Kisa cha yaya wa msimu na tuhuma za mauaji………! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kisa cha yaya wa msimu na tuhuma za mauaji………!

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by Mtambuzi, Mar 30, 2012.

 1. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #1
  Mar 30, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280

  Live Court – judgment of Louise Woodward:  The Closing Argument that convicted Louise Woodward  Eye To Eye: Barry Scheck (CBS News)
  Ndio kwanza alikuwa amemaliza masomo yake ya sekondari na kama wafanyavyo maelfu ya vijana waishio barani Ulaya na Amerika mara wamalizapo masomo yao, binti huyu aliyekuwa na umri wa miaka 18 wakati huo Louise Woodward aliamua kujiunga na mpango ujulikanao kama
  Au Pair.

  Au Pair ni neno lenye asili ya Ufaransa, lenye maana ya "sawa na." Neno hili limebeba maana pana sana kiasi kwamba nikisema nieleze itachukua sehemu kubwa ya habari hii. Labda nieleze tu kwa kifupi tu kwamba Au Pair ni mpango maalum ulioanzishwa barani Ulaya, ukianzia nchini Ufaransa ambapo pindi wanapomaliza masomo yao ya sekondari kabla ya kujiunga na vyuo vikuu, vijana hupata fursa ya kwenda katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kujifunza tamaduni tofauti, lakini wakiishi kwenye familia mwenyeji kwa mkataba wa kufanya kazi ya uyaya katika familia husika kwa malipo kidogo huku wakipata huduma zote zinazostahili katika familia ile kama mmoja wa wanafamilia na sio kuchukuliwa kama watumishi wa ndani.

  Mpango huu huhusisha mabinti zaidi na kimsingi hutakiwa kusomea kozi ya uyaya kwa muda usiopungua miezi mitatu ili ajue namna ya kutunza watoto wadogo. Hivyo mnamo mwaka 1996, Louise Woodward, binti wa Kiingereza aliyekuwa akiishi katika mji mdogo wa Elton nchini Uingereza, alijiunga na mpango huo kupitia kwa mawakala maalum ambao walifanikiwa kumpatia nafasi ya kwenda kuishi nchini Marekani katika mji mmoja uliopo katika jimbo la Hampshire. Louise Woodward hakuupenda sana mji ule kwa sababu haukuwa na tofauti sana na mji alikotoka.

  Hivyo aliamua kuhama kwa kuwatumia mawakala walewale. hatimaye alifanikiwa kupata nafasi katika mji mwingine uitwao Boston uliopo katika jimbo la Massachusetts. Louise alijiunga na familia ya madaktari wawili mtu na mkewe, Sunil Eappen na Deborah Eappen ambao walikuwa na watoto wawili wa kiume, wa kwanza alikuwa akiitwa Brandon aliyekuwa na umri wa miaka miwili na Mathew aliyekuwa na umri wa miezi tisa. Louise aliahidiwa kulipwa mshahara wa dola 115 kwa wiki.

  Lakini haikuchukuwa muda uhusiano wake na familia aliyokuwa akiishi nayo ukawa sio mzuri, na hiyo ilitokana na Louise kutumia muda mwingi kwenye Klabu za usiku akistarehe na vijana wenzie kila siku baada ya muda wa kazi. Mara nyingi Louise alikuwa akikwaruzana na wenyeji wake kwa sababu ya kurejea nyumbani usiku wa manane, hivyo alikuwa anachelewa kuamka ili kuwatayarishia watoto chai hasa Brandon ambaye alitakiwa kwenda Shule ya chekechea asubuhi.

  Mnamo Januari 31, 1997, uhusiano wa Louise na wenyeji wake ulifikia katika hatua mbaya baada ya wenyeji wake hao kutishia kumfukuza pale nyumbani kwao iwapo hatabadilisha mwenendo wake. Ilipofika Februari 4, 1997, siku nne tu tangu familia ile izozane na Louise na kutoa tishio la kumfukuza pale nyumbani kwao, ndiyo siku ambayo Louise alipopata balaa ambalo hatakuja kulisahau maishani mwake.

