Kisiwa chenye hazina

Red Giant

JF-Expert Member
Mar 9, 2012
15,658
20,886
KISIWA CHENYE HAZINA

Mtunzi: Robert Louis Stevenson,1883.
Mtafsiri: F johnson na Edwin W Brenn, 1928.
Marekebisho: Pictuss, 2021.

Pictuspublishers@gmail.com

Kinapatikana ndani ya maktaba app by pictuss.

1620910118331.png


SURA YA KWANZA: MZEE KAPTENI



Kuna mabwana wameniomba niandike habari zote za kisiwa chenye hazina tokea mwanzo mpaka mwisho, nisifiche hata neno moja ila pale mahali palipo kisiwa chenyewe tu, kwa sababu hazina nyingine zipo mpaka leo na bado hazijafukuliwa. Basi katika mwaka huu wa kumi na saba, naanza kushika kalamu yangu na kujaribu kukumbuka zamani, wakati baba yangu alipokuwa na nyumba ya wageni. Siku moja mzee mmoja baharia alikuja kupanga kwetu. Mzee huyu alikua na kovu la pigo la upanga usoni, na hata sasa naweza kuukumbuka uso wake ulivyokuwa.

Nakumbuka sana, kwani naona kama ni jana tu, alipofika alikuwa na sanduku lake kubwa likimfuata nyuma katika gari. Alikuwa mrefu, mwenye nguvu, tena mnene, na rangi yake nyeusi kidogo; nguo zake zilikua kuukuu zilizochafukachafuka. Kucha zake zilikua zimepasukapasuka, na hilo kovu alilokuwa nalo usoni lilikua liking’aa kuliko uso wake. Tena nakumbuka sana jinsi alivyokua akitazama huku na huku alipokua akiimba wimbo mmoja ambao alipenda kuuimba mara kwa mara katika siku za baadaye:

‘Watu kumi na tano Yoh-ho-ho-ho.

Juu ya sanduku la mfu Yoh-ho-ho-ho.

Na chupa ya mvinyo Yoh-ho-ho-ho.'

Basi akaja akabisha mlangoni kwa fimbo yake, na baba yangu alipofungua mlango, akaagiza kikombe cha mvinyo, akainywa kwa kusukutua kinywa kwanza apate kuona utamu wake vizuri, kisha akasema, “Mahali hapa ni pazuri na nyumba nayo ni nzuri. Je, Rafiki, watu wengi huja hapa kupanga?”
Baba yangu akajibu, “Watu wanaokuja si wengi.”
Basi yule mzee baharia akasema “Vema basi,mahali hapa patanifaa sana.” Akamwita yule mwenye gari akamwambia alete sanduku lake, tena amsaidie kulichukua na kuliweka nyumbani. Halafu akasema, “Mimi sina makuu, kama nikipata chakula changu na mvinyo na mahali pa kutazama meli zinazopita, basi sina haja ya kitu tena.
Na mimi ninaitwa ‘Kapteni’.”Basi akampa yule mwenye gari ujira wake.

Yule mwenye gari alituambia kuwa yule mzee baharia alifika kwenye gari lililofika mjini asubuhi, akauliza habari ya nyumba za wageni, ndipo akaambiwa kuwa nyumba yetu ndiyo bora, basi akamwambia amletee sanduku lake katika gari. Basi hatukuweza kupata habari Zaidi ila hii tu.

Yule mzee Baharia yaani Kapteni alikua mtu mkimya kabisa, na mchana kutwa alishinda pwani akitazama baharini huku na huku kwa darubini yake, na kila jioni alikaa katika chumba cha kunywea mvinyo. Mara nyingi alikua akiulizwa neno alikuwa hajibu na baada ya siku chache tulimzoea na kufahamu alikua hataki kujishughulisha na watu, ndipo tukamuacha kukaa kimya. Kila jioni aliporudi kutoka kutembea aliuliza mabaharia wengine wamepita na kwanza tulifikiri ya kuwa anamtaraji rafiki mwenziwe baharia, lakini badaye tulifahamu ya kuwa alitaka kuepukana nao. Mabaharia wengine walipokuja kupanga pale nyumbani kama walivyokua wakifanya mara kwa mara, yeye huja kuchungulia dirishani kwanza ili apate kuwaona kabla hajaingia humo ndani. Tena katika siku wanazokuwapo mabaharia wengine yeye huwa kimya kupita desturi ya siku zote. Mimi nilijua habari zote, kwa sababu siku moja aliniita faraghani na kuniahidi kunipa fedha kila mwezi kuwa ujira wangu ili siku zote niwe nikiangalia sana na kumwambia mara tu nikimwona baharia mwenye mguu mmoja.

Pengine mwisho wa mwezi nilipokuwa nikienda kudai ujira wangu, alikua akinitazama tu lakini kabla ya kupita juma nzima alikua akiniita na kunipa, akaniambia nizidi kupeleleza

Kwa kufikiri kwangu mara nyingi nilikuwa nikiota ndoto; hata siku moja nikaota kumwona baharia mwenye mguu mmoja tu, niliota mguu wake mmoja umekatikia penye goti, au penye paja. Kwa kweli ndoto hizo zilinitisha mno nikaona kuwa nastahili kupewa fedha zile. Na ingawa niliogopa kuja kumwona baharia mwenye mguu mmoja, yule mzee Baharia, Kapteni nilimwogopa zaidi ya watu wote wengine. Pengine ni sababu alikunywa mvinyo kupita kiasi, na hivyo ndipo tulipopata kumsikia akiimba wimbo wake kwa sauti kubwa: ‘na chupa ya mvinyo, yo-ho-ho-ho.’ Na alipokuwa amelewa alikuwa anakuwa mtu wa kutisha kweli kweli tena hushurutisha kila mtu kuimba pamoja naye, wala hakumruhusu hata mtu mmoja atoke nje ya nyumba mpaka aishe kulewa na kushikwa na usingizi.

Hasa yaliyowatisha watu yalikuwa ni hadithi alizozisimulia, hadithi za kutisha zilizohusu kunyonga watu, kuwatosa baharini, na matendo maovu mengine katika nchi za mbali. Kwa kujigamba kwake mwenyewe alisema kwamba alikua akiishi miongoni mwa watu walio waovu kabisa kuliko wote waliojaliwa na Mungu kusafiri baharini; na maneno aliyoyatumia yalishtusha watu kwa namna yalivyokuwa ya matusi. Mara nyingi baba yangu alikua akisema kwamba sifa ya nyumba yake itaharibika kabisa, na watu wengi watakataa kuja kupanga kwake tena kwa sababu ya tabia ya mtu huyo.

Mara moja tu ndipo nilipomwona kukasirika kabisa. Ilikua siku moja bwana daktari kaja kumtazama baba yangu ambae alikuwa mgonjwa, naye huyu kapteni alilewa sana siku hiyo akaanza kuimba kwa sauti kuu:

‘Watu kumi na tano Yoh-ho-ho-ho.
Juu ya sanduku la mfu Yoh-ho-ho-ho.
Na chupa ya mvinyo Yoh-ho-ho-ho.’

Mara ya kwanza niliposikia maneno yake, ‘Sanduku la mfu’ nilifikiri kama ni sanduku lile kubwa alilokuja nalo, na mara nyingi niliota katika ndoto zile za baharia mwenye mguu mmoja. Bwana daktari ndiyo kwanza asikie wimbo ule, nae akawa hataki kelele. Alafu yule kapteni akapiga meza kwa kishindo kikubwa, na sisi tuliokuwa tumemzoea, tukajua kuwa hii ndiyo ishara ya mzee kapteni kushurutisha watu wanyamaze, ila Bwana Daktari hakuwa na habari akaendelea katika maongezi yake. Mara kapteni akageuka kumtazama na kupiga meza mara ya pili na kumtukana, akimwamuru anyamaze.

Bwana Daktari akageuka kumuuliza, "Je,wasema na mimi?” Na alipomwambia ndiyo, akasema, "Basi mimi ninayo maneno machache nitakayokwambia. Ndiyo haya: Kama wewe utaendelea kunywa namna unavokunywa sasa, dunia itafarakana na mtu mwovu na mchafu.”

Lo! Hasira zilioje! Mzee kapteni aliruka gafla na kuvuta kisu chake kutaka kumpiga Bwana Daktari. Lakini yeye hakustuka hata kidogo ila alimwambia kwa upole, "kama usipoweka mara moja hicho kisu chako katika ala yake, nakwambia kuwa utahukumiwa na kunyongwa bila shaka.”

Basi baada ya kutazamana kidogo Mzee Kapteni akaweka kisu chake katika ala na akakaa na kununa kama mbwa aliyepigwa. Bwana Daktari akaendelea kusema, “Na sasa, maadam najua kuwa wewe wakaa mtaa huu, lazima nikuangalie sana. Mimi ni kadhi wa serikali, na nikipata habari ya matata yako kidogo tu, basi nitafanya niwezavyo upate kufukuzwa katika nchi hii." Basi Akaondoka akaenda zake. Na Mzee Kapteni akakaa kimya kabisa kwa mda wa siku nyingi.


