Kisutu: Waliokuwa Wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania wapandishwa Kizimbani kwa kuharibu Noti

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,802
11,961
WALIOKUWA watumishi wanane wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na wenzao watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka sita likuwemo kuharibu noti 460,000 za 10, 000 na kuisababishia benki hiyo hasara ya zaidi ya bilioni 4.6.

Watumishi hao wa BOT ni Mariagoretha Kuzugala, Henry Mbowe, Asha Sekiboko, Cecilia Mpande, Agripina Komba, Zubeda Mjewa, Khadija Kassunsumo na Mwanakheir Omary.

Washitakiwa wengine ni Alistides Genand, Shukuru Mchegage, Musa Chengula, Zaituni Chihipo na Respicius Ishengoma ambao walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Godfrey Isaya.

Wakisomewa mashitaka hayo na jopo la mawakili wanne wa serikali likiongozwa na Wakili wa serikali Mkuu Poul Kadushi, ilidaiwa kuwa kati ya Januari mwaka 2017 hadi Septemba 30 mwaka 2019, watumishi hao wa BOT kwa kuvunja majukumu yao ya kazi waliwezesha utendekaji wa kosa la kuongoza genge la uhalifu.

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa, katika tarehe hizo na maeneo hayo, jijini Dar es Salaam, washitakiwa Genand, Mchegage, Chengula, Chihipo na Ishengoma wakiwa si watumishi wa BoT, kwa kushirikiana na watumishi hao wa BoT kwa makisudi, waliwezesha kutendeka kosa uharifu wa kupanga.

Katika shitaka la tatu , ilidaiwa kwamba, katika tarehe hizo jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote bila ya kuwa na kibali na kutokuwa wazalendo, washitakiwa wote waliharibu noti kwa kukata noti 460,000 za 10,000 sawa na Sh bilioni 4.6.

Mawakili hao wa serikali waliendelea kudai kuwa, katika tarehe na maeneo hayo, jijini Dar es Salaam, kwa mawasilisho ya kilaghai, kwa kujua na kwa mpango wa kitapeli washitakiwa wote walijipatia faida ya sh bilioni 1.533 kutoka BoT baada ya kuwasilisha noti hizo BoT.

Shitaka la tano la utakatishaji fedha ilidaiwa kuwa watumishi hao wa BoT na wenzao hao walijihusisha katika miamala tofauti ya sh. Bilioni 1.533 wakati wakijua zilitokana na kosa tangulizi la uhalifu wa kupangwa na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika shitaka la sita, washitakiwa wote katika tarehe hizo jijini Dar es Salaam, waliisababishia BoT hasara ya sh Bilioni 4.6.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa hao walielezwa kwamba, mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi hivyo watapelekwa mahabusu hadi upelelezi utakapokamilika.

Wakili Kadushi alidai, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamlika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ambapo ilipangwa Desemba 28 mwaka huu.
IMG-20201214-WA0026.jpg
IMG-20201214-WA0027.jpg
 

Attachments

  • IMG-20201214-WA0027.jpg
    IMG-20201214-WA0027.jpg
    96.7 KB · Views: 3
Back
Top Bottom