  Ilikuwa ni asubuhi, Louise alikwenda kumuamsha Mtoto Mathew aliyekuwa amelala kitandani, alipofika kabla hajamuamsha alimkuta akipumua kwa shida na hata rangi ya ngozi yake ilikuwa imebadilika. Kwa mujibu wa maelezo yake, Louise alisema, alijaribu kumnyanyua mtoto Mathew na kumtikisa kidogo kwa ajili ya kutaka kumuamsha, lakini Mathew hakuonesha dalili za kuamka. Akiwa amechanganyikiwa, Louise aliamua kupiga simu ya dharura ya kuomba msaada. Haukupita muda mrefu mtoto Mathew alikimbizwa katika Hospitali ya watoto ya Boston, lakini hakurejewa na fahamu hata pamoja na kupatiwa huduma ya kwanza.

  Kutokana na hali yake kuwa mbaya, ilibidi awekewe mashine maalum ya kusaidia mapigo ya moyo kwa ajili ya kusukuma damu. Hata hivyo siku tano baadae madaktari waliamua kuzima ile mashine na kutangaza kifo cha mtoto Mathew. Kwa mujibu wa Madaktari bingwa waliokuwa wakijaribun kuokoa maisha ya mtoto Mathew, walitoa maoni yao kwamba, mtoto yule alitikiswa sana na hivyo kupata athari kwenye ubongo. Madaktari hao waliongeza kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa mtoto Mathew kugongeshwa kwenye kitu kigumu kama vile ukuta.

  Louise alikamatwa akituhumiwa kusababisha kifo cha mtoto Mathew Eappen. Huo haukuwa ni mkosi kwa Louise Woodward peke yake bali pia kwa kampuni iliyomtafutia nafasi hiyo ya kuishi na familia ile, kwani mpaka wakati ule, ile kampuni ilikuwa na kesi nyingine ya madai. Ilikuwa ikidaiwa kulipa fidia ya dola milioni 100 kufuatia familia moja kumtuhumu binti wa Au Pair waliotafutiwa na kampuni hiyo, kumuuwa mtoto wao mwaka 1991. Safari hii Kampuni ya EF iliyomtafutia kazi Louise iliamua kujizatiti kifedha na kuamua kumuwekea Louise wakili maarufu na ghali nchini Marekani aitwae Barry Scheck.

  Wakili Barry Scheck alijizolea umaarufu nchini humo baada ya kuhusika kama kiongozi wa jopo la mawakili waliokuwa wakimtetea mwigizaji na mwanamichezo maarufu nchini humo O.J Simpson, aliyekuwa akituhumiwa kwa mauaji ya aliyekuwa mke wake waliyetalikiana mwaka 1995. Jopo hilo la mwakili waliyokuwa wakimtetea O. J Simpson lilibatizwa jina la "Dream Team."

  Kwa upande mwingine kukamatwa kwa Louise Woodward nchini Marekani kwa kutuhumiwa kwa mauaji kulipokelewa kwa hisia tofauti nchini Uingereza, hasa katika mji alikotoka wa Elton. Mmoja wa wanafunzi aliyesoma naye nchini Uingereza alimwelezea Louise kama binti muungwana asiye na makuu na anayependwa na kila mtu aliyemzunguka. "Ni msichana asiyependa hata kuuwa inzi na mwenye mapenzi makubwa kwa watoto na anayependa kucheza nao." Alisema msichana huyo.

  Mama yake Louise, Sue Woodward, akimtetea mwanaye, alimuelezea kama mtu asiyeweza kutenda ukatili wowote kwa watoto, kutokana na kuwa na mapenzi nao. Nayo familia aliyowahi kuishi nayo huko New Hampshire walishangazwa na habari za tukio lile, na walisema kwamba, kutokana na jinsi walivyoishi na vizuri na Louise hawadhani kabisa kwamba angeweza kumdhuru mtoto wao au mtoto wa mtu mwingine. "Kuna wakati aliniita bafuni ili niondoe buibui kwa sababu alikuwa anaogopa kumuuwa." Hiyo ndivyo alivyomewelezea Louise mama wa familia hiyo.

