Kizimbani

Mlenge

R I P
Oct 31, 2006
2,125
2,291
Kizimbani
Sura ya 1: Kukamatwa - Mazungumzo na Bibi Gurubaki - Kisha Bi Basitena


Lazima pana mtu aliyekuwa anatembeza maneno ya urongo kuhusu Josefu K., kwani mwenyewe alijua hakufanya kosa lolote lakini, siku moja asubuhi, alikamatwa. Kila siku saa mbili asubuhi aliletewa kiamsha kinywa na mpishi wa Bibi Gurubaki - Bibi Gurubaki alikuwa ni mama mwenye nyumba - lakini leo hakufika.

Na hilo halikuwahi kutukia hapo kabla. K. alisubiri muda kidogo, akichungulia kutokea kwenye mto alioulalia amuone yule mama mzee aliyeishi nyumba mkabala na ambaye alikuwa akimuangalia K. kwa makini isivyokuwa kawaida yake, na mwishowe, akiwa na njaa na aliyekanganyikiwa, alipiga kengele.

Mara hiyo palikuwa na hodi mlangoni na mwanaume mmoja aliingia. Hakuwa amewahi kumuona mtu huyo hapo nyumbani. Alikuwa mwembamba lakini mkakamavu,nguo zake zilikuwa nyeusi na zilizomkaa vyema, zikiwa na pindo nyingi na mifuko, vichuma na vifungo na mkanda, vyote vikiwa vyaashiria ya kuwa mtu wa kazi hakuna kuremba lakini visivyokuwa bayana ni vya matumizi yepi hasa.

"We nani?" aliuliza K., akiwa amekaa nusu wima kitandani kwake.

Yule mtu, hata hivyo, alipuuza swali kana kwamba kuwasili kwake tu kulitosha kukubaliwa, na alijibu kirahisi,

"Ulipiga kengele?"

"Ana alitakiwa awe ameshaniletea kiamshakinywa changu," alisema K.

Alijaribu kubaini yule mtu alikuwa ni nani hasa, awali kimyakimya, kwa kumwangalia tu na kumtafakari, lakini yule mtu hakutulia tuli muda mrefu wa kumwezesha kushangaliwa zaidi. Badala yake, alienda mlangoni, akaufungua kidogo, na kumwambia mtu ambaye bila shaka alikuwa nyuma tu ya mlango, "Anataka Ana amletee kiamshakinywa chake."

Palikuwa na kicheko kidogo kwenye kile chumba jirani, na haikuwa wazi kutokana na sauti iliyosikika iwapo walikuwa watu wengi wakicheka

Yule mtu asiyejulikana hakuweza kumtambua zaidi ya aliyoyajua tayari, lakini sasa alimwambia K., kama ambaye anatoa ripoti. "Hilo haliwezekani."


"Hii itakuwa ni mara ya kwanza hilo kutukia," alisema K., wakati akiruka kutoka kitandani na kwa haraka akivaa suruali yake. "Nataka kuona ni nani aliyeko chumba jirani, na ni kwa nini Bibi Gurubaki ameachia nisumbuliwe hivi."

Mara moja alibaini kwamba hakuhitajika kuyasema yote haya kwa sauti, na kwamba kwa kufanya hivyo atakuwa kiaina ametambua mamlaka yao, ingawa hilo halikuonekana ni la muhimu kwake kwa wakati huo.

Hivyo, angalau, ndivyo yule asiyejulikana alivyochukulia, kwani alisema, "Hudhani ingekuwa vema ukabakia ulipo?"

"Sitaki kubakia hapa wala kuongeleshwa na wewe mpaka pale utakapokuwa umejitambulisha."

"Nilimaanisha ni kwa faida yako mwenyewe," alisema yule asiyejulikana na kufungua mlango, mara hii bila ya kuambiwa.

Chumba jirani, ambacho K. aliingia polepole zaidi ya alivyokusudia, kilionekana kwa harakaharaka kiko vilevile kama kilivyokuwa jioni ya jana yake.

Ilikuwa ni sebule ya Bibi Gurubaki, imesheheni samani, vitambaa vya mezani, vyombo vya udongo na picha. Pengine palikuwa na nafasi zaidi kidogo leo, lakini kama ndivyo haikuweza kuonekana kirahisi, hususan kwa vile tofauti kuu ilikuwa ni uwepo wa mwanamume aliyekuwa ameketi jirani na dirisha lililokuwa wazi akiwa ameshikilia kitabu ambacho sasa aliinua macho yake kuacha kukisoma.

