Kitila Mkumbo: Je, Tanzania ina mtaala wa elimu

ESAM

JF-Expert Member
Mar 15, 2011
1,148
2,000
Je, Tanzania tuna mtaala wa elimu?

Kitila Mkumbo

WIKI ya kwanza ya Bunge la 10 lililoanza Januari 29, mwaka 2013 lilitawaliwa na hoja mbili binafsi kuhusu elimu. Hoja ya kwanza ni ile iliyowasilishwa na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba, kuhusu kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa elimu ya juu. Hoja hii haikuwa na msisimko mkubwa kutokana na ukweli kwamba hapakuwa na kitu kigeni katika hoja yenyewe kwa kuwa mambo aliyoyawasilisha Mheshimiwa Nchemba yamezungumzwa mara nyingi na wadau mbalimbali, ndani na nje ya Bunge, na kimsingi hoja yenyewe ilijengwa katika msingi wa sera ya elimu ya juu ya CHADEMA kama ilivyoanishwa katika ilani yake ya mwaka 2010.
Hoja iliyoonekana kusisimua ni ile iliyowasilishwa na Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Mheshimiwa James Mbatia. Hoja ilikuwa na msisimko kutokana na uzito wa hoja yenyewe na aina ya mbunge aliyewasilisha.

Wafuatiliaji wa mambo ya siasa za Tanzania wanaujua vizuri uanasiasa wa James Mbatia na hasa ubunge wake uliotokana na kuteuliwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete. Mbatia amekuwa na kazi kubwa ya kuthibitisha kwamba kuteuliwa kwake na Rais kuwa mbunge hakujafifisha taswira yake ya upinzani.

Kwa hiyo baadhi yetu tulikuwa tunasubiri kwa hamu Mbatia angesema nini katika hoja yake, na hasa kama angekuwa tayari kuirushia takataka mamlaka iliyomteua. Kwa kiasi kikubwa Mbatia alifanikiwa sana katika hoja yake, hasa kwa kuonyesha kwa ufasaha udhaifu mkubwa wa sekta ya elimu hapa nchini.

Pamoja na kwamba hoja ya Mbatia haikuwa ngeni miongoni mwa wadau wa elimu kwa kuwa alikariri mambo ambayo yameelezwa katika machapisho na matamasha mbalimbali nchini kwa miaka kadhaa sasa, ilikuwa ni hatua muhimu kwa kuwa udhaifu wa sekta ya elimu haujawahi kuanikwa bungeni kwa kiwango alichofanya Mbatia.

Kilichonisukuma kuandika makala haya ni baadhi ya maudhui yaliyomo katika hoja ya Mbatia, na hasa madai yake kwamba Tanzania haina mitaala ya elimu na kwamba nchi yetu haijawahi kuwa na mitaala ya elimu tangu tupate uhuru mwaka 1961.

Madai haya ya Mbatia sio mageni kwa sababu amewahi pia kukaririwa mara kadhaa katika vipindi vya televisheni akieleza kwa kujiamini kabisa kwamba nchi yetu haina mitaala ya elimu. Nieleze mapema kabisa kwamba madai ya Mbatia sio sahihi.

Kuamini anachokisema Mbatia ni sawa na kuamini kwamba nchi yetu haijawahi kuwa na mfumo rasmi wa elimu tangu mwaka 1961. Hii inaweza kumaanisha vile vile kwamba watu waliosoma tangu mwaka 1961 vyetu vyao, utaalamu na utaaluma wao ni batili kwa sababu haijulikani walijifunza nini na walijifunzaje!!

Bahati mbaya sana kwamba Wizara ya Elimu na Utamaduni ilishindwa kumjibu Mheshimiwa Mbatia na wabunge wengine kiufasaha ili waelewe vizuri dhana ya mtaala. Badala yake ubabe na mabishano ya kisiasa yalitawala hoja ya Mbatia. Matokeo yake wananchi wengi wanaelekea kuamini kwamba nchi yetu haina mitaala na pengine hii ndiyo sababu sekta ya elimu inayumba katika nchi yetu.

Pengine kabla ya kumuonyesha Mheshimiwa Mbatia kwamba nchi yetu siku zote imekuwa na mitaala ni vizuri nifafanue maana ya neno ‘mtaala'. Katika kufafanua maana yake, nianze kwa kukiri kwamba neno ‘mtaala' ni kati ya maneno yanayowatatiza sana wataalamu wa elimu duniani kutokana na kuwa na maana nyingi. Neno mtaala tumelitafsiri kutoka neno la Kiingereza liitwalo ‘curriculum', ambalo limetokana na neno la kilatini liitwalo ‘currere' lenye maana ya ‘mpangilio na utaratibu ambao mtoto hupitia katika kufikia utu uzima'.

Katika elimu neno mtaala (curriculum) linamaanisha utaratibu, mpangilio, muundo na maudhui ambayo mwanafunzi hupaswa kufuata na kukamilisha kama sehemu ya matakwa ya kupata tuzo fulani ya kielimu na kitaaluma. Neno mtaala vilevile lina maanisha matarajio, malengo na maudhui ambayo mwanafunzi anatarajiwa kuyakamilisha kabla ya kutunukiwa tuzo ya kitaaluma katika ngazi fulani.

