Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,742
- 40,873
Nitawaambia mawazo yangu, tatizo kubwa la Magufuli katika haya yote ni kuonekana kuwa hajali. Kwamba, yeye aliyesema kuwa ni "Rais wa wanyonge" na ambaye aliahidi kwa kuwaambia "sitowaangusha" anaonekana hajali kinachowakuta wanyonge, isipokuwa kama alikuwa ana maana nyingine ya "wanyonge". Faru na punda siyo wanyonge.
Yanapotokea matukio ambayo yanaashiria kuwepo kwa nguvu nyingine zinazotenda kazi nje au sambamba na nguvu za kawaida ni jukumu lake na serikali nzima kushtuka. Haipaswi kuonekana ni "kawaida" au "ni siasa". Yeye akionekana hashtuki na akionekana hajali ni wazi watu watahusisha yanayotokea kuwa ni baraka zake kwa kisingizio cha "ukimya maana yake ni kukubali".
Lakini upande mwingine; ukilinganisha na huko nyuma, leo mawaziri na wengine wana haraka ya kujibu badala ya kupuuzia - hata kama kwa kufanya hivyo wakati mwingine wanaonekana kuzua maswali zaidi kuliko majibu. Mnakumbuka tulivyohangaika na suala la Daud Mwangosi na ukimya wa serikali? tena Kamuhanda akahamishwa sijui sasa yuko wapi! Kina Kibanda na Ulimboka, kijana wa Igunga (kutokea Ubungo), kupigwa kwa wabunge Kiteto, kuvamiwa kwa wabunge Mwanza n.k Mojawapo ya mambo ambayo huwa yanatokea sana ni kuwa na Parallel structures katika law enforcements.
Miundombinu sambamba inawafanya baadhi ya watu katika usimamiaji wa haki kufanya mambo kwa kisingizio cha maslahi ya serikali wakati wanafanya hivyo na kuiharibu serikali. Sasa hivi kwa mfano, matukio yanayotokea yanaonekana au yanaoneshwa kuwa yanafanywa na serikali - kwa sababu serikali na hasa DPP na AG wanaonekana kutokujali kinachotokea.
Hapa US wengi mnajua shida mojawapo kama kule NY ni kuwa na corrupt police ambao nao wanatumia beji na nyadhifa zao kuendesha deals zao wengine wanafanya hivyo kabisa kwa kisingizio cha kulinda jamii.
Kulega lega kwa hali ya usalama au hata kuonekana kuwa watu hawako salama sana ni jambo linalopaswa kuishtua serikali yeyote. Binafsi nilitarajia kuwa baada ya matukio haya ya kutoweka au watu kutekwa au sintofahamu fulani basi hata kikao cha Baraza la Mawaziri kingeitishwa na hatua kuchukulia na ikibidi kupanguliwa kwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, IGP na wakuu wa upelelezi! Haiwezekani kabisa ikaonekana na kukubalika kuwa kuna watu wanaweza kufanya lolote, popote, na kwa yeyote.
Hili linanikumbusha lililotokea Kenya miaka kadhaa nyuma kwa wenye kumbukumbu; aliuawa mwanasiasa mashuhuri Kenya ambaye alitoweka kwanza. Wengi watamkumbuka kwa jina la Robert Ouko. Lakini tusije kufika huko maana bila kudhibiti haya matukio ya sasa huko mbeleni hayaepukiki haya ya mwanasiasa au mtu mashuhuri kutoweshwa na wote tujifanye tunashtuka na kushangaa.
[HASHTAG]#JPMAonesheAnajali[/HASHTAG]
Mwaka 2008: Niliandika haya kama utabiri wa kile kinachotokea sasa: Watoto wa Vigogo/Mafisadi wakianza kutekwa!
Na niliandika: Kama tunataka kweli kulinda rasilimali zetu hatuna budi kuimarisha usalama wa Taifa ili usiwe usalama wa wenye matumbo ya Taifa bali usalama wa hazina, mali, na raslimali za Taifa. Kama wale waliodhaminiwa kusimamia usalama wa taifa hili wameshindwa kufanya hivyo, kama waliopo katika safu za usalama wa taifa weshindwa kulinda usalama wa Taifa na badala yake wanahangaika na kutafuta watu wasiowahusu na kushiriki kwenye michezo michafu ya kisiasa basi waachie ngazi tu ili tukodi watu wengine waje watulindie usalama wetu kwani ndugu zetu wenyewe wametuuza! (SOMA HAPA JUU YA TAIFA KUTEKWA NYARA - 2008)