Kitila Mkumbo: Prof Ibrahim Lipumba ni Msomi mwana mapinduzi anayewania urais mara ya tano

Nyanya mbichi

JF-Expert Member
Nov 10, 2011
3,716
2,208
PROFESA Ibrahim Haruna Lipumba ni msomi aliyebobea katika uchumi. Ni msomi pekee katika Tanzania ya leo aliyejitoa na kutumikia siasa kikamilifu na kwa muda mrefu.

Katika makala haya tunajadili wasifu wa Profesa huyu na nafasi yake katika mbio za urais katika Uchaguzi Mkuu mwakani.
Ibrahim Haruna Lipumba alizaliwa Juni, 6, 1952 katika Kijiji cha Ilolangulu mkoani Tabora. Baba yake alikuwa mmoja wa waasisi wa chama cha TANU kilichopigania uhuru na alishiriki mkutano muhimu wa chama hicho mwaka 1958 uliojadili umuhimu wa kuharakisha uhuru wa Tanganyika. Kwa hiyo Profesa Lipumba alizaliwa na kukulia katika familia ya kisiasa.

Kimsingi hata yeye Profesa Lipumba alikuwa kada wa TANU na baadaye CCM tangu akisoma hadi alipokuwa anafanya kazi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadhi ya watu waliosoma naye Mlimani walishtuka waliposikia anagombea urais kupitia chama cha upinzani, Chama cha Wananchi (CUF).
Alisoma shule ya wamissionari wa Uswidi (Swedish Free Mission Primary School (1959-1962) na Shule ya Msingi ya Juu ya L.A. (L.A. Upper Primary School) kutoka mwaka 1962 hadi mwaka 1966. Lipumba alisoma katika Shule za Sekondari Tabora (1967-1972) na Pugu (1971-1972).

Profesa Lipumba alisoma elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akihitimu shahada ya kwanza katika uchumi mwaka 1976 na shahada ya umahiri mwaka 1978. Profesa Lipumba alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliofaulu vizuri sana katika ngazi zote hizo na hivyo kuajiriwa kama mhadhiri msaidizi katika idara ya uchumi mara baada ya kumaliza masomo yake ya shahada ya kwanza.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Ibrahimu Lipumba, wakati huo maarufu kama Nguruyu, ndiye aliyekuwa mwanafunzi bora katika Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii akiwa amepata daraja la kwanza la juu kabisa akiwa na alama tano (GPA 5), ambayo ilimwezesha kupata zawadi ya Makamu Mkuu wa Chuo katika Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii.

Profesa Ibrahim Lipumba pia ana shahada ya uzamivu (Ph.D.) kutoka katika Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani, ambacho ni miongoni mwa vyuo vikuu bora 10 duniani.

Kifamilia, Profesa Lipumba ana mke na watoto wakubwa wawili. Hata hivyo, Profesa Lipumba amekuwa si mtu anayependa kuzungumzia mambo ya familia yake hadharani.

Kikazi, Profesa Lipumba ni mwanataaluma aliyebobea katika uchumi akijikita katika biashara ya kimataifa na fedha, maendeleo ya uchumi na uchumi wa kilimo.

Alianza kazi kama mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupanda ngazi hadi kufikia ngazi ya profesa mshiriki mwaka 1989. Mwaka 1993 hadi 1995 alikuwa profesa mwalikwa katika Kituo cha Maendeleo ya Uchumi katika Chuo cha Williams nchini Marekani. Mwaka 1996 hadi 1998 alikuwa mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Uchumi (UNU/WIDER) kilichopo nchini Finland.

Profesa Lipumba alipata kuwa mshauri mwelekezi katika mashirika na taasisi kadhaa zikiwemo Benki ya Dunia, SIDA, Global Coalition for Africa, COMESA, NORAD, DANIDA, Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland, na Benki Kuu ya Tanzania.

Profesa Lipumba alipata kusoma na/au kufanya kazi na baadhi ya wachumi maarufu duniani, wakiwemo Profesa Joseph Stiglitz aliyekuwa mshauri wa uchumi wa Rais Bill Clinton na baadaye mchumi wa Benki ya Dunia.

Alipata kusoma na kufanya kazi na Profesa Jeffrey Sacchs ambaye ametajwa mara mbili na Jarida la Times kuwa miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi zaidi duniani.

Profesa Lipumba alipata pia kufanya kazi na Profesa Hernando de Soto, mchumi maarufu wa Peru. Huyu ndiye ‘aliyekodishwa' na Rais Benjamin Mkapa kuja kuanzisha mkakati wa kurasimisha biashara za wanyonge kama sehemu ya kukuza kipato cha Taifa, maarufu kama Mkakati wa Kurasmisha Raslimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA).

