Kisa cha Sindbad baharia na safari saba

SEHEMU YA 15



Baada ya kutayarisha chelezo wakaniweka juu yake wakanipa mikate vipande saba na gudulia la Maji, wakanishusha mle pangoni, halafu wakaliziba kwa lile jiwe wakaenda zao.
Nilipogusa chini nikajikuta nimo katika pango kubwa lililoka na harufu mbaya sana ya maiti, lilikua limejaa mifupa ya binaadamu walioteremshwa mle, nilijibwaga chini nikajilaumu, Sindbad yote haya yasingetokea kama si tamaa yako! Bora ungekufa mlimani au baharini kuliko humu pangoni! Nikiteseka kwa was was wa kufa,
Nilijilaza mle kwa muda wa saa kadhaa huku nimejaa fikra na mawazo ya kukata tamaa. Niliposhikwa na njaa nilikula kipande kidogo cha mkate nikanywa na maji kidogo, halafu nikaenda kujilaza pembeni nilipopaondoa mifupa.
Baada ya muda ile mikate na Maji yaliniishia nikawa sina la kufanya ispokua kusubiria kifo, lakini siku moja wakati nilipokua nimejinyoosha, mara niliskia lile jiwe likifunguliwa na pale pangoni palionekana kundi la waombolezi ambao walimteremsha ndani mfu mwanaume aliefuatwa na mkewe aliepiga makelele huku ameahikilia mikate saba na gudulia la maji.
Lile pango lilipozibwa nilinyanyuka taratibu kutoka pale pembeni nilipokaa, nikachukua pande la fupa la paja la mtu kutoka katika moja ya yale marundo ya mifupa, nikamrukia yule mwanamke nikamtwanga nalo kichwani na mara ile ile alianguka chini na kufa hapo hapo.
Halafu nilichukua ile mikate saba na lile gudulia lake la maji vikanifaa kwa siku kadhaa, nilipoishiwa tena lile jiwe likaiinuliwa akashushwa mfu mwanamke aliefuatwa na mumewe. Nae alikabili kifo kama maskini yule mwanamke wa kwanza.
Kwa njia hii nikaishi kwa majuma kadhaa nilimuuwa kila alieteremshwa mle na kuila mikate yake nakunywa maji yake, siku moja wakati nilipokua nimelala mahali pangu pa kila siku, niliamshwa na sauti ya mwendo iliotokea karibu nami, nikashtuka, nikanyanyuka, nikachukua fupa langu nikaelekea kule ilikotokea ile sauti.
Kwa ajili ya lile giza totoro lililotanda kote, kwa shida nikaona kijinyama kikikimbia, nikakifuata huku nikijikwaa gizani kwa ile mifupa iliyotapakaa kote mle mpaka nikafika mwisho wa lile pango ambako niliona Nuru ya mwangaza iliyoongezeka ukubwa kadri nilivyoisogelea, nilipoikaribia yule mnyama aliruka akajipenyeza mle ilimotoka ile Nuru akatoweka.
Kwa furaha nyingi isiyoweza kukisika, nikatambua kuwa nimefika penye tundu ambamo wanyama mwitu waliovutiwa na harufu ya ile mizoga ya maiti mle pangoni, waliingilia kutoka upande wa pili wa lile bonde kuja kuila, hapo bila kusita sita nilipafukua pale mahali mpaka ile tundu ikawa kubwa, nilijipenyeza huku nikitambaa kwa mikono na miguu mpaka nikatokea ufukweni upande wa pili penye mwamba mreefu uliokwenda juu.
Nilipojikuta nipo nje kuonekanako mbingu na ardhi nilipiga magoti nikamshukuru mungu kwa kuokoka kwangu, kwa ajili ya ule mwangaza wa jua na hewa safi nilioivuta, baada ya muda nikahisi vizuri, nilijaa furaha isiokua na kifani kwa kuona uzuri wa mbingu, mawingu na ardhi.
Nikawa na nguvu za kutosha baada ya muda nikarudi tena mle pangoni ambako niliichukua mikate yangu iliobakia, nikakusanya na vitu vingi vya tunu ambavyo vilizikwa mle pamoja na maiti, nikavifunga vizuri kwa nguo za wale wafu nikavibeba nje ufukweni.
Basi nikabaki pale kwa muda wa siku chache nikitizama baharini kwa upeo wa macho toka asubuhi hadi jioni,
Siku moja wakati nilipokua nimekaa chini ya jabari nikiomba mungu aniokoe, mara niliona kwa mbali tanga la chombo kilichokua kikielekea kule nilikokua, mara ileile nilinyanyuka nikachukua chuka nikaifunga vizuri kwenye fito nikaanza kuipepea juu kwa nguvu kama bendera huku nikikimbia huko na huko pale ufukweni nikipiga kelele.
Kwa bahati nzuri mabaharia wa kile chombo waliona ishara yangu wakashusha mashua wakanifuata wakaniokoa,
"Umefikaje pale kwenye ufukwe?" Akaniuliza kwa mshangao mkubwa nahodha wa ile merkebu, akiendelea, "katika safari zangu zote za kupitia sehemu hizi za upweke sijawahi kumuona mtu yoyote!"
"Bwana wangu" nikamjibu "niliokoka kutoka katika merkebu moja iliozama karibu na ule ufukwe siku nyingi zilizo pita, furushi hili ulionalo ndicho kitu cha pekee nilichoweza kukiokoa, " nilimficha ukweli isije ikawa mle merkebuni mna raia wa kisiwa kile.
Basi nikatoa lulu ya thamani kutoka mle furushini nikamkabidhi nahodha nikamwambia: "tafadhali pokea lulu hii kama shukrani zangu kwa kuyaokoa maisha yangu. Lakini yile nahodha akasema "si desturi yutu kupokea malipo kwa tendo jema, tumewaokoa wengi waliovunjikiwa na merkebu zao, tukawalisha na kuwavisha, mwisho tukawasafirisha tikawafikisha watakako huku sisi tukiwapa wao zawadi. Kwani ni mwenyezi mungu tu ndie atowae.
Nikamshukuru kwa moyo wangu wote nikamuombea kila la kheri.
Basi ile merkebu iliendelea na safari yake tukifika kisiwa hadi kisiwa. Bandari hadi bandari huku nikifurahi kuelekea kwetu, lakini kumbukumbu za maiti na wafu waliojaa mle pangoni zikawa zanijia mara kwa mara ndotoni na kunishtua.
Mwisho kwa uwezo wa mwenyez mungu tukawasili basrah Salama salmini ambako nilipumzika kwa muda mfupi halaru nilielekea Baghdad kupitia mto Tigris.
Nilifika kwetu huku nimebeba hazina iliojaa kila namna ya vitu vya tunu na bidhaa ghali.
Nilipokelewa mikono miwili na ndugu, jamaa na marafiki. Baada ya kupumzika niliuza bidhaa zangu na vile vitu vyangu vya tunu, nikatoa sadaka kwa maskini, mayatima na kwa watawa. Nikabaki nikifurahia maisha.
* * * * * * * * * * * * * * *
Na hayo waungwana ndio yalionipata katika safari yangu ya nne, kesho in sha Allah nitawasimulia yalionipata katika safari yangu ya tano.
Baada ya karamu ya jioni Sindbad Baharia alimkabidhi Hindbad Hamali reale mia za dhahabu akimiaga na kumwambia aje tena kesho.
Basi wageni wote wakaaga wakaenda zao makwao huku wakistaajabia yale yaliompata mwenyeji wao.
Itaendelea...
 
