Klabu za soka nchini ziuzwe kwa watu binafsi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Klabu za soka nchini ziuzwe kwa watu binafsi

Discussion in 'Sports' started by nngu007, Mar 12, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Mar 12, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 58
  Trophy Points: 145
  Klabu za soka nchini ziuzwe kwa watu binafsi
  KLABU kubwa za soka nchini ni Simba na Yanga.

  Hilo halina ubishi na ndizo zinazotawala midomo ya Watanzania wengi na ndizo zinazoandikwa na kutangazwa na vyombo vya habari kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko zingine zilizomo nchini.

  Hilo linafanya kila kunapokuwa na mechi baina ya klabu hizo mbili ambazo zinaitwa ‘watani wa jadi’, tambo, maneno na ujivuni, hufanyika ili mradi kuhakikisha kuwa ushindani upo na ni wa uhakika baina ya timu za soka za klabu hizo.

  Umaarufu wa Simba na Yanga unatokana na mchezo wa soka, ingawa klabu hizo zilianzishwa kama za michezo na si za soka, kama ambavyo sasa zinaonekana kuwa kwa ufadhili wote kuelekezwa kwenye soka badala ya michezo mingine iliyokuwapo, ikiwa ni pamoja na ngumi na hata michezo ya jadi ya bao, karata na dhumna.

  Viongozi wakuu wa nchi hii walihusika kikamilifu katika kuanzishwa kwa klabu hizo kisiasa, hususan Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume (wote marehemu).

  Na hivi sasa mjane wa Karume, Mama Fatma, ni mmoja wa wadhamini wa klabu ya Yanga. Pamoja na klabu hizi kuongoza kwa umaarufu, lakini ndizo pia zinazoongoza kwa migogoro, ambayo hapo awali ilikuwa ikisababishwa na timu mojawapo kutofanya vizuri inapokuwa imepembana na hasimu wake.

  Kutimuliwa kwa makocha wa timu hizo baada ya moja kufungwa lilikuwa jambo la kawaida. Leo, kocha anaondoka si kwa kutimuliwa kutokana na timu kufungwa, la hasha, ni kutokana na kudhulumiwa maslahi yake au kuvurugwa kwa mkataba wake.

  Na hilo limekuwa likichangiwa na viongozi wa klabu hizo na si wanachama au mashabiki kama timu zilipokuwa zikifungwa.

  Hivi sasa klabu hizi ambazo zinamilikiwa na ‘wananchi’ zimekuwa zikiingia katika kizungumkuti pale zinapotafuta viongozi wapya, hasa baada ya waliopo kuanza kuvurugana kwa si sababu nyingine, bali za kimaslahi- ya kifedha au umaarufu - na kusambaratishana.

  Yanga sasa iko katika muktadha huo, ambapo viongozi wake wanajiengua mmoja baada ya mwingine kila kukicha. Sina haja ya kutaja nani kaondoka lini na nani atafuata lini, itoshe kusema tu kuwa ndani ya Yanga kuna tatizo la viongozi na si uongozi.

  Yanga kama ilivyo Simba, kumegeuka kuwa sawa na ‘shamba la bibi’, ambako kila mtu anaingia anachuma anachokitaka na kwenda kutumia na familia yake.

  Wanaingia watu masikini kwenye uongozi, lakini mwisho wa muhula wanatoka wakiwa matajiri, kwa kunyonya wachezaji wa timu hizo.

  Wanaingia watu wenye fedha zao, lakini kwa kuwa wanalenga umaarufu wa kisiasa, kila mtu anaibuka kwa upande na nafasi yake na wanapoonekana ni mafahali wawili wasiokaa zizi moja, mizengwe inaanza na ndipo mwenye ubavu dhaifu anajiondoa akilalama kuwa anatukanwa na fedha zake.

  Kama kuna watu wanatukanwa ndani ya klabu hizi ni wachezaji na hawa watukanwa na viongozi mpaka mashabiki wao na kutungiwa kashfa na tuhuma hata zisizo na msingi zikiwamo za kuuza mechi pale wanapokuwa wameshindwa, lengo kuwadhulumu haki yao.

  Hatujasikia mchezaji kakimbia timu kwa sababu ya kutukanwa. Viongozi tumewasikia. Lakini hawa ndio wale wanaoingia Yanga au Simba kutafuta umaarufu ili hatimaye wagombee uongozi wa kisiasa nchini, kwa sababu bila ngazi nchi hii hupandi unakotaka kufika.

  Wapo ambao ngazi hukatika wakadondoka wasisikike tena, lakini wapo wanaofaulu na kukaa juu. Migogoro ndani ya Yanga na Siomba haitakwisha hadi hapo tutakapoondokana na dhana ya”Yanga au Sinmba ina wenyewe kaka”.

  Wenyewe hao ambao hawana mchango wowote zaidi ya kuwaibia wachezaji na wadhamini na kujinufaisha wao.

  Mbona haya hayapo Azam FC? Dawa ya hayo haipatikani Loliondo au kwingineko ni kwa wanachama na mashabiki kukubali klabu hizi ziwe kampuni na ziendeshwe kitaalamu, au ziuzwe kwa matajiri waziendeshe kama inavyofanyika Ulaya na kwingineko.

  Angalieni mfano wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), haimilikiwi na wanachama, bali mtu.

  Timu zinatakiwa kuwa chini ya mtu ambaye atahakikisha mahitaji ya wachezaji yanatekelezwa kwa sababu wachezaji ndizo injini za timu, na wengine wenye mapenzi yao wabakie kushangilia na kununua bidhaa za timu ili kuziimarisha kimapato.

  Kwa nini tusikie wamiliki na mameneja wa Chelsea au Manchester United na si wanachama na viongozi wa timu hizo?

  Tuachane na walaji katika klabu zetu ili wachezaji wapewe kipaumbele na migogoro ibakie kwa mtu na familia yake. Muda wa viongozi na wanachama kupika migogoro klabuni umekwisha tunataka maendeleo ya soka sasa.
   
Loading...