"Ulipaswa ubakie chumbani kwako! Franzi hakukuambia?"

"Na ni nini hasa mnachokitaka?" alisema K., akimwangalia huyu asiyejulikana mpya na kurudi kwa yule aliyeitwa Franzi, ambaye alikuwa amebakia pale mlangoni.

Kupitia kwenye dirisha lililokuwa wazi, alimbaini tena yule ajuza, aliyekuja karibu na dirisha mkabala ili aweze kuendelea kuona kila kitu. Alikuwa anaonyesha ufukunyuku ambao kwa kweli ulikuwa kama vile ukimuonyesha anaazeeka vibaya.

"Nataka kumuona Bibi Gurubaki...," alisema K., akijongea kama ambaye anataka kujinasua toka kwa watu wale wawili - japokuwa walikuwa wakisimama mbali naye - na walikuwa wanataka kuondoka.

"Hapana," alisema yule mtu aliyekuwa dirishani, ambaye alirusha kitabu chake mezani na kuinuka.


"Huwezi kwenda wakati ukiwa umekamatwa."

"Hivyo ndivyo inavyoonekana," alisema K. Kisha aliuliza "Na kwa nini nimekamatwa?"

"Hilo ni jambo ambalo haturuhusiwi kukuambia. Nenda chumbani kwako na usubiri hapo. Mwenendo wa mashitaka unaendelea na utaelewa kila kitu huko baadae. Kwa kweli si kazi yangu kuwa kirafiki nawe hivi, na natumaini hakuna mwingine, zaidi ya Franzi, atakayesikia kuhusu hilo, kwani naye ameenenda kirafiki kwako kuliko anavyopaswa, yeye mwenyewe, kwa mujibu wa kanuni. Ukiendelea hivi kuwa na bahati njema kama hivi ulivyonayo kwa maafisa wanaokukamata basi unaweza kutambua kwamba mambo yako yaenda vizuri."


K. alitaka kuketi, lakini akaona kwamba, ukiacha kile kiti karibu na dirisha, hapakuwa na mahali popote chumbani ambapo angeweza kukaa. "Mtajipatia fursa ya kujionea wenyewe ukweli wa mambo yote haya," alisema Franzi na watu wote wawili walitembea kumfuata K. Walikuwa ni wakubwa sana kuliko yeye, hasa yule mtu wa pili, ambaye mara kwa mara alimpiga begani. Wawili wale walishika shati la kulalia la K, na kuwambia angetakiwa sasa avae shati lenye ubora hafifu zaidi sana, lakini kwamba wangebakia na lile shati lake la usiku pamoja na nguo zake zengine na wangemrudishia kesi yake ikiisha vizuri.

"Ni vema kwako kama ukitupatia sisi vitu hivi kuliko ukaviacha stoo," walisema. "Vitu huwa na tabia ya kupotea vikiwa stoo, na baada ya muda fulani kupita huwa wanauza vitu, iwe kesi husika imeisha au la. Na kesi kama hii huweza kukaa kwa muda mrefu, hususan hizi ambazo zimekuwa zikiibuka hivi karibuni. Wanaweza kukupa pesa za mauzo yake, lakini haziwezi kuwa nyingi kwani muhimu siyo bei ya kuuzia, bali ni ile ganji waliyojigawia, kadhalika vitu kama hivyo hupoteza thamani yake vinapopita toka mikono hii hadi ile, mwaka hata mwaka."

K. hakusikiliza kwa makini walichokuwa wakisema, hakuweka uzito mkubwa kwa vile ambavyo bado angekuwa anamiliki au kwa nani ambaye ataamua kitokee nini kuvihusu. Ilikuwa muhimu sana kwake kupata uelewa bayana wa mustakabal wake, lakini hakuweza kutafakuri vema ilhali watu wale walikuwa hapa, kitambi cha yule polisi wa pili - na tu wangeweza kuwa ni polisi - kilionekana rafiki vya kutosha, kikijitokeza kumuelekea, lakini pale K. alipoangalia juu na kuona sura yake kavu, kakamavu hakuona kama inalandana na mwili ule. Pua yake imara ilikuwa imepinda kuelekea upande mmoja kama vile inampuuza K. na kumteta kwa yule polisi mwengine. Watu hawa ni wa namna gani? Nini walichokuwa wanakiongelea? Wanatokea afisi ipi?