Kati ya mwaka 1991 na 1993, Profesa Lipumba alikuwa mshauri wa Rais Ali Hassan Mwinyi katika mambo ya uchumi. Ni katika kipindi hicho tuliposhuhudia sera za soko huria zikishika kasi nchini na kuzikwa rasmi kwa Azimio la Arusha.

Aidha, katika kipindi hicho Profesa Lipumba alikuwa Kamishina wa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma. Ndiyo kusema, Profesa Lipumba alishiriki kikamilifu katika kutungwa kwa sera ya kubinafsisha mashirika ya umma iliyozaliwa kipindi cha urais wa Mwinyi na utekelezaji wake kupamba moto wakati wa Rais Mkapa.

Kiitikadi, Profesa Lipumba anaamini zaidi katika sera za soko huria na falsafa ya uliberali, ambayo ndiyo itikadi mama ya Chama cha Wananchi (CUF). Kimsingi, mtazamo wa sera wa Profesa Lipumba ndiyo unaotekelezwa na serikali ya Chama cha Mapinduzi tangu wakati wa Mwinyi.
Kwa ubobezi wake na mlingano wa mtazamo kifalsafa na kisera na serikali ya CCM, na kama tungekuwa Taifa linalojali taaluma na utaalamu zaidi kuliko kujali tofauti za vyama, pengine Profesa Lipumba ndiye aliyefaa zaidi kuwa Waziri wa Fedha katika kipindi hiki ambapo nchi yetu imeyumba sana katika sera za uchumi.

Hii ni kwa sababu falsafa na sera za kiuchumi za serikali ya Mkapa na hata ya sasa ndiyo imekuwa falsafa ya Profesa Lipumba na kwa kweli yeye ndiye mtunzi wake wakati akiwa mshauri wa uchumi wa Rais Mwinyi.

Kwa hiyo, wasifu mkuu wa Profesa Lipumba kisiasa ni ubobezi wake katika mambo ya uchumi, na uwezo wake wa kuelezea sera zake za uchumi katika lugha ambayo mtu yeyote anaweza kuielewa na kuikubali.

Wasomi kadhaa wa uchumi niliozungumza nao wanaamini kwamba Profesa Lipumba ndiye mchumi bora zaidi hapa Tanzania. Aidha, pamoja na kwamba yupo katika siasa, Profesa Lipumba ameendelea kuheshimika katika taaluma ya uchumi duniani.
Hata hivyo, taaluma yake imekuwa haitumiki ipasavyo hapa nyumbani kwa sababu watawala wetu hujali ufuasi wa vyama zaidi kuliko utaalamu wa mtu katika kupanga watu katika nafasi nyeti za kazi.

Katika ulimwengu wa taaluma, tunaweza kusema Profesa Lipumba ni msomi mwanamapinduzi. Wasomi wanamapinduzi hujihusisha moja kwa moja na harakati za kisiasa zenye lengo la kufanya mabadiliko ya kiutawala katika nchi.

Kundi hili la wasomi hushiriki kikamilifu katika harakati za kisiasa zinazolenga kuondoa tabaka la wanasiasa waliopo madarakani.
Kwa hiyo wasomi wa kundi hili hujiunga na vyama vya siasa vilivyopo ama huanzisha vyama vyao kama njia ya kueneza falsafa zao na uwanja wa kupigania mabadiliko.

Katika historia ya nchi yetu mfano mwingine wa msomi mwana mapinduzi ni Profesa Abdulrahman Babu aliyeanzisha na kuongoza chama cha Umma kilichoshiriki kikamilifu katika kung'oa tabaka la Waarabu Zanzibar, na baadaye kushiriki kikamilifu katika harakati za kuking'oa Chama cha Mapinduzi hadi alipofariki.

Kwa hiyo Profesa Lipumba ni kati ya wasomi wachache walioamua kujitoa mhanga na kushiriki harakati za mabadiliko ya utawala, na kuacha masurufu mengi yanayoambatana na usomi. Na hii ndiyo sifa ya kwanza muhimu ya Profesa Lipumba.

Kwa ubobezi wake katika mambo ya uchumi, Profesa Lipumba angeweza kubaki kufanya kazi za kitaaluma na kutajirika kwa kufanya kazi za kutoa ushauri elekezi na kuzunguka duniani akitoa mihadhara ya kitaaluma.

Nilipozungumza na viongozi wanaofanya naye kazi katika CUF walinieleza kwamba sifa moja muhimu sana ya Profesa Lipumba ni uadilifu na ni mtu anayependa utaratibu na kuheshimu mipaka ya nafasi yake. Kama Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba amekuwa hajihusishi kabisa na maswala ya fedha bali anaviamini vyombo vya utendaji katika chama chake.

