SoC01 Kisa cha Kweli: Mtoto Aliyebakwa na Baba yake kwa Mwaka Mzima

Stories of Change - 2021 Competition

Faith Luvanga

Member
Aug 21, 2018
14
15
Jioni baada ya kutoka shule, Faraja* aliingia ndani na kuona jinsi vyombo vilivyokuwa vimevurugwa na kuvunjwa. Maumivu ya kumbukumbu za ugomvi wa wazazi wake usiku kucha wa jana yalimfanya ashindwe kuvumilia na kuangua kilio. Kwa bahati mbaya, mama yake hakuwepo nyumbani kumfariji, kwani alikuwa ameondoka kunusuru maisha yake ili asiendelee kupokea kipigo kutoka kwa Mzee Mpili*. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Bi Koko* kuondoka baada ya kupigwa na Mzee Mpili.

Faraja alikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu, lakini ugumu wa maisha ulimkuza zaidi ya uhalisia wa umri wake. Mzee Mpili alikuwa mlevi, na wakati wote alikuwa akimpiga mkewe. Licha ya ukatili kwa mkewe, Mzee Mpili alijitahidi kuonesha upendo kwa wanawe, lakini ilikuwa vigumu kwa Faraja na wadogo zake watatu kumwamini kutokana na hali yake ya ulevi na ugomvi wakati wote.

Faraja hakuwa na budi kujivika majukumu ya umama kwa kuwapikia wadogo zake na kuhakikisha kuwa wameoga na kuwapandisha kitandani. Majira ya saa 2:30 usiku, ndipo Mzee Mpili aliporudi akiwa ananuka pombe.

“We Faraja!” Mzee Mpili alimwita mwanaye kwa sauti ya ulevi huku akijikwaa wakati wa kuingia ndani.
Sauti yake ilisababisha kimya cha ghafla kwa Faraja na wadogo zake waliokuwa wakipiga kelele na kucheka chumbani baada ya kumaliza kula wakijiandaa kwenda kulala.

“Mama yenu nimemfukuza! Chizi yule,” alisema Mzee Mpili huku akikalia kiti kilichokuwa kimevunjika kutokana na ugomvi wa asubuhi baina yake na Bi Koko.

Faraja alisimama kwenye mlango wa chumba akimwangalia baba yake kwa jicho la mashaka. Machozi yalimlenga, asijue cha kumjibu baba yake.

Baada ya kimya cha dakika kadhaa, Mzee Mpili akanguruma, “Lete ugali. Mzee wa nyumba ana njaa.” Kwa haraka, Faraja akamwandalia ugali, kisha akawaambia wadogo zake wakae kimya wakati baba yao akila. Kivuli cha Mzee Mpili kilichotokana na mwanga wa kibatari kilimfanya aonekane kama zimwi lililokula watoto wakati akila ugali.

“Yule chizi wenu nimemfukuza leo,” Mzee Mpili alimwambia Faraja baada ya kutoa vyombo, akimrejea Bi Koko.
“Siwezi kulala mwenyewe na baridi hii ya Njombe. Twende tukalale chumbani kwangu.”

“Lakini baba…” Faraja alijaribu kujitetea.

“Sitaki kusikia chochote, twende!” Mzee Mpili alimvuta Faraja mkono na kufunga mlango wa chumba kwa ndani.

Faraja hakuamini alichokiona.

“Leo utanipa anachonipa yule chizi,” Mzee Mpili alisema huku akimvua nguo Faraja. Alijaribu kupiga kelele bila mafanikio, kwani alizibwa mdomo kwa kutumia mto. Juhudi zake za kujikwamua kutoka kwenye mikono ya Mzee Mpili pia hazikuzaa matunda, alikuwa na nguvu kumzidi. Faraja alipata maumivu makali sana; machozi yalimtoka, alimlaumu Mama yake kwa kumleta duniani, lakini zaidi alimlaumu Baba yake ambaye badala ya kumlinda, alikuwa chanzo cha maumivu yale.

Baada ya kumaliza haja yake, Mzee Mpili alimuonya Faraja kwa ukali kuwa hapaswi kumwambia mama yake kwa kuwa mama yake ni chizi, ndiyo sababu ya kumfukuza nyumbani, na kuwa ikitokea akamwambia mtu mwingine yeyote basi angemuua. Maneno hayo yalikuwa na nguvu kubwa ya kumfanya Faraja kufunga kinywa licha ya maumivu anayoyapitia.

Huo ulikuwa mwanzo tu wa safari ya mateso ya Faraja. Mzee Mpili aliendelea kumwingilia kimwili kwa kumbaka na kumlawiti mwanaye kwa kipindi cha mwaka mzima.