Juu ya hayo, K. alikuwa anaishi kwenye nchi huru, kila mahali amani, sheria zote zilikuwa bora na zikifuatwa, ni nani hawa waliothubutu kumweka kizuizini nyumbani kwake mwenyewe? Siku zote alikuwa akichukulia poa maisha kadiri alivyoweza, kushughulika na mambo kadiri yanavyojitokeza, kutojali wakati ujao, hata pale kila kitu kilipoonekana kiko hatarini.

Lakini kwenye hili haikuonekana ni kitu muafaka kufanya hivyo. Angeweza kuchukulia yote haya kama utani, utani mkubwa ulioasisiwa na wafanyakazi wenziwe wa benki kwa sababu fulani zisizojulikana, au pia pengine kwa vile leo ilikuwa ni kumbukumbu yake kuzaliwa ya thelathini, vyote hivyo vingewezekana bila shaka, pengine alichotakiwa tu kufanya ni kuwacheka polisi kwa namna fulani nao wangecheka pamoja naye, labda walikuwa ni wafanyabiashara kutoka kona ya mtaani, walionekana ni kama wangeweza kuwa - lakini hata hivyo alidhamiria, tokea mara ile alipomuona yule mmoja aitwaye Franzi, kutopoteza fursa yoyote aliyonayo ngaa kidogo kuhusu watu hawa.

Palikuwa na hatari ndogo kwamba watu baadaye wangesema hakuweza kuelewa utani, lakini - ingawa hakuwa kwa kawaida ya kujifunza kutokana na uzoefu - angeweza pia kuwa na matukio yasiyo muhimu fikrani mwake wakati ambapo, tofauti na marafiki wake walio waangalifu zaidi, alitenda bila tafakari kabisa kuhusu nini kingeweza kutokea na ikambidi ateseke kwa sababu hiyo. Hakutaka hayo yajirudie, walau si wakati huu; kama walikuwa wakiigiza naye angeigiza pamoja nao.

Bado alikuwa na muda. "Niruhusuni," alisema, na akaharakia baina ya wale polisi wawili na kuingia chumbani mwake. "Inaonekana ana busara vya kutosha," aliwasikia wakisema nyuma yake. Pindi alipoingia chumbani kwake, kwa haraka alifungua droo la meza yake ya kuandikia, kila kitu kilikuwa kimepangiliwa vema lakini kwa mhemko wake hakuweza kupata mara hiyohiyo nyaraka za utambulisho alizokuwa akizitafuta. Hatimaye aliweza kupata kibali chake cha baiskeli na ilibakia kidogo tu arejee nacho kwa wale mapolisi pale alipotambua kwamba hakina maana, hivyo akaendelea kutafuta mpaka alipopata cheti chake cha kuzaliwa. Punde tu baada ya kurejea chumba kilichofuata mlango wa upande mwingine ulifunguliwa na Bibi Gurubaki alikuwa anataka kuingia. Alimuona kufumba na kufumbua, kwani mara tu alipomtambua K. alitahayari, akaomba msamaha na kutokomea, akifunga mlango nyuma yake kwa makini. "Ingia tu," K. angeweza kusikika akisema mara hiyo. Lakini sasa alikuwa amesimama katikati ya chumba makaratasi yake yakiwa mkononi mwake na bado akiangalia ule mlango ambao haukufunguliwa tena.


Alibakia vivyo hivyo mpaka pale alipogutuliwa na kelele ya yule polisi aliyeketi kwenye meza ndogo kwenye dirisha lililokuwa wazi na, kama K. sasa alivyoona, alikuwa akila kiamshakinywa cha K.
"Kwa nini hakuingia?" aliuliza.
"Haruhusiwi," alisema yule polisi mkubwa. "Uko kizuizini, au sio."
"Lakini nawezaje kuwa niko kizuizini? Na iliendaendaje mpaka ikawa hivi?"
"Unaanza tena," alisema yule polisi, huku akidumbukiza kipande cha mkate wenye siagi kwenye kiriba cha asali. "Hatujibugi maswali kama hayo."
"Itawabidi mjibu," alisema K. "Hizi hapa ni nyaraka zangu za utambulisho, sasa nanyi mnionyeshe zenu na bila shaka nataka kuona hati ya kukamatwa."
"Mungu wangu!" alisema yule polisi. "Katika sintofahamu kama uliyoko, bado unadhani unaweza kuanza kutoa amri, siyo? Haitakusaidia lolote kutuudhi, hata kama unadhani itakusaidia - tuko upande wako kuliko mtu yeyote mwingine unayemfahamu!" "Unajua, hiyo ni kweli, ni vema ukaamini hivyo," alisema Franzi, akiinua kikombe cha kahawa mkononi mwake ambapo hakuupeleka kinywani mwake lakini alimtizama K. kwa namna ambayo pengine ilikusudiwa kuwa na maana kubwa lakini haikuweza kueleweka.