SURA YA PILI: KUTOKEA NA KUTOWEKA KWA MBWA MWEUSI

Baada ya siku chache, nakumbuka kuwa siku moja baba yangu alikuwa hajiwezi sana hata ikamlazimu mama yangu kukaa pamoja naye kumuangalia, mimi nilikuwa nikitandika meza tayari kumwandalia Mzee Kapteni, maana yeye kama ilivyokuwa desturi yake alikwenda pwani kutembea basi mara mlango ukafunguliwa na mtu akaingia ndani; mtu huyo alikua mrefu na mkono wake mmoja ulikatika vidole viwili, tena ijapokuwa alikua na upanga kiunoni, nafikiri hakuwa shujaa.

Nikamuuliza haja yake, nae akaniambia nimletee kikombe cha mvinyo; basi nilipokuwa nikienda, akaniita, "Njoo, njoo hapa karibu.” Hata nilipomkaribia akaniuliza, “Je, unamtandikia meza rafiki yangu?” Nikajibu, “Simjui rafiki yako.” Akasema, “Vema, lakini jina la rafiki yangu ni Kapteni. Ana kovu la pigo la upanga usoni. Basi sasa niambie kama rafiki yangu yumo humu.”

Nikamwambia, “Rafiki yako amekwenda kutembea pwani.”
Basi akakaa mlangoni kumngojea, na kuitazama njia niliyomwonesha. Mara kitambo kidogo tukamwona Mzee Kapteni anakuja. Yule mgeni akasema, “Haya sasa na tuingie ndani tujifiche nyuma ya mlango, ili Mzee akifika tupate kumshtusha.”

Tukaingia ndani tukajificha nyuma ya mlango, lakini nilijua kuwa huyu mgeni ni mwoga sana. Kwani upanga wake katika ala ulilegea, na mara kwa mara alikua akimeza mate kwa hofu aliyokuwa nayo.
Basi Mzee Kapiteni akaja akafungua mlango kwa kishindo akaingia ndani, wala hakugeuka kutazama mkono wa kulia au kushoto, ila akaendelea tu mpaka mezani nilipoweka chakula chake. Mara yule mgeni akamwita akasema “Mzee” na Mzee Kapteni akageuka kwa upesi kabisa, hata uso ukampauka kwa kugutuka, akawa kama mtu alieona zimwi. Yule mgeni akasema, “Je! Mzee umenisahau? Humkumbuki rafiki wa zamani?”

Mzee Kapteni akashikwa na bumbuwazi kama mwenye kigugumizi. Kisha naye akamwita, “Mbwa mweusi!” Yule mgeni akajibu, “Mimi ndiye mbwa mweusi nimekuja kukutazama rafiki yangu wa zamani. Ah Mzee! Ama mimi na wewe tumeona mambo mengi tangu vidole vyangu vilipokatika.”

Mzee Kapteni akajibu, “Kweli! Na sasa umeniona ndiyo wataka nini? Sema, wataka nini?”
Basi wakaniamuru niwaletee mvinyo, kisha wakaniambia nitoke chumbani niwaache peke yao wasemezane wala mimi nisiwepo karibu kusikiliza. Basi nikawaacha. Na kwa muda sikusikia sauti ila ngurumo tu, lakini mara nikasikia sauti ikisema, “Hapana! Hapana! Hapana kabisa! Kama ni kunyongwa vema tunyongwe sote pamoja.”

Mara tena nikasikia kelele za ghasia nyingi na matusi na vishindo vya meza na viti kutupwatupwa, na milio ya panga zikipambana. Punde nikasikia kama mtu alieumizwa sana akiugua na nikamuona yule mgeni aliyeitwa mbwa mweusi akitoka mbio na huku akifukuzwa na yule Mzee Kapteni, na damu ikimtoka yule mgeni kama maji. Mara nikamwona mzee akimtupia tena upanga kwa nguvu zake na kama ungalimpata ungalimpasua pande mbili, lakini kwa bahati haukumpata, akazidi kukimbia, ijapokuwa alikwisha umizwa sana. Mzee Kapteni akasimama kiasi kidogo kama mtu mwenye wazimu kwa hamaki, alafu akaingia ndani ya nyumba, na mara akapepesuka kutaka kuanguka. Nikamuuliza kama umeumizwa, nikatoka kwenda kumletea mvinyo ili apate kujiburudisha, lakini mara nilipotoka chumbani nikasikia mkoromo mkubwa mno, nikarudi mbio, nikamkuta amelala chini. Basi na mama yangu akawa amesikia zile kelele akatoka na kunituma kumwita Bwana Daktari.

Alipokuja Bwana Daktari tukamuuliza ameumia wapi. Bwana Daktari akajibu, “Kuumia! Hakuumia hata kidogo! Mtu huyu ameshikwa na kiharusi kama nilivyomwonya juzi.” Basi akatwaa bakuli na kisu chake kumtoa damu, na baadaye kidogo Mzee akainuka tena, na mara alipomwona Bwana Daktari akakunja uso, lakini aliponiona mimi akawa hana neno. Badaye akauliza, “Je, Mbwa mweusi yupo wapi?”

Bwana Daktari alikuwa hana habari ya mambo yaliyopita, akajibu, “Hayupo mbwa mweusi hapa ila yule wa Maungoni mwako tu. Wewe umezidi kunywa mvinyo hata umepatwa na kiharusi kama nilivyokuonya juzi, nami nimekuponya, nusura ufe.”
Basi tukamsaidia kumwinua, tukamweka kitandani na Bwana Daktari akamwambia,
“Sasa tulia usilewe, kama ukinywa hata tone moja la mvinyo fahamu ndiyo mauti yako.” Basi tukatoka chumbani na Bwana Daktari akaniambia kuwa sasa yu salama, lakini kama akishikwa na kiharusi tena atakufa.
 
SURA YA TATU: DOA JEUSI


Kupata saa sita nikaenda tena kumtazama mzee Kapteni na kumpelekea maji, nikamkuta ana homa, tena yu dhaifu sana, akasema, “Jim, wewe tu ndiye unayenisaidia, wengine wote wananichukia kabisa. Basi kumbuka kuwa mara kwa mara nimekupa fedha kwa ajili ya ujira wako, na hivi sasa lazima unisaidie.” Akanena, "Jim tafadhali niletee kikombe cha mvinyo.”

Nikamjibu “Bwana Daktari amekataza,asema…”
Lakini Mzee Kapteni alinikatiza maneno,akasema, “Madaktari wote ni wapumbavu na wala hawajui desturi za mabaharia kama mimi. Mimi nimekaa sana nchi za joto, na huko nimeona rafiki zangu na wenzangu wakifa kwa homa kali ila mimi tu niliokoka kwa ajili ya kunywa mvinyo. Kama nisipopata mvinyo nitakufa. Haya Jim, nenda kanitilie kikombe kimoja tu.”

Basi kwa vile alivyoanza kufanya gasia na kelele nyingi na kwa sababu niliogopa kuwa atamwamsha baba yangu aliyekuwa mgonjwa sana, nikaridhia kumpa kikombe kimoja. Basi alipouliza habari, nikamwambia, “Bwana Daktari ameagiza kwamba lazima ulale kitandani muda wa siku saba.”
Akasema, “Juma nzima! Siku saba! Siwezi kabisa kulala hapa kwa muda wa siku saba, maana kama nsipojificha watanitia doa jeusi mkononi kabla ya siku saba kupita. Na hivi sasa nadhani wananitafuta, lakini ngoja tu nitawashinda – hawataniweza kabisa.” Akajaribu kuondoka kitandani tena lakini hakuweza. Baada ya kujinyoosha kidogo kupumzika, akasema, “Jim, ulipata kumwona yule baharia? Yule aliekuja leo?
Nikamwuliza, Yule anayejiita Mbwa Mweusi?”
Akaitikia, “Ee ama yule ni mtu mwovu kabisa, lakini wale wenzake ni waovu zaidi. Basi nisipoweza kuondoka na kukimbia, nao wakinitia mkononi doa jeusi, fahamu kuwa wanalolitaka ni sanduku langu. Ukiona hivi ni lazima uondoke upesi, upande farasi uende upesi sana kwa Bwana Daktari ukamwambie habari zote. Maana mimi nilikuwa nahodha msaidizi katika meli ya Mzee Flinti. Nami ni mimi peke yangu ninayepajua hapo mahali. Maana mwenyewe alinipa habari, alipokuwa akifa aliniusia lakini kama wasiponitia doa jeusi, usiseme neno, kaa kimya tu.”

Nikajibu, “Sawa, lakini doa jeusi hilo ni kitu gani?
Akajibu, “Ni wito, yaani kwa mfano ni kipande cheupe cha karatasi au kitu chochote cheupe, upande mmoja umetiwa rangi nyeusi na upande mwingine umeandikwa maneno ya kifo chako, au kutolewa katika chama au kukubashiria yatakayokupata. Hivi ndivyo ilivyokuwa desturi yao. Lakini kama wakiniita nitakwambia. Wewe kazi yako ni kuangalia sana, mimi na wewe tutagawana sawa kwa sawa.”

Basi jioni ile baba yangu akafa, na katika kushughulika kutengeneza mazishi nilisahau kabisa habari za Mzee Kapteni, muda wa siku chache, ingawa nilimwona mara mojamoja akijikokota kuja mezani kula chakula chake.

