Kituo cha afya chalemewa na wajawazito

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
270
KITUO cha Afya cha Mafiga, katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro , kimezidiwa na uwingi wa wajawazito wanaojifungua wanaofikia wastani wa watoto 500 hadi 600 kwa mwezi.

Uwezo wa kituo hicho ni kuwahudumia wajawazito wanaojifungua watano hadi saba, lakini idadi hiyo imeongezeka na kufikia 15 hadi 30 kwa siku na wauguzi wanalazimika kufanya kazi kwa muda mwingi kuwahudumia wajawazito hao asubuhi hadi usiku.

Kaimu Mganga wa kituo hicho, Dk. Magdalena Kongera, alibainisha hayo Desemba 7 mbele ya Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Mohamed Abood, alipokitembelea kituo hicho akifuatana na baadhi ya watendaji wakuu wa manispaa hiyo kutafuta maoni na kusikiliza kero za wagonjwa na wananchi wengine.

Kabla ya kutembelea kituo hicho, mbunge huyo alianza kukagua ujenzi wa daraja la Mwere, ambalo mara baada ya kukamilika litapunguza msongamano wa magari kwa kiasi kikubwa katika njia kuu iliyopo ndani ya manispaa na pia alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Dk. Kongera alisema Kituo hicho mbali na kupokea wajawazito wengi, pia kimekuwa kikiwahudumia wananchi wengi zaidi kutoka kata za pembezoni, zikiwemo za Mafiga na Chamwino na sehemu ndogo ya wananchi wa vijiji vya Wilaya ya Mvomero.

“Tuseme kwamba kituo chetu sasa kimebeba jukumu la kuwahudumia wananchi wengi wa Manispaa ya Morogoro, wagonjwa wa kawaida na wajawazito wanaofika kujifungulia hapa, kwa siku wajawazito 15 hadi 20 wanajifungua na wakati mwingine hufikia 30,” alisema Dk. Kongera.

Alisema wajawazito wenye matatizo makubwa wakati wa kujifungua, wamekuwa wakihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na wale ambao hawana matatizo, wakihudumiwa na kituo hicho.

Pamoja na kuzungumzia hayo, Dk. Kongera alisema kituo hicho kinakabiliwa na uhaba wa vifaa vya maabara na kuomba kuwezeshwa vifaa hivyo ili upimaji wa damu na magonjwa mengine ufanyike kwa umakini na usahihi.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Ibrahim Mahizo alisema kiwango cha kujifungua kwa wajawazito, inakadiriwa kwa mwezi wanafikia wajawazito 500 hadi 600.

“Katika idadi hii iliyotolewa na Kaimu Mganga wa kituo, wastani kwa mwezi inafikia wajawazito 500 -600, hiyo ni kazi kubwa sawa na hospitali …na tunawaomba wenzetu wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro watusaidie,“ alisema Dk. Mahizo mbele ya mbunge huyo.
 
Back
Top Bottom