K. alijikuta mwenyewe, bila kukusudia, akiwa katika mjadala wa kimya na Franzi, lakini ndipo alipopiga mkono wake kwenye karatasi zake na kusema, "Hizi hapa nyaraka za utambulisho wangu."

"Na unataka sisi tuzifanye nini?" alijibu yule polisi mkubwa, kwa sauti. "Namna unavyoenenda, ni vibaya kuliko mtoto. Nini hasa unachotaka? Unataka mashitaka haya makuu, fedhuli yanayokukabili yaishe haraka kwa kuzungumza nasi kuhusu kitambulisho na hati ya mashitaka? Sisi ni watu wa kutumwa tu, ndivyo tu tulivyo. Maaskari wa ngazi za chini kama sisi aghalabu hatuwezi kutofautisha mwanzo au mwisho wa kitambulisho, kile tu tupaswacho ni kukuchunga kwa masaa kumi kwa siku na kulipwa. Ni hivyo tu tulivyo. Kumbuka, tunachoweza kufanya ni kuhakikisha kwamba maafisa waandamizi tulio chini yao wanajua ni aina gani ya mtu ambaye wanaenda kumkamata, na kwa nini akamatwe, kabla hawajatoa hati ya kukamatwa. Hakuna makosa hapa. Mamlaka zetu kadiri nijuavyo, nami nawajua tu wale wa ngazi za chini kabisa, hawaendi kuokoteza hatia miongoni mwa umma; ni wenye hatia ndio huwavuta waje, kama vile sheria inavyosema, na hulazikimika kututuma sisi maafisa wa polisi. Hiyo ndio sheria. Unadhani wapi patakuwa na makosa hapo?"

"Sijui hiyo sheria," alisema K.

"Bahati yako mbaya hiyo," alisema yule polisi.

"Inawezekana ipo tu mawazoni mwenu," alisema K., akitaka, kwa namna fulani, kubadili mawazo ya wale polisi, na kuyafanya mawazo yao yawe kwa manufaa yake au kujiwekea mazingira rafiki pale.

Lakini yule polisi alisema akimpuuza, "Utajua wakati ikikuathiri." Franzi alijiunga, na kusema,

"Angalia Wilemu, jamaa anakubali hajui sheria na wakati huohuo anasisitiza hana hatia."

"Uko sawa kabisa, lakini hatuwezi kumfanya aelewe chochote," alisema yule mwengine.

K. aliacha kuongea nao; kwani, alijiwazia, kweli ni lazima niendelee kujichanganya kuendelea kuongea na majuha namna hii? - na wenyewe wanakiri ni wa ngazi ya chini kabisa. Juu ya hayo, wanazungumzia vitu ambavyo hawana hata chembe ya uelewa. Ni kwa sababu tu ya ufyatu wao wanaweza kujiamini vile. Ninahitaji tu kuwa na maneno machache na mtu mwenye nafasi kwenye jamii kama yangu na kila kitu kitakuwa wazi isivyomithilika, wazi sana kuliko mazungumzo marefu na wawili hawa yanavyoweza kufanya. Alitembea huku na kule kwenye nafasi iliyo wazi mle chumbani mara kadhaa, upande wa pili wa mtaa aliwea kumuona yule bibi, ambaye, sasa, alikuwa amemvuta babu mmoja, mzee kuliko yeye, mpaka dirishani na mikono yake bibie ilikuwa imemzingira.

K. ilimbidi amalize futuhi hii, "Nipelekeni kwa mkuu wenu," alisema.

"Pindi akitaka kukuona. Si kabla," alisema yule polisi, yule aitwaye Wilemu. "Na sasa ushauri wangu kwako," aliongeza, "ni uende chumbani kwako, endelea kutulia, na subiri uone nini kitafanyika kukuhusu. Ukichukua ushauri wetu, hutajichosha kufikiria vitu pasi na faida, na utaweza kujikusanya kwani pana mengi yatakayotarajiwa toka kwako. Hukututendea sisi tunavyostahili baada ya kuwa wema sana kwako, unasahau kwamba sisi, vyovyote tulivyo, bado ni watu huru nawe siyo, na kwa hilo tu tumekuzidi sana. Lakini licha ya yote hayo bado tuko radhi, kama una hela, tukaenda kukuletea kiamshakinywa toka kwenye mgahawa upande wa pili wa barabara."