Mambo yakawa hivi hivi mpaka siku aliyozikwa baba yangu, na saa tisa mchana nilikuwa nimesimama mlangoni nikimfikiria baba yangu na kukumbuka siku za uhai wake. Mara nikasikia mtu anakuja, nikamjua ni kipofu kwa kuwa nilisikia akigonga gonga kwa fimbo yake aliyoitumia kujiongoza njia. Nikamtazama nikamuona amejifunga kitambaa cha macho kilichomfika hata puani. Alikuwa mzee sana tena mdhoofu mno. Nikasema katika nafsi yangu kuwa tangu kuzaliwa kwangu sijaona mtu wa kutisha kama huyu. Hata alipofika karibu na nyumba, akasimama akasema kwa sauti ya unyonge, Hivi hapa hapana wa kuniambia nimefika wapi? Mimi ni kipofu maskini ya Mungu niliyepofuka macho katika kuitetea nchi ya mfalme wetu mtukufu.”
Sasa nikawa sina budi kumjibu huyu masikini kipofu, nikasema, “Uko hapa karibu na nyumba ya wageni.”
Naye akanena, “Kweli nasikia sauti na sauti yenyewe ni ya kijana mwanamume. Tafadhali mwanangu niache nikushike mkono wako upate kuniongoza.”

Basi nikampa mkono wangu, yule kipofu akanishika kwa nguvu sana nami nikashtuka sana hata nikajaribu kuutoa mkono wangu nisiweze. Basi akawa amenishika vile vile akasema “Haya nipeleke kwa Mzee Kapteni.”
Nikajibu, “Bwana, sithubutu kukupeleka.”
Akasema, “Aha ni hivyo! Basi kama usiponipeleka upesi nitakuvunja mkono.” Na wakati ule aliposema hivi akaupopotoa mkono wangu nikidhani umeteguka kabisa, nikalia sana kwa uchungu, nikasema, “Bwana kasema nisithubutu kukupeleka si kwamba ni kwaajili ya mimi tu, kwaajili yako wewe pia, maana huyo mzee kapteni si kama alivyokuwa. Siku hizi hukaa kimya tu, na upanga wake wazi mkononi.”

Basi akasema, “Haya! Haya! Twende sasa hivi.” Nami kwa kuwa niliogopa nikawa sina budi kumpeleka; hata nilipofika nikafungua mlango wa chumba nikaita, Bwana Kapteni, rafiki yako amekuja kukutazama.” Mara Mzee Kapteni akainua macho na ingawa alikuwa amelewa sana, mara ulevi ukamtoka, akataka kuondoka kitini asiweze. Alikuwa kama nguvu zilimwisha.

Basi yule kipofu akasema, “Bill kaa hapo hapo kwani japokuwa ni kipofu sioni, lakini hata ukijongeza kidole chako naweza kukusikia. Ewe kijana mwanamume, ushike mkono wake wa kulia uulete karibu na mkono wangu wa kulia.” Basi nikafanya yote aliyoniamuru, ndipo nilipomwona akitia kitu katika kiganja cha mkono wa yule mzee kapteni mara akaufumba.

Hata alipokwisha kufanya hivi, yule kipofu akanena, “Sasa kazi imekwisha," mara akauacha mkono wa Mzee Kapteni, akatoka chumbani na kwenda mbio sana, nikasikia kishindo cha fimbo yake ikigonga kupapasa njia.
Basi sisi, yaani mimi na Mzee Kapteni tukawa tumepigwa na bumbuwazi kabisa na akili zikaturuka tusijue la kufanya. Lakini baadaye yule Mzee Kapteni akafumbua mkono wake akasema, Saa nne! ninayo masaa sita, ngoja tutawashinda tu.” Akainuka, lakini katika kuinuka kwake akajishika kooni, na mara akagugumia na akaanguka chini kifudifudi.
Nikainama upesi kumshika na kumwita mama, lakini bure haikufaa kitu kwani alikuwa amekwisha shikwa tena na kiharusi. Kuna jambo sikulielewa, tokea mwanzo sikumpenda mtu huyu, lakini nilipomwona na kutambua kuwa amekwisha kufa, nikalia sana na machozi yakabubujika kama maji. Katika siku chache hizi hii ni mara ya pili kukutana na maiti, na labda ndo ilikua sababu ya mimi kulia sana hivyo.


SURA YA NNE: SANDUKU

Sikukawia kumhadithia mama yangu habari zote nilizozijua tokea mwanzo hata mwisho, nasi tukajiona tumo katika hatari ya kuwa labda wale watu wanaomtafuta Mzee Kapteni watakuja tena. Tulimdai fedha yule maiti, na tulijua sana kuwa kama wakija wale watu wanaomtafuta Mzee Kapteni, na ikiwa wote ni kama yule Mbwa Mweusi na yule Kipofu, hatutapata kitu.

Nilikumbuka jinsi alivyoniusia yule Mzee Kapteni kabla ya kufa kwake, kuwa nikiona hivyo niende nikamwarifu Bwana Daktari, lakini sikupenda kumwacha mama yangu peke yake bila ya mtu wa kumwangalia. Kwa woga tuliokuwa nao, tulikua tukisikia sauti hata ndogo tu, tulishtuka.
Basi ikawa ilitulazimu kufanya jambo. Tukaonelea ni bora tukaombe msaada kijijini, ndipo tukakimbia vivi hivi wala hatukuwahi kuvaa hata kofia. Kijiji chenyewe tulichokimbilia hata haukuwa mbali sana, lakini kabla hatujaufikia tukaona taa zimewashwa, kwa kuwa ni jioni na giza lilianza kuingia

Basi tulivyoingia kijijini tukaenda kupata msaada wa watu tusipate, watu wote walikataa kutusaidia, na kila tulipozidi kuhadithia hatari na shida zilizotupata ndivyo wao walivyozidi kukataa. Hata mwisho mmoja wao alikubali kwenda kumwarifu Bwana Daktari, lakini hapana hata mmoja aliyekubali kufuatana nasi kwenda kulinda nyumba yetu.

Mama yangu alikuwa hodari sana, akasema, “Siwezi kupoteza fedha zangu bure, na ikiwa hapana mtu atakayekubali kwenda kutusaidia, basi mimi na mwanangu Jim tutakwenda peke yetu.”
Basi mtu yule akaenda kumwita Bwana Daktari, ikawa mimi na mama yangu kuondoka kurudi kwetu, ijapokuwa tuliogopa sana.

Hata tulipofika nyumbani tulikuta maiti ameshakauka kabisa, tukavuta pazia kusudi wale watu wanaomtafuta Mzee Kapiteni wasije wakachungulia ndani. Sasa ikawa kazi ya kutafuta ufunguo wa lile sanduku, ndipo nikamkabili maiti kwa hofu sana nikatazama chini yake nikaona mfano wa kipande cha karatasi mfano wa shilingi moja, na upande mmoja umetiwa rangi nyeusi; nikakiokota na kukitazama upande wa pili nikaona yameandikwa wazi wazi maneno haya, “utauawa saa nne usiku.”
Basi nikamwambia mama yangu, “Ah, kumbe huyu Mzee Kapiteni alikua na nafasi mpaka saa nne! Na madam sasa ni saa moja tu, tunayo nafasi nyingi ya kufanya kazi yetu.”
Basi nikaaanza kutafuta ufunguo,nikatia mkono katika kila mfuko wa nguo zake, nikatoa fedha kidogo na uzi na sindano, na tumbaku ya kuvuta kidogo, na kisu, na kibiriti na dira; lakini ufunguo sikuuona hata nilipotazama shingoni, ndipo nalipouona umefungwa na uzi aliouvaa shingoni. Nikaukata ule uzi nikautoa ufunguo; tukaenda mpaka huko kulikokuwa na lile kubwa tupate kulifungua.

Sanduku lenyewe lilikuwa kama yale yanayotumiwa na mabaharia siku hizi, lakini limebonyea kwa kugongwagongwa wakati wa safari zake. Basi mama akafungua sanduku na kuinua kifuniko chake na mara tukasikia harufu ya tumbaku na lami. Juu palikuwa na nguo na chini kulikuwa na vitaka taka vingine kama dira, kopo, tumbaku na fedha za namna mbalimbali na saa moja ya fedha.

Hatukuona kitu kingine cha thamani isipokuwa zile fedha na saa, hata tulipotoa koti la mvua lililokuwamo humo sandukuni, tukaona bunda moja limefungwa kwa kitambaa kilichoimarishwa kwa mafuta, na tulipoliondoa tukaona mfuko. Basi mama akatwaa ule mfuko na kumimina vitu vilivyokuwamo, ndipo tulipoona sarafu nying za dhahabu za nchi mbali mbali. “Mimi si mwizi, nitatwaa za kutosha kujilipa haki yangu tu, wala sizidishi,” alisema mama yangu. Basi tukaanza kuzitenga mbali mbali namna za dhahabu, na wakati tunafanya hayo nikasikia fimbo ya yule kipofu ikigonga gonga, nikaogopa mno, nikataka mama achukue upesi upesi dhahabu zote tupate kukimbia lakini hakukubali. Kule kugonga gonga kulipokwisha pita tukashukuru, tukavuta pumzi tena, mara tukasikia mtu akipiga mbinja, tukashtuka sana, hata mama akasema, “Haya sasa twende zetu, nitachukua hizi tu.” Na mimi nikachukua lile bunda lililofungwa kwa kitambaa cha mafuta.

Basi tukatoka chumbani tukaja nje, na sasa ule ukungu uliokuwa umetanda ukaanza kuondoka. Tulitambua kuwa tukianza kukimbia kuelekea kijijini tutaonekana, na mbaya zaidi sauti nyingi zilianza kusikika, zikienda kuelekea nyumbani kwetu, tena watu hao walikuwa na taa zao. Basi mimi na mama yangu tukaamua kujificha chini ya daraja dogo linaloelekea kwenye nyumba yetu. Kutoka hapo tuliweza kusikia yaliyokuwa yakizungumzwa. Basi mwisho wake tukazisikia sauti zimefika nyumbani, hapo nilimsikia yule kipofu akiwaamrisha wenziwe akinena, “Haya, haya, ingieni ingieni, ingieni!” Pengine aliwatukana kwa vile walivyokawia.
Wengine walimsikiliza wakaingia ndani, lakini walitoka upesi wakasema, “Mzee Kapteni amekwisha kufa, amekwisha kufa.”
Lakini yule kipofu alizidi kuwatukana na kusema, “Tafuteni katika mifuko yake, na wengine mkalichukue sanduku lake kubwa.”
Basi ikawa kimya kidogo, na baadaye nikasikia sauti ya mtu mmoja akisema, “Piu, (nikafahamu kuwa hili ndilo jina la yule kipofu) kumbe kuna watu wengine waliotangulia kufika. Sanduku limekwishafunguliwa na vitu vingine vimeshatupwa huku na huku.”
Basi yule kipofu akawauliza, “Je kile tukitakacho kipo?”
Akajibiwa, “Kipo, fedha na dhahabu hizi hapa.” Yule kipofu akakasirika sana, akapiga kelele kwa ghadhabu akasema, “Hizo sizo ninazotaka, nataka yale maandishi ya Flinti.”
Akajibiwa mandishi hatuyaoni kabisa, labda yako katika mifuko ya maiti.” Mradi wakatafuta wasipate wanachokitaka, na yule kipofu akasema, “ni wale watu wenye nyumba, ni yule kijana aliyeyachukua. Heri kama ningemtoa macho yake. Walikuwa hapa sasa hivi; haya watafuteni.”

Basi mara ikawa ghasia nyingi. Kwanza wakatutafuta nyumbani wasituone. Mara tukasikia mtu akipiga mbinja mara mbili, nikafahamu kuwa hiyo ni ishara ya kuwaonya wale maharamia kuwa kuna hatari kubwa inayo wakaribia. Mmoja wao akasema “Haya twendeni zetu, hii ni mara ya pili kupigiwa mbinja.”

Yule Piu kipofu akasema, “Oh! Hapana kitu, huyu tokea zamani ni mwoga tena ni mpumbavu. Msimsikilize, lazima tuwapate wale wenye nyumba. Hawawezi kuwa mbali. Iwapo ningekuwa naona! Alilaani Piu.”

Kweli wengine walikuwa wameshughulika sana kutafuta, lakini nadhani wengine walikuuwa wamesimama tu na kwa hivyo yule kipofu alizidi kuwahimiza akanena,” Haya ati, njia ya kupata fedha kwa kadri mzitakazo zi karibu, nanyi mnakaa bure tu. Hapana hata mmoja wenu alithubutu kumpelekea Mzee kapteni doa jeusi! Na mimi ni kipofu! Mnataka niwe maskini, niwe ombaomba badala ya kuishi raha mustarehe sababu ya uzembe wenu? Hata kama mngekuwa na moyo wa funza aliye ndani ya biskuti kufika sasa mngekuwa mmekwisha kuwakamata.”

Mmoja akajibu “ndiyo, lakini ya nini, nasi tumekwisha pata dhahabu? Labda wameyaficha yale maandishi tu.”
Yule kipofu aliposikia hivi alikasirika sana, akaanza kuwapiga kwa fimbo yake, nao wakamtukana; ikawa ghasia moja kwa moja. Kugombana kwao ndiyo ilikuwa salama yetu, kwa kuwa wakati wa ugomvi tulisikia farasi wanakuja kasi, na mara tukasikia mlio wa bunduki na upesi maharamia wote wakatawanyika na kukimbia isipokuwa yule kipofu tu, naye wenziwe walimwacha, labda sababu ya kutaharuki au sababu ya kisasi kwa matusi yake na kuwapiga kwa fimbo, sifahamu. Akawa anakwenda huku na huku, maskini haoni, na kila akienda aliita, Wenzangu e-eh! Wenzangu mbona mmeniacha? Mbwa mweusi, Diki, John, mbona mwaniacha peke yangu! Msiniache ndugu zangu njooni mnisaidie.” Mara tukaona watu wanne watano wamepanda farasi wanakuja kasi barabarani. Sasa yule kipofu akaingiwa na hofu akawa anahangaika kweli kweli na kukimbia huku na huku akitafuta mahali pa kujificha, akaanguka akainuka, akaanguka tena mara ya pili, na safari hii akawa yuko chini ya miguu ya farasi. Yule mpanda farasi kuona hivi akajaribu kumsimamisha farasi wake asiweze, farasi akamkanyaga na kumtupa pembeni. Piu akapiga kelele kubwa sana na kisha akatulia kinya kabisa. Ikawa sasa yuko chini amelala kifudi fudi wala hajiwezi tena.

Hata tulipotoka pale mahali tulipojificha nikawatambua wale watu, kuwa walikuwa ni askari wa forodhani, na mmoja wao alikuwa ni yule kijana aliyeenda kumwita Bwana Daktari, sasa habari ikawa imeshafika kwa Bwana Mkubwa wa Forodhani kuwa kuna meli iliyoingia pwani kwa siri, naye akaja mbio pamoja na watu wake kutazama mambo yalivyo.

Yule kipofu alikuwa amekwisha kufa, mimi na mama yangu tulirudi nyumbani na wale askari wakazidi kuwatafuta wale maharamia wasiwapate, kwani walipofika baharini walikuta wamekwisha kujipakia melini na meli yao iko baharini inakwenda zake.

Lo! Ghasia gani nyumbani, kila kitu kimevunjika vunjika kwa zahama zao. Na yule mkubwa wa wale askari akasema, “Hawa wamekwisha chukua fedha na dhahabu zote, basi walikuwa wakitafuta nini tena?”
Mimi nikasema, “Nadhani walikuwa wakitafuta hili bunda.” Naye vile vile akataka kulichukua lakini mimi sikukubali kumpa, nikamwambia kuwa nitampelekea Bwana Daktari, naye akajibu, “Vema, hivyo ni vizuri zaidi, maana yeye ndiye kadhi wa serikali.”


Basi wale watu wakaondoka kwenda zao na mimi nikapandishwa nyuma juu ya farasi wa mkubwa wa yule askari, akanichukua kunipeleka kwa Bwana Daktari nipate kumwelezea yote yaliyotokea.
 
SURA YA TANO: NYARAKA ZA KAPTENI

Hata tulipofika kwa Bwana Daktari, akatukaribisha, tulimkuta akiongea na bwana mmoja jina lake Treloni. Basi yule mkubwa wa askari akaanza kusimulia habari zote alizozijua. Walipokwisha sikia habari zote wakanisifu sana kwa namna nilivyokuwa hodari. Na yule Bwana Daktari akataka nimpe lile bunda nililokwenda nalo. Nikipompatia alilitazama kama vile vidole vyake vinawashwa kulifungua lakini hakufanya hivyo, badala yake akakiweka kwenye mfuko wa koti lake.

Kisha nikapewa chakula nikala. Hata alivyotoka yule mkubwa wa askari wakaanza kusimulia Habari za yule Flinti ambaye alisemekana kuwa bunda lile la byaraka ni lake. Yule bwana Treloni akasema, “Flinti alikuwa katili kupita maharamia wote baharini kwa kazi za kunyang’anya watu mali zao.
Watu wote walimwogopa. Naye alikuwa Mwingereza. Wahispania walikuwa wanamuogopa sana kiasi kuna wakati nilikuwa najivunia kuwa ni muingereza. Mimi mwenyewe nimeyaona kwa macho yangu matanga ya meli yake, ijapokuwa meli yangu ilikuwa tayari kuondoka bandarini sikuthubutu kuondoka kwa kumwogopa yeye, ikanilazimu kungoja mpaka siku ya pili.”

