Kompyuta 21 ‘zadoda’ Sekondari kukosa umeme

Averos

JF-Expert Member
Aug 6, 2010
993
695

KOMPYUTA 21 zilizotolewa na mfadhili katika Shule ya Sekondari Buyango Wilaya ya Missenyi , mkoani Kagera zimegeuka mzigo baada ya kushindwa kuzitumia kutokana na kukosekana kwa umeme.
Diwani wa Kata ya Buyango, Justus Rukaza pamoja na kumshukuru aliyetoa kompyuta hizo, alisema anaendesha kampeni ya kuwatafuta wafadhili wengine watakaosaidia upatikanaji wa nishati ya umeme ili kompyuta hizo zifanye kazi.

Kwa mujibu wa diwani huyo kompyuta hizo zilitolewa zaidi ya mwezi mmoja uliopita na Mwenyekiti wa Shirika la Tideso , Aseri Katanga anayeishi nchini Uingereza ambazo hata hivyo hazijawanufaisha wanafunzi na walimu kama ilivyokusudiwa kutokana na kukosekana kwa umeme.“Kompyuta zilizotolewa na mfadhili ni nzuri na zinafanya kazi tuliziwasha kwa kutumia jenereta kwa majaribio, zinaendelea kutunzwa hapo shuleni mpaka utakapopatikana ufumbuzi wa umeme”, alidai diwani huyo.

Pia alisema mikakati inayoendelea kwa sasa ni pamoja na kutafuta wafadhili watakaowezesha kupatikana kwa umeme wa nguvu ya jua wakati ikisubiriwa mikakati ya muda mrefu ya upatikanaji wa umeme.
Rukaza aliwarushia lawama baadhi ya wanasiasa wilayani Missenyi aliodai kwa nyakati tofauti wamekaririwa wakidai upelekaji wa umeme kwa maeneo ya vijijini kwa sasa sio kipaumbele cha wananchi.

Akitetea kauli yake diwani huyo alisema pamoja na kuwa ni wananchi wachache wenye uwezo wa kumudu gharama za umeme vijijini, lakini upatikanaji wake utawarahisishia upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii ukiwamo uanzishaji wa miradi midogomidogo.

Pia alidai kauli za aina hiyo zitachelewesha hata maendeleo ya elimu kama ilivyo sekondari ya Buyango ambayo haiwezi kunufaika na msaada wa kompyuta kutokana na kukosekana kwa umeme.Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Buyango, Emmanuel Rugambwa hakuweza kupatikana kwa njia ya simu ili kuzungumzia mikakati ya shule hiyo ya kuhakikisha wanafunzi na walimu wao wananufaika na msaada uliotolewa.


 
Back
Top Bottom