Bila kutoa jibu lolote kwa ofa hiyo, K. alisimama tuli kwa muda fulani. Pengine, kama angefungua mlango wa kile chumba kingine au hata wa kwenda nje, wawili wale wasingethubutu kumzuia, pengine hilo lingekuwa ni njia rahisi ya kumaliza suala zima hili, na kulihitimisha. Lakini pengine wanemkamata, na kama angetupwa aanguke chini angepoteza, kiaina, ujanja wote aliowazidi. Kwa hiyo aliamua suluhisho la hakika zaidi, kuachilia mambo yaende kama yalivyo, na akaenda chumbani kwake bila neno lingine toka kwake au kwa wale polisi.

Akajitupa kitandani mwake, na kutoka juu ya meza ndogo ya chumbani alichukua tufaa zuri aliloliweka pale jioni ya jana yake kama kiamshakinywa chake. Na hilo likawa ndicho kiamshakinywa pekee alichokipata na hata hivyo, kama alivyothibitisha punde tu alivyopata mego la kubwa, la kwanza, lilikuwa ni bora zaidi ya kiamshakinywa ambacho angeweza kukipata kwa hisani ya wale polisi toka kwenye ule mgahawa mchafu. Alijisikia vema na mwenye kujiamini, alishindwa kazini kwake benki asubuhi hii lakini hilo lingeweza kupotezewa kwa sababu ya cheo chake kikubwa pale. Kwani lazima kweli atume maelezo yake? Alitafakari kuhusu hilo. Hakuna ambaye angemwamini, na kwa namna hii ili aweze kueleweka, angeweza kumleta Bibi Gurubaki kama shahidi, au hata wale wenza wawili wazee wa upande wa pili wa mtaa, ambao pengine hata saa hii walikuwa njiani kuelekea kwenye lile dirisha lililo mkabala.

Ilimshangaza K., walau ilimtatiza alipoliangalia kwa mtazamo wa wale polisi, kwamba wamefanya aende chumbani na wakamwacha peke yake, mahali ambapo alikuwa na njia kumi tofauti za kujiua. Hata hivyo, wakati huohuo, alijiuliza, muda huu akiliangalia kwa mtazamo wake mwenyewe, sababu zipi angekuwa nazo kufanya hivyo. Kwa sababu wawili wale walikuwa wameketi chumba jirani na wamekula kiamshakinywa chake, labda? Ingekuwa ni ujuha mtupu kujiua, hata kama angetaka kufanya hivyo, ujuha ambao ungemfanya asiweze kujiua. Pengine, kama wale polisi wasingekuwa na welewa mdogo, ingeweza kudhaniwa kwamba walifikia hitimisho hilohilo na kwa sababu hiyo hawakuona hatari yoyote kumuacha akae chumbani pekee. Wangeweza kumchunga sasa, kama wangetaka, na kuona namna alivyoenda kwenye lile kabati lililoko ukutani ambapo aliweka chupa ya pombe kali, jinsi alivyofakamia glasi yake moja kama mbadala wa kiamshakinywa chake na ambavyo alikunywa glasi ya pili ili kujipa ujasiri, na glasi ya mwisho kama tahadhari kwa uwezekano mdogo kwamba ingeweza kuhitajika.


Kisha aligutuliwa na kuitwa kwa sauti kubwa toka kile chumba kingine mpaka akajikuta ameng'ata ile glasi. "Afande anataka kukuona!" sauti ya mmoja ilisema. Ni ule ukubwa tu wa sauti uliomshanga, kelele hii kali, ya ghafla, ya kijeshi, ambayo hakuweza kutegemea kutoka kwa polisi aliyeitwa Franzi. Yenyewe aliiona amri ile ni muruwa. "Hatimaye!" alijibu, akafunga kabati na, pasi na kuchelewa, aliharakia chumba jirani. Wale polisi wawili walikuwa wamesimama pale na wakamkimbiza arudi chumbani mwake kana kwamba lilikuwa ni jambo lililotarajiwa.

"We ukoje?" walipiga kelele. "Unadhani utaenda kumuona Afande ukiwa umevaa pekee shati lako, eeh? Angeagiza upigwe, na sisi na wote!"

"Haya wajemeni twendeni!" alisema K., ambaye tayari alikuwa amesukumwa mpaka kwenye kabati lake, "kama mkinifuata mpaka kitandani kwangu mnategemeaje kunikuta nimevaa nguo za kutokea jioni."