Wataalamu wengine wa elimu wameeleza maana ya mtaala kwa urahisi zaidi kwa kusema kuwa ni mtiririko na maudhui ya masomo ambayo mwanafunzi huchukua katika ngazi fulani ya elimu. Maana hii ni sawa na maana ya neno linaloshabihiana na mtaala linaloitwa muhtasari au ‘sylabus' kwa Kiingereza. Hata hivyo, katika elimu mtaala ni mpana zaidi ya muhtasari wa somo, pamoja na kwamba muhtasari au syllabus ni sehemu ya mtaala (curriculum). Ndio kusema kuwa muhtasari wa somo ni sehemu ya mtaala lakini peke yake hauwezi kuwa mtaala.

Kuna aina mbalimbali za mitaala. Kuna mitaala ambayo imeandikwa na ambayo haijaandikwa. Kuna mitaala inayoonekana na isiyoonekana. Kimsingi mtaala ni mambo yote ambayo mwanafunzi hupitia katika kujifunza tangu anapojiunga na mfumo rasmi wa elimu hadi anapohitimu katika ngazi fulani ya elimu, ikiwemo malengo ya elimu, maudhui, njia na nyenzo za kujifunzia na njia za tathmini. Mtaala huonekana na kutafisiriwa kwa njia mbalimbali zikiwemo malengo ya elimu, muundo wa elimu, maudhui ya elimu, nyaraka za elimu na mihtasari ya masomo ya elimu katika ngazi mbalimbali. Kimsingi si rahisi kuwa na nyaraka moja na ukaiita mtaala kwa sababu mtaala ni mkusanyiko wa nyaraka nyingi. Baadhi ya nchi wamechukua malengo ya elimu ya jumla pamoja na muhstasari wa mihtasari ya masomo mbalimbali wakayaweka pamoja na kisha wakaita mtaala wa elimu katika ngazi mbalimbali. Hata hivyo, sio kila nchi ina mtaala mmoja ulioandikwa.

Kwa maelezo ya hayo, utaona kwamba haikuwa rahisi (pamoja na kwamba haikuwa vigumu) kumpatia Mheshimiwa Mbatia nakala ya mtaala wa elimu Tanzania. Ingekuwa mimi ndiye Waziri wa Elimu ningeweza kuchukua nakala ya muhtasari mmojawapo wa somo nikampatia Mbatia na ningekuwa nimempatia mtaala. Vilevile ningeweza kuchukua ‘Prospectus' ya moja ya vyuo vikuu nchini nikampatia Mheshimiwa Mbatia na ningekuwa nimempatia Mtaala wa Chuo Kikuu. Kimsingi kama Waziri Kawambwa angeamua kuleta nakala za mitaala ya elimu Tanzania huko bungeni ukumbi wa Bunge usingetosha!

Nchi yetu ina malengo, mfumo, muundo, utaratibu, mpangilio na maudhui ya elimu katika kila kazi. Tuna malengo ya jumla na mahususi ya elimu katika ngazi mbalimbali za elimu ambayo yameanishwa katika nyaraka mbalimbali. Aidha, tuna mihtasari ya kila somo katika kila ngazi ambayo imeainisha, pamoja na mambo mengine, malengo ya jumla na mahususi ya elimu na maudhui na njia ambazo mwanafunzi atajifunza katika kila ngazi husika.

Tuna utaratibu wa wazi kabisa juu ya lini mtoto anaanza shule na lini anamaliza, na anatakiwa afanye nini ili aende katika ngazi nyingine ya elimu. Haya ndiyo mambo yanayounda mtaala wa elimu. Sasa kutokuwa na nyaraka moja iliyoandikwa na ikaitwa ‘mtaala' haimaanishi kwamba nchi yetu haina mtaala. Ni sawa na kusema Uingereza haina Katiba kwa sababu tu Katiba yake haijaandikwa katika waraka mmoja unaoitwa Katiba.

Tafiti ambazo zimefanywa na mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi yameonyesha waziwazi kabisa kwamba matatizo ya elimu Tanzania hayatokani na kutokuwa na mtaala au kuwa na mitaala dhaifu, bali udhaifu wa utekelezaji wa mitaala, ikiwemo mazingira magumu na dhaifu ya kufundishia na kujifunzia.

Ni vizuri wanasiasa wetu wakajenga utamaduni wa kupata ushauri wa kitaaluma na kitaalamu kutoka kwa wataalamu na wanataaluma wa maeneo husika kabla hawajatoa kauli nzito bungeni zinazoweza kusababisha msuguano na mtafaruku usio wa lazima katika jamii. Ni vizuri pia wakajenga tabia na utamaduni wa kutumia marejeo ya kitafiti badala ya hisia katika kujenga hoja ndani na nje ya Bunge.

____________________

Hili ni darasa tosha kutoka kwa Dk. Mkumbo kwa anayetaka kufahamu dhana ya mtaala kwa ujumla.

Asante sana

 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom