Kisa Cha Malecela Na Mawaziri Wa Sasa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kisa Cha Malecela Na Mawaziri Wa Sasa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by maggid, Aug 12, 2010.

 1. m

  maggid Verified User

  #1
  Aug 12, 2010
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180
  Na Maggid Mjengwa (Makala hii ilichapwa Raia Mwema majuma mawili yaliyopita)

  HISTORIA ni mwalimu mzuri. Ili tuweze kutafsiri na kuyaelewa yanayotokea sasa na kuyaelewa yatakayotokea kesho, tuna lazima ya kuangalia na kutafsiri kilichotokea jana.


  Na hii ni moja ya maana ya kusoma na kutafsiri alama za nyakati.
  Kuna kisa cha uchaguzi wa mwaka 1985. Mzee John Malecela alikuwa bado na ujana wa kisiasa. John Malecela, katika uchaguzi ule mkuu wa mwaka 1985, ndiye alikuwa waziri pekee katika baraza la mawaziri lililovunjwa ambaye hakurudi bungeni.

  John Malecela alikataliwa na wapiga kura wake, hakurudi bungeni. Kwanini?
  Kwa mujibu wa maandiko ya wasomi watafiti, Bw. Mvungi na Bw. Amos Mhina (Searching for a people MP?), anguko la John Malecela lilitokana na kukosa uzoefu na mahusiano mazuri na wapiga kura katika ngazi za chini.

  Huyu alikuwa John Malecela ambaye ndugu yake Job Lusinde ndiye alikuwa mbunge aliyemtangulia jimbo la Dodoma Mjini. Malecela alibwagwa na injinia asiye na uzoefu wa kisiasa anayeitwa Mazengo Yohana.

  Hata hivyo, katika hili la mahusiano na watu, watafiti wale katika maandiko yao kwenye kitabu kiitwacho Tanzania: Democracy In Transition, kwa mtazamo wangu, wameshindwa kubainisha sababu nyingine iliyochangia kuharakisha anguko la John Malecela wa wakati huo. Hili lilihusiana pia na mahusiano kati ya John Malecela wa wakati huo na wapiga kura wake.

  Na hapa inahusu kauli ya John Malecela wakati huo akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi. Katikati ya kilio cha watumiaji wa njia ya reli ya kati (TRC) juu ya huduma mbaya za shirika hilo la reli, miaka ile ya 80, Bw. John Malecela alipata kukaririwa akitamka kuwa hakukuwa na tatizo la huduma mbaya na kwamba wenye kufikiri hivyo, "They can go to hell!"- kwamba wanaweza kwenda kuzimu.

  Katika sanaa ya mawasiliano tunaamini kuwa sentesi moja inayotamkwa na mwanasiasa yaweza kumjenga au kumbomoa kabisa kisiasa. Kwa John Malecela, kauli yake ile ataishi asiisahau; maana, pamoja na kuwa tulikuwa katika mfumo wa chama kimoja, redio moja ya taifa na magazeti matatu, bado wananchi waliweza kufikisha shutuma zao kwa Malecela juu ya kauli yake ile.

  Na kilichotokea katika uchaguzi mkuu uliofuata wa mwaka 1985 ilikuwa ni kwa wapiga kura wa Dodoma Mjini kushindilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la kisiasa la John Malecela. Walifanya hivyo kwa niaba ya Watanzania wengine na hususan watumiaji wa reli ya kati.

  Malecela aliangushwa vibaya katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo. Hakupata ubunge, na hivyo hakuweza kuwa waziri.

  Na hakika, Malecela alijifunza, na hata aliporudi tena kwenye ulingo wa kisiasa, Mzee John Malecela, hata hii leo, amekuwa ni makini sana katika kuchagua maneno anapowasiliana na umma.

  Nahofia kuwa yaliyomkuta Mzee wetu John Malecela miaka zaidi ya 20 iliyopita yatakuja kuwafika mawaziri kadhaa wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete. Yatakuja pia kuwafika wabunge wengi waliomaliza muda wao.

  Kwanini? Wapiga kura bado wanakumbuka, si matendo yao na hususan ahadi walizotoa ambazo hazikutimizwa, wanakumbuka pia baadhi ya kauli za kejeli kwa wapiga kura kutoka kwa baadhi ya wabunge na mawaziri.

  Kuna kosa kubwa linalofanywa na wanaotafiti hali ya kisiasa na hasa kuelekea uchaguzi mkuu. Wengi wa watafiti wanalenga zaidi katika kuchambua mienendo ya wagombea na kampeni zao. Watafiti hawa wamesahau kutafiti mienendo ya wapiga kura ambao kimsingi ndio wenye uchaguzi na maamuzi ya nani awe kiongozi wao.