"Hiyo haitakusaidia," alisema polisi, ambaye muda wote alikuwa kimya sana, karibia na kuwa mwenye huzuni, pale K. alipoanza kupayuka, na kwa namna wakamchanganya au, kwa kiasi fulani, ikamrudisha kwenye fahamu zake.

"Taratibu za ajabu!" alilalamika, huku akiliinua koti lake kutoka kwenye kiti na kuliweka mikononi mwake kwa muda mfupi, kama ambaye analishikilia kwa ukaguzi wa wale polisi. Walitikisa vichwa vyao.

"Lazima liwe koti jeusi," walisema.

Hapo, K. alilitupa sakafuni lile koti na kusema - bila hata yeye mwenyewe kujua alikuwa anamaanisha nini kwa kusema hivyo - "Sawa haitakuwa kesi kuu hivyo."

Wale polisi wakacheka, lakini wakaendelea kusisitiza, "Lazima liwe koti jeusi."

"Haya ni sawa tu kwangu kama yatafanya mambo yaende haraka," alisema K. Alifungua mwenyewe kabati, alitumia muda mrefu akichakura nguo zote, na kuchagua suti yake nyeusi bora kuliko zote ambayo ilikuwa na jaketi fupi ambalo liliwashangaza sana wale waliokuwa wakimfahamu, na pia alitoa shati jipya na kuanza, kwa makini, kuvaa. Kwa siri alijiambia kwamba amefanikiwa kuharakisha mambo kwa kuwazembeza polisi wasahau kumwambia aoge. Aliwatazama kuona kama wanaweza kukumbuka hatimaye, lakini ni wazi wazo hilo halikuwapitia mawazoni mwao, ingawa Wilemu hakusahau kumtuma Franzi kwa afande akiwa na ujumbe usemao kwamba K. alikuwa anavaa.

Mara alipokuwa amemaliza kuvaa, K. ilimbidi kumpita Wilemu wakati akienda kupitia chumba jirani kwenda kile kingine kinachokifuata, mlango ambao ulikuwa umefunguliwa pakubwa. K. alijua vema sana kwamba chumba hiki kilikuwa hivi karibuni kimepangishwa kwa mpiga taipu aitwaye 'Bi Basitena'. Alikuwa na mazoea ya kwenda kazini mapema sana asubuhi na kurejea nyumbani amechelewa sana, na K. hakuwahi kuongea naye zaidi ya maneno machache ya kusalimiana. Sasa, meza yake iliyokuwa karibu na kitanda ilikuwa imesogezwa katikati ya chumba ili itumike kama dawati la mahojiano, na afande alika nyuma ya meza hiyo. Alikuwa amekunja nne, na mkono mmoja alikuwa ameutupa nyuma ya kiti.


Kwenye kona moja ya chumba kile palikuwa na vijana watatu waliokuwa wakiangalia picha za Bi Basitena ambazo alikuwa ameziweka kwenye kipande cha nguo kilichokuwa ukutani. Kwenye komeo la dirisha lililokuwa wazi palikuwa na blauzi nyeupe. Kwenye lile dirisha upande wa pili wa mtaa, walikuwapo tena wale wenza wazee, ingawa sasa idadi yao ilikuwa imeongezeka, kwani nyuma yao, na mrefu hasa kuwazidi, alisimama mwanamume aliyevaa shati lililofunguliwa vifungo na hivyo kuonyesha kifua chake na ndevu zake nyekundu staili ya mzuzu ambazo alizikusanya na kuzifinya kwa vidole vyake.

"Josefu K.?" aliuliza afande, na pengine kwa dhumuni tu la kutaka K. atambue uwepo wake wakati akiangalia huku na kule kwenye chumba. K. aliitikia kwa kichwa.

"Nathubutu kusema ulikuwa umeshangazwa vilivyo na yote yanayojiri asubuhi hii," alisema afande huku, kwa kutumia viganja vyake viwili, akisukumia mbali vitu vichache vilivyokuwa kwenye meza iliyokuwa karibu na kitanda - mshumaa na kiberiti, kitabu na kibweta cha kutunzia pini vilikuwapo pale kana kwamba ni vitu ambavyo angevihitaji kwa shughuli zake mwenyewe.

"Hakika," alisema K., na akaanza kupata ahueni kwamba sasa, hatimaye, yuko mbele ya mtu mwenye kuelewaelewa, mtu ambaye anaweza kuongea naye kuhusu hali aliyoko.

"Hakika nimeshangazwa, lakini hakuna namna nimeshangazwa sana."

