Kisa chenye kujifunza: Wosia wa baba

Slim5

JF-Expert Member
Jan 7, 2014
28,108
37,643
KISA CHENYE MAFUNZA

C n P.

Wosia wa baba.

Kuna bwana mmoja muumini aliyekua na hekima na busara, Mola alimjaalia utajiri mkubwa na alikua akiishi na watu vizuri. Kila mtu alikua akimtaja kwa wema na ukarimu. Alipofika umri wa utu uzima alianza kuandamwa na maradhi yasiyokwisha na hatimae akawa anadhoofu siku hadi siku, Hekima yake ilimtuma awaite watoto wake na kuanza kuwausia juu ya maisha gani waishi baada yake.

Aliwausia kila mmoja peke yake na kuwaweka wazi kuwa anaona kama anakaribia kufika mwisho wa maisha yake, Kila siku kaburi linazidi kumsogelea na umri unakatika huku maradhi yakimzidia. Watoto wake walihuzunika sana wakakosa amani.

Baba aliwataka wanawe wote waondoke na abaki na mtoto mmoja mkubwa, walipotoka wote alimwambia mwanangu inama kidogo nikupe wasia wangu, Mtoto aliinama akisikiliza kwa makini sauti ya baba yake iliyokua ikisisikika kwa chini na yenye mkwaruzo kwa kuzidiwa na maradhi, Baba akasema: “Mwanangu wosia wangu kwako ni usimamie mazishi yangu, watakapo nikosha kabla ya kunivika sanda chukua soksi yangu yeyote ya zamani univishe katika mguu wangu wa kushoto”.

Baada ya muda baba aliaga dunia na vilio vikatawala.
Watu walijaa kuja kutoa pole familia na kuanza taratibu za maziko, familia ilimteua mmoja wa Maimamu awe kiongozi katika kuosha maiti na kutengeneza sanda, walipomaliza kuosha kijana alikumbuka wosia wa baba yake, akaenda kuchukua soksi ili aipeleke kabla sanda haijafungwa, akamwambia Imamu samahani baba aliusia avalishwe soksi moja kabla hajatiwa sandani baada ya kukoshwa. Imam kwa mshtuko alimjibu kijana kwa upole kuwa haiwezekani japo wosia wa marehemu unahifadhiwa, huyu hapaswi kuvishwa chochote zaidi ya sanda, kijana machozi yakimmwagika aliendelea kuhimiza wosia wa baba yake na kukatokea mzozo, wanasema avalishwe wengine asivalishwe. Imam akasema wamtafute Sheikh mtaalamu wa sheria za dini ilia atoe maelekezo, Sheikh alitafutwa na kuletwa msibani akawatuliza vijana na kuwaeleza kuwa wosia wa marehemu huwa unafatwa lakini si kila mahala, Marehemu hawezi valishwa soksi kwa kuwa si sehemu ya sanda.

Kuna mzee jirani yao alisimama na kumfata kijana wa marehemu, akamwambia Baba yako alinipa barua nikupe kabla ya mazishi, kijana akaipokea huku anatetemeka akaifungua na barua yenyewe ilikua inasomeka hivi:
“Mwanagu umeshuhudia mzozo ulipotaka kukamilisha wosia wangu, hawakukuruhusu kunivisha japo soksi moja tu tena ya zamani, nimekuachieni mali nyingi na sasa ni za kwenu tambueni kuwa siku mtakapoondoka duniani hamtavishwa hata soksi na wala hamtoondoka na mali yeyote zaidi ya sanda zenu, hivyo mcheni mola wenu na tumieni mali hizo katika njia inayomridhisha yeye”.

Hili ni somo kubwa sana, tujitahidi kuwa wema na kujiondoa kwenye gereza la umimi, ubinafsi na tuishi na watu vizuri, mali zetu sii kitu bali ubinadamu wetu ndio wenye thamani kuliko mali zenyewe.
 
Kwakua ni simulizi sawa. kwa imani yangu hata akitaka kuzikwa Na kibuyu cha mbege hamna wa kupinga.ndio maana kiongozi mmoja juzi mila kwanza hayo mengine baadae
 
Hosia huu Naomba uwafae matajiri mabinafsi na Binadamu wote wenye kudharau wenzao kwa nyadhifa au Mali walizonazo Tulikuja Duniani tu uchi tulipozaliwa na Siku ya mwisho tutaenda hivyo hivyo kuishi kwa kutendea wengine wema ndio thawabu ya pekee
 
Back
Top Bottom