Basi yule Bwana Daktari ambaye aliitwa Levesi akasema, “Labda bunda hili lina hati au barua ndani yake zinazoelezea mahali alipoficha mali, fedha na dhahabu zote alizoiba.”
Basi yule Treloni akasema, "basi ikiwa ni hivyo mimi nitanunua meli tusafiri nayo mpaka tukaigundue mali hiyo.”
Basi wakaleta mkasi wakakata nyuzi zilizoshonewa bunda katika kitambaa kilichotiwa cha mafuta. Kwanza wakatoa kitabu kidogo kilichoandikwa michoro michoro na maneno mengine ya upuuzi tu. Na kurasa nyingine zina tarakimu kama hesabu, na mwingine mna tarakimu za namana wanazotumia mabaharia kuonyesha majira ya meli, basi kwanza hatukufahamu, lakini badaye tukatambuwa kuwa ni idadi ya meli alizozizamisha na kuzinyang’anya mali. Tena katika bunda lile mlikuwamo na kifurushi kidogo kilichotiwa mhuri; tukatazama tukaona ramani moja ya kisiwa na alama ya majira yake na majina ya hori na milima na kila Habari inayotakiwa na nahodha kwa kufikisha meli katika kisiwa hicho. Tukaona alama tatu za X zilizowekwa kwa wino mwekundu. Mbili upande wa kaskazini na moja upande wa kusini magharibi. Pembeni ya hii alama ya mwisho kulikuwa na maandishi madogo yaliyoandikwa, "mali nyingi zimefichwa hapa.” Na nyuma ya ramani kumeandikwa hivi:
Mti mrefu mlima wa darubini upande wa kaskazini ya mashariki hatua kumi.
Vipande vya fedha vimewekwa kaskazini; waweza kuviona kama ukifuata mlima hatua ishirini kwa upande wa kusini mwa jabali jeusi lenye sura ya mtu.
Si kazi kuzipata silaha zilizofukiwa mchangani upande wa kaskazini mwa hori ile ya kaskazini.

Mimi J.F

Basi mimi ingawa sikuweza kufahamu yale yote, lakini yule Treloni na Bwana Daktari walifurahi sana. Bwana Treloni akasema, “Kesho nitakwenda mjini na baada ya siku chache tutakuwa na meli yetu wenyewe nzuri, kisha tutakwenda wote Pamoja kutafuta mali hiyo iliyofichwa na maharamia hao.”
Basi sote tukakubali kwenda Pamoja na sote tukaapishana viapo kwamba Habari zote hizi tutaziweka siri.

SURA YA SITA: MELI TAYARI

Kwanza tulidhani kazi ya kupata meli ya kutufaa itachukua siku chache, lakini kwa kuwa, shughuli zilikuwa nyingi kazi hii ilichukua siku nyingi. Basi wakati huo wote mimi nilikaa kungojea tu. Na kwa sababu nilikuwa kijana mdogo, na hii ndiyo ilikuwa safari yangu ya kwanza, nikawa na hamu sana, na kila mara nilikuwa ni kama nikiwa mwenye kuota ndoto. Mara nyingine nilikuwa nikijiona kama ninayetembea katika kisiwa chenyewe, na wakati huo nikawa nikitazama ramani. Pengine nilijifanya kama niliye melini nakaribia kisiwa kutoka upande wa kusini au upande wa kaskazini, na pengine nilijifanya kama niliyekaa katika kisiwa chenyewe cha hazina.

Mradi siku zilipita hivi hivi hata siku moja tukapata barua kutoka kwa Bwana Treloni kutuarifu kuwa ameshapata meli na sasa kila kitu ni tayari. Na hiyo barua iliandikwa hivi.

Nimekwisha nunua meli na sasa tayari kusafiri. Na jina la meli hiyo ni Hispaniola. Nilitaka niajiri mabaharia 20 lakini mwanzo nilipata taabu kuwapata. Sasa taabu hiyo imekwisha kwani siku moja kwa bahati nilikutana na mtu mmoja aliyeniomba kazi ya upishi na jina lake ni John Fedha, na ana mguu mmoja tu, na wa pili umekatika katika vita ya kuitetea nchi yetu. Nami nimemwonea huruma nimempa kazi ya upishi, kwani atafaa kuwa mpishi katika safari yetu. Basi alipozijua shida zangu alitangaza kwa rafiki zake na kwa muda wa siku chache hizi nimepata watu wa kutosha.
Basi sasa rafiki yangu njoo upesi, na huyo Jim Hawkins anaweza kwenda kwao kwa siku moja apate kuagana na mama yake, na kisha aje huku upesi. Nimekwisha kufanya mipango kuwa kama tukichelewa katika safari yetu meli ingine itaondoka kutufuata mwisho wa mwezi Agosti. Jina la nahodha msaidizi ni Aro, na nahodha mwenyewe ni mzuri lakini mkali sana.
Wakatabahu,
John Treloni.

Basi nilipopata Habari hii nikawa sina raha hata kidogo, nikataka nisafiri tu nikaenda kuagana na mama yangu, na nilipoona kuwa amekaa vizuri nikaondoka nikaenda mji wa Bristol huko kuliko meli yetu.
Nilipofika nikaenda pwani kutembea, nikakuta meli bandarini na bwana Treloni na bwana Levesi na mabaharia wote tayari, nikauliza, “bwana, tutatoka lini bandarini?”
Nikaambiwa, “kesho tutaondoka” Loo! Kesho safari inaanza, kesho tutaondoka kutafuta kisiwa cha hazina.
 
SURA YA SABA: JOHN FEDHA

Asubuhi nilipokwisha kula, Bwana Treloni akanipa barua na kuniambia nimpelekee John Fedha, akanionesha nyumba yake karibu na pwani. Basi nikafurahi kupata nafasi ya kutembea, na kutazama meli na mambo mengineyo mjini. Hata nilipofika katika nyumba ya John fedha nikakuta nyumba imejaa wageni na hao wote wanazungumza kwa kelele nyingi, hata nikaogopa kuingia. Lakini nilipokuwa katika kungoja akaja mtu mmoja kutoka ndani ambaye nilimtambua moja kwa moja kuwa ndiye ninayemtafuta. Mguu wake wa kushoto ulikuwa umekatika pajani, alikuwa akijikongoja kwa fimbo na ingawa alikuwa na mguu mmoja lakini aliweza kwenda upesi sana. Mtu huyo alikuwa mrefu sana na mwenye nguvu. Tena alikuwa mcheshi.

Basi nawaambia kuwa hiyo siku ya kwanza niliposikia habari za huyu John Fedha mrefu, nilishuku kuwa ndiye yule aliyetajwa na Mzee Kapteni, lakini nilipomwona nikatambua kuwa siye; maana nilikwisha muona yule mzee Kapteni na yule Mbwa Mweusi, na yule kipofu Piu, nikaona sasa nawajua maharamia namna walivyo, hata nilipomuona huyu, nikamuona katika namna nyingine kabisa, kwa kuwa alikuwa amevaa nguo safi na tena ni mcheshi.

Basi nikajipa moyo, nikaingia ndani na kumuuliza kama yeye ndiye John Fedha, akajibu, "ndiye." Basi nikampa ile barua kusoma kisha akanishika mkono, akasema, "Wewe ni msaidizi wangu katika safari hii, nami nimefurahi sana kuonana nawe."

Basi palepale mgeni mmoja akaondoka kwa haraka sana, akatoka nje. Nami nilikuwa nimekwisha muona. Kumbe alikuwa ni yuleyule Mbwa Mweusi! Basi mara nilipomtambua nilipiga kelele, "Huyo! Huyo Mbwa Mweusi huyo! Mkamateni, mkamateni Mbwa Mweusi!"
Basi wakatoka wengine kujaribu kumkamata wasiweze. Yule John Fedha akauliza, "Je, huyo ni nani?"
Nikamueleza habari zote zilizotokea katika nyumba yetu, na kuwa huyo ni mmoja katika maharamia waliokuja kufanya ghasia katika nyumba yetu.

Basi aliposikia hayo akageuka na kuwauliza wale wageni,

“Nani aliyekuwa akiongea na mtu yule?”
Mmoja wao akajibu, “kwa nini?”
Jan Fedha akamuuliza, “kwani wewe umepata kumwona yule kabla ya hii leo?”
Akajibu, “La! sijapata”
Akasema “wala hujui jina lake, sivyo?”
Akajibu, “Ndiyo silijui kabisa jina lake.”
Basi kumwona yule mbwa mweusi mle ndani ya nyumba, shaka ile niliyokuwa nayo mara ya kwanza ikanirudia kwa nguvu, nikamtazama sana yule John Fedha, lakini kwa namna alivyoshughulika kupeleka watu kumtafuta kwa bidi, ni kawa shaka imenipungua moyoni.

Basi ghasia zilipotulia kidogo akaniambia tufuatane pamoja tukaondoka tukashika njia. Humo njiani akanisimulia Habari nyingi za meli na namna za kazi za melini na Habari za nchi mbali mbali, na maongezi yake yalikuwa matamu, nikasahau yale niliyokuwa nikishuku.

Hata tulipokwisha fika tukaambiwa kuwa siku ile ile saa kumi jioni lazima wote tujipakie melini ili tuwe tayari kutoka bandarini asubuhi na mapema.

SURA YA NANE : BARUTI NA BUNDUKI


Meli yetu ya Hispaniola ilikuwa imetia nanga bandarini nasi tukaingia mashuani tukaenda mpaka kwenye ngazi ya meli, tukapanda melini. Ndipo nilipoona kuwa kati ya nahodha na bwana Treloni liko neno. Nahodha alikuwa mtu mkali na alikuwa mtu wa kukasirika na baadaye kidogo baharia mmoja akaja akamwambia bwana Treloni kuwa ametumwa na nahodha kuomba nafasi ya kusema naye.

Basi mara nahodha mweyewe akatokea na bwana Treloni akamuuliza, “Je nahodha Smolet, wataka kuniambia nini? Natumaini kuwa mambo yote yanakwenda sawa?”
Nahodha akasema, ni afadhali niseme wazi wazi nisifiche neno hata moja. Na kwa hivyo sina budi kukwambia kuwa safari hii siipendi, wala mabaharia siwapendi, hata yule nahodha msaidizi simpendi, basi kwa ufupi ndio haya ninayotaka kukwambia.”

Hata alipokuja bwana Levesi akaona kuwa hawa watavumbua ugomvi kama asipowatuliza, basi akajitia kati, akasema, “wewe bwana nahodha umesema maneno ya kubania bania. Mimi pia nataka kujua maana ya maneno uliyosema, kwanza umesema safari hii huipendi, kwa nini?”
Nahodha akajibu, “mimi nilipokubali safari hii niliambiwa kwamba mahali tuendapo ni siri, na amri zenyewe zilitiwa katika bahasha na kutiwa mhuri mpaka siku za mbele. Basi mimi sikukataa, ila sasa naona kuwa hata mabaharia wanajua Habari zote, tena japokuwa mimi ni nahodha lakini sijaambiwa Habari yoyote. Basi nakuuliza kuwa hii ni haki? Pili nimesikia safari hii ni ya kwenda kutafuta hazina; hayo nimeyasikia kwa mabaharia wakisemezana wenyewe kwa wenyewe. Basi naona kuwa safari za kutafuta hazina ni hatari, hasa zinapokuwa za siri.”
Bwana Treloni akakasirika akasema, “Mimi na labda hata meli huipendi, na mimi mwenyewe pia?”
Nahodha akasema, Hasha hayo mimi siwezi kusema maana sijaona kazi ya meli hii, lakini nikitazama naona kuwa ni meli nzuri,”
Bwana Daktari, Livesi akasema, “Tena ulisema kuwa huwapendi mabaharia. Je, kwani hawajui kazi zao?”
Nahodha akajibu, Hasha, siwapendi tu, kwani ni desturi ya nahodha mwenyewe kuwachagua mabaharia wake.”
Bwana Livesi akajibu, “kweli tumekosa, maana hatukujua desturi hii, basi tuwie radhi. Tena ulisema kuwa humpendi nahodha msaidizi tuliemchagua; kwa nini?”
Nahodha akajibu,” kweli simpendi maana nimeona anaongea na kunywa pombe pamoja na mabaharia, na hii si desturi kabisa, maana yeye ni mkubwa hafai kuzungumza kabisa na wadogo zake.”
Basi bwana Livesi akamuuliza, “ je ni hayo tu uliyonayo moyoni?”
Nahodha akajibu, mmemsikiliza kwa Subira nyingi na sasa zidini kunisikiliza. Naona mabaharia wameweka akiba yetu ya baruti na bunduki katika ngama ya gubeti, basi mimi naona afadhali kuziweka katika ngama iliyo chini ya shetri. Tena nimepata Habari kuwa wale watu wenu wanne mliokuja nao wamewekewa walale katika gubeti moja Pamoja na mabaharia wengine. Mimi naona heri wangepata nafasi pembeni ya shetri. Tena neno moja lingine, nimeambiwa mnayo ramani ya kisiwa tena ina alama zilizoandikwa kwa kuonyesha mahali ilipofichwa hazina, na kuwa njia ya kufuata ni hivi na hivi, (akataja majira) basi simjui aliyetoa Habari hii, ila neno moja nataka kusema, “yaliyopo kwenye ramani hiyo yanatakiwa kuwa siri hata kwangu na nahodha msaidizi, kinyume na hapo najiuzulu unahodha.”

Basi Bwana Livesi akasema, “sasa nafahamu barabara kuwa unataka tufiche Habari, na tena kufanya shetri ya meli iwe kama boma na kuweka humo baruti na bunduki zote, je, unataraji uasi nini?”
Nahodha akasema, “siwezi kusema ivyo maana kama ingekuwa ivyo nisingeweza kukubali safari hii. Lakini mimi ni nahodha tu, na kazi yangu ni kuweka kila kitu salama niwezavyo.”
Basi akaondoka huku nyuma Bwana Treloni na Bwana Livesi wakazidi kuongea kidogo. Bwana Livesi akasema, “Treloni, nadhani tumebahatika kupata watu wawili hawa wenye heshima na busara huyu nahodha na yule John Fedha mrefu.”
Bwana Treloni akajibu, naona kuwa John Fedha ni mtu wa heshima lakini huyu nahodha nadhani vitendo vyake havistahili mtu mzima mwenye heshima na mwenye ujuzi na kazi yake.”

Basi tukaja juu tukaona kuwa watu wamekwisha kutoa baruti na bunduki, wameziweka chini ya shetri, na nahodha na yule nahodha msaidizi wanasimamia.
Basi walipokuwa wakishughulika kufanya kazi hii, akaja John Fedha, na alipowaona wanavyofanya akawauliza, “Je, mwafanya nini?”
Mmoja wao akajibu ”tunahamisha baruti na bunduki.”
Akajibu, Lo! Tukifanya hivi tutachelewa kuondoka.
Mara nahodha akatokea kumwamrisha aende chini jikoni akafanye kazi yake. John Fedha akatoa saluti akaenda zake, sasa nahodha akaniona mimi nimesimama bure, mara akanigeukia akasema, “na wewe nenda ukafanye kazi yako ya kumsaidia mpishi, mimi sipendi kuona umesimama bure bila kazi; haya nenda!”
 
Mambo ya Bujibuji haya, akianzisha hadithi anaweka yote, no need to say TO BE CONTINUED
 
SURA YA TISA: SAFARI BAHARINI

Basi usiku ule ikawa kushughulika kutengeneza kila kitu tayari kupakia melini, na marafiki za mabwana hawa wakaja kuwaaga. Ingawa nilichoka sana baada ya kumaliza kazi, sikuweza kushuka chini nikasimama sitahani kutazama mambo yanavyokwenda.
Watu walipokuwa wakifanya kazi, mmoja wao akasema, “Haya jamaa tuimbe, na tujitie moyo.” Mara wakaanza kuimba wimbo ule ule uliokuwa ukiimbwa na maharamia;

‘Watu kumi na tano Yo-ho-ho-ho.
Juu ya sanduku la mfu Yo-ho-ho-ho.
Na chupa ya mvinyo Yo-ho-ho-ho.’

Basi niliposikia wimbo huu nikaanza kufikiri mambo haya yote yalivyoanza, nikawa kama nimuonaye tena machoni mwangu yule Mzee Kapteni. Mara wakaanza kung’oa nanga na matanga kutweka, hata yalipoanza kushika upepo safari ikaanza tukatoka mlangoni, ndipo nilipopata usingizi. Huu ndio mwanzo wa safari yetu kwenda kutafuta hazina.

Siwezi kuhadithia mambo yote yaliyotokea katika safari hii, ila yatosha kusema kuwa safari yetu ilikuwa nzuri. Meli ilikuwa na mwendo, na mabaharia nao walikuwa Hodari wa kazi yao na manahodha pia walikua Hodari zaidi. Lakini kabla hatujafika kwenye kisiwa cha hazina yalitokea mambo ambayo sina budi kuyasema. Kwanza yule nahodha msaidizi, Aro alikuwa kama nahodha mkuu alivyombashiri. Alikuwa hana amri kabisa na watu hawakumwogopa hata kidogo. Lakini haya si yote, kabla hazikupita siku nyingi, alionekana na macho mekundu na ulimi hautamki maneno vizuri na ishara nyingine za ulevi. Mara nyingi ilimlazimu kwenda chini katika shetri kwa sababu ya kulewa, pengine alianguka na kujiumiza, na pengine alilala mchana kutwa hajiwezi kabisa.

Hapana mtu aliyejua mahali alipatia ulevi huo, maana ulevi wote tuliokuwa nao melini ulikuwa ukitolewa kidogo kidogo, na akiulizwa kitu alichokunywa yeye hucheka tu, na kusema kwamba amekunywa maji tu!
Basi kwa hivyo alikuwa akiwashawishi mabaharia kufanya mambo yasiyofaa wala hakufaa kwa kazi ya nahodha msaidizi. Hata siku moja usiku akatoweka wala hakuonekana tena, tukasema kuwa labda katika ulevi wake ametumbukia baharini.

Sasa tukawa hatuna nahodha msaidizi, na kama ilivyo desturi serahangi mmoja akapandishwa cheo akapewa kazi yake; na jina la serahangi huyo lilikuwa Ayubu. Mtu mmoja katika mabaharia jina lake Israel Hands, alikuwa hodari sana katika kazi yake, na tena alikuwa msiri wa John Fedha na kila mara walikuwa wakizungumza Pamoja.

John Fedha, yaani mpishi wetu, au kama alivyoitwa na wenzake ‘Babekiu’ alikuwa mtu wa ajabu sana kwa namna alivyokuwa akiweza kuzunguka melini kwa mguu mmoja na fimbo yake, ijapokuwa meli mara nyingine ikienda mrama sana. Mabaharia wote walimstahi sana na kumtii.
Jiko lake siku zote lilikuwa safi kabisa, na jikoni alikuwa na tundu lililokuwa na kasuku. Pengine aliniita na kunikaribisha vizuri, akisema ‘’njoo hapa, Hawkins nikusimulie visa mbalimbali na hadithi. Kaa umsikilize kasuku wangu jina lake Kapteni Flinti, akibashiria vyema safari yetu.”