"Haukushangazwa sana?" aliuliza yule afande, huku akiuweka mshumaa katikati ya ile meza na kuvirundika vitu vingine kuuzunguka.

"Pengine hunifahamu vema," K. kwa haraka alisisitiza. "Ninachomaanisha ni ..." hapa K. alinyamaza kuongea na kuangalia huku na kule kuona wapi aketi. "Naweza kuketi, sivyo?" aliuliza.

"Hiyo si kawaida," alisema afande. "Ninachomaanisha ni...," alirudia K. kusema bila kusubiri, "kwamba, ndio, nimeshangazwa sana lakini pale mtu unapokuwa umeishi kwenye dunia hii kwa miaka thelathini na ikakubidi kujipigania kwenye kila kitu, ambayo ndiyo yamekuwa maisha yangu, hapo unakuwa mhimilivu kwa vitu vya kushangaza na unavichukulia poa. Hasa siyo kwa yale yaliyotokea leo."

"Kwa nini hasa siyo yale yaliyotokea leo?"

"Nisingependa kusema kwamba nayaona yote haya kama utani, mnaonekana mmejitaabisha sana kuweka mipangilio yote hii kwa hili kuwa utani. Kila mtu kwenye nyumba hii lazima angekuwa mshiriki wa utani huo kwa ajili yenu, na hilo lingekuwa limeshazidi kinachoweza kuwa utani. Kwa hiyo sitaki kusema kwamba huu ni utani."

"Swadakta," alisema afande, akitizama kuona ni njiti ngapi zimebaki kwenye kibiriti.

"Lakini kwa upande mwingine," K. aliendelea, akizunguka kumtazama kila mmoja pale na hata kutamani angeweza kufanya wale watatu wamsikilize waliokuwa wakiangalia zile picha, "kwa upande mwingine hili haliwezi kuwa ni muhimu vile. Hii inatokana na ukweli kwamba nimekamatwa, lakini siwezi kufikiri hata kosa dogo kabisa ambalo kwalo ningestahili kukamatwa. Lakini hata hilo ni nje ya muktadha, swali kuu ni: Nani anayetoa amri ya kukamatwa? Afisi ipi inashughulikia jambo hili? Ninyi ni maaskari? Hakuna mmoja wenu aliyevaa sare, labda kile mlichovaa" - hapa akamgeukia Franzi - "kimekusudiwa kuwa ni sare, kwa kweli ni zaidi ya suti ya safari. Nataka majibu bayana kwa maswali yote haya, na nina hakika kabisa kwamba pindi mambo yakiwekwa wazi tunaweza kuagana kwa amani."

Afande alikitupa mezani kwa nguvu kile kiberiti.

"Unafanya kosa kubwa," alisema. "Hawa jamaa na mimi hatuhusiki aslan na masaibu yako, kwa kweli ni kama hatujui chochote kukuhusu. Tungeweza kuvaa sare kama ilivyo sahihi na sawia na vile upendavyo na wala hali yako isingezidi punje kuwa mbaya zaidi sababu hiyo. Na kuhusu iwapo uko kwenye mashitaka, siwezi kukupa jibu lolote lililo wazi zaidi ya hayo, hata mimi sielewi iwapo uko au la. Uko kizuini, upo sahihi kabisa kwenye hilo, lakini sijui zaidi ya hayo. Pengine maafisa hawa walikuwa wakipiga soga nawe, kama ndivyo hilo liliishia hapo tu, soga. Lakini siwezi kukupa jibu lolote kwa maswali yako, lakini naweza kukupa kijiushauri: Ungekuwa heri kufikiri kidogo kuhusu sisi na nini kitakuja kukutokea, na ufikiri zaidi kuhusu wewe mwenyewe. Na uache kuleta zahama lote hili kuhusu unavyojihisi huna hatia; haujionyeshi vibaya kivile, lakini kwa zahama lote hili unajiharibia. Na shurti upunguze pia kuongea. Karibu kila ulichokisema hata sasa kimekuwa ni vitu ambavyo tungeweza kuvibaini wenyewe kutoka kwenye mwenendo wako, hata kama ungesema si zaidi ya maneno machache. Na yale uliyoyasema hayakuwa sawia ya kukusaidia."

K. alimtazama kwa muda mrefu yule afande. Hivi huyu mtu, pengine kijana kuliko yeye, alikuwa anampa mhadhara kama vile mwalimu darasani? Je, alikuwa anaadhibiwa alivyo mkweli kwa kufokewa? Na hakuweza kujua lolote kuhusu sababu za kukamatwa kwake au wale waliokuwa wakimkamata? Alighadhibika kinamna na akaanza kutembea huku na kule.


