Kisa cha Mzee Suwal Mohamed alivyomtorosha Mwalimu Nyerere

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,913
30,255
Jana ilikuwa siku nzuri na ya furaha kubwa kwangu kwa kutembelewa nyumbani na rafiki yangu Guled Issa ambae kwa miaka mingi tukijuana kwa sauti na kuandikiana mtandaoni.

Jana kanifikia kwangu tukaonana uso kwa macho.

Tumezungumza mengi na katika kubwa alilonikumbusha ni makala aliyoniletea miaka saba iliyopita ambayo ilikuwa niichape katika blog yangu.

Hili halikufanyika.

Baada ya yeye kuondoka nikaingia Maktaba na nikaikuta.

Tufaidi sote makala hiyo hapo chini:

MZEE SUWAL MOHAMED ALIVYOMTOROSHA MWALIMU NYERERE ASIKAMATWE NA MAKACHERO

na Guled Issa

Mzee Suwal Mohamed ni moja ya majina ya mashujaa yanayopaswa kuingia katika historia ya mashujaa waliojitolea katika kuwakinga viongozi wa harakati za uhuru wasidhalilishwe na wakoloni wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.

Mfano wa Mzee Suwal ni moja ya mifano mingi ambayo hii leo haifahamiki na wala hakuna juhudi ya kuhifadhi kumbukumbu hizi.

Labda kama ingelikuwa si kisa kilichomkuta yeye na wenzake baada ya uhuru historia hii ya huyu mzee isingelifahamika kamwe.

Kijografia Mzee Suwal Mohamed alikuwa anaishi Arusha kwa sasa ni Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara.

Mzee Suwal alikuwa Mtanganyika mwenye asili ya Kisomali.

Baada ya Tanganyika kujipatia uhuru wake mwaka 1961, Meja Jenerali Muhidini Mfaume Kimario akishika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani kuanzia mwaka 1983 mpaka 1989 katika kipindi chake kama waziri mwenye dhamana alipata kuwanyima amani wazee wa Kiislamu Watanzania wenye asili ya Kisomali katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mtwara na sehemu mbalimbali nchini kwa kuwakamata kila mara.

Jambo la kukamatwa mara kwa mara kwa wazee hawa liliwanyima amani ya kuishi katika makazi yao na baada ya kuchoshwa na kadhia hii ndipo wazee hawa wakakata shauri la kumuendea Mwl Julius Nyerere ili ku mfikishia malalamiko yao.

Wazee hawa walipoonana na Nyerere wakamwambia kuwa katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika sote tulikuwa pamoja tukishirikiana kudai uhuru sasa iweje leo baada ya Tanganyika kuwa huru thamani yetu ipotee.

Mzee mmoja katika wazee hao Mzee Suwal Mohamed akamkumbusha namna yeye na Mwl. Nyerere huko Arusha walivyokumbana na mkasa wa Nyerere kutaka kukamatwa na serikali ya Waingereza wakati wa vuguvugu la kupigania uhuru.

Mzee Suwal akamkumbusha Nyerere kisa kizima cha kutaka kushikwa na serikali ya Kiingereza mjini Arusha.

Ilikuwa hivi.

Katika harakati za Tanganyika kupigania uhuru Mwl. Julius Kambarage Nyerere akiwa mjini Arusha, akihamasisha watu kuunga mkono Tanu, kulipatikana hatua za kutaka kukamatwa Nyerere na serikali ya kikoloni ya Muiingereza ndipo kwa bahati nasibu mzee mmoja mwenye asili ya Kisomali akamchukua Nyerere kwa gari yake aina ya Land Rover na kutokomea nae mpaka msituni umbali mrefu kutoka mjini ili kukwepa kushikwa na serikali ya Muingereza.

Inasemekana kulikuwapo na watu wenye magari yao na wangeweza kumsaidia lakini hawakuonesha nia ya kutoa msaada wowote kwa Mwl. Nyerere.

Baada ya kufika msituni Mwl Nyerere alitaka kumlipa Mzee Suwal malipo kama shukrani ya kumuokoa na balaa hilo lakini kitu cha kushangaza kama sio kustaajabisha kwa moyo aliokuwa nao Mzee Suwail akamwambia Nyerere kuwa amefanya msaada ule kama moja ya mchango wake katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.

Baada ya Nyerere kukumbushwa mkasa huu alisikitika sana kisha akaomba aitwe Waziri wa Mambo ya Ndani Meja Jenerali Muhidini Mfaume Kimario na kuulizwa kuhusu kadhia ya wazee wale.

Mwl. Nyerere alimwambia Meja Jenerali Kimario kuwa kwa kitendo cha kuwasumbua wazee wale si jambo jema, akaongezea kusema kuwa wakati Tanganyika inafanya harakati za kudai uhuru pale Moshi alipokulia Muhidin Kimario walikuwapo majasusi wa wakoloni wakiitumikia serikali ya Kiingereza wakipinga harakati za Tanganyika kuwa huru, hawa wazee wakati huo walichangia mchango wao hadi ikawa sababu ya kupatikana uhuru.

Mwl. Nyerere alitoa amri kusipatikane mtu wa kuwasumbua wale wazee na wapatiwe haki sawa na Watanganyika wengine bila kubaguliwa kwa namna yoyote ile.

Nyerere alimuuliza Mzee Suwal Mohamed kama ile Land Rover yake iliyomuokoa bado ipo, Mzee Suwal akamjibu ipo.

Bila kusita Nyerere alimuomba Mzee Suwal ailete Land Rover yake hiyo ili iwekwe kama kumbukumbu, naye mzee Suwal bila khiyana aliipeleka Land Rover yake hiyo Makao Makuu ya nchi Dodoma na ikahifadhiwa kama kumbukumbu ya uhuru.

Hii ilikuwa ni miaka ya 1988 mpaka 1989.
Mzee Suwal Mohamed alifariki mwaka 1995.

PICHA: Guled Issa akiwa Maktaba na picha ya tatu ni Meja Jenerali Muhidin Kimario.

1684954904834.jpeg

1684954979591.jpeg

1684955011776.jpeg



 

Attachments

  • 1684955051739.jpeg
    1684955051739.jpeg
    49.4 KB · Views: 18

Similar Discussions

Back
Top Bottom