Basi yule kasuku kila aliposikia jina lake kutajwa mara alianza kulia, “vipande vya dhahabu, vipande vya dhahabu!” Hakunyamaza mpaka tundu lake lilipofungwa kwa kitambaa.
Basi yule Babekiu akaeleza kuwa yule kasuku amesafiri sana Pamoja naye, basi alijifunza maneno yale alipoona watu wakitoa vipande vya dhahabu katika meli zilizozama baharini.

Watu waliandaliwa vizuri na hasa chakula kilikuwa kizuri sana. Pipa moja la machungwa liliwekwa stahani na kila mtu aliyekuwa akitaka alikuwa akienda kuchukua. Bwana nahodha hakupenda desturi hii, akasema, “si vizuri kuwabembeleza mabaharia namna hii, wataharibika.”
Lakini pipa lilitokea kuwa la msaada sana, kwani kama lisingewekwa hapo stahani tusingalijua yanayotokea, na kwa hivyo tungaliangamia sote. Ilikuwa hivi :
Tulikuwa tumekaribia kisiwa cha hazina, na sote tulikuwa tumefurahi kufika nchi kavu tena, basi nilipokwisha maliza kazi yangu nilitamani kula chungwa nikaenda kuchukuwa moja, basi kwa kuwa pipa lilikuwa kubwa na machungwa yamebaki machache, tena chini kabisa, nikaingia ndani ya pipa ili nichukue moja. Basi nilipoingia, sijui kwa nini, nikashikwa na usingizi na kulala lakini kabla sijapitiwa na usingizi, nikasikia mtu akikaa kwa kishindo karibu. Hivyo nikaamka nikataka kutoka katika pipa, mara nikasikia sauti ya John Fedha, na nilipokwisha sikia maneno kadiri ya kumi hivi nikafurahi kujiona nimo ndani ya pipa, nikakaa kimya kabisa huku nikitetemeka kwa maneno niliyoyasikia.


SURA YA KUMI: NDANI YA PIPA LA MACHUNGWA

Kwanza nikasikia sauti ya John Fedha. Alisema, “Ndiyo Flinti alikuwa nahodha, na mimi nilikuwa mtu wa kutazama Habari za vyakula. Kishindo kile kilichompofua macho Piu ndicho kilichonikata mguu.”
Sauti nyingine alisema, “huyo Flinti alikuwa bora kuliko wengine wote.”
Basi John Fedha akajibu, “kweli lakini hata wengine nao walikuwa wanaume vile vile. Mimi hapo nilipokuwa nikisafiri pamoja na Flinti, nilipata kuweka akiba ya shilingi elfu ishirini, ambazo ninazo hata leo, wako wapi watu wa zamani wa Flinti? Wengi wamo humu humu katika meli hii.”
Basi niliposikia haya nikazidi kusikiliza, ndipo nilipomsikia John Fedha akisema, “Basi Habari za maharamia ni hivi; huishi kwa kuvumilia taabu nyingi, tena hunyongwa kama wakikamatwa, lakini hula chakula chema sana, na mwisho wa safari hupata fedha nyingi sana.
Wengi hupoteza fedha zao lakini mimi si kama hao, zangu naziweka na kama nikijaliwa kupata umri wa miaka hamsini nitaacha kazi nipumzike.”

Basi mara akaja mtu mwingine akauliza, “Je, tutaendelea namna hii kwa siku ngapi? Mimi nimechoka kabisa kuamrishwa na huyu nahodha; mimi nataka niingie katika shetri nile chakula cha mabwana pamoja na mvinyo wao.”
John Fedha akajibu, “wewe hufikiri! Lazima tuendelee kama tulivyoendelea sasa. Hatufanyi kitu mpaka dakika ya mwisho. Huyu nahodha tuliye naye anaweza kuongoza meli hii, na yule Bwana Treloni anayo ramani, na tena tunaye Bwana Daktari anaweza kututunza je, wataka nini zaidi? Basi fikra yangu ni hii. Kwanza tusubiri mpaka wakwishe kupavumbua mahali palipofichwa hazina, tena lazima wasaidie kuipakia, kisha sisi tutafanya la kufanya.”

Mmoja akasema, “Vema na hayo usemayo nayo kweli, lakini nani ajuaye kuongoza meli na majira yake? Na tena nyinyi hamwezi kuacha ulevi. Meli ngapi nimeziona zikipanda miamba? Na watu wangapi nimewaona wakinyongwa? Na hayo yote ni kwa sababu ya haraka haraka tu.”
Mtu mmoja akauliza, “Subiri tu; wakati ukifika patakuwa mauti tu; kwani hatutabakiza hata mtu mmoja, tutawauwa wote. Ila jambo moja nitakalo ni kumwua yule bwana Treloni na kumnyonga kwa mikono yangu mwenyewe. Haya nipe chungwa, naona kiu.”
Loo! Niliposikia maneno haya nikaogopa kabisa na laiti kama ningalikuwa na nguvu ningaliruka kutoka pipani kujiokoa nafsi yangu, lakini wapi! Miguu na moyo ulikuwa umepooza kabisa. Ndipo niliposikia mtu akiondoka na mara mtu mwingine akamshika akasema
“Acha upuuzi huo, ya nini kula machungwa na mimi ninao ufunguo wa ghalani kulimo wekwa mvinyo! Twendeni tukanywe mvinyo, kisha nikamsikia mwingine akimwambia John Fedha ya kuwa “hapana mtu mwingine atakaye kubali” ndipo nilipoamini kuwa hata sasa wapo wengine walio waaminifu.
Basi wakaletewa mvinyo wakaanza kunywa, na punde nikaona mwangaza,nikabaini kuwa mwezi umetoka; ndipo nilipomsikia mtu aliyekuwa akilinda zamu akinena, "nchi kavu! Nchi kavu!”
 
SURA YA KUMI NA MOJA: BARAZA LA VITA


Basi mara ikawa ghasia nyingi na wote wakakimbilia kutazama; nikaona nimepata nafasi ya kutoka mle pipani, nikazungukazunguka hata nikaona nimepata njia ya gubeti, nikawakuta wengine.
Kwa kusini tuliona vilima vidogo viwili na nyuma yake tuliona kilima kirefu zaidi. Na katika kuona kwangu hivi nikawa kama mtu ninayeota ndoto. Mara nikazinduka kwa kusikia sauti ya Nahodha akitoa amri zake kubadilisha majira. Akauliza “je kuna mmoja wenu aliepata kuona nchi hii?”
John Fedha akajibu, “Bwana mimi nimepata kuiona. Safari moja tulishuka hapa kupakia maji ya kunywa.”
Nahodha akasema, “nadhani mahali pa kutia nanga ni kule upande wa kusini, nyuma ya kisiwa kidogo, sivyo?”
Akajibu, “ndiyo kisiwa kile kinaitwa kisiwa cha mifupa, maana ndipo mahali walipopapenda maharamia zamani. Na kilima kile cha nyuma kinaitwa kilima cha Darubini kwa sababu kinafaa sana kutazama meli zinazopita.”
Basi nahodha akasema, “Njoo uitazame ramani niliyo nayo kama mahali hapa ndipo.” Basi akaenda kutazama, lakini hakupata aliyoyataka. Maana yeye alitamani kuona ramani yenye alama, kumbe sivyo, ilikuwa mpya isiyo na alama yote ila zile za majira ya mahali.

Mimi nilistahajabu alivyokiri kukijua kisiwa kile. Basi nahodha na Bwana Treloni na Bwana Livesi wakaondoka, nami nikawa nafikiri jinsi ya kupata nafasi ya kusema nao, na kueleza yote niliyoyasikia. Mara Bwana Livesi akaniita na kuniambia nikamchukulie tumbaku yake alioiacha sitahani. Nikaenda kuchukua tumbaku, niliporudi nikasema, “niwieni radhi mabwana, nataka kusema maneno yangu machache kwani nina Habari zangu za kutisha sana.
Nao walibaini kwa namna ya uso ulivyobadilika, wakajua ni habari nzito sana. Hata kabla ya kuwahadithia, Bwana Daktari akasema “Vema ahsante. Basi sasa rudi kazini,” Nami nikarudi.
Mara nahodha akapiga kifilimbi chake na mabaharia wote wakakusanyika. Akasimama mbele yao akasema, “Imekuwa kama siku kuu. Nimefurahi kwa namna ya kila mtu alivyofanya kazi yake na sasa mabwana wametoa ruhusa mfanye karamu na sisi tunafanya karamu yetu vile vile.” Basi watu wakafurahi sana na mabwana wale watatu yaani Bwana Treloni, Bwana Livesi na nahodha, wakashuka chini katika shetri na baadaye kidogo wakatuma mtu kuja kuniita.