Hakuna aliyemzuia kufanya hivyo na alikunja shati, akajishika kifua, na kunyoosha nywele zake, akawafuata wale watu watatu, akasema, "haileti maana," hapo wale watatu wakageuka kumuangalia na wakamfuata wakiwa na sura za kazi. Mwishowe alisimama tena mbele ya dawati la afande. "Mkurugenzi wa Mashtaka Hasiterera ni swahiba wangu," alisema, "naweza kumpigia simu?"

"Bila shaka," alisema afande, "lakini sijui hilo litasaidia nini, nadhani mna maongezi binafsi unayotaka kuongea naye."

"Litasaidia nini?" K. alipiga kelele, ikiwa ni kukanganyikiwa zaidi ya kukasirika. "Mnajiona ninyi ni nani? Unataka kujua itasaidia nini wakati mnaendelea kufanya kitu kisicho maana kadiri inavyowezekana? Yaani kinaweza kukufanya ulie! Hawa jamaa kwanza walinifuata, na sasa wanaketi au kusimama vivi hivi hapa na kunisomba nije hapa mbele yako. Itakuwa na faida gani, kumpigia simu mkurugenzi wa mashitaka wakati inasemekana niko kizuizini? Haya basi, sitapiga simu hiyo."

"Unaweza kumpigia kama unataka," alisema yule afande, akinyoosha mkono wake kuelekea chumba cha nje ambako simu ilikuwako, "tafadhali, endelea, nenda kapige simu yako."

"Hapana, nimeghairi," alisema K., na kwenda dirishani. Upande wa pili wa mtaa, watu walikuwa bado wapo pale dirishani, na ilikuwa hivi tu pale K. alipokwenda dirishani kwake walipoanza kuonyesha kutahayari vile walivyokuwa wakichungulia kimyakimya yaliyokuwa yakiendelea. Wale wenza wazee walitaka kuinuka lakini yule mtu aliyesimama nyuma yao akawatuliza.

"Tuna hadhira fulani pale," alisema K. kumwambia afande, kwa sauti hivi, huku akiwaonyeshea kwa kidole chake cha shahada. "Ondokeni," kisha aliwaambia wa ng'ambo ya mtaa. Na watatu wale walirudi nyuma hatua chache, na wale wenza wazee walijikuta nyuma ya yule mtu aliyewakinga kwa upana wa mwili wake na kuonekana kana kwamba, kwa kuzingatia mwenendo wa mdomo wake, alikuwa anasema kitu ambacho hakikuweza kueleweka kwa aliye mbali. Hata hivyo, hawakupotelea kabisa, lakini yaelekea walikuwa wakisubiria wakati muafaka ambao wangeweza kurejea dirishani pasipo kuonwa.

"Watu wadaku, wasio na mafikara!" alisema K. huku akigeukia chumbani. Afande pengine alikuwa ameubaliana naye, walau K. alidhani kwamba hicho ndicho alichokiona kutokea kwenye kona ya jicho lake. Lakini iliwezekana pia kwamba hakuwa hata akisikiliza kwani mikono yake ilikuwa imewekwa imara kwenye meza na alionekana akilinganisha urefu wa vidole vyake. Wale polisi wawili walikuwa wamekaa kwenye droo lililofunikwa na blangeti lenye rangirangi, wakisugua magoti yao. Wale vijana watatu walikuwa wameshika viuno na walikuwa wakiangalia huku na kule pasipo mpangilio. Kila kitu kilikuwa tuli, kama katika afisi ambayo imesahauliwa.

"Kwa hiyo wajameni," alisema K., na kwa muda huo ilionekana kana kwamba alikuwa akiwabeba wote mabegani mwake, "inaonekana kama vile shughuli yenu na mimi imekwisha. Kwa maoni yangu, ni vema sasa tukasitisha sintofahamu ya iwapo mnatenda inavyostahili au isivyostahili, na kulifikisha suala hili kwenye hitimisho la amani kwa kupeana mikono. Iwapo mpo na mawazo kama haya, basi tafadhali..." na alitembea kwenda kwenye dawati la afande na kumnyooshea mkono wake.


ITAENDELEA -- Imefasiriwa kutoka hadithi moja ya miaka zaidi ya 100 iliyopita, iliyoandikwa kwa Kijerumani.
 
Kama namuona huyo jamaa akifungua mlango kidogo na kusema, "anataka Ana amletee kiamsha kinywa."😀😀

Halafu mkuu nilikucheki PM.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom