Kisa Cha Yusuf Athumani Marsha, Peter Mbimbwo na Julius Nyerere Mwanza 1950s

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
17,755
24,963
KISA CHA YUSUF ATHUMANI MARSHA, PETER MBWIMBO NA JULIUS NYERERE MWANZA 1950s

Tuanze na Peter Mbwimbo.

Peter Mbwimbo ameandika kitabu, ''Peter D. M. Mlinzi Mkuu wa Mwalimu Nyerere.''

Wakati TANU inaundwa na harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika zinaanza Peter Mbwimbo alikuwa katika kikosi cha
Special Branch.

Kazi ya Special Branch kama makachero wa wakoloni ilikuwa kuwachimba wapigania uhuru kutaka kujua mipango yao dhidi ya Waingereza na kuizima au kuivuruga kabisa.

Hiki kikosi kilikuwa kinaogopewa sana na TANU.

Peter Mbwimbo alikuwa Mwanza, Kanda ya ziwa ambako harakati za kudai uhuru zilikuwa kwa hakika zimeshamiri chini ya uongozi wa wazalendo kama Paul Bomani na Saadan Abdu Kandoro.

Upande wa pili Bukoba Ali Migeyo alikuwa anawasha moto mkali dhidi ya Waingereza kiasi kupelekea kupigwa mabomu, kukamatwa kushtakiwa na kufungwa jela ya Butimba Mwanza.

Sasa tuje kwa Yusuf Athumani Marsha.

Yusuf Athumani Marsha alikuwa mmoja wa wana TANU mstari wa mbele na kijana maarufu hapo mjini Mwanza.

Yusuf Athumani Marsha anakumbukwa kwa uhamasishaji wake uliojaa shamrashamra.

Nimemfahamu Mzee Marsha akiwa mtu mzima katika miaka ya 1980 akiishi kwenye jumba lake la fahari Mtaa wa Nyamwezi kona na Faru.

Miaka hiyo Mtaa wa Nyamwezi nyumba iliyokuwa ya gorofa ni hiyo ya Mzee Marsha peke yake.

Nyumba hii ilikuwa ya muungwana wa Kimanyema, Hakimu wa Mahakama ya Kariakoo, Nassor Kiruka na yeye nyumba hii aliwapangisha African National Congress (ANC) maarufu wakijuikana kwa jina moja, ''Congress,'' President wake Zuberi Mtemvu, mahasimu wakubwa wa chama cha TANU.

Miaka ile mtu akikuita wewe ni Congress maana yake anakuita wewe ni msaliti adui mkubwa wa Watanganyika.

Wenyewe hawakujali wakijiita, ''Congress Mwamba usiovunjika.''

Nakumbuka siku moja tuko Mtaa wa Lindi nyumba aliyokuwa akiishi Bi. Mruguru bint Mussa mama yake Ally Sykes kabla ya kufariki mwaka wa 1974.

Tulikuwa mazikoni.
Bi. Mariam shangazi yake Ally Sykes amefariki.

Zuberi Mtemvu na Ally Sykes tukiwa pale tumekaa katika majamvi wakaanza kutaniana na kuchokozana.

Zuberi Mtemvu anaisema vibaya serikali ya Nyerere watu wanasikiliza wanacheka.

Mara Zuberi Mtemvu kamnyooshe kidole Ally Sykes huku anacheka kile kicheko cha kebehi na ushabiki anawaambia watu, ''Huyu Ally na marehemu kaka yake Abdul na Nyerere walikuwa wanakifanyia fitna chama changu Congress kife.''

Bwana Ally kageuka kaikumbuka TANU yake na marehemu kaka yake Abdul na Nyerere anamwangalia Mtemvu anamwambia, ''Kumbe nyinyi Congress bado mpo sisi tulidhani tumekumalizeni.''

Likatoka jibu kwa mbali pembeni ya jamvi nyuma kabisa, ''Bwana Ally sikiliza, ''Congress ni mwamba usiovunjika.''

Vikaanguka vicheko kila pembe.

Mzee Marsha akiendesha Mercedes Benz nadhifu rangi ya njano na nathubutu kusema kwa ufahamu wangu kuwa kwa wakati ule alikuwa yeye, Hamza Kassongo na Ally Sykes Waafrika pekee katika mji wa Dar es Salaam waliokuwa wanapanda Mercedes Benz.

Hizi gari aina ya Benz zina historia yake katika mji wa Dar es Salaam.

Katika miaka ya 1960 hata kabla ya uhuru wa Tanganyika kulikuwa na vijana wawili Dar es Salaam waliokuwa wakiendesha Mercedes, Abdulwahid Sykes na Abbas Abdulwahab.

Turejee miaka ya 1950.

Nyerere amekwenda Kanda ya Ziwa yuko mjini Mwanza amekaa na Yusuf Athumani Marsha bila shaka ofisi ya TANU wanazungumza na hapo walipo walikuwa wanaweza kumuona kila apitae nje.

Peter Mbwimbo akapita na Yusuf Athumani Marsha akamuona.
Yusuf Marsha akamuita aje pale walipo.

Kwenye kitabu chake Peter Mbwimbo anaeleza yaliyopitika pale ndani siku ile.

Mbwimbo anasema Mzee Marsha akamfahamisha Nyerere jina lake na kazi anayofanya.

Ni wazi kuwa Mbwimbo alihisi fedheha kutambulishwa kama kachero wa Special Branch wanaomwinda Nyerere na wana TANU usiku na mchana.

Mwalimu kwa utaratibu baada ya kumsikiliza Bwana Marsha na mazungumzo mengine akamuomba amruhusu Mwimbo kuendelea na shughuli zake akisema bila shaka yuko kazini asipoteze muda wake pale.

Mwimbo akashika hamsini zake akaondoka mahali pale.

Yusuf Athumani Marsha ni mmoja katika ya wazalendo wengi ambao michango yao katika kupigania uhuru wa Tanganyika haifahamiki.

Baada ya kumsoma Mzee Marsha katika kitabu cha Peter Mwimbo nikawa natafuta historia ya Mzee Marsha pamoja na picha zake wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.

Leo baada ya kipindi kirefu kupita nimebahatika kuletewa picha za Yusuf Athumani Marsha na mmoja wa watoto wake.

Picha hizo nimeziweka hapo chini ili sote tufaidi.
Narejea tena kwa Peter Mwimbo.

Ukisoma kitabu cha Mwimbo utashangazwa na mapenzi aliyonayo kwa Julius Nyerere.

Kila anapolitaja jina lake kitabuni patafuatia maneno ya heshima kubwa kumwadhimisha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Sijapatapo kumsoma mwandishi anaeandika namna hii.
Hakika ukoloni una changamoto zake.

Mwimbo kachero aliyekuwa anamwinda Nyerere na wale aliokuwanao katika TANU akaja kuwa anampaenda Nyerere na mlinzi wake.

Ukikisoma kitabu cha Peter Mwimbo utapata yakini bila ya chembe ya shaka kuwa kama mlinzi wa Mwalimu Nyerere, Mwimbo alikuwa tayari kujitolea maisha yake na kwa lolote kunusuru maisha ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Katika kitabu chake Mwimbo anaeleza namna alivyofanikiwa kumtorosha Mwalimu Nyerere kutoka Ikulu na kwendanae mafichoni kusikojulikana baada ya maasi ya Tanganyika Rifles mwaka wa 1964.

Maelezo ya Mwimbo yamepishana na maelezo niliyopewa na Mzee Kitwana Kondo ambae kama Mwimbo na yeye alikuwa Special Branch wakati wa ukoloni.

Napenda kuhitimisha na Mzee Marsha.

Mzee Marsha nilimfahamu kwa karibu kupitia rafiki yangu marehemu Said Ibrahim ambae walihusiana kwa nasaba.

Hivi ndivyo nilivyoweza kupata fursa ya kuingia nyumbani kwake na kuijua familia yake.

Kwenye nyumba yake ukumbi wake alipokuwa anakaa na kupokea wageni wake ulikuwa juu gorofani na ukuta mzima ulijaa picha zake wakati wa harakati za TANU za kudai uhuru akiwa Mwanza na kwengineko.

Mzee Marsha akipenda kusali Msikiti wa Shadhli ambao ulikuwa jirani na nyumbani kwake ingawa angependa angeweza pia kusali Msikiti wa Makonde.

Alikuwa na kawaida ya kusali sehemu maalum habadilishi kiasi naamini wenyeji wa msikiti ule walipakwepa kukaa hapo wakiamini kuwa mwenye nafasi yake atatokeza wakati wowote.

Mzee Marsha alikuwa akiingia msikitini moja kwa moja atakwenda kwenye saa ya msikiti kupiga funguo.

Saa hii ilikuwa sawa sawa na sehemu anaposimama yeye kusali.
Miaka ile saa za umeme zilikuwa bado hazijashika.

Akimaliza kutia saa ufunguo na kurekebisha majira na saa yake ya mkononi atasimama kusali suna kisha atakaa kusubiri sala.

Mzee Marsha alikuwa mtu wa maskhara sana.
Tukifika nyumbani kwake kikawekwa chakula mezani basi atatukaribisha tule.

Ukisema umeshiba atakubembeleza ule hata kidogo.

Ukiendelea kuwa mkaidi utamsikia anasema, ''Mimi sikuiteni kulima nakuiteni tule chakula kama hamtaki basi.''

Hii ndiyo namna ya watu waliomzunguka Julius Nyerere wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.

Inasikitisha kuwa leo hii hakuna anaewajua si majina yao wala kama kweli watu hawa walipata kuwapo.

1661031653182.png

1661031714480.png
1661031739101.png
1661031791575.png
 

kina kirefu

JF-Expert Member
Dec 14, 2018
7,432
7,006
Bila shaka yuko kazini mwacha aende zake

Kazi yakurushaga mawe gizani pengine unamsemelea unayemwambia anajua kwamba huyo nimemtuma
 

barafu

JF-Expert Member
Apr 28, 2013
6,728
32,743
Huyu atakuwa ni baba wa Kocha Wa Mpira aliyehudumu Taifa Stars na team mbalimbali akiitwa Marsha wa Mwanza?
 

Similar Discussions

1 Reactions
Reply
Top Bottom