  Lakini maelezo yote hayo hayakusaidia Louise kumtoa katika tuhuma za mauaji, kwani mnamo13, Februari 1997, alitolewa katika Gereza la Framingham lenye ulinzi mkali akiwa na pingu zake na kufikishwa katika mahakama ya Boston ambapo alisomewa mashitaka ya kuuwa kwa kukusudia. Alielezwa kwamba, kama akikutwa na hatia atahukumiwa kifungo cha maisha jela bila uwezekano wa Parole.

  Watu wa Massachusetts na wale wa nyumbani kwao nchini Uingereza waliokuwa wakimtetea, walionya kwamba, Louise asichanganywe na wafungwa waliokubuhu katika uhalifu kwa sababu binti yule ni mgeni pale nchini Marekani na asiyejua sheria na nchi hiyo. Wakati akisubiri kesi yake ianze kusikilizwa rasmi, mambo hayakuwa yakimwendea vizuri. Vyombo vya habari nchini humo vilivyokuwa vikiripoti kesi yake vilikuwa havimtendei haki, kwani, vilikuwa vimeshamtia hatiani kabla hata ya shauri lake kusikilizwa.

  Lakini kabla ya shauri lake kuanza kusikilizwa Louise aliamua kwenda kufanyiwa usaili na wataalamu wanaotumia kifaa maalum kinachotumika kupimia uongo (polygraph) au (Lie Detector). Akifanyiwa usaili huo na daktari Bingwa wa fani hiyo, David Raskin, Louise aliulizwa maswali mengi kuhusiana na tuhuma za kuhusika na kumuumiza mtoto Mathew na kusababisha kifo chake. Dr. Raskin alikuwa anarejea maswali yote Louise aliyoulizwa na Polisi, wakati akiandikisha malezo yake.

  Akitoa majibu ya kipimo hicho, Dr. Raskin alisema, Louise alijibu maswali yote kwa ufasaha na kwa kujiamini kwa kiwango cha asilimia 95 kwa mujibu wa kipimo hicho. Matokeo ya Dr. Raskin yalikuja kuhakikiwa baadaye na Daktari mwingine bingwa wa fani hiyo aitwaye Charles Honts, ambaye alikodishwa na timu ya mawakili wa Louise.

  Naye Dr. Charles Honts alipata majibu sawa sawa na Dr. Raskin. Hata hivyo ushshidi huo haukupokelewa mahakamani kama ushahidi wa kumtoa Louise hatiani. Kutokana na vyombo vya habari katika jimbo la Massachusetts nchini humo kuandika ile kesi kila kukicha huku vikionekana dhahiri kumandamiza Louise, Jopo la mawakili waliokuwa wakimtetea Louise lilitoa ombi maalum la kutaka shauri lile lihamishiwe katika jimbo lingine ili haki itendeke, lakini jopo la majaji waliokuwa wakiendesha kesi hiyo, walipinga ombi hilo.

  Kesi hiyo ilianza kusikilizwa rasmi mnamo Februari 13, 1997, na ilianza kwa upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na mwendesha mashtaka Martha Coakley kuleta madaktari bingwa wanane wa neurosurgeon, ophthalmologist, radiologist, na wawili wa pathologists ambao ndio waliokuwa wakimhudumia mtoto Mathew tangu alipofikishwa hospitalini akiwa hajitambui. Miongoni mwao pia alikuwepo mtaalamu wa kuchunguza unyanyasaji kwa watoto (Child Abuse). wakitoa ushahidi wao wataalamu hao walidai kwamba, kifo cha mtoto Mathew kilisababishwa na kitendo cha kutikiswa kwa nguvu sana.

  Hata hivyo upo utata uliojitokeza kwenye neno alilotumia Louise Woodward Polisi wakati akiandikisha maelezo yake. Louise alisema, "I popped the baby on the bed." Na hapo ndipo ulipozuka utata wa lugha kati ya Waingereza na Wamarekani. kwani kwa Waingereza neno "Popped" lina maana ya "kuweka." ("Put" or "Placed") Na Louise alipoulizwa zaidi kuhusiana na neno hilo alisema alikuwa anamaanisha kuwa alikuwa anamuweka mtoto kitandani, wakati neno hilo lina maana tofauti kabisa kwa Kiingereza cha Wamarekani.

