Buchanan
JF-Expert Member
- May 19, 2009
- 13,199
- 1,969
- PROFESA MWAKYUSA ATAKA MAELEZO YA DAKTARI
WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa ametaka kupewa maelezo ya kina kuhusu afya ya Rais Jakaya Kikwete ikiwa ni siku chache baada ya kiongozi huyo wa nchi kudondoka wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za CCM kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaa.
Tukio hilo la kuanguka kwa Rais Kikwete la Agosti 21 mwaka huu ni la tatu tangu mwaka 2005 baada ya kuanguka siku ya mwisho ya kampeni za CCM mwaka 2005 na kuishiwa tena nguvu mwaka jana wakati akihutubia waumini wa Kanisa la AIC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba. Pia imeripotiwa kuwa aliwahi kuanguka nchini Ubelgiji wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Alipodondoka mwaka 2005, ilielezwa kuwa ilitokana na kufunga lakini daktari wake alitoa taarifa ndefu baada ya Rais Kikwete kudondoka tena mwaka jana, akieleza kuwa hali hiyo ilitokana na uchovu baada ya kusafiri safari ndefu iliyomtoa Italia, Marekani, Dar es salaam, Arusha na baadaye Mwanza.
Hadi sasa hakuna taarifa rasmi ya serikali kuhusu tukio la Jumamosi iliyopita, lakini CCM imeshaeleza kuwa JK alidondoka kutokana na kufunga. Jumamosi Kikwete alipatiwa matibabu kwa muda mfupi kabla ya kurejea jukwaani kumalizia hotuba yake na siku iliyofuata aliendelea na kampeni mkoani Mwanza.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Profesa Mwakyusa alisema amemtaka daktari wa rais ampe maelezo ya kina kuhusu kuanguka kwa kiongozi huyo wa nchi pamoja afya yake kwa ujumla.
Nisingependa kitu kama hicho kimtokee Rais Kikwete... imeniathiri sana. Lakini pamoja na kwamba daktari wake amekwishatoa maelezo, tayari nimemtaka anipe maelezo ya kina kuhusu kilichotokea pamoja na hali halisi ya afya ya rais, alisema Profesa Mwakyusa.
Kwa mujibu wa maelezo ya daktari wake, kuanguka kwa Rais Kikwete kulitokana na kupungukiwa na sukari kulikosababisha kushuka kwa shinikizo la damu, kutokana na kufunga mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Profesa Mwakyusa, ambaye alikuwa daktari wa rais wa serikali ya awamu ya kwanza, alisema hatua yake inalenga kuhakikisha rais hapatwi na hali kama hiyo tena.
Lengo ni kujipanga vizuri ili hali kama hii isijitokeze tena, alisema Profesa Mwakyusa.
Profesa Mwakyusa, ambaye amepita katika nafasi ya ubunge (CCM) Jimbo la Rungwe Magharibi kutokana na kukosa mpinzani, alisema kwamba kulingana na hali halisi ya mazingira ilivyojitokeza atafuatilia kwa karibu afya ya rais.
Kulingana na hali ilivyo kwa kweli nitafuatilia kwa karibu afya ya rais; nitafanya kazi ya ziada ili kusitokee tena tatizo kama hili, alisema Profesa Mwakyusa.
Profesa alisema suala la afya ni nyeti na kwamba kadri umri unavyoongezeka, ndivyo uwezekano wa kupata magonjwa unaongezeka.
Hapa ndipo tunaposema kinga ni bora kuliko tiba na pia kinga ni nafuu kifedha kuliko tiba, alisema
Profesa Mwakyusa alikwenda mbali zaidi na kusema: Pamoja na kwamba kila kiongozi wa kitaifa ana daktari wake binafsi na suala la ugonjwa ni siri, wizara italazimika kuweka mapango maalumu wa kufuatilia afya zao, ikiwamo kujua mpangilio wa vyakula wanavyokula na kama wanafanya mazoezi kulingana na ratiba.
Wakati huohuo, Profesa Mwakyusa alisema Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ipo katika mpango wa kutoa elimu ya kuhamasisha upimaji wa afya kila mara pamoja na kutoa huduma hiyo bure.