Tunaishi na matukio haya katika jamii zetu. Faraja ni mfano tu wa wahanga wa matukio haya. Dada, mama, kaka na ndugu zetu wengine ni wahanga wa ukatili huu kila siku. Takwimu kutoka Shirika la Takwimu la Taifa (NBS) zinaonesha kuwa kulikuwa na matukio 38,560 ya ubakaji na ulawiti nchini kati ya mwaka 2016 na mwaka 2020. Hii ni sawa na wastani wa matukio 21 ya ubakaji na ulawiti kila siku.

Kwa bahati mbaya, matukio haya ya ukatili, mara nyingi huwa hayaripotiwi. Upatikanaji wa haki kwa wahanga kama Faraja unatatizwa na uhalisia katika familia zetu wa kutaka matukio haya kumalizwa “kindugu” bila kupelekana mahakamani.

Tunapaswa kuelewa kuwa matukio mengi ya ukatili wa kingono hufanywa na watu wa karibu zaidi, aghalabu ndugu. Kiuhalisia, matukio 8 kati ya 10 ya ukatili wa kingono hufanywa na watu wanaofahamika kwa mhanga.

Athari za matukio ya ukatili wa kingono si za kimwili tu, ukatili huu huharibu saikolojia ya wahanga kwa kuwafanya wajihisi kutokuwa salama katika jamii na kuendelea kuishi katika hali ya wasiwasi kwa kipindi kirefu cha maisha yao. Zaidi, matukio haya huondoa muunganiko wa kijamii na imani iliyojengeka kwa kipindi kirefu. Kwa mfano, si rahisi kwa Faraja kuamini kuwa Mzee Mpili atakuwa mlinzi wake kama mzazi wa kiume baada ya vitendo hivyo.

Zipo njia nyingi za kuzuia kuendelea kutokea kwa matukio haya katika jamii zetu. Njia ya muhimu zaidi ni kuzungumza kuhusu matukio haya kila yanapotokea. Kadiri tunavyoyafumbia macho na kuyanyamazia, ndivyo matukio haya yanavyozidi kukita mizizi katika jamii. Kumbuka, jipu haliponi kwa kufunikwa, bali kwa kutumbuliwa bila kujali maumivu yatakayojitokeza katika mchakato.

Badala ya kuwatenga na kuwanyanyapaa wahanga wa matukio ya ukatili wanapojitokeza kuzungumza yaliyowasibu, jamii inapaswa kuwapongeza kwa ujasiri wao na kuwa karibu nao ili wajihisi kuwa wana thamani na wanapendwa.

Kwa wanaotenda matukio haya ya ukatili wa kingono, au wanaofikiri kumfanyia mtu yeyote ukatili wa kingono, unapaswa kuwaona watu wengine kwa zaidi ya unavyotaka kuwatendea kingono. Sababu kubwa ya kutenda ukatili wa kingono ni tamaa ya mwili na nia ya kuonesha uwezo wa nguvu juu ya unayemtendea ukatili huo. Kumbuka hao ni ndugu zetu, watoto wetu, wake zetu, nk., ambao tunapaswa kuwa sababu ya furaha, ulinzi na faraja kwao badala ya kuwa chanzo cha machozi na maumivu yao.

Kwa sasa, Mzee Mpili anatumikia kifungo cha miaka 30 katika Gereza la Mkoa wa Njombe, na hii ni baada ya Bi Koko kurejea nyumbani na kugundua mwendo wa tofauti kwa mwanaye. Baada ya kufuatilia, alifanikiwa kuhakikisha Mzee Mpili anaswekwa ndani, akishirikiana na Ustawi wa Jamii, licha ya Mzee huyo bedui kuwahonga polisi na kumgeuzia kesi Bi Koko kuwa alimpiga na kumuumiza mwanaye.

Kisa cha Mzee Mpili ni funzo kwa wote wenye nia ovu ya kutenda ukatili wa kijinsia. Usidharau nafasi yako katika kuhakikisha jamii inakuwa sehemu salama ya kuishi bila mtu yeyote kuogopa kubakwa au kulawitiwa.

Asante sana kwa kusoma andiko hili. Tafadhali lipigie kura ili liweze kushinda.

* Hiki ni kisa cha kweli kilichotokea Mkoani Njombe mwaka 2020, hata hivyo, majina yote yaliyotumika si halisi ili kulinda faragha ya mhanga (Mtoto Faraja). Baadhi ya matukio katika simulizi yametungwa kwa ufanisi wa kisanaa ili kukidhi haja ya mwenendo wa simulizi.
 
Back
Top Bottom