  Hata hivyo Louise akitumia neno hilo hilo la "Popped" alikiri kwamba kuna wakati aliwahi kumuangusha mtoto Mathew na hivyo kudhihirisha kuwa hakuwa mwangalifu kwa mtoto. Polisi aliyemuhoji mara baada ya tukio hilo alidai kwamba, Louise hakuwahi kutumia neno "Popped" wakati akiandikisha maelezo yake bali alitumia neno "Dropped." Kwani alisema, She "dropped" the baby on the bed. Hii ikiwa na maana kwamba alimuangusha mtoto kitandani wakati fulani.

  Wataalamu wote walioletwa na upande wa mashtaka waliieleza mahakama kwamba, kifo cha mtoto Mathew kilitokana na tatizo la kutikiswa kwa nguvu, ambapo lilimletea mtoto huyo athari katika fuvu la kichwa. Hata hivyo, mtaalam aliyeletwa na mawakili wa Louise kwa gharama kubwa ili kuufanyia uchunguzi mwili wa mtoto huyo ili kutegua kitendawili hicho, aliieleza mahakama kwamba athari zilizoonekana kwenye fuvu la kichwa zilitokea wiki tatu nyuma kabla ya mtoto huyo kufariki. Hiyo ilikuwa ni katika kudhihirisha kwamba familia ya Eappen inafahamu kuhusu kuumia mkwa mtoto Mathew.

  Nao upande wa mashtaka uliendelea kumtuhumu Louise kwamba, ni msanii anayeweza kucheza na maneno, kwani amekuwa akiieleza mahakama nusu ukweli nusu uongo. Upande huo wa mashtaka uliendelea kumtuhumu Louise kwamba, hakwenda nchini Marekani kuwa mlezi mzuri wa watoto bali alitaka Viza ya kuingia nchini Marekani ili kustarehe kwenye klabu za usiku. Kwani alikuwa akitumia kitambulisho bandia ili kuingia kwenye klabu za usiku kwa sababu alikuwa na umri chini ya miaka 21. Na hiyo ndiyo ikachukuliwa na upande wa mashtaka kwamba Louise hakuwa ni mu wa kuaminika. Kwa kuongezea upande huo wa mashtaka ulisema kwamba Louise alikuwa na jukumu maalum la kuwa mlezi wa mtoto wa familia ya Sunil Eappen, lakini kulikuwa na wakati anakesha kwenye klabu za usiku na rafiki zake, kitu ambacho kilikuwa kinasababisha awe anachelewa kuamka asubuhi kuwaandalia chai watoto, tabia iliyosababisha wenyeji wake watishie kumfukuza kazi siku chache kabla ya mtoto kulazwa hospitalini. Hivyo hali hiyo ilitafsiriwa kama, Louise aliamua kuwa mzembe kwa makusudi na kupelekea kumuangusha mtoto.

  Louise akikanusha madai hayo, aliiambia mahakama kwamba, hakuwahi kukasirishwa na tishio la kufukuzwa na wenyeji wake na wala hakuwahi kuiwekea kiburi familia hiyo. Binti mmoja aitwae Kathleen Sorabella aliyeitwa kutoa ushahidi dhidi ya Louise aliiambia mahakama kwamba, siku moja kwenye mstari wa kukatia tiketi ya kuingia kwenye tamasha la muziki alikuwa nyuma ya Louise, na hapo ndipo Louise alipomueleza kuwa haipendi ile kazi ya uyaya anayoifanya katika familia ya Eappen. Louise aliituhumu familia hiyo kuwa ilikuwa ikimwekea masharti magumu ya muda wa kutoka na wa kurudi nyumbani akienda kwenye starehe zake.

  Binti mwingine aitwae Ryhana Augustin ambaye ni rafiki wa karibu wa Louise na aliyekuwa akifanya kazi ya uyaya katika mpango huo wa Au Pair kama alivyokuwa Louise, aliielezea mahakama jinsi Louise alivyowahi kumlalamikia kuhusu kuwekewa masharti ya kutoka pale nyumbani na pia alilalamikia watoto wa familia ile kwamba ni watundu na wanalialia hovyo.

  Kesi hii ilizua mabishano makubwa ya kisheria baina ya pande mbili, yaani ule upande wa mashtaka na ule wa utetezi na ilileta mvuto wa aina yake kwenye vyombo vya habari nchini Marekani na Uingereza. Hata hivyo ilimalizika kusikilizwa kwake hapo mnamo Oktoba 30, 1997.

  Baada ya saa 26 za mashauriano ya kina, baraza la washauri wa mahakama lilikuja na uamuzi wa Louise kupatikana na hatia ya kuuwa kwa kukusudia, ambapo kwa mujibu wa sheria ya jimbo la Massachusetts, hukumu yake ni kati ya kifungo cha maisha kama adhabu ya juu au kifungo cha miaka 15 ikiwa ni adhabu ya chini kabisa.

  Mnamo oktoba 31, 1997, Mheshimiwa Jaji Hiller Zobel alimhukumu Louise Woodward kutumikia kifungo cha maisha jela.

  Baada ya hukumu hiyo, Louise alisema, "Ningependa kuweka bayana kwamba, sina hatia, sijawahi kumuumiza mtoto Mathew, na sijui kilichomtokea na wala sihusiki na kifo chake."

  Louise alitolewa nje ya mahakama akiwa na pingu na huku akitokwa na machozi. Alisindikizwa na ulinzi mkali kurejeshwa katika gereza la Framingham ili kuanza kutumikia kifungo chake cha maisha jela. Hukumu hiyo ilizua malalamiko miongoni mwa jamii ya Waingereza na Wamarekani wakipinga uamuzi wa mahakama wa kumfunga kifungo cha maisha Louise.

  Nchini Uingereza katika mji alikotoka Louise wa Elton wakazi wa mji huo waliandamana kupinga hukumu hiyo. Nalo Gazeti la Daily Mail la nchini Uingereza liliibuka na habari hiyo likiwa limepambwa na kichwa cha habari kikubwa ukurasa wa mbele kisemacho, "Haki Haikutendeka"

  Nchini Uingereza na Marekani, Louise Woodward alipata umaarufu mkubwa. Na baadhi ya vyombo vya habari vilitaka Louise aachiwe huru, na pia kulichapishwa fulana zenye maandishi yasemayo "Free Louise" na ziliuzwa kama njugu. Na nje ya Jela ya Framingham raia wa marekani waliokuwa wakipinga hukumu hiyo walisimama na mabango yaliyoandikwa, "haki ya Louise imenyongwa na serikali ya Marekani"

  Naye kiongozi wa jopo la mawakili waliokuwa wakimtetea Louise, Barry Scheck akiongea na wandishi wa habari, alisema kwamba, Baraza la washauri wa mahakama, halikumtendea haki Louise. Hata hivyo tumaini pekee la Louise lilikuwa kwa Jaji wa mahakama hiyo aliyemhukumu. Kwani mara baada ya kusoma hukumu, Mheshimiwa Jaji Hiller Zobel akionekana asiye na furaha alizipa pande mbili zilizohusika na kesi ile zikutane naye siku tatu baadae ili wawasilishe taarifa zao za mwenendo wa kesi ili kuangalia uwezekano wa kupitia upya ile hukumu, na ikiwezekana ipunguzwe.

  Wakati huo huo nao upande wa familia ya mtoto Mathew iliunga mkono hukumu ya kifungo cha maisha alichofungwa Louise. Akionekana kuridhishwa na hukumu hiyo, mama wa mtoto Mathew, Deborah Eappen alisisitiza kwamba, ni vyema Louise akatumikia kifungo cha miaka 15 jela ndipo uangaliwe uwezekano wa kufungwa kifungo cha nje (Parole).

  Siku tatu baadae pande mbili zilikutana na baada ya mashauriano yaliyodumu kwa takriban saa 20 hivi, Muheshimiwa Jaji Zobel, alikuja na uamuzi wa kubatilisha hukumu yake, na kwa maneno yake mwenewe alisema, "baada ya pande mbili kukutanana kupitia uamuzi wa kumkuta Louise Woodward na hatia ya kuua kwa kukusudia, na kutokana na ushahidi uliotolewa, tumeona tutakuwa hatukutenda haki, hivyo, Louise Woodward amepatikana na hatia ya kuua bila kukusudia na anahukumiwa kifungo cha siku 279 jela."

  Kwa kuwa hizo ni siku ambazo alishakaa jela wakati akisubiri hukumu, aliachiwa huru na hivyo kuungana na familia yake nchini Uingereza.

  Louise aliendelea na masomo yake ya elimu ya juu na baadae alisomea sheria katika chuo cha London South Bank University na kupata Digree hapo mnamo July 2002. Mnamo mwaka 2004 alijiunga na taasisi moja ya ushauri wa kisheria iitwayo Ainley North Halliwell iliyoko Oldham huko Greater Manchester nchini Uingereza akiwa kama mwanafunzi akichukua mafunzo ya vitendo.

  Hata hivyo mwaka uliofuata aliachana na mpango huo ili apate kujifunza ujuzi mwingine. Alijiunga na mafunzo ya kucheza dansi (Ballroom) pamoja na kufundisha kucheza Muziki wa Kilatini (Latin Dance) huko katika mji wa Chester.
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 2. Mamzalendo

  Mamzalendo JF-Expert Member

  #2
  Mar 30, 2012
  Joined: Dec 29, 2010
  Messages: 1,664
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 135
  Thanks for the stori,lakini mara nyingi muuaji ndio anajua ukweli,
   
 3. Cantalisia

  Cantalisia JF-Expert Member

  #3
  Mar 30, 2012
  Joined: Sep 26, 2011
  Messages: 5,229
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 135
  Heshima yako baba,dah!hii story tamu sn,ni wengi wanaenda jela bila hataia km huku kwetu ndio kbs hakuna cha watalam cjui wapime ubongo na maelezo yako wala nn,mara nyingi mtuhumiwa anatengenezewa maelezo ambayo ni tofauti na aliyotoa ili mradi hakuna haki!Ila nilitaman hii story iendelee naona imeisha gafla!
   
 4. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #4
  Mar 30, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Ni Ijumaa nyingine tena, kama kawaida, leo nimewaletea kesi hii ya yaya wa msimu kutoka kule nchini Uingereza ambaye alituhumiwa kwa mauaji ya mtoto Mathew aliyekuwa na umri wa miezi tisa wakati huo nchini Marekani.

  Bado natafuta kesi za hapa nchini na za Afrika kwa ujumla hususan zile za ukanda huu wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, na nikizipata nitaendelea kuwawekea hapa.

  Kesi hii ya Binti wa Kiingereza ilileta ubishani mkubwa sana wa kisheria na pia ilivutia watu wengi sana nchini Marekani kwenyewe na Barani Ulaya. Nimejaribu kuwawekea Youtube inayoonyesha jinsi kesi hiyo ilivyokuwa ikirindima mahakamani.

  Naamini wote tutajifunza kutokana na mkasa huu........................

  Nawatakia mapumziko mema ya mwishoni mwa juma.
   

  Attached Files:

 5. GIUSEPE

  GIUSEPE JF-Expert Member

  #5
  Mar 30, 2012
  Joined: Mar 8, 2011
  Messages: 206
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 35
  Asante kwa story nzuri sana.
   
 6. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #6
  Mar 30, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  _206598_matthew_eappen_150_02-11-98.jpg
  Mtoto Mathew wakati wa uhai wake

  _29232_eappens.jpg
  Wazazi wa Mathew, Sunil na Deborah Eappen
   
 7. Riwa

  Riwa JF-Expert Member

  #7
  Mar 30, 2012
  Joined: Oct 11, 2007
  Messages: 2,601
  Likes Received: 234
  Trophy Points: 160
  Ahsante Mtambuzi kwa hizi kesi unazotuletea kila Ijumaa...huwezi amini, one of the things I always look forward to on every Friday, is to read this! Naomba ikiwezekana Ijumaa moja utuletee kesi ya O.J.Simpson!
   