Baadhi ya hospitali nchini India hutoa huduma ya kupima afya bure. Hata sisi tuna mpango mkakati wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma hii bure kwenye hospitali za serikali, alisema Profesa Mwakyusa.
Rais Kikwete aliyefuatana na mgombea mwenza, Dk Mohamed Gharib Bilal alianguka dakika 16 baada ya kuanza kuhutubia. Aliishiwa nguvu wakati akizungumza na walinzi wake walimdaka na kumtoa jukwaani.
Rais alipelekwa kwenye gari maalum la wagonjwa lililokuwepo uwanjani hapo kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza.
Dakika 14 baadaye alirejea jukwaani huku uso wake ukiwa unaonyesha kuchoka na akaendelea na hotuba yake kwa dakika tano kabla ya kwenda kuketi meza kuu kwa dakika mbili na kisha kuondoka uwanjani hapo.
Akiwa amesindikizwa na walinzi zaidi ya watu watano kurudi jukwaani, Kikwete alisema: "CCM oyee; jamani nimefungulia... niliishia kwenye suala la rushwa.''
Kitendo hicho cha Rais Kikwete kukata ghafla hotuba yake kwa mara ya pili kiliwashtua mamia ya watu waliohudhuria mkutano huo na kusababisha baadhi yao kuanza kulia.
Umati wa watu hao, wengi wakiwa wamevaa nguo za rangi ya kijani na njano ambazo ni rangi za CCM, uligubikwa na vilio na kelele huku kila mmoja akizungumza maneno yake.
Tukio hilo lilishuhudiwa na familia yake akiwamo mkewe Mama Salma, baadhi ya watoto wake, marais wastaafu na viongozi wa serikali na chama.
Tukio la kwanza lilitokea kwenye viwanja hivyo hivyo vya Jangwani Oktoba 30, 2005, wakati anahitimisha kampeni za chama hicho. Siku hiyo Kikwete akiwa mgombea wa CCM alionekana kuishiwa nguvu ghafla na kudondoka na baadaye kundolewa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi.
Baadaye ilitolewa taarifa kwamba, uchunguzwa na daktari umeonyekana kuwa ni mzima na kwamba hali hiyo ilisababishwa na uchovu uliotokana na pilika nyingi za kampeni na wakati huo akiwa amefunga kwa kuwa ulikuwa ni mwezi wa Ramadhan.
Tukio la pili lilitokea Oktoba 4, mwaka jana wakati akihutubia mamia ya watu katika maadhimisho ya miaka 100 ya kanisa la African Inland Church (AIC) kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusiana na tukio hilo, vilieleza kwamba Rais Jakaya Kikwete, ambaye alikuwa akihutubiwa akiwa amekaa, aliishiwa nguvu jukwaani kisha kubebwa wasaidizi wake kumpeleka katika chumba maalumu kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza.
Tukio hilo pia lilizusha hofu kubwa na kubadilisha shamra shamra hizo za kidini kuwa majonzi na simanzi. Baadaye alipata nafuu na kurejea kumalizia shughuli hiyo.
Baadhi yao walifanya sala kumuombea kiongozi huyo, ili Mungu ampe nguvu na afya njema ili aendelee kuwatumikia Watanzania.
Baadaye Rais Kikwete alisema: Wakati nikihutubia, ninakumbuka ghafla nilihisi kuishiwa nguvu na hiyo inatokana na kukaidi ushahuri wa madaktari wangu ambao waliniambia nisisafiri kuja Mwanza.
Jamani poleni sana kwa hali iliyotokea nilijisikia vibaya, mwili uliishiwa nguvu, ndiyo maana mliona nilibebwa. Wataalamu wangu walinikataza ili niupumzishe mwili nikakaidi.
Baada ya kusema hayo, Rais Kikwete aliendelea na hotuba yake, akiwa ameketi kwenye kiti, lakini hata hivyo sauti yake ilianza kufifia na kusikika kwa mbali na hivyo kulazimika kukatisha hotuba.
Tukio la nne ni wakati alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, katika serikali ya awamu ya tatu. Aliaguka akiwa uwanja wa ndege wa jijini Brussel nchini Ubelgiji alipokuwa akielekea nchini Cuba. Alilazwa kwa takribani saa nane na baadaye aliendelea na safari.
Source: MWANANCHI