Kitendo cha kuwakaribisha wawekezaji kwa pupa bila kuwa na mipango binafsi ya kupamba | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kitendo cha kuwakaribisha wawekezaji kwa pupa bila kuwa na mipango binafsi ya kupamba

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BRUCE LEE, Jan 3, 2011.

 1. BRUCE LEE

  BRUCE LEE JF-Expert Member

  #1
  Jan 3, 2011
  Joined: Dec 11, 2010
  Messages: 2,089
  Likes Received: 1,158
  Trophy Points: 280
  Mheshimiwa Rais, nitakueleza na kuwaeleza Watanzania wote mtazamo wangu na wa watu wanaofikiri sana na wazalendo wanaoipenda nchi hii hata zaidi wanavyojipenda wenyewe wanasemaje kuhusiana na juhudi zako za kusafiri kila siku kwenda ulaya na amerika kuongea na matajiri na kuwashawishi wao na serikali zao kuja kuwekeza katika nchi hii.

  Umekuwa ukiongea mara kwa mara katika vyombo vya habari kuwa huu ni wakati wa utandawazi na pia Tanzania ni lazima iyakubali mabadiliko haya na pia iende sambamba na dunia.
  Ni kweli Mheshimiwa tunakubaliana na wewe ni sawa kabisa lazima tukubali hiki ni kipindi cha utandawazi (globalization) na ni sawa kwenda sambamba na dunia lakini ni lazima tujiulize maswali, je tumejiandaaje kukabiliana na huo utandawazi?

  Tuna uhakika tutafaidika na utandawazi huo na pia hauta athiri maendeleo yetu pamoja na tamaduni zetu?

  Bwana Rais tupo tunao amini kitendo cha kuwakaribisha wageni waje kwa wingi kuwekeza na kutufundisha aina mbalimbali za biashara wanazo kuja kuwekeza ni kitendo cha kuurudisha ukoloni pamoja na ile hali ya kuishiwa ubunifu pamoja na miundo mbinu itakayo tuwezesha kutatua matatizo yetu wenyewe bila kuhitaji sana misaada ya watu wa nje.

  Naamini kabisa bado tunakumbuka mnamo mlango wa mwisho wa Karne ya 18, wazungu mabepari wa huko Ulaya na Amerika walikuwa tayari wameisha pitia mapinduzi ya kilimo pia tayari walikuwa wameisha gundua mashine mbalimbali ambazo zili wawezesha kuendelea mpaka kufikia kufanya mapinduzi ya viwanda(industrial revolution) na hali hiyo ilipelekea wakoloni hao kuanza kuhaha kutafuta sehem mbalimbali ambazo wataweza kupata malighafi zinazotakiwa katika viwanda vyao pia masoko ya bidhaa zao pamoja na sehemu zingine ambazo wataweza kuwekeza.

  Wazungu hao wanafiki na mafisadi waliweza kuwatuma ma ajenti wao kuja huku Afrika kwa kutumia Mwamvuli wa dini na biashara, kwani ma ajenti wa ukoloni huo walikua ni wamisheni, wapelelezi na wafanya biashara.

  Wamisheni hao walimsaliti Mungu wao kwa kulitumia Jina la yesu kama njia ya kuingiza ukoloni ndani ya Afrika, kwanza kuwaharibu Wa afrika kisaikolojia kwa kuwafanya wazidharau dini zao na mila zao na kuukubali utamaduni wa kigeni na dini hiyo mpya ya kikristo, pamoja na hayo yote wamisheni hao walikua wakituma ripoti huko walipotoka ya kuwaeleza hali halisi ya afrika na upeo wa ufahamu wa wa Afrika pamoja na uwezekano wa kupata kila wananchohitaji ndani ya Afrika.

  Pia wafanya biashara walikua wanakuja na vitu visivyo na thamani ya sawasawa na dhahabu pamoja na alimasi ambazo walitumia kubadilishana na viongozi wetu wa kipindi hicho, na hao hao wafanya biashara walifanya kazi ya kuwasainisha ma chifu wetu mikataba ya uongo na kilaghai ambayo ilikua inaonyesha kuwa watu hao wana karibishwa kuja kuwekeza huku na kufanya vyovyote watakavyo.

  Hali hiyo ilipelekea mnamo mwezi wa 12 mwaka 1884, kansela wa Ujeruman bwana Von otto man Bismack kuwaita mafisadi wote wa ulaya waliokuwa wanapanga mikakati ya kuja kutuibia huku Afrika, aliwaita katika mji wa Berlin huko ujerumani na lengo kuu lilikuwa ni kuligawa Bara la Afrika katika makundi mbalimbali na kuliwekea mipaka ambayo itawawezesha wasiingiliane katika utawala wao na hali hiyo itawaepusha kupigana na kudumisha udugu wao huo wa kifisadi.

  Bwana Rais naamini kabisa unajua fika katika mkutano huo wa kuliwekea bara letu mipaka ulifanywa na wazungu watupu na hakuna mwafrika au mtu mweusi yoyote aliehusishwa kutoa mawazo yake juu mipaka hiyo pia uchorwaji wa mipaka hiyo haukujali mahusiano yaliyokuwepo kati ya jamii moja na nyingine na ndio maana usishangae ukawakuta wajaluo wakenya na watanzania au wamasai wa Kenya na Tanzania au wanyasa wa Malawi na wa Tanzania.

  Ndugu zangu wananchi MKWERE anatambua fika Wazungu sio watu wazuri kwani walianza kutugawa tokea zamani na pia wakapandikiza chuki kati ya mwa afrika mmoja na mwenzake lakini cha ajabu, Rais wetu kawafanya watu hao kuwa marafiki zake na kuwaomba waje kwa wingi kuwekeza na kuchukua Rasilimali zetu kwa maslahi yao binafsi.

  Historia haitwasahau akina Chifu Mkwawa, shaka zulu,Zwangendaba,Mirambo na Isike, ambao walipambana na serikali za kikoloni zilizojiweka madarakani kimabavu na kuanza kuwatumikisha babu zetu kwenye mashamba ya mikonge na kazi ziingine za kinyonyaji.

  Pia historia haitawasahau akina Abushiri bin Salim, Hassani Omar Makunganya,Kinjekitile Ngwale na Dedan kimath ambao waliuawa kwa kunyongwa na wajerumani na waingereza kutokana na ujasiri wao wa kuupinga utawala wa kigeni na uzalendo wao wa kutetea maslahi ya Taifa hili ambalo wateule wa Rais wameligeuza kuwa la kifisadi na la wezi wakubwa wanaotuibia mabilion ya shilling kwa maslahi yao binafsi.


  Ikumbukwe kuwa miongoni mwa sababu za kuja kwa wakoloni wa kipindi hicho ilikuwa ni pamoja na kutafuta maeneo ya kuwekeza kama vile ardhi kubwa kwa ajili ya mashamba pamoja na sehem zote zenye madini na pia uanzishaji wa viwanda vidogo kwa ajili ya kuondoa makapi katika malighafi hizo kabla hajiapelekwa ulaya.

  Sasa tumuulize Bwana Rais, iweje hao wazungu waasi na wababe waliotumia nguvu nyingi ku uingiza ukoloni pamoja kuanzishaji uwekezaji ndani ya afrika katika kipindi hicho walipingwa katakata na babu zetu mpaka wakafikia kuingia vitani?


  Je akina Kinjekitile Ngwale walikuwa ni wajinga kuanzisha na kupigana vita ya majiamaji dhidi ya wajerumani?

  Kwanini babu zetu walikataa katakata mali zetu zisitumiwe na wageni lakini wewe Rais unajisifia hadi kwenye vyombo vya habari kuwa kila ukienda nje unafanikiwa kuwa shawishi wawekezaji waje kuwekeza nchini kwetu?

  Hivi una amini hali hiyo itasadidia kupambana na umasikini wetu?
  Na tokea wawekezaji hao wameanza kuwekeza unaweza tueleza ni kwa asilimia ngapi umefanikiwa kupunguza umasikini?

  Bwana Rais sisi hatuna imani na hao wawekezaji wanaokuja kuwekeza kwani haohao ni wajukuu wa wakoloni waliotunyonya na kutu dhulumu mali zetu kwa maslahi yao na nchi zao za huko ulaya, sasa iweje leo serikali za kiafrika ziwaone wao ni wazuri na bila wao hatuwezi endelea?

  Hali hiyo inatuenyesha kuwa msheshimiwa Rais hauna watu makini katika serikali yako ambao wanakosa ubunifu na ujasiri wa kuanzisha miradi endelevu ambayo ingewezesha kutumia rasilimali zetu tulizonazo kwa ajili ya maslahi ya taifa na pia mipango hiyo inastahili iendane sambamba na mchakato mzima wa kupambana na umasikini.

  Ina huzunisha sana kusikiliza bunge la Nchi hii likikalia kulumbana kuhusu matumizi ya bajeti ya nchi hii wakati zaidi ya nusu ya bajeti ni pesa zinazotolewa na Nchi wa Hisani kuchangia bajeti hiyo.

  Inakera kumsikia Waziri Mkuu wa Nchii hii akiwaambia kwa kuwabembembeleza viongozi na watendaji wa wilaya waache matumizi mabaya ya pesa za halmashauri kwa kununua magari ya kifahari na badala yake zitumike katika miradi mbalimbali.

  Bwana Rais ni kama mchezo wa kuigiza tunaposikia mabilioni ya shilingi zinazopatikana kutokana na uwekezaji na uuzaji wa rasilimali zetu lakini cha ajabu maisha yanazidi kuwa mabaya kwa mwananchi wa kima cha chini na haoni faida inayopatikana na mchakato mzima wa uuzaji na ukaribishaji wa wawekezaji katikai nchi hii.

  Inatia aibu sana kuona wilaya kama ya Geita ambayo dhahabu safi inatoka na kwenda kuijenga miji mikubwa ya huko Canada haina hata uhakika wa huduma ya umeme wa kudumu pamoja na maji safi na salama ya kunywa na hata hiyo lami yenyewe inayopita hapo ni ya kiwango cha chini kabisa na haifanani hata kidogo na mali inayotoka chini ya milima iliyopo hapo Geita.

