Kisutu, Dar: Hukumu ya Kesi namba 456 ya Jamhuri dhidi ya JamiiForums kutolewa Januari 22, 2020

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,797
11,959
=====
UPDATE:

Hakimu Simba ameshindwa kusoma hukumu Desemba 06, 2019 na hivyo hukumu hiyo itasomwa January 22, 2020

====

Wakuu,

Kesho, Desemba 06, 2019 kutakuwa na hukumu ya mojawapo ya kesi zilizofunguliwa na Jamhuri dhidi ya Mkurugenzi wa Jamii Media Co. Ltd na mwanahisa, Mike William ambapo ni katika shauri namba 456 la mwaka 2016 lililokuwa likisikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu jijini Dar es Salaam mbele ya Hakimu Thomas Simba.

Hukumu hii inakuja ikiwa ni karibu miaka mitatu tangu Maxence alipokamatwa na Polisi mnamo Desemba 13, 2016 na kushikiliwa kwa muda na kisha kutupwa Keko kwa siku 3. Aidha, mnamo Januari 26, 2017 Mwanahisa wa Jamii Media Co Ltd, Micke William aliongezwa kwenye shauri hili.

1.jpg

Kuhusu shauri hili
Shauri hili lilifunguliwa mnamo Desemba 16, 2016 pamoja na mashauri mengine mawili - shauri namba 457 na 458.

Awali, Washtakiwa walishtakiwa kwa Kuzuia Uchunguzi wa Polisi kwa kushindwa kutoa taarifa muhimu za Mwandishi (anayedaiwa kuwa mwanachama wa JamiiForums.com kwa jina la Fuhrer – JF Expert Member) aliyeandika kuhusu kampuni ya Oilcom ikidaiwa kukwepa kodi na kuchakachua mafuta katika bandari ya Dar es Salaam.

Polisi walikuwa wakihitaji mambo manne kuhusu mwanachama huyo: Walihitaji Barua pepe ya Mwanachama huyo, Namba zake za simu, IP Address pamoja na mada nyingine zote alizowahi kuanzisha.

Baada ya Upelelezi kukamilika, Jamhuri iliwaleta mashahidi wao na baadae Hakimu aliwakuta watuhumiwa wakiwa na kesi ya kujibu. Washtakiwa walianza kujitetea katika shauri hilo ambapo awali walidaiwa kuzuia upelelezi wa Polisi kwa kutotoa ushirikiano kwa Polisi kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao kifungu cha 22(2), lakini wakati kesi hii ikiendelea mnamo Novemba 2017, hati ya mashtaka ilibadilishwa na Jamhuri na kuwa shtaka lilioonyesha watuhumiwa walikuwa ‘wakiharibu au kuchezea data' kinyume na Sheria Makosa ya Mtandao kifungu cha 22(1) kwa Kiingereza “Intentionally and unlawfully destroy, delete, alter, conceal, modify, renders computer data meaningless, ineffective or useless with intent to obstruct or delay investigation”.

2.jpg

Hakimu alisisitiza kubadilishwa kwa hati hiyo pamoja na kuwa kesi ilishaanza kusikilizwa na mashahidi kuletwa isingeathiri utoaji wa haki.

Kuchelewa kwa utetezi

Katika shauri hili washtakiwa walitakiwa kujitetea Machi 14 na Machi 19 mwaka huu baada ya kukutwa na Kesi ya kujibu mnamo Februari 22, 2019 lakini kutokana na kuahirishwa kwa shauri hili mara kadhaa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za Hakimu kuomba udhuru, Wakili wa Jamhuri kutokuwepo na Wakili wa Jamhuri kubadilishwa, Washtakiwa walianza kujitetea Agosti 05, 2019.

DC58335A-0CA9-4E05-BEF4-9E63FF2FC361.jpeg


MASHAHIDI KATIKA SHAURI HILI

Pamoja na kubadili hati ya Mashtaka, Jamhuri ilileta Mashahidi ambao kimsingi walioongozwa na Mawakili wa Jamhuri kutoa ushahidi kuhusu Washtakiwa kutotoa Ushirikiano Polisi.

Shahidi wa kwanza alikuwa Ramadhan Kingai kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Dar(alikuwa Deputy ZCO), wakati anatoa ushahidi wake alisema kuwa Mwananchi aitwaye Usama Mohammed, Afisa Msimamizi wa Mauzo ya rejereja katika kampuni ya Oilcom (T) Ltd alifika ofisini kwao na malalamiko kuwa alisoma habari JamiiForums kwamba kampuni yake ya Oilcom (T) Ltd imetuhumiwa kukwepa kodi Bandarini na kuiibia Serikali na akasema taarifa hizo hazina ukweli wowote.

SSP Kingai alidai kuwa waliiomba JamiiForums taarifa za aliyeanzisha mada kutokana na shauri lililofunguliwa na Usama ili wafanye uchunguzi wa kina kuhusu taarifa hizo na kwamba aliyeziandika akaisaidie Polisi.

Shahidi wa pili alikuwa Peter Kayumbi anayefanya kazi Ofisi ya Upelelezi Kanda Maalum akiwa kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandao. Kikubwa alichotolea ushahidi ni kwamba waliandika barua kwa Mkurugenzi wa JamiiForums kutaka taarifa za mtu aliyeandika kuhusiana na Oilcom (T) Ltd kukwepa kodi na kuchakachua mafuta, lakini taarifa hizo hawakuzipata.

Aidha, alikiri kuwa kuna kifungu cha kisheria kinachowataka kuiomba Mahakama kudai taarifa endapo mtoa huduma kama JamiiForums anakataa kutoa ushirikiano lakini wao hawakukitumia kifungu hicho na moja kwa moja walienda kufungua kesi. Pia, alikiri kuwa mshtakiwa wa pili yupo kwenye shauri hili kimakosa.

Shahidi wa tatu alikuwa ASP Fatuma Kigondo ambaye pamoja na mengine, alisema Polisi waliomba taarifa za mteja bila kutaja ni kwa mujibu wa sheria gani.

Shahidi wa nne katika shauri hili alikuwa Usama Mohamed ambaye ni Afisa Msimamizi wa mauzo ya rejareja wa Oilcom (T) Ltd. Usama alikiri kwenda Polisi kulalamika kuwa kuna mdau wa JamiiForums anaichafua kampuni yake lakini pia alisema anajua Washtakiwa wanashtakiwa kwa kuzuia upelelezi na si kuichafua kampuni kama malalamiko yake yalivyokuwa.

Hata hivyo, Ushahidi pekee ambayo ilikuwa nakala ya chapisho (printed copy) uligonga mwamba mahakamani.

KIELELEZO PEKEE KILIGONGA MWAMBA MAHAKAMANI

Itakumbukwa pia katika shauri hili upande wa Jamhuri uliwasilisha kielelezo cha ushahidi kilichochapishwa kutoka mtandaoni, lakini Mawakili wa Utetezi walipinga kielelezo hicho kwa hoja na Mawakili wa Jamhuri kukitetea.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili juu ya kielelezo hicho, Hakimu Simba alisema kielelezo hakiwezi kutumiwa kwa kuwa hakijakidhi vigezo vitano muhimu vinavyotakiwa kwa kielelezo cha ushahidi cha kieletroniki.

USHAHIDI WA UTETEZI (DEFENSE) KATIKA SHAURI HILI

Katika utetezi wake, Maxence Melo huku akiongozwa na Wakili wake, Peter Kibadala alibainisha katika Kipindi anachodaiwa kutotoa ushirikiano kwa Polisi ni kweli alikuwa Mkrugenzi wa Jamii Media lakini Micke hakuwemo yaani hakuwa mmoja wa Wakurugenzi.

Alibainisha kuwa hakuna mtandao unaoendeshwa chini ya Jamii Media Co. Ltd. Aliongeza kuwa kwa mujibu wa leseni ya biashara ya Jamii Media, ilisajiliwa kuendesha na kufanya kazi ya matangazo sio mitandao ya kijamii.

Maxence alifafanua kuwa Sheria za Kimataifa zinazoongoza Mitandao zinataka Wamiliki wa Mitandao kuwa Sera ya Faragha pia waliangalia Katiba ya Tanzania Ibara ya 18 inayolinda faragha ya mtu.

Shauri jingine linalofanana na hili lililoisha

Ikumbukwe kuwa, mnamo Juni 01, 2018 shauri jingine namba 457 kama hili [lilihusu Kampuni za CUSNA Investment na Ocean Link kuandikwa JamiiForums(sawa na Olicom (T) Ltd) kudaiwa kukwepa kodi bandarini Dar na kunyanyasa wafanyakazi wa kitanzania] washtakiwa waliachiwa huru na Hakimu Godfrey Mwambapa baada ya kukutwa hawana kesi ya kujibu.

SHAURI JINGINE LINALOENDELA

Bado kuna shauri namba 458 linalohusu JamiiForums kutokutumia kikoa cha do.Tz na kuzuia upelelezi wa Polisi, upelelezi unaodaiwa kuhusiana na benki ya CRDB kuandikwa JamiiForums. Awali lilikuwa likisikilizwa na Hakimu Victoria Nongwa na sasa linaendelea kusikilizwa mbele ya Hakimu Huruma Shaidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu.

Mwisho
Tukutane Kisutu kesho kuisikiliza hukumu ya shauri hili kwani uamuzi utakaotoka una athari (aidha chanya au hasi) kwa Tasnia ya Habari na Uhuru wa Kujieleza nchini. Aidha, inatazamiwa kuwa uamuzi huu unaweza ukatoa mwanga wa usalama wa watoa taarifa na watumiaji wa mitandao upoje kisheria hapa nchini.

Kwetu sisi Wanahabari, kesi hii ni muhimu kujua hatma ya ulinzi wa Vyanzo vya Taarifa (source) ukizingatia kuwa ni nyenzo muhimu kwa mwandishi.
 
Back
Top Bottom