SEHEMU YA 16



Nilipopata fahamu na kufumbua macho lile zee bado lilikua mabegani mwangu japokua sasa lililegeza kidogo miguu nipate kupumua. Lakini lilipoona nimepata nafuu likausukuma mguu wake mmoja tumboni mwangu likanipiga teke kwa mguu wake wa pili kunilazmisha ninyantuke nitembee nalo chini ya miti lichume matunda lile.
Kila nilipo simama au kukataa kutimiza matakwa yake lile zee lilinipiga teke, kwa hiyo sikua na lakufanya ispokua kufanya lilivyotaka. Basi kutwa likawa limeganda mabegani mwangu, nikawa mtumwa wake. Usiku nililala huku nimelibeba, kulipokucha liliniamsha kwa kunipiga teke na kuniamrisha nilibebe nielekee nalo kwenye miti likachume matunda.
Basi likawa linanikojolea, linaninyea mabegani mwangu kila kulipokucha na kulipokuchwa, na kila liliposhikwa na njaa lilinilazmisha kwa mateke nilipeleke kwenye miti likachume matunda. Kusema kweli nikajuta na kujilaani kwa kulisaidia, nikawa naomba lifilie mbali ili niepukane na balaa ile.
Baada ya majuma kadhaa ya mateso kupita kiasi, siku moja kwa bahati nzuri nilitokea mahali palipoota mamumunye mengi, chini ya mti mmoja nikaona mumunye moja kubwa kavu, tupu, nikainama nikalichukua baada ya kulisafisha vizuri nikalikamulia zabibu zilizoota kwa wingi pale kisiwani, nikaliziba vizuri nikalining'iniza mtini nikaliacha yale maji ya zabibu yachachuke.
Nilipolirudia baada yasiku chache huku nikiwa bado nikilibeba lile zee, nikaona lile mumunye limejaa divai kali safi, nilipoinywa ikanipa nguvu nikaanza kuhisi mwepesi bila kujali ule mzigo nilioubeba.
Lile zee lilipoona jinsi vidai ilivyonipa nguvu, nalo likaitamani, likataka lionje, sikuthubutu kulikatalia basi lilinyakua lile mumunye mikononi mwangu likalipeleka kinywani, likaanza kulegea na kuyumba yumba upande mmoja hadi mwengine huku miguu yake ikiacha ile kabari yake shingoni mwangu.
Ghafla bila kutazamia nikalibwaga chini kwanguvu likabaki kimyaa! Bila kukawia nilinyanyua jiwe kubwa lililokua karibu nikaliponda nalo kichwani, nikaliulia mbali huo ndio ukawa mwisho wa mtesi wangu, mungu asimrehemu!
Nilipoliuwa lile zee nikajaa furaha kwa uhuru wangu, nikaanza kukizunguka kile kisiwa kwa muda wa majuma kadhaa nikila matunda na nikinywa Maji ya chemchemi iliobubujika na kutiririka pale kisiwani nikifurahia uhuru wangu.
Siku moja wakati nilipokua nimekaa ufukweni nikitafakari kwa yale yalionisibu. Mara kwa mbali niliona tanga la merkebu ikielekea pale kisiwan, ilipofika karibu ikatia nanga na wasafiri waliokuwemo wakashuka huku wamebeba guduria zao kwa madhumuni ya kujaza maji safi.
Bila kukawia niliwakimbilia, waliponiona walishtuka wakastaajabu wakanizunguka huku wakitaka kujua mimi ni nani na ninatoka wapi, nilipowahadithia yote yalionisibu wakaniambia, "ni ajabu kubwa kua umeliokoka lile zee la bahari kwani wewe ndie mtu wa kwanza kufanya hivyo!"
Basi baada ya kuteka Maji ya kutosha na kuchuma matunda mengi. Wale mabaharia walinichukua mpaka kwa nahodha wao alienipokea kwa ukarimu mkubwa na alieyasikiliza kwa mshangao mkubwa masaibu yangu. Baada ya muda merkebu iling'oa nanga tukasafiri kwa siku nyingi, siku moja tukatia nanga kwenye bandari kwenye jiji moja lililokua kwenye kilele cha mwamba linalojulikana na wasafiri kama jiji la manyani kwa sababu ya idadi kubwa ya manyani yaliofika pale kisiwani usiku.
Tuliposhuka, nikaongozana na mmoja wa wafanya biashara tukaenda mjini kwa madhumuni ya mimi kutafuta kazi, mara tukakutana na kundi la watu waliokua wakielea kwenye lango la jiji huku wamebeba magunia yaliojaa mawe madogo madogo, mwenzangu akanipa gunia akaniambia "lijaze mawe uwafuate wenzako Hawa mpaka huko waendako ukafanye watakavyofanya, kwa kufanya hivyo utajipatia riziki zako."
Basi nikaufuata ushauri wake. Nikajaza mawe mle guniani nikajiunga na lile kundi la watu huku mwenzangu akiwaambia "jamani huyu ni mtu alievunjikiwa na merkebu yake huko baharini, tafadhalini mfundisheni namna ya kujipatia riziki yake na mwenyezi mungu atawalipa mema.
Tulipokua mbali kutoka jijini tukafika katika bonde pana lililojaa minazi mingi mirefu sana ilionyooka wima kwenda juu kufikia kiwango cha watu kutoweza kuipanda. Tulipoikaribia nikaona idadi kubwa ya manyani ambao walipotuona tu wakapanda kileleni.
Hapo wenzangu walitua magunia yao wakaanza kuyashambulia yale manyani kwa yale mawe, na mimi nikafanya kama walivyofanya, Yale manyani kwa ghadhabu yakaanza kutushambulia kwa kuchuma nazi na kututupia, hizi nazi tulizikusanya na kuzitia maguniani mwetu yalipojaa tukarejea mjini na kuziuza sokoni.
Nilipopata fedha za kutosha kiniwezesha kurejea kwetu, nikapanda merkebu iliokua ikielekea basrah nikiwa na shehena kubwa ya Nazi.
Wakati wa safari yetu tulitia nanga visiwa vingi nilikouza zile nazi kwa bei kubwa, nyingine nikabadilishana na wafanya biashara wengine kwa mdalasini, pilipili manga na viungo vingine, tulipofika kwenye kisiwa cha bahari iitwayo bahari ya lulu, niliwaajiri wapiga mbizi, baada muda nikawa na lulu nyingi za thamani kubwa.
Kutoka hapo tulingoa tukasafiri kwa siku nyingi mpaka tukawasili basrah Salama salmini. Baada ya mapumziko ya siku chache nilielekea Baghdad huku nimesheheni vitu. Vya thamani kubwa.
Nilipofika kwetu nilikaribishwa mikono miwili na ndugu jamaa na marafiki, nikawatunukia zawadi za thamani na nikatoa sadaka kwa maskini na mayatima na wajane.
Na huo ndio mwisho wa kisa kilichonipata katika safari yangu ya tano waungwana. Kesho in sha Allah nitawasimulia yalionipata katika safari yangu ya sita, akamalizia kusimulia Sindbad Baharia.
******************************
Maakuli ya jioni yalipomaliza. Sindbad Bavaria alimpa Hindbad Hamali reale mia za dhahabu halafu wrote wakaenda zao makwao huku wakistaajia Yale walioyasikia.
Itaendelea.
 
SEHEMU YA 17




Siku ya sita Hindbad Hamali aliwasili tena na baada ya wageni wengine kufika Sindbad Baharia aliwasimulia wageni wake Yale yaliyompata katika safari yake ya sita.
SAFARI YA SITA YA SINDBAD
Baada ya kuishi kwa muda mrefu na utajiri wangu kuongezeka kupita kiasi kwa biashara nilizozifanya, akaanza Sindbad.
Siku moja nilijiwa na wafanya biashara wakanisimulia mengi juu ya safari zao za ng'ambo na faida walizozipata huko, hayo yakanitia hamu ya kusafiri tena na kuzitembelea nchi za mbali. Basi baada ya kukata shauri nilinunua bidhaa nyingi nikajitayarisha na safari nyengine baharini.
Na muda ulipo wadia nilijiunga na wafanya biashara wenzangu tukapanda merkebu moja kubwa. Kwa uwezo wa mwenyezi mungu tulisafiri kutika bahari mojahadi nyengine, kisiwa kimoja hadi chengine, na kutoka jiji moja hadi jengine, tukifanya biashara na kujipatia faida kubwa. Hata siku hiyo wakati tulipokua tukisafiri katika bahari kuu, mara nahodha wetu alianza kupiga kelele kama mtu mwenye wazimu, "mungu wangu wee! Tumeangamia!" Alipaza sauti.
Tulipomuona katika hali ile ya kupiga mayowe huku akizichana nguo zyetu? na kunyofoa ndevu zake, tulimwendea na kumuuliza taliomsibu. Akatujibu, "mnauona ule mlima mrefu tunaoukabili ulionyooka wima mbele yetu? Hatutaokoka Abadan,
Kwani chini yake pana mwamba hatari sana, bila sisi kujua tumepoteza njia yetu na upepo mkali unaovuma sasa unatuelekeza kule kwenye ule mwamba, inavyojulikana mpaka sasa hakuna hata yeyote aliokoka kutoka kwenye ule mwamba. Kwa hiyo tuombeni mungu huenda kati yetu yupo walii ambae dua zake zitakubaliwa na mwentezi mungu.
Kusikia maneno Yale tukapiga magoti tulianza kumuomba mungu. Nahodha nae akapanda mlingotini kuangalia tunakoelekea, jitihada zake zote za kuokoa maisha merkebu yetu kwa kuielekeza kwengine ilishindikana. Basi baada ya muda upepo mkali ulituelekeza kule mlimani. Tulipoukaribia, bahari ikazidi kuchafuka na Maji yalizunguka kwa nguvu na kuifanya merkebu yetu izunguke kama pia na kuugonga ule mwamba mara mbili tatu na kuvunjika vunjika na kuzama mara moja.
Wengi walikufa, wachache mm nikiwa mmoja wao tukawahi kuushika ule mwamba na kwa shida na jitihada kubwa na kwa uwezo wa mwenyezi mungu tukaweza kuokoka na kuupanda, tulipofika juu tukaona tupo kwenye kisiwa chenye miti mikubwa na ufukweni upande wa pili wa kile kisiwa pametapakaa mbao za merkebu zilizoangamia pamoja na robota za bidhaa mbali mbali na vitu vingi vya thamani na vya tunu vilivyomwagika kutoka katika masanduku yaliofikishwa pale na kupasuka.
Pale ufukweni tukashuhudia pia mifupa ya watu walioangamia kutokana na merkebu zao kuvunjika mwambani.
Basi nikawa nazunguka zunguka na kuzikagua zile bidhaa zilizotapakaa pale ufukweni, wakati nilipokua nikifanya hivyo mara nilitokea kwenye mto uliokua ukielekea pangoni mlimani badala ya kuishia baharini.
Bila kukawia nikaufuata kule ulipikua ukielekea, pale ukingoni mwambani nikaona pia panang'aa johari nyingi, almasi, zumaridi, yakuti, lulu na feruzi. Na pale majini paliota namna ya majani ya pekee yaliochanganyika na kaharabu, namna ya gundi iliyomiminika kutoka jabalini kuelekea baharini.
Hapo nyangumi wengi wakubwa walitoka baharini na kula ule mchanganyiko, matumbo yalipowajaa na kupata joto kwa ajili ya mlo huo, nyangumi walitapika ambari tenye harufu nzuri ilioenea pwani nzima. Basi sisi tuliokoka kufa maji, tukawa hapo ufukweni tukingojea mauti.
Hivyo basi wengi wa wenzetu mmoja mmoja wakaanza kufa baada ya kuishiwa na sehemu ya chakula chao na kwa kula majani, sisi tuliobaki tukawaosha na kuwazika, baada muda wenzangu waliobaki mmoja mmoja nao waliobaki walianza kuugua mpaka wakamalizika wote nikabaki peke yangu.
Nilipomzika mwenzangu wa mwisho nikatambua sasa mauti yalikua yakinikabili mimi, hapo nikajibwaga chini nikalia nikajuta "afadhali ningekufa kabla ya wenzangu kwani wangeniosha na kunizika."
Basi baada ya maombolezo hayo nilinyanyuka nikaanza kuchimba shimo reefu pale pwani, nikifikiri "nikiona wakati wangu wa kufa umewadia nitajilaza humu nife mumo humo shimoni, bila shaka baada ya muda upepo utanifukia kwa mchanga."
Wakati nilipokua nikijitaarisha kufa nikajilaani na kujuta kwa kufanya safari nyingi baharini badala ya kuishi kwetu raha mustarehe.
"Kwanini Sindbad" nikajiuliza "usiridhike ukabaki nyumbani Baghdad? Je, hukua na utajiri wa kutosha kuishi mpaka kufa kwako?"
Wakati nikifikiria hivyo nikawa nazunguka zunguka pale kwenye ukingo wa ule mto nikiuangalia jinsi ule mto unavyotoweka mle pangoni, mara nikajiwa na fikra "mto huu" nikajiambia "bila shaka kuna ulikoanzia na unakoishia, kama unaingia mlimani kutoka upande huu nilipo, bila shaka unatokea upande mwengine kwenye mwangaza. Kwa hiyo nikiufuata kwa kupanda chombo fulani, mkondo wake unaweza kunichukua, ukanifikisha wanakoishi wanadamu.
Kama siku zangu hazijaisha mwenyezi mungu ataniongoza Salama salmini. Nikiangamia ni bora kuliko kukaa hapa na kungojea mauti." Basi nikitiwa nguvu na mawazo haya nikaanza kukusanya magogo na mbao zilizotapakaa pale zilizovunjika kutoka katika merkebu zilizoangamia.
Nikazifunga imara pamoja kwa kamba nene nikajitengenezea chelezo nilipomaliza nikapakia mafurushi ya vile vitu vya tunu vilivyotapakaa pale pwani; na mengine nikajaza ambari, halafu baada ya kumuomba mwengez mungu nikakisukuma chelezo changu mtoni nikakidandia.
Mkondo wa waji ukanichukua kwa kasi na baada ya muda nilijikuta nimo gizani mle pangoni, kwa kasi ya ule mkondo chelezo kilianza kugonga gonga mwambani kulia na kushoto, ghafla ule mto ukawa mwembamba ikanibidi nijilaze kifudi fudi kwa kuogopa kichwa changu juu mwambani, lile giza na ile hali ta hatari niliojikuta nimo, ikanifanya nijute kutika kule kisiwani kwenye mwangaza.
Itaendelea...
 