  Bwana Rais tunaamini kuwa unajua madini yanatumiwa vizuri sana na wa Botswana na wanamibia na pia hali hiyo imepelekea kubadilisha hali za maisha za watu wa sehemu hizo kwa kuwaboreshea huduma muhimu za jamii pamoja na kuwalipa mishahara inayoenda sambamba na gharama za maisha wanayoishi.

  MKWERE napenda kukufahamisha ya kwamba Wananchi wengi sasa tunatambua hali halisi ya ugumu wa kazi wanayokutana nayo ndugu zetu wanaofanya kazi migodini na pia tunajua fika ni jinsi gani wamiliki hao wa migodi walivyo na jeuri pamoja na kuwafanyia ndugu zetu unyama huko migodini pamoja na kuwadhalilisha huku wakiamini hakuna wakuwafanya lolote ukizingatia wao ndio wamiliki wa migodi hiyo ambao dhamana ya umiliki huo wamepewa na Serikali.

  Tunatambua fika katika jimbo la Tarime katika mgodi wa Nyamongo kumekuwa hakuna amani kabisa na wamiliki wa mgodi huo wamekuwa wakionyesha dharau zao waziwazi kwa Wananchi na kufanya wanavyo taka bila kujali hali hiyo itawaathiri vipi watanzania.

  Tunatambua kuwa maji yaliyokuwa yamechanganyikana na dawa zenye sumu amabayo hutumika huko migodini katika shughuli mbalimbali ndio yaliochanganyika na vyanzo vya maji ya mto tigite huko tarime na matokeo yake sumu hiyo ilisababisha vifo vya mifugo mingi pamoja na binadam, pia hali hiyo ilipelekea baadhi ya watu kupatwa na magonjwa hatarishi ya ngozi lakini cha ajabu wamiliki wa mgodi huo walitetewa sana na vyombo vya dola na matokeo yake kesi hiyo ikaisha kimyakimya Kama kesi za mafisadi wa epa, rada, ndege ya rais pamoja na Richmond.

  BABA RIDHIWANI, naomba utambue kuwa sasa Watanzania wanaelewa kila kitu kinachoendelea na pia wanaujua ufisadi ni nini na pia wanawafahamu kabisa mafisadi ni akina nani na jinsi gani wanavyo tuangamiza na kuyafanya maisha yetu kuwa magumu kila kukicha.

  Kipindi cha Mwalimu Nyerere sio kwamba alikuwa hajui kama nchi hii ilikuwa na hazina kubwa ya madini pia inavivutio mbalimbali vya kitalii, mwalimu alikuwa anayajua hayo yote tena zaidi ya Mtanzania yoyote, pia nilazima ifahamike kuwa hata kipindi hicho mafisadi wa ulaya walikuwa wanatamani sana kupata nafasi ya kuja kuwekeza na kutaka kutuibia kama wanavyo fanya sasa hivi, lakini cha ajabu ni lazima tujiulize kwanini mwalimu nyerere hakuwapa nafasi watu hao?

  Kwanini Baba wa Taifa alikuwa akiwafukuza kama mbwa na kuwafanya wajione ni wajinga na wasio na nguvu za kuweza kuingia kwetu na kutuibia pamoja na kutunyanyasa?

  Nasikitika sana kuwaona watu waliokuwa wafuasi wazuri wa Mwalimu Nyerere ambao walipata nafasi ya kukaa nae na kufanya nae kazi muda mrefu wameshindwa kujifunza kabisa somo la uzalendo na utawala bora.

  Kwa kudhihirisha kuwa kipindi cha mwalimu Nyerere wafuasi wake na wateule wake walikua ni wazalendo na walioiheshimu miiko ya uongozi pamoja na utawala bora ni pamoja na kitendo cha wafanya kazi wote wa ngazi za juu kutowapeleka watoto zao kuwasomesha nje ya nchi tena kwa gharama kubwa ya pesa zinazotokana na kodi za wavuja jasho masikini wa kima cha chini.

  Mama Maria Nyerere, mke wa Baba wa taifa aliithibitisha kauli hiyo kwa kusema kuwa kipindi cha utawala wa Mwalimu hadi watoto wa waliokuwa wa mabalozi wa Tanzania katika Nchi za nje walikuwa wanasoma hapahapa Nchini ingawa wazazi wao walikuwa wapo mbali wakilitumikia Taifa hili, na hali hiyo ilidumu kwa muda mrefu mpaka Mwalim Nyerere mwenyewe alipowaruhusu wawasomeshe watoto wao huko huko.

  Bwana Rais inasikitisha kuona ni jinsi gani mawaziri na wakurugenzi wa serikali yako wanavyowapeleka watoto wao huko Ulaya na Amerika katika vyuo vya huko na matokeo yake wengi wao wamekuwa wakifanya anasa na kutumia vibaya pesa za umma huko wanapokwenda kusoma ila cha kushangaza wanapo rudi ndio hupatiwa nafasi muhimu katika sekta nyeti zinazohitaji umakini na uelewa wa hali ya juu.

  Inasikitika kumuona kiongozi wa Nchi ambae alikuwa ni Mwanafunzi wa Mwalimu Nyerere, anasahau mafundisho ya mzee huyo na kuamua kuwa Mwizi na Fisadi mkubwa ambae amejiuzia shamba kubwa katika maeneo ya morogoro huko mtibwa, pamoja na kujiuzia kiwanda cha makaa ya mawe huko mbeya ambacho kilikuwa kikijulikana kama Anben, jina ambalo watu wenye akili za kufikiria waliweza kutambua kuwa ni ufupisho wa majina ya watu wawili ambao ni mke na mme, na majina hayo ndio ya wamiliki wa Mgodi huo ambao serikali ya China iliisaidia serikali yetu kuujenga Mgodi huo kwa Gharama kubwa karibu shilingi trillion 4.

  Chakushangaza watu hao walijiuzia Mgodi huo kwa shilling million 700, ila cha kushangaza zaidi, watu hao walilipa shilingi million 70 tu.
  Na baada ya hapo mgodi huo ulianza kuchukua tenda za `serikali na kujipatia mabilioni ya shilling ambayo yalitakiwa kutumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo ambazo zimelala na kupelekea kuwafanya watanzania wazidi kuchanganyikiwa na ugumu wa maisha ambayo unawachanganya zaidi ya kitu chochote.

  Mgodi huo wa makaa ya mawe ulinunuliwa na aliyekuwa Mwanafunzi safi wa Mwalimu ambae Mzee huyo alimshika mkono na kumzungusha nchi nzima na kumnadi kwa watanzania kuwa anastahili kuwa Rais na kiongozi safi wa watu masikini, masikini mzee huyo hakujua kuwa alikuwa anamnadi chui alievaa ngozi ya kondoo, bepari mpenda utajiri, fisadi msaliti, tena mwizi asie na huruma kwa anaemuibia.

  Kiongozi huyo ndio aliekuwa kinara wa ubinafsishaji alipokuwa madarakani na pia ndio aliewakaribisha waewekezaji kwa pupa na baada ya kuonja asali ya ufisadi iliyotengenezwa kutokana na jasho pamoja na damu ya wanyonge nayeye ndio akaamua kuanza kutuibia waziwazi huku akishirikiana na mke wake katika kujiuzia rasilimali za Taifa kuanzia ardhi, mgodi wa makaa ya mawe pamoja na shamba la miwa la huko mtibwa.

  Wawekezaji karibu wote wanaokuja kuwekeza hapa kwetu hawaji na nia ya kushikirikiana na sisi kupambana na umasikini wetu bali huja kutafuta faida kubwa na kujilimbikizia mali na baada ya kufaidikia vya kutosha waondoke zao na kutuachia umasikini uendelee kututeketeza.

  Kuna mifano hai mingi tu ambayo imejionyesha dhahiri baada ya sekta flani kuuzwa au kupewa hisa muwekezaji flani kuonyesha hali ya kulegalega ndani ya muda mfupi.

  Mheshimiwa Rais ni dhahiri wewe na serikali yako unautambua mgogoro uliopo kati ya kampuni mpya inayomilikiwa na wahindi ya TRL na wafanyakazi wake, kampuni hiyo iliwarithi kutoka katika kampuni iliyokuwa chini ya usimamizi wa serikali ambayo ilijulikana kama Tanzania railways cooperation.(TRC).

  Serikali ililitangaza shirika hilo kuwa limefisilika na pia haliwezi kujiendesha hivyo basi serikali imeamua kuliuza` kwa wawekezaji wa kihindi. Ukweli umebaki palepale na shirika hilo limekuwa linasuasua tokea siku ya kwanza ambayo Wahindi hao walikabidhiwa dhamana ya kuliendesha shirika hilo.

  Mheshimiwa Rais imedhihirika kabisa hujali na pia hauna uzalendo wala uchungu wa hali ngumu za`maisha zinazo wakabili watanzania ambao ni wafanyakazi wa shirika hilo, Wahindi hao wameshindwa kuwalipa mafao yao wastaafu kama ilivyo stahili pia wahindi hao wameshindwa kabisa kuliendesha shirika hilo kwa ajili ya maslahi na maendeleo ya taifa ingawa pia na wao wanastahili kupata faida.

  Inasikitisha sana kuona Sumatra wanalikagua shirika hilo na kugundua kuwa mabehewa pamoja na injini za wahindi hao hazina viwango vinavyostahili katika uendeshaji wa shughuli hizo, pia cha kushangaza baada ya mizengwe ya hapa na pale matokeo yake serikali inawaruhusu watumie mabehewa hayo kwaajili ya usafirishaji wa abiria pamoja na mali zao.

  Ilikuwa tarehe 13 mwezi wa 10 mwaka 2009. siku hiyo wafanaya kazi wa TRL waliweza kufanya mgomo na kuongea na vyombo vya habari mojakwamoja bila uoga na kuwaeleza ukweli kuhusiana na mazingira ya rushwa yanayohusiana na utolewaji wa vibali kwa wahindi hao kutumia mabehewa yao mabovu ambayo kwa njia moja hau nyingine yanaweza hatarisha maisha ya watanzania , wafanyakazi hao waliongea kwa uchungu mbele ya kamera za vituo vya televisheni kuwa wanashindwa kuuelewa uongozi wa serikali yetu na jinsi gani wanavyolipeleka Taifa hili kuzimu,.

  Wafanyakazi hao walifikia kusema kuwa wanaamini kabisa mabehewa pamoja na injini zetu za zamani zilizokuwepo zinaweza kukarabatiwa na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi ya hayo ya wahindi ambayo yanaonekana kuwa yameshatumika sana na pia yameshachoka na ni mabovu sana na pia hayana hata milango ya dhharura na pia yamewekewa nondo kwenye madirisha na hali hiyo inadhihirisha kuwa endapo itatokea ajali basi uwezekano wa watu wengi kupoteza maisha yao ni mkubwa kuliko ya wale watakao salimika.

  Swali la msingi kwa mheshimiwa Rais pamoja na serikali yake kwa ajumla, hivi wakati shirika hilo la TRC linaiingizia serikali hasara mpaka kufikia hali ya kufilisika, je serikali ilikuwa wapi?

  Na pia na hao wahusika wakuu waliotumia vibaya madaraka yao pamoja namatumizi mabaya ya faida iliyokuwa inapatikana je serikali yako iliwachukulia hatua gani?

  Mheshimiwa Rais unataka kutuambia kuwa wakurugenzi wakuu wa lililokuwa shirika la TRC pamoja na watendaji wa ngazi juu hauwatambui?

  Na kama unawatambua je umewachukulia hatua gani za kinidhamu? Au unataka tukuite joka la kibisa ambalo linatisha kwa umbile lake lakini halina sumu na wala halina madhara ya aina yoyote?

  Inatia aibu sana kuona ni jinsi gani watanzania wanadanganywa na serikali pamoja na vyombo vya habari eti kua wao ni masikini sana na pia bila wawekezaji hatuwezi fika, acha unafiki mheshimiwa Rais unawajua wote wanaousababisha umasikini wa wa Tanzania na pia unaelewa fika hao wawekezaji hawaji kutusaidia balI ndio wanakuja kututawala na kuturudisha kwenye biashara ya utumwa ambao unazidi hata ule waliotumikishwa wazazi wetu katika kipindi kile cha ukoloni wa zamani.

  Rais sera zako pamoja na mipango yako hasa katika mambo yote yanayo husu uwekezaji hazina mchango wala msaada wa aina yoyote ambao unalenga kumsaidia mtu masikini sana ambae hana kazi wala elimu ya kutosha kupambana na umsikini wake unaomkabili.

  Si swala la TRL na TRC tu linawaacha midomo wazi wazalendo pia hata sakata la uendeshaji wa kampuni ya Ndege ya Tanzania ijulikanyo kama ATC, imejulikana pia shirika hilo linaendeshwa kwa hasara kubwa ambayo serikali imeshindwa kabisa kuliendesha na pia imeonekana linajiendesha kwa hasara kubwa zaidi.

  Rais, inauma sana kuona ni jinsi gani umekosa watu makini na wachapakazi katika serikali yako na matokeo yake umejawa na mafisadi wezi, wabinafsi na wasio na huruma wala uzalendo wa kulinusuru taifa hili.

  Inatia aibu sana kusikia shirika kubwa linalobeba jina la Taifa halina hata ndege 10, lakini linawafanyakazi zaidi ya 200 ambo wote wanategemea kulipwa mishahara na posho zingine ambazo zinatokana na uendeshaji wa shirika hilo.

  Hata mtoto mdogo wa darasa la 5, akiambiwa habari hii atagundua kweli Tanzania na serikali yake ni kichwa cha mwendawazimu, iweje ndege pungufu ya 5 ziweze kuwapatia mishahara wafanyakazi zaidi ya 200?

  Inatia aibu sana kuona shirika hilo la ndege halina hata ndege moja inayokwenda ulaya na amerika wakati jirani zetu wa Kenya wana hadi ma ajenti katika viwanja vikubwa vya ndege kama heathrow huko uingereza `na mimi mwenyewe niliwaona majenti wa Kenya air ways huko shiphol international air port , uholanzi katika mji wa Amsterdam.

  Rais wewe ndio unatakiwa kutia changamoto na kuwa mkali katika mchakato mzima wa kuwawajibisha wafanya kazi wazembe na wasio wazalendo ambao wamejawa na tamaa za kujipatia utajiri harakaharaka pasina kuwa na mipango halali na thabiti ya kupambana na umasikini ambao unawatesa mno karibu watanzania wote.

  Swala la uwekezaji na kuawakaribisha sana wawekezaji wa nje ni la kibepari na wote tunaelewa ubepari ni unyama, tena ni unyama ambao unafanywa na binadam na wala sio wanyama kwani wanyama hawana mfumo huo.

  Mheshimiwa Profesa Issa SHivji ameongea kinaga ubaga tena bila hata kuficha katika siku ya kumbukumbu ya mwalimu nyerere, Profesa Shivji ameongea waziwazi na kusema kabisa ufisadi ni wizi mkubwa unaofanywa na viongozi wa juu wa serikali katika utolewaji wa dhamana za uwekezaji pamoja na tenda mbalimballi kwa wawekezaji ambao waweza kuwa ni wageni au wazawa kama Rostam Aziz amabae ni mtajwa sana katika mambo yote yanayohusu ufisadi mkubwa unaofanyika serikalini pamoja na kuhusishwa na tuhuma ambazo zinaelezea kuwa kuna uwezekano wa hata pesa zake kuwa zilitumika kumuweka Rais huyu madarakani.

  Inasikitisha kuwaona watu kama akina Profesa Shivji wakiongea kwa huzuni mkubwa na kubaki midomo wazi huku wakiona dhahiri ni jinsi gani vijana hawa wenye tamaa za ufisadi na utajiri walivyoingia madarakani kwa pupa na kuamua kuiuza hii nchi kwa marafiki zao wageni huku wakijipatia mali nyingi za haramu ambazo huzitumia katika mambo ya anasa kama kuwanunulia vimada wao ,magari ya kifahari pamoja na ulevi uliopindukia ukiambatana na zinaa.

  Kuna mifano mingi sana ambayo inaonyesha ni jinsi gani watanzania hawajalielewa somo la uwekezaji na utandawazi, ingawa serikali yako imekuwa ikiupambia huo utandawazi kwenye vyombo vya habari pamoja na kuusifia sana huku wewe mwenyewe Mheshimiwa Rais umekua ukiongea tena bila hofu pamoja na kusifia ni jinsi gani unavyoitangaza Tanzania kwenye soko la kimataifa na sasa karibu kila tajiri duniani anajua kabisa Tanzania panafaa kwa uwekezajia na pia wengi wao wamekuwa wakimiminika usiku na mchana kuja kuwekeza na kutuletea pesa nyingi sana ambazo sisi tusio na ajira na ambao hatuna vyeo serikalini hatujui matumizi yake wala matunda yake.

  Bwana Rais kwa macho yangu mwenyewe nimemuona Mzee wa kimasai anaejulikana kwa jina la skadeli akilia kwa huzuni mbele ya kamera za kituo cha star televisheni kilichopo Mwanza, mzee huyo alidiriki kuongea kwa majonzi na kusema hivi kweli huyu Nyerere angekuwepo angekubali kuona ni jinsi gani tuna nyanyasika ndani ya Nchi yetu eti kisa muwekezaji?

  Mzee huyo alifikia hatua ya kusema waziwazi kuwaambia watanzania ya kwamba mwenye macho haambiwi tazama, na serikali yetu tayari imeisha tusaliti kw aasilimia mia na kuamua kuturudisha kwenye biashara ya utumwa bila sisi wenyewe kujua.

  Imefikia hatua ya kwamba muwekezaji anakuja na anauziwa ardhi ya watu bila wao kutaarifiwa na matokeo yake watu hao hulazimishwa kuondoka kwa nguvu kutoka sehemu zao na kupewa wawekezaji hao kama ilivyo watokea jamii ya wamasai wanaoshi maeneo ya loliondo,watu hao
  Walilazimishwa na serikali kuondoka katika maeneo yao waliokuwa wanaishi tokea enzi za mababu zao huku wakienedelea na mila zao pamoja na ufugaji wa mifugo yao ambayo ni ngombe, mbuzi pamoja na kondoo.

  Mzee huyo alisema kwamba kuna matajiri flani wa Kiarabu wamekuja na kuwekeza katika maeneo hayo, mzee huyo alisema kuwa serikali imeawuzia warabu ardhi yao pamoja na mbuga zao pamoja na vyanzo vyao vya maji, ili waendeshe shughuli za uindaji katika maeneo hayo.

  Warabu hao baada ya kupatiwa hati miliki za `sehemu hiyo walichukua uamuzi wa kuwafukuza wamasi hao kutoka katika eneo hilo huku wakipewa msaada na serikali, waarabu hao wamekuwa wakiwafanyia ukatili wa ajabu vijana wa kimasai ambo wamekuwa wakionekana katika maeneo hayo ambayo sasa yapo chini ya miliki ya warabu hao. Vijana hao wa kimasai wamekuwa wakipigwa sana na walinzi wa warabu hao na hata kunyanganwa mifugo yao.

  Wamasai hao walilazimishwa kuhama kutoka katika makazi yao na kuelekea katika maeneo makame ambayo hayana vyanzo vya maji wala majani kwa ajili ya malisho ya mifugo yao, wamasai hao wamekuwa wakiteseka sana tena bila hata ya kupata msaada wowote kutoka serikalini na hali hiyo imepelekeamifugo yao kufa mara kwa mara kutokana na ukosekanaji wa chakula na maji ya kunywa.

  Bwana Rais naamini kabiasa hapo ulipo kuna televisheni na pia kuna redio na pia unawasaidizi wako wengi ambao nilazima watakuwa wanakupatia habari za muhimu kuhusu shida na taaabu zinazo wapata wapiga kura wako waliokuweka madarakani ili uwatumikie na kuwatatulia matatizo yao ya kimaisha lakini cha ajabu wewe na serikali yako mmekuwa na tabia ya kukaa kimya sana mpaka watu baki wakiingilia ndio mnajitokeza.


  Napenda kutumia nafasi hii kuwaweka wazi watanzania kuwa wamasai hao kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili, wamefikia hatua ya kuuza ngombe zao kati ya shilling 2000 na elfu 5000. inatia uchungu sana kusikia ngombe anauzwa shilling elf 5000, eti kisa kuna Mwarabu ameuziwa ardhi na mbuga ya wanyama ili aendeshe shughuli za uwindaji wakati mzawa na mzalendo wa nchi hii akitaabika na kunyanyasika mpaka kuuza mali yake kwa bei ya kutupa.

  Swali la msingi kwa Bwana Rais, je hao Waarabu wanaowanyanyasa wamasai baada ya serikali yako kuwamilikisha ardhi hiyo je kuna Mtanzania yoyote anaweza kwenda arabuni na kupewa ardhi ya Warabu na kuhatarisha maisha ya wazawa wa huko arabuni?

  Rais, werevu mwingi mbele giza laiti kama mngekuwa mnatumia hata muda wenu kidogo kufikiria mustabali wa Taifa hili si dhani kama mngekuwa mnafanya maamuzi ya hatari kama hayo ambayo mwisho wa siku yanaweza hatarisha amani ya nchi nzima kwani yanayowakuta wamasai hayana tofauti na ya wakutao wakazi wa bhuliyankulu, kakora, buzwagi na maeneo yote ambayo wawekezaji wamekuwa wakipewa haki na kulindwa sana zaidi hata ya wazawa na wazalendo wa nchi hii ambao babu zao walitumikishwa kwenye mashamba ya mkonge ya wa wajerumani pia walipigana vita ya majimaji pamoja na nyinginezo katika hali ya kulikomboa Taifa hili na kumpatia mtanzania uhuru ambao aliutolea jasho pamoja na damu yake.

  Kama kweli serikali ya Rais kikwete inania ya kupambana na umasikini wetu ikae chini pamoja na wananchi ili kupanga mipango endelevu na mbinu thabiti kama walivyofanya wachina, wakorea pamoja na wajapani.
  Inatia aibu kuwaona watu masikini sana lakini Rais wao hadi viongozi wao wa wilaya wakitembelea magari ya thamani sana na kuishi maisha ya anasa ambayo hayafanani kabisa na hali halisi ya maisha ya watanzania wa kima cha chini ambao wengi wao hawajui mpaka lini wataendelea kuteseka na kunyanyswa na wageni ambao wana karibishwa na mafisadi wa nchi hii kuja kuendelea kutuibia na kutufanya sisi tuendelea kuwa masikini wa kudharauliwa na hata na majirani zetu.

  NAHITIMISHA kwa kutoa ushauri kwako wewe mheshimiwa Rais pamoja na viongozi wenzako au wasaidizi wako wote uliowapa dhamana ya kuupigia debe na kuupambia uwekezaji, ni lazima mtambue kuwa muwekezaji yoyote anaekuja kuwekeza hapa nyumbani ni mfanyabiashara tena anaetokea katika nchi zilizokomazwa na mifumo ya kibepari.

  Bwana Rais naamini kabisa wewe na wateule wako mnatambua fika kuwa msingi mkuu wa ubepari ni unyonyaji. Na mara zote bepari anapokwenda kuwekeza sehemu huwa anakwenda na nia moja ambayo ni kuhakikisha anawanyonya watu wanaomzunguka kwa kadri ya uwezo wake ili aweze kupata faida kubwa.

  Hivyo basi kitendo cha kuruhusu utandawazi na uwekezaji kwa asilimia mia ni sawasawa kabisa na kuruhusu matajiri wa kibepari waje na wazidi kutu nyonya kadri ya uwezo wao na pia ni lazima ifahamike kuwa mara zote yule anaenyonywa ndio huwa mhanga wa unyonyaji hivyo basi bila shaka kadri Rais wetu na wenzake wanapozidi kuwakaribisha wawekezaji hao ndio wanavyozidisha ile kasi ya unyonyaji ambayo nayo huongeza ile kasi ya ongezeko la masikini kuwa wengi sana na kuwafanya matajiri au mabepari wachache kumili kila kitu.

  Enyi viongozi tuliowapa dhamana ya kutuongoza hebu fumbueni macho yenu pamoja na akili zenu na pia mshaurini Rais ajaribu kutambua kuwa hao wawekezaji hawatuletei faida bali wao ndio wanakuja kutafuta faida na kutunyonya kwa nguvu zao zote ila kinacho wasaidia ni kwamba tayari wameisha gundua kuwa viongozi wa kiafrika huwa hawana utaratibu wa kufikri sana kabla ya kufanya maamuzi na pia tayari wameisha kuwa na tamaa za kujilimbikizia mali na utajiri wa hali ya juu hivyo basi ukiwapa pesa nyingi wata kupa kila kitu pamoja na uhuru wa kufanya mambo yako tena bila bughdha ya aina yoyote na matokeo yake baada ya muda mfupi zile pesa zilizohongwa kwa viongozi hao zitakuwa zimesharudi na pia watapata faida kubwa ingawa yaweza chukua muda mrefu kidogo kabla haija patikana.
  Nilazima Mtanzania aambiwe ukweli ingawa serikali yake inamtanguliza na baiskeli ya miti kuelekea utandawazi ni lazima aambiwe huko njiani atakutana na magari ya kisasa pamoja na treni za umeme.


  Rais nilazime utufahamishe kuwa ingawa unafanya juhudi kubwa sana katika kuvitangaza vivutio vya uwekezaji lakini serikali yako imeshindwa kutoa nishati ya umeme ya kudumu nchi nzima na hali hiyi imepelekea kuwe na mgawo wa nishati hiyo kila kukicha na pia lazima watanzania wafahamu ingawa wawekezaji wanakuja kuwekeza ila ni asilimia 11 tu ya watanzania ndio wanaotumia hiyo nishati ya umeme na karibu ya asilimia 10 wapo mjini na ni asilimia moja tu ndio wapo vijijini.

  Rais nilazima kabla haujatupeleka huko kwenye soko huria pamoja na uwekezaji utufahamishe ni mpaka lini mkulima wa Tanzania ataendelea kuwa mtumwa na mhanga anaeteswa na njaa kutokana na kilimo duni anachotegemea mvua pamoja na jembe la mkono na hali hiyo humfanya azidi kuwa masikini na mtu anaedharauliwa kuliko mtu yoyoe nchini.

  Inasikitisha sana kuona Tanzania inaruhusu uwekezaji na ubinafsishaji wakati robo tatu ya watanzania hawana hata mitaji midogo ya kuendesha biashara ndogondogo za kujikimu, hali hiyo haihitaji elimu ya chuo kikuu kuichanganua, ukweli utabaki palepale kuwa wenye mitaji na mabepari kutoka nje ndio watakuja na wameisha anza kuja na mitaji yao tayari kututawala na kutumia ardhi yetu pamoja na mali zetu kwaajili ya faida yao wao.

  NDUGU WANANCHI TAYARI TUMEANZA KUUZWA KWA WAGENI NA TAYARI WANA HAKI YA KUMILIKI ARDHI YETU NA KUJIGAWIA MALI ZETU WAO PAMOJA NA VIONGOZI WETU AMBAO TAYARI WAMEISHATUSALITI.

  Inatia uchungu sana kuona ardhi ya miji mikubwa ikimilikiwa na wageni ambao wamejenga mahoteli yao ya kifahari na vitega uchumi mbalimbali ambavyo kutokana na hali ngumu ya maisha iliyosababishwa na ufisadi hata asilimia 20 ya wazalendo haiwezi kufanya hata robo ya mambo hayo yanayofanywa na wageni.

  Naamini kuna watu wengi wanayajua mambo niyaelezayo hata zaidi yangu lakini kutokana na hofu pamoja na tamaa za kuyapenda sana maisha ya hapa duniani na kuogopa nguvu za mafisadi wamekaa kimya ingawa wana elimu kubwa sana ambayo kama wakiamua kuwa elimisha watanzania pengine tunaweza tukalinusuru Taifa hili haraka iwezekanavyo.
  Ndio serikali imekuwa na tabia ya kuwatetea watendaji wake hasa wale wanaohusishwa sana na ufisadi pamoja na wizi wa mali zetu na kutuzidishia ujinga umasikini pamoja na maradhi ambavyo Mwalim nyerere alijitahidi kwa nguvu zake zote kupambana na vitu hivyo na kwa asilima kubwa alijitahidi na hakuna kiongozi yoyote ambae ameweza kujaribu kufikia hata robo yake.

  Tunatambua fika kuna watanzania wazalendo kama akina Said Kubenea ambao wanajitahidi kutumia nguvu ya kalamu kufikisha ujumbe na kuifumbua macho jamii kutokana na swala zima la ufisadi na umuhimu wa kuwa wazalendo na kuwa na uchungu wa maslahi ya kitaifa, watu hao kama akina Kubenea wamekuwa wakikutana na vikwazo vingi kuanzia nguvu za dola hadi zinginezo ambazo haziwezi elezewa kwa ufasaha zaidi, mafisadi ambao wengi wao wana nguvu ya dola wamekuwa wakimtishia maisha yake pamoja na hata kujaribu kumuua kwa kummwagia tindikali, ila nawa hakikishia kuwa haki itasimama hata yeye au mimi au mzalendo mwingine yoyote akiuawa kwaajili ya maslahi ya taifa, watakuja tu wengine nao watasimama kidete na kuitetea haki mpaka itasimama.

  TUNAHITAJI KATIBA MPYA AMBAYO ITAKUWA DIRA YA KUTUPELEKA KANANI.
   
 2. Ngalikihinja

  Ngalikihinja JF-Expert Member

  #2
  Jan 3, 2011
  Joined: Sep 1, 2009
  Messages: 16,419
  Likes Received: 3,767
  Trophy Points: 280
  Hapana ................. MODS angalau ungelimiti idadi ya maneno kwenye kila post.............. otherwise tunakoelekea page moja itakuwa na post moja................

  Kwa kusoma TITLE........You have a point
   
 3. K

  Kakalende JF-Expert Member

  #3
  Jan 3, 2011
  Joined: Dec 1, 2006
  Messages: 3,259
  Likes Received: 33
  Trophy Points: 135
  Hizi makala ndefu hivi kusoma tabu, weka utangulizi kisha attachment atayependa atasoma kwa wakati wake!
   
 4. BRUCE LEE

  BRUCE LEE JF-Expert Member

  #4
  Jan 3, 2011
  Joined: Dec 11, 2010
  Messages: 2,089
  Likes Received: 1,158
  Trophy Points: 280
  ok tafanya hivyo ngoja niweke attachment
   
Loading...