisiasa na kijamii, hadi mwaka 1961.

Tofauti kati ya watawala hao wawili ni kwamba, Ujerumani ilitawala moja kwa moja bila kushirikisha watawala wa kijadi waliokuwepo, wakati Uingereza iliwatumia watawala hao kutimiza malengo yao.

Vuguvugu la Vita ya Pili ya Dunia lililomalizika mwaka 1945, lilichangia kuwapo kwa wazalendo walioanza kudai uhuru.
Mwaka 1954, wazalendo wa Tanganyika walianzisha chama chao, TANU chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere baada ya kukiboresha kilichokuwa chama cha wafanyakazi , TAA.

Chama hicho ndicho kilichowaongoza Watanganyika kupata uhuru wao mwaka 1961. Mbali na TANU, kulikuwa na vyama vingine vya siasa kama vile ANC, AMNUT na UTP.

Baada ya kupata uhuru, uchumi wa Tanganyika kwa kiasi kikubwa na wazalishaji wadogo, huku wamiliki wakubwa wa uchumi wakiwa ni wenye asili ya Kiasia.

Kipindi hicho pia kilishuhudia Tanganyika ikijiunga na Jumuia ya Afrika Mashariki iliyozihusisha nchi za Kenya, Uganda na Zanzibar. Jumuia hiyo ilizishirikisha nchi hizo katika huduma za reli, bandari, anga, posta na simu, ushuru na forodha.
Licha ya jumuia hiyo kuwa na malengo ya kuziunganisha nchi hizo kifedha na kisiasa, ilikufa mwaka 1977.

Mwaka 1964, Tanganyika iliungana na Zanzibar na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku vyama vya TANU na ASP vikitawala. Vyama hivyo viliendelea kutawala hadi mwaka 1977 vilipoamua kuungana na kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM).

Utawala wa Mwalimu Nyerere

Akiwa rais wa kwanza wa Tanganyika na baadaye Tanzania, Mwalimu Nyerere aliasisi na kutumia sera ya Ujamaa na Kujitegemea na mwaka 1967 alianzisha Azimio la Arusha lililonadi sera hiyo.

Chini ya mfumo wa chama kimoja ulioanzishwa rasmi mwaka 1965, Mwalimu Nyerere alieneza sera yake. Mwaka 1967 alitaifisha mashirika yote yaliyokuwa yakimilikiwa na watu binafsi na kuyafanya kuwa ya Serikali. Mwaka 1974 aliasisi vijiji vya ujamaa ambavyo hata hivyo havikufanikiwa sana.

Mbali na hayo Ujamaa ulilenga kuondoa umasikini na kuleta usawa kwa kufanya kazi kwa pamoja na kuboresha huduma za jamii na kupunguza utegemezi wa wahisani. Azimio hilo pia liliweka misingi ya maadili ya uongozi kwa wanasiasa na watumishi wa umma.

Mwalimu Nyerere alifanikiwa kudumisha umoja wa Watanzania ambao uliimarisha amani. Katika kipindi chake, Tanzania ilishinda vita vya Uganda vilivyomng’oa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Idd Amin Dada.

Vilevile, chama tawala CCM kimeendelea kubadilisha viongozi wa nchi kwa amani, huku Tanzania ikiendelea kuheshimika kimataifa.

Hata hivyo, hadi mwaka 1985 wakati Mwalimu Nyerere anastaafu, hali ya uchumi ilikuwa mbaya, huku kukiwa na uzalishaji hafifu katika kilimo, kupanda kwa mfumuko wa bei, kuibuka kwa masoko holela, madeni mengi na nchi kurejea katika utegemezi kwa wahisani.
Mfumo wa chama kimoja ulidhoofisha utendaji wa bunge, huku haki za binadamu zikikandamizwa, vyama vya kiraia navyo havikupewa nafasi, huku watumishi wa umma na vyombo vya dola kama vile polisi na jeshi vikiwa vyombo vya chama tawala.

Baada ya kustaafu kwa Mwalimu Nyerere, ilipendekezwa kuwa kipindi cha urais kiwe ni kwa miaka 10 kilichogawanyika katika awamu mbili za miaka mitano.

Utawala Rais Ally Hassan Mwinyi

Mwaka 1985, Ally Hassan Mwinyi alishika madaraka kama rais wa pili wa Tanzania. Tofauti kubwa kati ya utawala wa Mwalimu Nyerere na Mwinyi ni kubadilika kwa sera za Ujamaa na Kujitegemea kwenda kwenye mfumo wa soko huria.

Kwa kiasi kikubwa, Mwinyi alikubaliana na masharti ya vyombo vya fedha vya kimataifa (Benki ya Dunia- WB) na Shirika la Fedha Ulimwenguni-IMF).

Masharti hayo ni pamoja na mipango ya kubana matumizi kwenye huduma za jamii, mfumo wa soko huria na biashara ya nje na kuanzishwa kwa vyama vingi vya siasa.

Mfumo wa vyama vingi

Mfumo wa vyama vingi ulirejeshwa mwaka 1992 baada ya Rais Mwinyi kuunda tume iliyokuwa chini ya Jaji Mkuu wa Tanzania Francis Nyalali (hayati0 ambayo ilikuwa na kazi ya kuwauliza Watanzania kama wanakubaliana na mfumo huo au vipi.

Matokeo ya tume hiyo yalionyesha kuwa, asilimia 80 ya Watanzania bado walitaka kuendelea na mfumo wa chama kimoja huku asilimia 20 tu ndio waliotaka vyama vingi.

Hata hivyo, Serikali ililazimika kuukubali mfumo wa vyama vingi ili kukubaliana na masharti ya nchi wahisani na vyombo vya fedha vya kimataifa.

Licha ya kurejeshwa kwa mfumo huo, bado Serikali iliendelea kuteua vyombo vya kusimamia uchaguzi (Tume za Uchaguzi) bila kuvishirikisha vyama vyote vya siasa hali iliyoendelea kuzua wasiwasi wa uhali wa uchaguzi.

Pamoja na kubadilishwa kwa mifumo hiyo, bado maendeleo hayakupatikana, badala yake, kulikuwa na ongezeko la vitendo vya rushwa vilivyoashiria kuporomoka kwa maadili ya uongozi wa umma na wanasiasa.

Utawala wa Rais Benjamin Mkapa

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa aliikuta nchi ikiwa katika hali mbaya kiuchumi.
Hata hivyo, hakutofautina sana na Mwinyi isipokuwa aliongeza mapato katika bajeti ya Serikali kutokana na misaada ya wahisani.

Alijitahidi pia kurudisha imani ya wahisani kwa kupunguza madeni ya Serikali.

Vilevile, alizidisha kubinafsisha mashirika ya Serikali kwa kuunda Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC).

Vilevile, Mkapa alichochea uwekezaji kwenye rasilimali za umma kama vile madini, misitu na wanyamapori.

Pamoja na mazuri mengi aliyofanya, Mkapa ambaye alitangazwa kuwa mtu safi na Mwalimu Nyerere alipokuwa akimpigia debe kwa mara ya kwanza, hadhi yake ikaanza kuchafuka.

Kuchafuka huko kulitokana na kashfa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujianzishia biashara binafsi wakati akiwa Ikulu, kununua ndege ya kifahari ya rais, ununuzi wa rada kutoka Kampuni ya BAe System ya Uingereza kwa dola za Marekani 40 milioni badala ya bei halisi ya dola 5 milioni.


Pia, wizi wa fedha za Malipo ya Akaunti ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT)na kuwauzia nyumba za serikali watumishi wa Serikali na viongozi wa CCM.

Mbali na hayo, Mkapa pia alipambana na watu walioonekana kumkosoa. Katika wakati wake, Mkapa hakuwa na urafiki mzuri na vyombo vya habari.

Vilevile, alipambana na viongozi wa vyama vya upinzani kiasi cha kusababisha machafuko. Kwa mfano mauaji ya wafuasi wa CUF Januari 27 2000 kisiwani Pemba.

Utawala wa Rais Jakaya Kikwete

Kama ulivyo mtiririko wa marais kuanzia kwa Mwinyi, utawala wa Rais Kikwete umeendelea kuwa huria, tangu kwenye uchumi hadi siasa.

Kikwete aliyeingia madarakani ikiwa ni miaka 10 tangu alipojitokeza kwa mara ya kwanza mwaka 1995, ambapo aliwekwa kando ili kumpisha Mkapa amekuwa zaidi msemaji kuliko mtendaji.

Lakini, miaka 10 aliyokaa pembeni alitumia vyema mtandao wake kujijenga kifedha na kifalsafa. Mtandao huo uliundwa na watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Katika kampeni zake aliahidi maisha bora kwa kila Mtanzania, ahadi ambayo hadi leo imeshindikana.

Akiwa katika awamu yake ya pili ya urais, Kikwete ameshindwa kusimamia uchumi kiasi cha kuporomoka thamani ya Shilingi kutoka sh1,000 kwa dola ya Marekani aliyoikuta wakati wa Mkapa hadi sasa Sh1,700.


Mfumuko wa bei umepanda kutoka asilimia sita hadi asilimia 19, huku utendaji wa nchi kimataifa (International Development Association Country Performance) ukishuka kutoka nafasi ya nne hadi ya 22.


Katika kipindi hicho pia, kumeshuhudiwa, kushuka kimaadili kwa viongozi wa umma na wanasiasa, huku mwenyewe akilaumiwa kwa kuwa na safari nyingi nje ya nchi zisizokuwa na faida kwa Taifa.
Hata hivyo, Kikwete anasifika kwa kuongeza uhuru wa vyombo vya habari na kuruhusu kuwepo kwa mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya.


Rais Kikwete ndiye kiongozi pekee wa nchi aliyeruhusu waziri mkuu wake, Edward Lowassa ajiuzulu kwa kashfa ya mradi tata wa umeme wa dharura wa Richmond.


Matatizo yanayoikumba Tanzania
Hadi sasa Tanzania inakabiliwa na umaskini mkubwa, rushwa kubwa na ndogo, ukuaji mkubwa idadi ya watu, ukosefu wa mitaji, uzalishaji mdogo wa kilimo na miundombinu hafifu.
Nini kifanyike?

Wakati Kikwete akimalizia muda wake madarakani miaka mitatu ijayo, Watanzania wana changamoto kubwa ya kutafuta rais mwingine.

Msuguano wa makundi ndani ya CCM unaweza kuleta rais mzuri kama utatumika vizuri. Kama Watanzania watakuwa na utashi mzuri wa kisiasa wanaweza kuibuka vyema kidemokrasia katika Afrika.

chanzo. Kuanzia utawala wa Nyerere hadi Kikwete, Watanzania tunakwenda wapi?
 
Back
Top Bottom