 8. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #8
  Mar 30, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  lwoodwardDM070307_228x451.jpg
  Louise alivyo sasa, akiwa na mchumba wake........

  231459_1.jpg
   

  Attached Files:

 9. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #9
  Mar 30, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Dr. Riwa, Heshima kwako.
  Nimefurahi kusikia kwamba na wewe umepata kaugonjwa ka kuchungulia hapa kila Ijumaa ili kujua kama nimeweka kesi gani. Kuhusu kesi ya O. J. Sompson, bado naifanyia kazi kwani ni ndefu sana na ina lugha ya kitaalamu zaidi ambayo inahitaji kamusi iliyokwenda shule. Nisikukatishe tamaa, nimeshafika nusu katika kuiandika habari hiyo, na Mungu akipenda Ijumaa zijazo nitaiweka hapa.

  Naomba kila mwenye kumbukumbu na kesi yoyote yenye kufundisha asisiste kunijuza na mimi nitaidadavua na kuiweka hapa ili tusome kwa pamoja.

  pamoja daima.
   
 10. KIKUNGU

  KIKUNGU JF-Expert Member

  #10
  Mar 30, 2012
  Joined: Nov 24, 2011
  Messages: 853
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 35
  Aisee Mtambuzi,hii kesi ilinionyesha vitu vingi sana kuhusu Waengereza,kuanzia ushiriki wa media kwenye kutetea raia wake na hata serikali bila kusahau raia wenyewe.
  Raia mmoja wa UIngereza kupata masaibu nje ya Uingereza regardless yuko guilt or not anaonekana innocent na serikali ita-play part kubwa sana ya kumsaidia raia wake.

  Kuanzia na media,tabloids newspapers kama THE SUN,NEWS OF THE WORLD,THE DAILY MAIL nk yalikuwa yanachimba habari za LOUISE tangu alipokuwa mtoto mpaka hapo alipofikia ili tu kuonyesha kwamba sio mtu ambae angeliweza kufanya kitendo kama kile.Vyombo vya habari vilihamia karibu na nyumba ya wazazi wake kwa kipindi kirefu sana.Na kwa njia moja au nyingine vili-play part kubwa sana kuachiwa kwake.

  Kwa upande wa serikali kuna fununu kwamba kulikuwa na pressure kubwa sana kutoka serikali ya Uingereza ya kutaka kuachiwa kwake japo kwa hili ni doubt kidogo kwani indendence ya mihimili hii miwili yaani serikali na mahakama kwa wenzentu iko second to none.Wakati wote kesi inaendelea Tonny Blair was then PM alikuwa anai-update house commons ya kile kilichokuwa kinaendelea kwenye kesi ile.


  Nilichojifunza kwenye kesi hii ni double standard ya Waingereza kwamba kuanzia vyombo vya habari,Majority ya wananchi wake na serikali kwa ujumla vilishatoa hukumu ya not guilt kwa LOUISE hata kabla ya kesi kuisha.


  Asante sana Mtambuzi kwa kunikumbusha story hii kwani nami nilikuwa na kimbelembele cha kununua gazeti la The SUN kwa kisingizio cha kusoma ile kesi kumbe nilikuwa naangalia "PAGE THREE" te te te,kwani nilipigwa marufuku kununua hilo gazeti by my other half.
   
 11. KIKUNGU

  KIKUNGU JF-Expert Member

  #11
  Mar 30, 2012
  Joined: Nov 24, 2011
  Messages: 853
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 35
  Mtambuzi usisahau kesi ya uhaini ya kina Father Tom please
   
 12. PetCash

  PetCash JF-Expert Member

  #12
  Mar 30, 2012
  Joined: Mar 20, 2012
  Messages: 1,680
  Likes Received: 170
  Trophy Points: 160
  Nilipoona kichwa cha habari niliona kawaida ila man, Its a very interesting case. Kwa kweli ni wachache sana ambao hupata insight za mahakamani, wengi hatujui kinachoendelea huko hadi yatukute ya kutukuta. Its so nice of you to bring this to our attention.Long live mtambuzi (Oracle?)
   