Kitabu cha alfu lela ulela kwenye kitabu cha pili(vipo vitabu tisa) kilichofasiriwa na Adam Hassan kimendika vizuri sana kisa hiki.
Wapi kinapatikana maana nakumbuka syllabus yetu ya Darasa la tano 1970. Kingine kilikuwa Hekaya Za Abunwas. La sita Mashimo ya Mfalme Suleiman. Darasa la nne tulikuwa na Hadith za Hiawadha na Hadith za Essopo. Darsa la tatu tuna Robinson Crussor. La kwanza na la pili tuna Someni kwa Furaha unakutana na Paulo mchafu usje kucheza na sisi, Safari za Bulicheka na Wagagagigikoko wake!!!!
 
Umenikumbusha hadithi za mwalimu wangu vedastus kyamwenge.hivi huwa mnatunga au mnasimuliwa na wahenga pia!???
 
Wapi kinapatikana maana nakumbuka syllabus yetu ya Darasa la tano 1970. Kingine kilikuwa Hekaya Za Abunwas. La sita Mashimo ya Mfalme Suleiman. Darasa la nne tulikuwa na Hadith za Hiawadha na Hadith za Essopo. Darsa la tatu tuna Robinson Crussor. La kwanza na la pili tuna Someni kwa Furaha unakutana na Paulo mchafu usje kucheza na sisi, Safari za Bulicheka na Wagagagigikoko wake!!!!

Aisee kuna wahenga na wahenga, mimi nimesoma late 80s/early 90s na hivi vyote havikuwa kwenye mfumo kabisa.

Ilikuwa labda ukipate ujisomee mwenyewe.
 
Back
Top Bottom