Kiongozi mmoja wa CUF alimwelezea Lipumba kama ‘kiongozi mwadilifu anayeishi uadilifu'. Nilipozungumza na viongozi wa chini kabisa wa CUF huko Buguruni walimwelezea Profesa Lipumba kama mtu anayeishi maisha ya kawaida na ni mtu wa kujichanganya kiasi kwamba wao hujisahau kama wapo na mtu anayeheshimika kitaaluma nchini na duniani.

Kwa muhtasari, Profesa Lipumba ana sifa tatu muhimu za kiongozi. Sifa ya kwanza ni kwamba Profesa Lipumba ana falsafa ya kisiasa anayoisimamia na amechora dira ambayo anaamini nchi inapaswa kufuata ili kujitoa katika umasikini.

Profesa Lipumba anaamini kwamba umasikini ndiye adui mkubwa wa Taifa hili na ili wananchi wajikomboe na umasikini lazima nchi ianzishe viwanda vitakavyoajiri watu wengi na kuzalisha bidhaa na kuliepusha Taifa kuwa la wachuuzi na dampo la bidhaa za nje.
Pili, Profesa Lipumba ni muadilifu na mtu anayefuata maadili na utaratibu wa uongozi. Hii si sifa utakayoikuta kwa viongozi wengi wa kisiasa nchini.

Tatu, Profesa Lipumba amejitoa mhanga kwa kuachana na masurufu mengi yanayoambatana na usomi na kushiriki moja kwa moja katika harakati hatari za kupambana katika kujaribu kuleta mabadiliko ya utawala. Kwa kifupi, Profesa Lipumba ni mpambanaji.
Udhaifu wa Profesa Lipumba unajitokeza katika maeneo makubwa mawili. Kwa mujibu wa viongozi wa CUF niliozungumza nao, na ambao wamefanya kazi na Profesa Lipumba kwa muda mrefu, eneo la kwanza la udhaifu lipo katika kufanya maamuzi.

Wanasema Profesa Lipumba ni kiongozi mwepesi kukubali maoni ya wengi bila kujali usahihi wa jambo lenyewe, hasa kama watu waliomzunguka wana nguvu. Ni mtu wa kukwepa lawama. Katika hili kiongozi moja wa CUF alikuwa wazi kabisa kwa kusema kuwa ‘Wazanzibari wamemzidi Profesa, hana uwezo wa kuwakabili na ni kwa sababu hii chama kimeendelea kudhoofika kwa upande wa Bara'.
Eneo la pili la udhaifu wa Profesa Lipumba ni ukweli kwamba kwa muda wote aliofanya siasa ameshindwa kujipambanua kwamba yeye ni kiongozi wa kitaifa aliye juu ya dini yake.

Mara nyingi Profesa Lipumba amejijengea taswira kama kiongozi anayepigania maslahi ya dini yake. Taswira hii ilikuja kuimarika zaidi mwaka jana pale ambapo alinaswa katika video akihamasisha waumini wa dini yake kujipanga kimkakati katika Uchaguzi Mkuu ujao akisisitiza kwamba ‘wenzetu wameshajipanga'.

Aidha, katika video hiyo Profesa Lipumba alionekana akikiri kwamba ‘alimsaidia Rais Kikwete kupata ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 kwa kile kilichotafsiriwa kama sababu za kulinda maslahi ya dini yake.
Profesa Lipumba hajawahi kutoa maelezo ni nini hasa alimaanisha katika video hiyo iliyonaswa na ambayo bado ipo katika mtandao wa YouTube.
Hata hivyo, inajulikana kwamba Profesa Lipumba na Rais Kikwete walikuwa ni marafiki wakubwa tangu walipokuwa wakisoma Mlimani na haijulikani kama urafiki huo uliwahi kukoma!

Kuna baadhi ya watu wanaosema kwamba Profesa Lipumba amegombea mara nyingi mno na kutaja kuwa huu nao ni udhaifu kwa kuwa anaonekana ni king'ang'anizi wa madaraka.

Lakini, kwangu hiyo si hoja ya msingi kwa kuzingatia mazingira ya siasa za upinzani katika Bara la Afrika. Katika mazingira haya, kugombea kupitia upinzani ni kujitoa mhanga, na si watu wengi walio tayari kujitoa mhanga hasa kwa mtu wa kiwango cha elimu na utaalamu wa Profesa Lipumba.

Aidha, siasa za upinzani ni siasa za mapambano na kugombea kupitia upinzani ni sehemu ya mapambano na si suala la kutafuta kula na madaraka tu kama ilivyo kwa chama tawala.
Aliyekuwa Rais wa Senegal Abdullah Wade, ambaye naye ni Profesa wa Uchumi, aligombea mara tano kuanzia mwaka 1978 na alikuja kushinda mwaka 2000.

Mfano mwingine ni Rais wa zamani wa Zambia, Michael Sata, maarufu kama King Cobra, aliyefariki dunia karibuni, ambaye alianza kugombea urais tangu mwaka 2001 lakini alikuja kushinda mwaka 2011.
Hitimisho

Hakuna shaka kwamba Profesa Lipumba ni kiongozi mwenye falsafa na dira. Ni Mtanzania aliyezaliwa na kukulia katika maisha ya kawaida na akafanya bidii katika kazi hadi kufika ngazi za juu kabisa za kitaaluma na kisiasa.

Profesa Lipumba ni mpambanaji asiyechoka. Ni kati ya wanasiasa waliozunguka zaidi nchi hii kwa gari na mguu.
Kitu kimoja ambacho kinamtenga mbali kabisa na wagombea wengine wanaotajwa ni ubobezi wake katika sera za kiuchumi na weledi wa kuzifafanua kwa kiwango ambacho binadamu yeyote mwenye akili za kawaida lazima aelewe.

Katika mazingira ambayo asilimia 63 ya wananchi wanataja umasikini na uchumi kama ndiyo matatizo ya msingi zaidi kwa Tanzania kwa sasa, pengine Profesa Lipumba ndiye ambaye angefaa kuwa Rais wetu wa awamu ya tano.

Bila shaka Profesa Lipumba atakuwa mshindani muhimu katika kutafuta mgombea wa muungano wa vyama vya upinzani kama vyama vinavyoshirikiana vitaruhusu ushindani katika kutafuta mgombea mmoja.

Tunamtakia Profesa Lipumba kila la kheri katika mbio zake za kutafuta ukuu wa nchi, pamoja na kwamba yeye mwenyewe aliniambia hajaamua kama atagombea au la.

Chanzo:Raia mwema
 
Kuna baadhi ya watu wanaosema
kwamba Profesa Lipumba
amegombea
mara nyingi mno na kutaja kuwa huu
nao ni udhaifu kwa kuwa
anaonekana
ni king’ang’anizi wa madaraka.
Lakini,

((((((((((@ kwangu hiyo si hoja ya
msingi
kwa kuzingatia mazingira ya siasa
za
upinzani katika Bara la Afrika.
Katika
mazingira haya, kugombea kupitia
upinzani ni kujitoa mhanga))))))))))


hapo kwenye blacket sasa mbona unawalalamikia viongozi wa juu wa chadema kuwa ni wapenda madaraka na hawapendi mabadiliko? naomba ufafanuzi proffesa@Kitila.

, na si
watu
wengi walio tayari kujitoa mhanga
hasa kwa mtu wa kiwango cha elimu
na utaalamu wa Profesa Lipumba.
Aidha, siasa za upinzani ni siasa za
mapambano na kugombea kupitia
upinzani ni sehemu ya mapambano
na
si suala la kutafuta kula na
madaraka
 
Cuf hakuna mtu mwenye sifa za uraisi??????

Toka aanze kugombea mtoto aliyezaliwa anafika mpaka chuo kikuu jamaa anagombea tu

Obsession gani hiyo???

Au ndio ubinafsi + uchu uliopitiliza??

Apishe wengine
 
Kwa CV ya lipumba ukimlinganisha na dr slaa,slaa anakua mkata majani yaani mtumishi wa shambani
 
MAKALA BY JULIUS MTATIRO TOLEO LA IJUMAA YA TAREHE 5 JUNI 2015
Kwa ufupiAlipata elimu ya msingi mkoani Tabora mwaka 1959 katika Shule ya Wamisionari wa Sweden waliokuwa Tanzania wakati huo, shule hiyo iliitwa “Swedish Free Mission Primary School”, alimaliza mwaka 1962 na akasoma Shule ya Kati (Middle School) mwaka 1962 – 1966 kabla ya kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari Tabora mwaka 1967 – 1972 kisha akaelekea mkoani Dar es Salaam na kusoma kidato cha tano na sita katika Shule Sekondari ya Pugu kati ya mwaka 1971-1972.

Historia yake

Ibrahim Lipumba ni mchumi wa kimataifa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF). Alizaliwa Juni 6, 1952 katika Kijiji cha Ilolangulu mkoani Tabora.

Alipata elimu ya msingi mkoani Tabora mwaka 1959 katika Shule ya Wamisionari wa Sweden waliokuwa Tanzania wakati huo, shule hiyo iliitwa “Swedish Free Mission Primary School”, alimaliza mwaka 1962 na akasoma Shule ya Kati (Middle School) mwaka 1962 – 1966 kabla ya kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari Tabora mwaka 1967 – 1972 kisha akaelekea mkoani Dar es Salaam na kusoma kidato cha tano na sita katika Shule Sekondari ya Pugu kati ya mwaka 1971-1972.

Alipata shahada mbili za kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mbili nyingine amezipata katika Chuo Kikuu cha Stanford, Marekani ambacho ni miongoni mwa vyuo 10 bora duniani. Shahada zote nne alizonazo ni za uchumi.

Alisoma na kupata shahada ya kwanza katika uchumi mwaka 1973 - 1976 na shahada ya Uzamili akiianza mwaka 1976 - 1978. Lipumba ni miongoni mwa Watanzania waliowahi kuweka rekodi nzito UDSM katika shahada ya kwanza, ndiye aliyekuwa mwanafunzi bora katika Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii akiwa amepata daraja la kwanza la juu kuliko wanafunzi wote (GPA 5) na alitunukiwa zawadi ya Makamu Mkuu wa Chuo katika Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii.

Profesa Lipumba alipojiunga Chuo Kikuu cha Stanford alisoma shahada mbili na kupata ufaulu wa heshima, kwanza alisoma na kuhitimu Shahada ya Uzamili mwaka 1977/1978 na kisha akasoma na kuhitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika uchumi kati ya mwaka 1978 – 1983. Kwa ujumla, elimu ya uchumi ya Profesa Lipumba imejikita katika masuala ya fedha na biashara za kimataifa na eneo la pili ni maendeleo ya uchumi na uchumi wa kilimo.

Kwa miaka mingi sasa Profesa Lipumba amekuwa mhimili mkubwa wa masuala mbalimbali ya uchumi duniani, ameshiriki katika majopo ya wanazuoni nguli wa uchumi duniani katika kutafuta mbinu bora za kusaidia nchi zilizoendelea na zinazoendelea ili kujikwamua kiuchumi. Ameshiriki moja kwa moja katika shughuli za kitaalamu kutathmini uchumi wa nchi nyingi duniani na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua, amefundisha katika vyuo vikuu vinavyoheshimika duniani na amewatumikia Watanzania katika nyanja za kiuchumi kwenye Serikali kadhaa.

Alianza ajira akiwa mhadhiri msaidizi UDSM na akawa mhadhiri mwandamizi baada ya kuhitimu PhD, alikuwa profesa mshiriki kuanzia mwaka 1989 kabla ya kuwa profesa miaka ya 1990.

Kimataifa amekuwa profesa mwalikwa katika Kituo cha Maendeleo ya Uchumi katika Chuo cha Williams Marekani 1989 – 1993, mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Uchumi (UNU/WIDER) kilichopo Finland mwaka 1993 – 1995.

Amekuwa akisimamia masuala ya uchumi wa dunia kwa ngazi ya ushauri wa kimataifa, amekuwa mchumi mshauri wa Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Duniani (IMF), UNDP, Sida, Norad, Danida, mashirika ya kikanda kama Comesa na baadhi ya nchi za Afrika, Ulaya na Asia.

Amefanya kazi kubwa za kiushauri ili kuinua mashirika mbalimbali ya umma nchini, amewahi kuwa mjumbe wa bodi ya TKAI, NIC, TWICO, Imara Wood Industries, Tume ya Rais ya kushughulikia masuala ya uchumi wakati wa Awamu ya Pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi, mwenyekiti wa tume kadhaa zilizoundwa na Rais za uchunguzi wa matatizo ya mashirika mbalimbali ya umma.

Profesa Lipumba amezaliwa na kukulia katika familia ya kisiasa. Baba yake mzazi ni miongoni mwa waasisi wa Tanu na alishiriki mkutano wa mwaka 1958 uliojadili kuharakishwa kwa uhuru wa Tanganyika. Mwenyewe amekuwa kada wa Tanu na baadaye CCM tangu akisoma hadi alipokuwa anafanya kazi.

Miaka michache baada ya vyama vingi kuanzishwa alijiunga na CUF. Moja ya mambo yaliyomsukuma ni kule kuona mambo mengi ambayo yeye na wenzake walikuwa wakiishauri Serikali ili kuinua uchumi wa nchi yalikuwa hayafanyiwi kazi au yanafanyiwa kazi kisiasa na matokeo yake uchumi unazidi kudidimia na umaskini unaongezeka. Profesa Lipumba ameoa na ana watoto wawili.

Mbio za ubunge

Profesa Lipumba hajawahi kugombea ubunge tangu alipojiunga na siasa.

Mbio za urais

Profesa Lipumba alianza mbio za urais mwaka 1995 kupitia CUF akaibuka nafasi ya tatu kwa asilimia 6.43, akiwa nyuma ya mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa (asilimia 61.82) na Augustine Mrema wa NCCR (asilimia 27.77).

Mwaka 2000, aligombea urais kwa mara ya pili na kushika nafasi ya pili akipata asilimia 16.26 ya kura zote. Huu ni uchaguzi ambao Rais Mkapa wa CCM aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 71.74 ya kura zilizopigwa.

Mwaka 2005, CUF ilimpa tena kazi hiyo kwa mara ya tatu, alipambana vilivyo na mwanasiasa maarufu wakati huo, Jakaya Kikwete wa CCM na kushika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 11.68. Kikwete alikuwa na asilimia 80.28.

Mwaka 2010, CUF ilimtaka akatupe karata kwa mara ya nne, safari hii aliibuka mshindi wa tatu kwa kupata asilimia 8.28 nyuma ya Rais Kikwete wa CCM aliyekuwa na asilimia 62.83 na Dk Willibrod Slaa wa Chadema aliyepata asilimia 27.05.

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Profesa Lipumba ni mmoja wa Watanzania mashuhuri wanaotajwa kuwa na sifa, uwezo, vigezo na nafasi ya kuwa Rais wa Tanzania, hasa ikizingatiwa kuwa vyama vya upinzani vyenye wabunge nchini vimeweka azimio la kusimamisha mgombea urais mmoja kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Mwezi uliopita akiwa mkoani Tabora alitangaza kwamba atachukua fomu na kukiomba chama chake kimpe fursa ya kufanyiwa tathmini na wagombea wengine wa Ukawa ili kumpata mtu mmoja atakayesimama katika nafasi hiyo.

Nguvu yake

Sifa na nguvu yake ya kwanza ni umaarufu na kuheshimika ndani na nje ya nchi. Hakuna mahali popote katika nchi hii utakapotaja jina lake watu wasimfahamu, lakini hata kimataifa wanamfahamu vizuri kwa uchapakazi wake na misimamo yake katika ukuzaji wa uchumi. Kinachonistaajabisha ni kuwa, si mtu wa kupenda kutumia umaarufu wake kufanya “siasa rahisi” (cheap politics). Anaamini kuwa siasa si ujanjaujanja wala jambo la masihara.

Lakini jambo la pili ni uadilifu na uwazi. Kwa bahati nzuri nimefanya kazi naye kwa zaidi ya miaka mitano na namfahamu katika eneo hili. Hata mara moja ndani ya chama chake hawezi kujaribu kuingilia masuala ya fedha na hayamhusu kabisa lakini pia anachukia mbinu zozote zile ambazo zinaweza kufanywa ndani ya chama chake na hata nje, ambazo zitaleta taswira ya kukosa uaminifu kwenye fedha.

Nadhani ndiyo sababu kuu kwamba CUF kwa muda mrefu imekuwa ikipata madhara kidogo katika ukaguzi wa hesabu zake za fedha, kulinganisha na vyama vingine vyote vinavyopokea ruzuku kutoka serikalini na hata michango ya wanachama.

Tatu, Profesa Lipumba ni mtu wa kawaida na anaishi maisha ya kawaida. Hupenda kufanya mazoezi mara kwa mara na haiwezekani apite bila kukusalimia. Nakumbuka mwaka 1995 alipoanza kampeni za urais alikuwa anatumia “kigari” cha milango miwili tu, wa dereva na wa kwake, alikitumia kuzunguka nchi nzima bila kuhofia kuwa hadhi yake si ya kuendeshwa na kigari kama kile. Ni wanasiasa wachache Afrika wenye ustahimilivu na maisha haya.

Ni Mtu wa kujitolea. Nimeshuhudia CUF ikimlipa kiongozi huyu shilingi milioni moja tu kwa mwezi za posho (CUF hawalipi mishahara). Kwa mwaka, anaweza kutumia posho yake ya miezi hadi sita akielekeza (posho nzima) ipelekwe mahali fulani kusaidia wagonjwa au watu wengine. Kuna wakati amewahi kuniagiza (nikiwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF), kupeleka posho yake yote ya mwezi kwa waathirika wa mabomu ya Arusha. Haishi kwa kutegemea siasa, anaamini siasa si ajira wala sehemu ya kujinufaisha na ndiyo maana hata mimi hadi leo hii nimekuwa na mtazamo na msimamo wa namna hiyo.

Mwisho, huenda ndiye mwanasiasa pekee (kwa siasa za kuanzia mwaka 1995 – 2015) aliyewahi kuzunguka Tanzania na kushuhudia matatizo ya wananchi kuliko mtu mwingine yeyote. Kila mwaka anatumia wastani wa siku hadi 130 akiwa kwenye ziara za ujenzi wa chama mikoani lakini kila baada ya miaka mitano kuanzia mwaka 1995 alipata wasaa wa kuzunguka, bila kupumzika, kwenye majimbo yote kuomba kura kwa wananchi. Sijui nani mwingine ameweka rekodi hii.

Udhaifu wake

Kwa siasa za Tanzania, moja ya udhaifu mkubwa wa Profesa Lipumba ni kuchukulia kila jambo kitaaluma, “He is too academic”. Hali hii inamfanya wakati mwingine asieleweke kwa watu wanaomsikiliza. Mathalan, anaweza kuhutubia wananchi na akatumia muda mwingi kutoa takwimu za Benki ya Dunia au masuala ya tafiti za kutaalamu. Watanzania wengi hawana elimu kubwa na hata waliosoma wana ufahamu wa kadri mno, kuwapangia mikakati ya uhuishaji wa siasa na nchi kitaaluma kunawafanya wasijue mipango inayoongelewa.

Kuna wakati huzungumzia masuala ya uchumi na maendeleo na akamaliza mkutano na waandishi wa habari, akishaondoka waandishi wanakufuata na kukuuliza mambo mengi yanayohitaji ufafanuzi. Akiwa mtu ambaye anatajwa kuwa na sifa na vigezo vya urais, udhaifu huu unamfanya asifikishe ujumbe wake wa mabadiliko kirahisi.

Pili, ni mtu aliyeweka familia yake mbali na siasa, Hili si jambo dogo. Kuna watu hawakumpigia kura katika chaguzi alizoshiriki kwa kupewa propaganda kali kuwa hana mke na hajawahi kuwa na mke wala mtoto. Ukweli ni kuwa Lipumba ana mke na watoto wawili wakubwa, ni mmoja wa wanasiasa wenye familia na ndoa imara huku akijua majukumu yake ya ulezi wa familia katika jamii. Sielewi kwa nini hapendi kuchanganya familia yake na siasa kwa sababu taswira anayoipata kwa jamii kutokana na uamuzi huo nadhani siyo nzuri. Ndiyo maana wengi wanadhani yeye ni “Senior Bachelor”.

Mwisho, kuna nyakati hatumii nafasi yake ya uenyekiti wa chama sawasawa. Ameacha mambo mengi yaamuliwe kwa mawazo, maoni na ushauri wa watu waliomzunguka kuliko kufanya uamuzi mgumu wakati mwingine akiwa mwenyekiti. Anataka kila jambo liamuliwe kwa pamoja na sikuwahi kuona hata mara moja akiamua jambo peke yake, sielewi kama ni lengo la kukwepa lawama za uamuzi au ni utaratibu wake. Kwa siasa za Afrika, kiongozi wa juu wa taasisi kuna nyakati nyingi tu anapaswa achukue uamuzi mwenyewe na abebe lawama mwenyewe kwani huwezi kuwa na uhakika kama watu wote waliokuzunguka wana uwezo wa kukushauri vizuri muda wote.

Nini kinaweza kumfanya apitishwe?

Mambo kadhaa yanaweza kufanya CUF impitishe kugombea urais na kurahisisha pia tiketi yake ndani ya Ukawa:

Moja, msomi mahiri wa uchumi katika ngazi ya kimataifa na kwa Tanzania, amekuwa akionekana kama mchumi bora zaidi kuliko wote. Profesa Kitila Mkumbo, Mhadhiri wa UDSM katika andiko lake juu ya kiongozi huyu, anaeleza kuwa “…Wasomi kadhaa wa uchumi niliozungumza nao wanaamini kwamba Profesa Lipumba ndiye mchumi bora zaidi hapa Tanzania. Aidha, pamoja na kwamba yupo katika siasa, Profesa Lipumba ameendelea kuheshimika katika taaluma ya uchumi duniani. Hata hivyo, taaluma yake imekuwa haitumiki ipasavyo hapa nyumbani kwa sababu watawala wetu hujali ufuasi wa vyama zaidi kuliko utaalamu wa mtu katika kupanga watu katika nafasi nyeti za kazi”. CUF na Ukawa nadhani vinahitaji mgombea mwenye sifa hii.

Pili, naamini kwa siasa za upinzani za Tanzania, Profesa Lipumba ndiye kiongozi pekee mwenye uzoefu mkubwa wa kusimamia masuala ya kimataifa kumshinda mtu mwingine yeyote. Ametumia sehemu kubwa ya maisha yake akisimamia miradi mikubwa ya kiuchumi katika nchi nyingi na mashirika ya kimataifa duniani. Uzoefu wa kimataifa ni turufu muhimu kwa kiongozi yeyote wa kisiasa.

Mwisho, ana uzoefu mkubwa na utendaji wa ngazi ya juu ndani ya Serikali kwa sababu amefanya kazi serikalini, ameshauri mambo mengi kuhusu uhuishaji wa mashirika ya umma, amekuwa mtu muhimu kiushauri kwenye miaka ya nyuma katika Benki Kuu ya Tanzania na nyinginezo. Rekodi hizi nadhani zinakifanya chama chake kimpe nafasi kubwa kabisa kumshinda mtu yeyote yule na huenda hata ndani ya Ukawa awaka na sifa za juu kuwashinda wanasiasa wengine.

Nini kinaweza kumwangusha?

Jambo moja tu ndilo naliona kama kikwazo kwake. Ikiwa makubaliano ya ndani ya Ukawa yataonyesha kuwa CUF haipaswi kutoa mgombea urais kwa sababu labda umoja huo umeamua mgombea atoke kati ya NCCR, NLD na Chadema. Hili peke yake ndilo linaweza kumkwamisha.

Asipochaguliwa (Mpango B)

Kwa mtizamo wangu, ikiwa hatagombea urais mwaka huu na labda kutochaguliwa na chama chake, Ukawa inaweza kumtumia kugombea ubunge kwenye majimbo ya Kinondoni, Segerea au Temeke. Watu wengi niliozungumza nao wanaumia kwa kumkosa bungeni.

Mfano wa umuhimu wake kwenye vyombo vya uamuzi wa mambo makubwa ya nchi ulijidhihirisha kwenye Bunge la Katiba. Nitaumia hatagombea urais halafu tena asigombee ubunge. Pia, ikiwa Ukawa itashinda uchaguzi wa mwaka huu, simuoni waziri mkuu bora wa Serikali ya kisasa kama Profesa Lipumba.

Lakini pia kama hatagombea urais nadhani atakuwa na jukumu la kuongoza chama chake kwa miaka minne ya kipindi chake ambacho nadhani ni cha mwisho kabisa, kuendelea kuishauri Serikali ijayo bila kujali itaundwa na Ukawa au CCM na kuendelea kufanya kazi za kitaalamu za kitaifa na kimataifa.

Hitimisho

Sikupata shida kumtathmini Profesa Lipumba kwa sababu nimefanya naye kazi kwa karibu. Watu waliofanya kazi chini yake wamejifunza bidii kazini, nidhamu, kutunza muda, kuchukulia siasa kama kazi ya kujitolea na kusaidia wananchi na kuamini kuwa siasa inawajibika kutumikia uchumi. Ni mmoja wa wanasiasa wa kweli na wanaochukia mikakati ya ki-propaganda hata kutoka ndani ya chama chake. Sielewi ni wanasiasa wangapi nchi hii wana uwezo, uthubutu, elimu, umashuhuri, wajibikaji na kujituma kama kiongozi huyu. Namtakia kila lililo jema katika safari yake ndefu katika siasa za Tanzania.

"safari ya upinzani sio ndugu ukiambiwa mtatiro huyu wa sasa ambaye ni mwenyekiti wa muda kuwa sio mtatiro aliyeandika haya huwezi kubisha, Makamba alisema uongo nao una benki"
 
Tabia ni ngozi ya mwili, ina maana prof lipumba kabadilika sana ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, Je haya maneno ya ndugu mtatiro hayaipi hoja ya ndugu zitto ya kutowaamini wanasiasa, Mrisho mpoto katika nyimbo zake kuna wimbo una ubeti wenye maneno haya "waliopo hatuwataki, wanaotaka tuwape hatuwaamini" ndo kinachoweza kuwa kinatukumba watanzania
 
Tabia ni ngozi ya mwili, ina maana prof lipumba kabadilika sana ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, Je haya maneno ya ndugu mtatiro hayaipi hoja ya ndugu zitto ya kutowaamini wanasiasa, Mrisho mpoto katika nyimbo zake kuna wimbo una ubeti wenye maneno haya "waliopo hatuwataki, wanaotaka tuwape hatuwaamini" ndo kinachoweza kuwa kinatukumba watanzania
Watu wanabadilika, na sio wanasiasa tu, rafiki, mke, mpenzi wote hakuna guarantee kuwa watakuwa watiifu na loyal kwako daima
 
Back
Top Bottom