Mwabhleja
JF-Expert Member
- Jan 27, 2016
- 1,351
- 2,061
"Acha ukweli usemwe, usiposemwa hakuna atakayekasirika hapa" hayo ni maneno yaliyowahi kusemwa na Tuntemeke Sanga. Alikuwa akijaribu kuelezea hisia zake juu ya mapungufu ya uongozi wa Mwl.Nyerere ambapo mara nyingine amri iliongoza nchi badala ya maafikiano, ubunifu, ushawishi na mafundisho juu ya vile mambo yanavyotakiwa kwenda.
Nimejaribu kuchunguza vema falsafa ya uongozi wa Mhe.Magufuli tangu aingie madarakani na kugundua kwamba hana vipaumbele maalumu jambo ambalo ni kama kuendesha gari pasi na kujua mwisho wako utakuwa wapi, pengine hii ndiyo mantiki ya Mhe. Edward Lowassa kuweka bayana kwamba uongozi wa Mhe. John Magufuli umekosa maono.
Mpaka sasa nchi inakabiliwa na changamoto kubwa tatu ambazo Mhe. Magufuli hajaziona kama zinafaa kuwa sehemu ya vipaumbele vyake.
1. Falsafa ya nchi: hii nchi haijulikani inaamini juu ya nini kwa maana inafikiri kijamaa wakati inaishi kibepari. Wadau mbalimbali walipendekeza juu ya kuwepo dira ya taifa itakayoongoza uendeshaji wa nchi kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa. Wananchi wake hawajulikani wanaishi ili waweje, wanasoma kwa sababu gani, wanasoma nini na kwanini wawe na mfumo huo wa maisha. Mwalimu alijitahidi kuweka misingi, Mhe.Magufuli anataka kujaribu lakini hana maono.
2. Soko huria: hili pia ni maarufu kama soko holela ambalo bado hakuna dalili za kupata suluhu. Nchi haina nafuu yoyote kwa wanyonge katika mfumo huu, leo hii Mhe. Magufuli anawatuma wakuu wa mikoa kuhakikisha vijana wanafanya kazi tena ikibidi kwa lazima lakini anasahau kwamba hayo yangefanyika zamani tusingekuwa na kina Diamond mijini maana watu wenye vipaji vya aina hii hupitia mlolongo mrefu wa kutoka kimaisha. Tuachane na hayo, wakulima vijijini wanalima mno, mwaka jana tani kibao za mahindi zilioza mkoani Ruvuma kisa kukosa soko. Huwezi amini kwamba kuna watoto hawakunuliwa nguo mpya kisa tu wazazi wao walizalisha sana hivyo mahindi yalikosa soko.
Kibaya zaidi kwenye soko huria, fedha nyingi haionekani ila ipo na inaumiza wananchi; makampuni ya simu yamehifadhi mapesa mengi ambayo pengine yangekuwa benki basi taasisi hizo zingepunguza hata kiwango cha riba kwa wakopaji masikini. Tofauti na mabenki yalivyo chini ya BOT, makampuni ya simu yanapiga faida bila taarifa za uhakika juu ya faida wanayopata.
3. Ombwe la uongozi: Fasiri kamili ya uongozi imepotea na badala yake imekuwa kwamba uongozi ni mkuu wa mkoa kuwadhalilisha walimu kama alivyofanya Magesa Mulongo huko Mwanza ili mradi tu mwandishi wa habari yupo. Uongozi umekuwa kuamrisha sana na kushauri kidogo, uongozi umekuwa camera nyingi na siyo makofi mengi ya walalahoi, uongozi umekuwa sifa badala ya wajibu n.k
Ni vema ukweli usemwe ili msingi bora wa kuimarisha ujenzi wa taifa imara kwa miaka hamsini ijayo uimarsh.we.