Kisa Cha Abunuas na mfalme...

kifupi kirefu

JF-Expert Member
Oct 29, 2018
539
3,507
KISA CHA ABUNUWASI NA MFALME JUHA.

Hapo zamani za kale Abunuwasi alimuendea mfalme akamwambia anaweza kumshonea suti ya thamani sana ambayo wenye dhambi watakuwa hawaioni na wasio na dhambi tu ndio watakuwa wanaiona.

Mfalme akampa kazi Abunuwasi ya kutengeneza suti ya aina hiyo kwa ajili yake. Kwa siku kadhaa Abunuwasi alijifungia katika chumba akawa bize anashona suti ya mfalme. Baada ya siku tatu, mfalme akamtuma msaidizi wake akaangalie kazi inavyoendelea.

Yule msaidizi akaingia chumba alichokuwa akishonea Abunuwasi lakini hakuona kitu japo alimuona Abunuwasi akifanya vitendo kama vile yuko bize anashona nguo.

Msaidizi akamwambia Abunuwasi, ‘Nimetumwa na mfalme niulizie umefikia wapi?” Abunuwasi akamjibu, “Kwani we huoni jinsi suti ilivyoanza kupendeza, ila bado namalizia nguo nyingine nataka kuanzia nguo za ndani ziwe ni hizi za kitambaa ambacho hakionekani kwa wenye dhambi”.

Hakika yule msaidizi alikuwa haoni kitu lakini ili aonekane hana dhambi akaanza kusifu jinsi nguo zilivyoshonwa kwa ufundi.

Akatoka na kurudi kumueleza mfalme kuwa Abunuwasi kamshonea nguo nzuri sana si za dunia hii kwa jinsi zilivyo nzuri.

Mfalme alifurahi sana, kesho yake akamtuma msaidizi mwingine, nae kama yule wa jana akarudi kwa mfalme na ripoti nzuri sana ya maendeleo ya koti, pia akaleta taarifa nzuri kuwa kesho yake Abunuwasi angemaliza kazi na angeleta nguo ili mfalme azivae.

Kesho yake mapema Abunuwasi akaingia katika kasri la mfalme akiwa kama kashika lundo la nguo, ambazo mwenyewe alisema wasio na dhambi tu ndio wataziona.

Wasaidizi wa mfalme wote hawakuwa wanaona kitu lakini walianza kupiga makofi wakisifu jinsi nguo zilivyokuwa nzuri, hamna aliyekuwa anataka kuonekana ana dhambi.

Hatimae Abunuwasi akamkabidhi mfalme nguo, mfalme nae hakuwa anaona kitu lakini ili asiambiwe ana dhambi akajidai eti naye anaziona akaanza kumsifu Abunuwasi kwa umahiri wake wa kuchagua rangi na hata ufundi wake mkubwa wa kushona.

Abunuwasi akamuomba mfalme azivae zile nguo, wakaingia faragha mfalme akavua nguo zake na akaanza kuvaa nguo asizoziona kwa msaada wa Abunuwasi.

Kwa vile alivua nguo zote na kuvalishwa mpya zisizoonekana, rohoni mwake alikuwa anajiona yuko uchi lakini akaona akitangaza haoni kitu wananchi wangemshangaa kuwa mfalme ana dhambi, hivyo akaendelea kusifia na kujiangalia kwenye kioo akisifu nguo zilivyompendeza. Kisha akalazimika kutoka nje ili wananchi waone nguo mpya za mfalme.

Wote walikuwa wanamwona mfalme yuko uchi lakini wakawa wanaogopa kuonekana wana dhambi hivyo kila mtu akawa anashangilia na kusifu uzuri wa nguo za mfalme.

Lakini ghafla mtoto moja mdogo kwa sauti kubwa akamuuliza baba yake, “Baba mbona mfalme yuko uchi?”.

Minong’ono ikaanza mwishowe watu wakaanza kumuunga mkono mtoto, mfalme nae sasa aibu ikamshika kwani alijua sasa watu wote wanamuona yuko uchi, akatimka na kujificha kwenye kasri lake na hadithi yangu imeisha hapo...
 
Ukiwa kiongozi, ukijaliwa hekima japo kidogo sana, cha kwanza ni kujitenga na watu wanafiki. Hata siku moja usijivunie watu wanafiki. Mnafiki anaenda na upepo. Dhamira kuu ya mtu mnafiki, ni kuhakikisja tumbo halilali na upepo bali wakati wote lijae chakula.

Mtu mnafiki akijua kwamba wewe kiongoza unapenda uonekane ni tofauti na wanadamu wengine, anaweza hata kulia na kujigaragaza chini usiku na mchana mbele ya kundi la watu, akisema mbele ya watu kuwa wewe kiongozi una mikono minne, na kutokana na mikono yako minne una uwezo kushinda watu wote kwa kila kitu.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Kitengo na mfumo wajameni fanyeni kazi iliyostahili. Huyu mtoto katokea wapi tena?
 
Back
Top Bottom