 13. TaiJike

  TaiJike JF-Expert Member

  #13
  Mar 30, 2012
  Joined: Dec 14, 2011
  Messages: 1,475
  Likes Received: 174
  Trophy Points: 160
  Asante Babu kwa kunikumbuka kila ijumaa.
   
 14. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #14
  Mar 30, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Sasa sijui nitafute ID itakayokuwa inatambulisha hizi kesi za kila Ijumaa ninazoweka humu.
  Kuna mdau mmoja alini PM wiki iliyopita na kuniuliza mbona haoni kitu wakati nilishaahidi kuweka makala kila Ijumaa! Kumbe nilishaweka kitambo lakini Heading ikamchanganya.
  Inabidi sasa muwe mnajua Automatically kuwa Ijumaa kuna kitu kinawekwa Sticky na MODS hapa MMU ili kuepuka maswali.

  Ahsante PetCash kwa kupoteza muda wako kusoma mandishi yangu....................LOL
   
 15. lukatony

  lukatony JF-Expert Member

  #15
  Mar 30, 2012
  Joined: Mar 25, 2011
  Messages: 428
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 35
  Shukrani mkuu!!kwanza hongera sana!!!ningependa tu kukujulisha kwamba mimi nami ni miongoni mwa watu amaye kila ijumaa lazima nikutafute!!kama alivyosema Dr Riwa,binafsi ningependa sana kupata mwenendo wa kesi ya O.J Simpson!pamoja na kesi ya bwana mmoja alinyongwa mwaka jana nchini marekani (niger) baada ya kukaa gerezani kwa zaid ya miaka 20,ilyokuwa na msisimko wa hali ya juu,ndani yake ikisemwa kuna ubaguzi wa rangi kama ilivyokuwa kwa O.J.Simpson!!!Pamoja mkuu hasa kwa sisi tulioipenda sheria na hakuna kilichotuzuia tukatekwa na wimbi la udaktari!!!!
   
 16. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #16
  Mar 30, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Mkuu lukatony Heshima yako........
  Umenichekesha sana, unajua hata mimi niliipenda sana sheria , lakini nimejikuta nimekuwa FUNDI MCHUNDO........Hivi sasa kwa kujifariji ndio najaribu kuandika visa na mikasa vinavyohusiana na Sheria.........LOL
  Nimeyapokea maombi yenu, na muda utakaporuhusu, nitawawekea hapa Kesi zote mlizoomba ili tupate kujifunza kwa pamoja.
   
 17. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #17
  Mar 30, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Mkuu nakushukuru kwa kutushirikisha kwa kile ukijuacho kuhusu kesi hii.
  Naamini yapo mengi ya kujifunza si kwa sisi kama wananchi bali hata viongozi wetu, hususan katika mfumo mzima wa sheria. Vitu kama DNA, na mfumo mzima wa kitabibu hasa kunapotokea utata kama huu, ni vyema tukajipanga ili kuepuka mkanganyiko kama huu.
   
 18. Leonard Robert

  Leonard Robert JF-Expert Member

  #18
  Mar 30, 2012
  Joined: Apr 22, 2011
  Messages: 9,150
  Likes Received: 2,472
  Trophy Points: 280
  mzee mtambuzi heshima kwako,kila ijumaa niko nawewe...
   
 19. Brown ad

  Brown ad JF-Expert Member

  #19
  Mar 30, 2012
  Joined: Feb 3, 2012
  Messages: 347
  Likes Received: 38
  Trophy Points: 45
  Kila napofuatilia mikasa yako kwakweli najikuta naanza kupata hofu yamungu na kutii sheria bila shurti.
  Maana kwa tanzania yetu ukipata kesi kama hiyo mpaka ushaidi wa kutosha upatikane na hukumu itoke umeshasota si chini ya miaka kumi,Eeh niongoze katika njia iliyonyooka.
   
 20. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #20
  Mar 30, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Juzi mwanangu NGADU kaniuliza, Baba unaandika Hadishi....... Mie nikamjibu, ndiyo, kisha akaniambia,
  Bashi ukimaliza nishimulie.....................
  Nasikitika sijamsimulia hadi leo..............
  Nakupa kazi leo itabidi umtwangie simu kisha umsimulie.................................LOL
   
Loading...