  Uzoefu wangu unaniambia kuwa wapiga kura wa Tanzania walio wengi hawatabiriki. Ukweli huo unathibitishwa kisayansi. Kutafiti mienendo ya wapiga kura wa Tanzania ni jambo la muhimu sana kwa sasa.

  Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, wapiga kura wa Tanzania, ukiondoa uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 ambapo Bw. Augustino Mrema aligombea urais kwa tiketi ya NCCR Mageuzi, chaguzi zilizofuata zimeonyesha kubadilika kwa mienendo ya wapigakura.

  Msisimko na idadi ya wanaojiandikisha na kupiga kura ikaanza kupungua. Kwanini? Wapiga kura wa Tanzania walibaini haraka kuwa chama tawala CCM, ambacho kilifaulu kuua nguvu za vyama vya upinzani na kuvifanya vyama vya upinzani vibaki majina tu, kilikwenda hatua nyingine mbele.

  Kwamba kiliondokana na mfumo wake uliowashirikisha wanachama wengi zaidi katika kuwatafuta wagombea wao wa ubunge kwa njia ya kura za maoni na kuiacha kazi hiyo kufanywa na kundi dogo jimboni lenye wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya wasiozidi 400.

  Hayo yakawa ni mazingira ya kuibuliwa na kuhalalishwa ' takrima' na rushwa nyinginezo. Wapiga kura wa Tanzania na hususan waliokuwa wakikipigia kura Chama cha Mapinduzi wakajikuta wanapigiwa kura na watu wachache ndani ya chama.

  Katika mazingira hayo, hata mbunge ambaye hakukubalika na wanachama wengi wa chama chake jimboni alihitaji kukubalika na zaidi ya nusu ya wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya wa chama chake. Kwanini basi waone umuhimu wa kwenda kujiandikisha na kupiga kura?

  Kwa uchaguzi unaokuja hali ni tofauti na hususan baada ya chama tawala CCM kuja na utaratibu mpya wa wagombea kupigiwa kura ya maoni baada ya kujinadi kwenye kata mbali mbali jimboni. Na katika hali hii, kwa tunaofuatilia mienendo ya wapiga kura, tumeshuhudia wimbi kubwa la wanachama wapya wakikimbilia kujiunga na CCM.

  Wengi wa wanachama hawa wapya ni vijana waliozaliwa au kukulia ndani ya mfumo wa vyama vingi. Ndio hawa waliozaliwa mwaka 1992 tulipoanzisha mfumo wa vyama vingi. Mwaka huu wanatimiza miaka 18, hivyo basi wana haki ya kupiga kura sambamba na kaka na dada zao waliozaliwa miaka ya 80 kwenda mbele.

  Ndio hao tunaowaita vijana wa sasa ambapo mwaka 1992 uliwakuta wakiwa hawajatimiza hata miaka 15. Wanachama hawa wapya wameibaini fursa ya kuondokana na viongozi wasiowafaa kwa kujiandikisha uanachama wa CCM na kwenda kushiriki kupiga kura ya maoni.

  Maana yake nini? Hii ina maana moja kubwa kuwa matokeo ya kura za maoni yatawaacha midomo wazi walio wengi. Hawataamini kuona majina ya vigogo, wakiwamo mawaziri, wakipigwa mieleka itakayoacha simulizi za muda mrefu.

  Kama hili litaachwa litokee bila watendaji ndani ya CCM kufanya hila ili kuwarudisha wabunge na mawaziri vigogo wenye majina makubwa, basi, hilo litaonyesha kuanza kukomaa kwa demokrasia ndani ya Chama Cha Mapinduzi.

  Na kwa jinsi hali ilivyo sasa, hakika huhitaji utafiti wa Redet kufahamu kuwa wapiga kura wengi wamejiandaa kuwaangusha wabunge wanaomaliza muda wao na hata mawaziri kupitia kura za maoni.

  Rushwa na takrima hazitasaidia sana kuepusha hali hii. Kwa mfano, kuna mbunge anayemaliza muda wake kule Morogoro. Katika uchaguzi mkuu uliopita, Bwana huyu alitoa takrima kwa kuandikisha majina ya wajumbe wote waliopokea takrima hiyo. Ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya wasiozidi mia nne.

  Bwana huyu aliwatisha wajumbe wale kwa kutamka: "Kama msiponipigia kura ilihali mmepokea cha kwangu, nitawasomea albadri . Wajumbe wale waliogopa albadri, wakampitisha! Lakini, kwa aliyoyafanya jimboni humo mbunge huyo, naambiwa kuwa wanachama zaidi ya elfu kumi wa CCM wa jimbo hilo wako tayari mbunge huyo anayemaliza muda wake asome albadri hata mara mia moja. Hawatampitisha!
   
Loading...