Kisutu, Dar: Mahakama yamuachia huru Tido Muhando, yamkuta hana hatia

n00b

JF-Expert Member
Apr 10, 2008
1,006
2,667
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando baada ya kumkuta hana hatia
====

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando.

Tido ameachiwa huru leo Ijumaa Januari 25, 2019 baada ya mahakama hiyo kumkuta hana hatia.

Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya upande wa mashtaka kushindwa kudhibitisha mashtaka yake.

Tido alifikishwa Kisutu kwa mara ya kwanza Januari 26, 2018, kujibu mashtaka matano.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 7/2018, Tido alikabiliwa na mashtaka matano, mashtaka manne ni ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni.

Agosti 27, 2018 Mahakama hiyo ilimkuta Tido na kesi ya kujibu baada ya Hakimu Shaidi kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa mashtaka.

Baada ya Tido kukutwa na kesi ya kujibu, alianza kujitetea.

Katika utetezi wake, Tido alidai kuwa mchakato mzima wa kuingia ubia wa kuhamisha TBC kutoka katika mfumo wa analojia kwenda digitali ulifanywa na bodi ya TBC.

Akihojiwa na wakili wa Takukuru alidai kuwa hakuna kitu alichokifanya bila ridhaa ya bodi na bodi ndiyo iliyomuagiza afanye mchakato wa awali na ulipokamilika aliwasilisha kwao, mwaka 2009.

Alidai kwamba hadi anaondoka TBC hakuna mtu yeyote aliyezungumzia suala hilo, si Serikali wala bodi.

Tido alipoulizwa na wakili wa Takukuru juu ya tofauti za mkataba aliongia na kampuni ya Chanel 2 group na ule wa Startimes alidai aliandikishiana nao mkataba wa makubaliano ya awali kwa sababu walikuwa wakitaka kuhakikishiwa kama wangeitwa na bodi ya TBC na kwamba aliusaini yeye peke yake.

Aliongeza kuwa katika mkataba halisi walioingia na kampuni ya Startimes aliusaini yeye na mwanasheria wa TBC.

Alibainisha kuwa Mkataba wa Startimes ndiyo mkataba halisi ambao waliandikishiana baada ya bodi kuridhia.

Tido amedai kuwa kutokana na sheria na taratibu za manunuzi, mkataba halali wa TBC lazima usainiwe na watu wawili ambao ni Mkurugenzi na Mwanasheria na pia lazima uwe na muhuri wa shirika.

Oktoba 30, 2018, Tido kupitia mawakili wake Martin Matunda (marehemu kwa sasa) na Dk Ramadhani Maleta walifunga ushahidi wa upande wa utetezi.

Miongoni mwa mashahidi wa upande wa mashtaka waliotoa ushahidi katika kesi hiyo ni pamoja na ofisa uchunguzi wa Takukuru, Victor Lesuya, Mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa TBC, Clement Mshana.

Tido Mhando ni miongoni mwa waandishi wa habari na watangazaji wakongwe nchini Tanzania.

Aliwahi kufanya kazi Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) kama Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili kabla ya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC.

Pia amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanspoti na The Citizen.

Aliwahi pia kufanyia kasi Sauti ya Ujerumani (Deutsche Welle), Sauti ya Amerika, na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) lilipokuwa linafahamika kama Sauti ya Kenya (VoK).

Zaidi, soma >> KISUTU: Tido Mhando afikishwa Mahakamani, asomewa mashtaka matano na kuachiwa kwa dhamana - JamiiForums
 
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando baada ya kumkuta hana hatia
visasi vya kishamba tu.

wote hawa hapa chini watashinda kesi zao na wanaweza kudai fidia kubwa itakayoweza kuifilisi sana serekali.... sema ni kwa sababu ya uoga wanaweza wakapotezea:

1. Rugemarila & co
2. Kitillya & co
3. Mwanyika & co
 
Back
Top Bottom