Hata nilipokwenda nikawakuta wamekaa mezani, na Bwana Treloni akaniuliza, “je, Hawikins, unayo maneno utakayo kutwambia?”
Nikaitikia, “Ehe,”
Akasema, “twambie “twambie,” Basi nikawaambia yote niliyoyasikia nilipokuwa mle ndani ya pipa, kisha wakaniambia nikae nikakaa.
Basi bwana Treloni akanena, "bwana nahodha, maneno yako uliyoyasema zamani yamekuwa kweli na mimi nakiri kuwa nimekosa. Sasa niko chini ya amri yako.”
Nahodha akajibu, Bwana hata mimi ninastaajabu, maana hawakuonesha hata dalili ya uasi. Lakini maadam sasa tumepata habari lazima tushauriane, kwanza hatuna budi tuendelee na safari yetu kwa sababu hatuwezi kurudi nyuma. Na nikitoa amri ya kurudi ndipo wataasi upesi zaidi. La pili, tuna nafasi kwa sababu wamesema kwamba watatuachilia mpaka tuivumbue hazina. La tatu naamini kuna wengine walio waaminifu. Basi naamini kwamba vita vitatokea sasa au baadaye; na fikra yangu ni hii; yani tuwe tayari, yaani siku moja wanapokuwa wamepoa bila kutarajia hujuma yoyote ni afadhali sisi tuanze kuwapiga wao. Wadhani kuwa wale watu uliowaleta wewe bwana Treloni watakuwa waaminifu?”

Akajibu, “kama mimi mwenyewe. Basi tutakuwa sisi watatu na watatu wengine na huyu Hawkins; tutakuwa saba waaminifu. Sasa lazima tusubiri tu kungojea wakati unaofaa.”
Bwana Livesi akasema, “Huyu Hawkins anaweza kutusaidia kuliko wengine wote. Maana mabaharia hawamwogopi, naye ataweza kupata Habari za mipango yao.”
Basi mimi nikajiona nimo katika shida kabisa, nikajiona sina nguvu hata kidogo, ingawa ilikuwa kwa bahati yangu tulipata Habari za hatari hii. Basi katika jumla ya watu ishirini na sita wako saba tu, na mmoja ndiyo mimi kijana mdogo tu, tunaoweza kuwaamini. Na upande wao wamepata wote waliobaki, yaani watu wazima kumi na tisa.

SURA YA KUMI NA MBILI: MAMBO YALIYONIPATA PWANI.

Asubuhi nilipoamka nikatazama kisiwa nikaona kwa namna nyingine kwa jinsi ukungu uliivyokibadili. Kile kilima kilichofunikwa na wingu isipokuwa juu tu kikawa kinaonekana kama kisiwa cha wafu. Moyo wangu ukawa mzito sana, nikaona kuwa hiki ni kisirani, nikaanza kujuta kuja katika safari hii.

Basi ikawa kazi kubwa sana kufika nchi kavu kwani upepo ulitulia kukawa shwari, kwa hiyo ikawa kazi kubwa kuvuta makasia. Watu wakaanza kunung’unika nikafahamu kuwa kwa kuona tu kisiwa wameanza kuingiwa na uasi, nao walikuwa tayari kutuulia mbali, kila amri iliyotolewa walitii lakini kwa nyuso za kukasirika, Ila John Fedha alikuwa akijaribu kuwatia moyo nayeye naye alikuwa akitii upesi na kwa furaha. Mwisho nahodha akamwambia Bwana Livesi, “naogopa kutoa amri nyingine isije vikatokea vita.” Kisha akafikiri sana mwisho wake akasema, Bwana waona sasa naogopa kutoa amri hata moja, maana watu wote wa tayari kuniasi, na wakiniasi basi vita tayari. Nikiwakaripia kwa sababu ya ulevi wao vile vile itaanzisha vita, na nisipowakaripia wafahamu pia ninawaogopa. Basi tumtumainie mtu mmoja tu.”

Bwana Treloni akauliza, “mtu gani huyo tunaemtumainia?”
Nahodha akajibu, “John Fedha. Maana hivi sasa yeye hataki uasi kwa kuwa hajapata nafasi ya kutengeneza mambo yake, nadhani kama tukiwapa nafasi ya kufanya mkutano, John Fedha ataweza kuwatuliza. Basi ni afadhali tuwape ruhusa ya kupumzika ifikapo mchana, na kama wakienda zao pwani sisi tutapigania ndani ya meli yetu, kama hawaendi zao, itakua shauri ya kupigana shetrini tukiwa. Lakini ikitokea wengine wamebaki basi John Fedha ataweza kuwarudisha wamekwisha kutulia.”

Basi wakakubali hivi, sasa ikawa kuwapa wale tuliowaamini kila mtu bastola, tena tukawaeleza habari za uasi tunaoutarajia, nao wakatii amri bila kusita.
Kisha Bwana nahodha akawakusanya mabaharia wote akawaambia, “Leo mmefanya kazi katika mazingira ya joto, na labda mmechoka. Basi sasa natoa ruhusa kwa wote wanaotaka kwenda pwani kutembea waende, na nusu saa kabla ya jua kuzama nitapiga bunduki kuashiria muda wa kurejea.”

Nadhani wale mabaharia walifikiri kuwa mara wakifka pwani, wataikuta hazina tayari, kwa namna walivyopokea Habari hizi; wakafanya ghasia na kelele katika haraka yao ya kufika pwani kwa mashua, basi wakatoka wakaenda zao pwani.

Basi bwana Nahodha alipokwisha kutoa ruhusa, akaondoka pale kusudi asiwasikie maneno ya uasi wanayosemezana wenyewe. Akamwachia John Fedha amalizie kutoa amri zote na kuwapeleka pwani.
Wote walishuka pwani, ila John Fedha akaacha watu sita melini, nikabaini kuwa watu sita hawatakuwa hatari kwa mabwana hivyo hawata hitaji msaada wangu. Hapo nikafanya jambo la ajabu, jambo ambalo lilitusaidia kuokoka. Nikashikwa na hamu ya kushuka pwani. Mara nikateremka tayari katika mtumbwi iliyokuwa tayari kutoka, nikaingia ndani yake nayo mara ile ukaondoka. Hakuna aliyejali uwepo wangu kasoro mtu mmoja tu aliyeuliza, "ni wewe Jim? Hakikisha huinui sana kichwa." Lakini John Fedha aliyekuwa kwenye mtumbwi mwingine aliniona na akataka sana kuhakikisha kuwa ni mimi, hadi aliniita. Hapo nilijutia uamuzi wangu wa kuja pwani. Loo! Walivuta makasia kweli kweli, na mtumbwi wetu ulikuwa mwepesi hivyo uliwahi kufika pwani kuliko ile mingine. Nikashuka na kutokomea vichakani, huku nyuma nilimsikia John Fedha akiita, "Jim, Jim." Lakini sikusimama, nikakimbia hadi nilipochoka.


SURA YA KUMI NA TATU: PIGO LA KWANZA


Nilipokwisha pumzika kidogo nikaanza kutembea tembea kutazama kisiwa namna yake. Nikapita katika pori kubwa nikaona nyoka wengi na maua makubwa ya ajabu mno. Nilipokwisha nikatokea mahali penye kinamasi, na baada ya kutembea tembea kidogo nikasikia sauti nikabaini kuwa wale mabaharia wengine wako karibu. Nikatambaa chini chini mpaka nikafika kwenye mti mkubwa nikajificha. Nilipotua kidogo kutazama nikamwona John Fedha na mtu mwingine wanaongea. John Fedha akasema, “Rafiki mimi nakupenda sana, na kama nisingekupenda usingeweza kutenda kitu, sasa mambo yote yangekwisha, tena nakwambia kama si mimi ungeuawa upesi.”
Yule mtu akajibu, ‘Fedha, wewe mzee tena mwenye akili zako; mbali ya hilo una fedha nyingi, tena nadhani Hodari. Je, mbona umekubali kuvutwa na hawa watu waovu? Mimi nasema nina hiyari kuuawa kuliko kuwaasi mabwana zangu.”
Basi mara tukasikia kishindo, wakanyamaza. Nikatambua kuwa huyo ni mtu mmoja wao wale waaminifu. Mara nikasikia ya mtu mwingine kama yeye, maana nilisikia sauti ya ghadhabu, sauti ya mtu akilia kwa maumivu na mwisho wake nikasikia sauti kali sana, kisha kukawa kimya. Mara yule mtu aliposikia sauti hii akaruka na kuuliza, "ni nani huyo?" John Fedha akajibu, "nadhani ni Alan amekataa kuasi." Yule mtu akasema, " umemuua Alan? Na mimi niue kama mbwa lakini siwezi kuasi." Aliposema hayo akageuka na kuanza kuondoka kuelekea ufukweni. Lakini kabla kajaenda mbali, mara John Fedha akatwaa gongo la mti na akampiga kwa nguvu sana, likampiga shingoni, akaanguka pale pale. Kabla ya kupata nafasi ya kuinuka John Fedha alimrukia akampiga kisu mgongoni mara mbili, nami nikajua kuwa amekwisha kufa. Basi John Fedha akakifuta damu kisu kwa majani, kisha akapiga kifilimbi chake, nikatambua kwamba anawaita watu wake.

Mradi nikajiona nimo katika hatari ya kuonekana, nikazidi kujificha. Mara wakaja mabaharia kutoka katika kila upande, nikaogopa sana, nikafikiri, Ehe, nitawezaje kurudi melini Pamoja nao, nahodha akipiga bunduki? Maana nimewaona wakiua, nao labda wakiniona na mimi wataniua tu. Basi nikatoka hapo nilipojificha nikaanza kukimbia sijui wapi, mradi niwe mbali tu na mabaharia wale wabaya. Nilipofika mbali kidogo nikasimama kupumzika, na hapo nikaona kitu kilichonitisha kabisa na moyo ukanipiga kwa woga.
 
Back
Top Bottom